Edo Kumwembe: Nimemkumbuka Anko Mrisho Ngassa katika ubora wake

Oldmantz

JF-Expert Member
Jan 24, 2023
430
996
Ghafla nimemkumbuka Anko Mrisho Ngassa katika ubora wake. maisha yanayoyoma kwa kasi. Kwa sasa yupo mitandaoni akiposti video zake na kuelezea kila anachokifanya katika maisha. Huku katika soka amebakia kuwa shabiki tu.

Baada ya Edibily Jonas Lunyamila kutamba sana katika soka kwa miaka mingi kama winga, Mwenyezi Mungu alituletea Anko Ngassa. Hawakuwahi kufanana kwa mambo mengi lakini pande za pembeni wanaweza kuwa wachezaji bora wa zama zao waliokabidhiana vijiti.

Ngassa alikuwa winga bora kwa sababu alikuwa ana kasi na matumizi mazuri ya akili katika eneo la mwisho. Angeweza kufunga mwenyewe kwa ustadi mkubwa na angeweza kupika mabao kwa wenzake. Kasi yake haikuwa ya mwendabure.

Achilia mbali mikimbio yake upande wa pembeni lakini Ngassa pia alikuwa na uwezo mkubwa wa kukimbia eneo la katikati na kusababisha madhara makubwa kwa wapinzani. Alichohitaji ni nafasi ya kukimbia tu. lakini hata kama kungekuwa na kundi kubwa la maadui mbele yake alikuwa na uwezo pia wa kupiga chenga.

Anabakia kuwa mfungaji bora wa muda wote katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania ingawa taifa hili lilibarikiwa kutoa wachezaji mahiri ambao wamewahi kukipiga katika timu ya taifa kwa mafanikio. Usiwasahau akina Zamoyoni Mogella.

Nimemkumba Anko Ngassa kwa sababu tatu za msingi. Sababu ya kwanza ninapomuonea huruma kwa kupishana na maisha ya soka ya kizazi hiki katika ngazi ya klabu. Ngassa alicheza mpira mkubwa na alifanya mambo makubwa katika klabu yake ya Yanga katika zama ambazo Yanga haikuishi hivi kiuchumi, kimawazo na kimafanikio.

Wakati ule walikuwepo watu walioonekana kuwa matajiri lakini wasingeweza kwenda Morocco kuweka kambi kama GSM walivyofanya. Wasingeweza kuiweka timu katika kambi ya kisasa kama ya Avic kama ambavyo sasa hivi Yanga wanakaa.

Kuna maandalizi mengi ya Yanga ya leo ambayo yamekuwa tofauti na Yanga ya zamani. Hata wachezaji wengi aliocheza nao hawakuwa na ubora mwingi kama hawa wa leo akina Khalid Aucho na wengineo. Najaribu kuwachomoa mawinga wawili wa sasa wa Yanga na naamini Yanga ingekuwa bora zaidi leo kama ingekuwa na Ngassa kuliko ilivyo sasa.

Wachomoe Jesus Moloko na Tuisila Kisinda kisha muweke Anko Ngassa katika ubora wake. Nadhani Fiston Mayele angefunga mabao mengi zaidi ya haya anayofunga sasa. Unaweza kuwauliza akina Boniface Ambani na watakuthibitishia hiki ninachokisema.

Sihitaji tubishane kuhusu Tuisila na Moloko dhidi ya Ngassa. Nadhani wote tunafahamu kwamba Ngassa alikuwa bora zaidi yao. Tatizo ni namna gani ambavyo Anko amepishana na zama hizi. Anko wa wakati ule katika kikosi hiki cha Yanga angekuwa staa mkubwa anayekaribiana kuhusudiwa na mashabiki kama ilivyo kwa Mayele.

Bernard Morisson ni mchezaji mzuri na mwenye kipaji kikubwa, inawezekana zaidi ya Ngassa. Lakini muda wowote ule namchukua Ngassa mbele ya Morrison kwa sababu Ngassa alikuwa bora kila wikiendi na kila uwanja wowote aliocheza soka.

Morrison ana homa ya vipindi. Kuna mechi anacheza vizuri halafu inayofuata hatuonyeshi makali yake. anaweza kupotea uwanja ni katika mechi tatu halafu akaibuka katika mechi moja. Ngassa hakuwa mchezaji wa namna hiyo.

Sababu nyingine ambayo imepelekea nimkumbuke Anko Ngassa ni namna ambavyo kila siku wachezaji wazawa wanavyopotea katika umuhimu ndani ya klabu kubwa. Sio tu kwa Yanga, lakini hata kwa Simba Ngassa angetamba upande wowote wa pembeni.

Muda pekee ambao ingebidi agawane umuhimu na mtu katika upande wa pembeni ni pale Simba walipokuwa na Jose Luis Miquissone. Pale kungekuwa na changamoto na nadhani mmoja angecheza kulia na mwingine angecheza upande wa kushoto.

Lakini kwa hali ilivyo sasa pale Simba, Ngassa ni bora kuliko Ousmane Sakho, ni bora kuliko Kibu Dennis, ni bora kuliko winga yeyote ambaye anapangwa pale Simba. huu ndio ukweli kwamba Ngassa amepishana na hivi vikosi vya dhahabu.

Amepishana na vikosi vya Simba na Yanga ambavyo vimeimarika pia kisaikolojia. Tangu mwanzo wa msimu huwa vinaangalia namna ya kufika hatua za robo fainali katika michuano ya Ligi ya mabingwa au ile ya shirikisho.

Wakati yeye anacheza hakufika robo fainali ya michuano yoyote katika ngazi ya klabu. Kufika makundi tu ilikuwa ni mtihani na hakuwahi kufika. Nadhani ni kwa sababu ya kupishana na vizazi hivi vya wakubwa ambavyo vimeimarika zaidi.

Bila ya kujali nafasi zao uwanjani kinachosikitisha zaidi ni kwamba katika maeneo ya mbele ya vikosi hivi wazawa wametoweka. Kijana Clemence Mzize anajaribu kuchomoza baada ya Fei Toto kutoweka. Hassan Dilunga katika Simba alikuwa mzawa wa mwisho kuwa tishio katika eneo la mbele akishirikiana na John Bocco.

Huku pembeni inasikitisha zaidi. kila nafasi inayojitokeza inakwenda kwa mgeni. Labda Simon Msuva pia aliitendea haki lakini kuanzia hapo zimekuwa nafasi za wageni. Wakati mwingine tunaishia kuwalaumu viongozi wetu kwa kusajili wachezaji wa kigeni lakini tuzungumze ukweli ni winga gani bora wa pembeni ambaye hachezi Simba na Yanga.

Hapa karibuni Simba na Yanga zimejaribu wachezaji wengi wa nafasi za mbele lakini ukweli ni kwamba wanashindwa kumudu mapigo pindi wanapoingia katika timu kubwa. Dogo ambaye nilimtegemea hivi karibuni, Dickson Ambundo naye anaonekana kuniangusha.

Vipi kuhusu rafiki yangu, Habib Kyombo? Mambo yanaonekana kwenda kombo pia pale Msimbazi. Vyovyote ilivyo, leo nimemkumbuka sana Anko Ngassa. Alitamba katika nyakati zake lakini nadhani hakutamba katika nyakati sahihi. Huu ungekuwa muda mwafaka kwake.

Mwanaspoti
 
Ngassa alichezea maisha mwenyewe alijifanya Yanga damu, alipoenda kwa majaribio westham alipewa program ya mazoezi yeye akakimbilia kuongeza make, Azam walipomsajili kwa pesa nyingi alijifanya anaikumbuka yanga hata timu ya Sudan ilipoleta ofa kubwa aliikataa yanga hivyo SI kweli alipishana na pesa
 
Dah! Nakumbuka miaka ile ya 2000's wakati Anko anasajiliwa kutoka Kagera kuja Yanga! Aisee alikuwa ni Anko kweli.

All in all, ukosefu wa nidhamu nje ya uwanja, na mahaba yake yaliyopitiliza kwa Yanga; bila shaka yamechangia kumfanya ashindwe kufikia kilele cha mafanikio yake kimaisha, hata baada ya kutundika daruga.
 
kipaji bila akili ni bure ndo maana wachezaji wanatakiwa kuwa na ma meneja
Nadhani ifike muda wachezaji wawe na mawakala sio mameneja. Lakini naunga mkono hoja yako Kua ni muhimu kwa wachezaji kua na USIMAMIZI mzuri.

Nimeanza kulifatilia soka la bongo tangu mwaka 2006. Nikiri wazi ukimtoa Luis miquesson na benard Morrison sijawahi kumuona winga wenye balaa kama la Mrisho ngassa. Kwangu ndiye mchezaji Bora zaidi Kwa upande wa wazawa niliyewahi kumshuhudia ligi kuu bara.

Angepata usimamizi mzuri naamini Anko angecheza ligi kubwa duniani
 
Nilimuona ngasa pale kwa mkapa akiisumbua Cameroon ya kina Etoo , Alex song , Rigobert song , geremi , billy tchato nk
Alikuwa pure talent aliyestahili kucheza ulaya alikosa msimamizi au mshauri na pengine alizungukwa na machawa
Nasikia sasahivi Ana academy yake ya kuibua vipaji vya soka
 
For Some of us tulianza kucheza nae chandim kabisa...Kombe la mbuzi and then kombe la Jimbo. Shule & viwanja kubadilishwa matumizi vikatuachanisha...it was a pure talent ingawa wakati huo tunacheza cha ndimu kulikua na vipaji vikubwa kuliko yeye ni vile inchi yetu haina utaratibu wa kuibua na kutunza vipaji...Juzi nimemuona David Beckam anamiliki club huko US...hiki ndo alipaswa kua nacho Ngasa ht kwa level ya hapa inchini..
Tunahitaji kuibua, kuendeleza na kutunza vipaji...Ngasa alipaswa kua tajiri mkubwa kwa kipaji chake too bad how his football career ended.
 
Mchezaji wangu bora tanzania niliyewahi kumshuhudia ni mrisho ngasa alikua na balaa kweli kweli.. mimi naamini ngasa ktk ubora wake ni zaidi ya morison na Luis Jose ila ngasa aliangukia ktk kizazi kisicho sahihi cha mpira wake
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom