Dkt. Ulimboka amuumbua mmoja wa wahusika wa utekaji wake!

vimon

Senior Member
Apr 3, 2008
183
195
Kamanda aliyehusika kumtesa Dr. Ulimboka na mmoja kati ya watu wanaounda tume ya kuchunguza unyama aliofanyiwa Dr. Ulimboka ameaibika mara alipoingia chumba alicholazwa Dr. Ulimboka aliweza kumtambua na kumwambia "Nirudishie simu na wallet yangu".

Kamanda alitoka wodini kainamisha kichwa.

Source (Mimi mwenyewe-nilikuwepo)

=======

Kutoka Gazeti la Mtanzania

NI UNYAMA!

*Dk. Ulimboka atekwa nyara, avunjwa taya na mikono
*Ang'olewa meno na kucha kwa koleo, apasuka kichwa
*Amtambua mmoja wa watekaji, asema aliwahi kumuona
*Dk. Nchimbi alaani tukio, aahidi uchunguzi utafanyika


MGOMO wa madaktari unaoendelea nchini umechukua sura mpya. Juzi usiku wa kuamkia jana, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Stephen Ulimboka, alitekwa na watu wasiojulikana.

Baada ya kutekwa na kupigwa vibaya na watekaji hao, Dk Ulimboka alitelekezwa katika msitu wa Mabwepande, uliopo katika Manispaa ya Kinondoni, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Kutokana na tukio hilo, daktari huyo aliokotwa jana saa 12 asubuhi na wananchi waliofika eneo alikokuwa ametelekezwa.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo, Msaidizi wa Dk. Ulimboka, Dk. Deogratius Michael, alisema:

"Jana (juzi) usiku, tulikuwa na Dk. Ulimboka maeneo ya Leaders Club Kinondoni na ghafla walifika watu watano wakiwa ndani ya gari aina ya Suzuki Escudo lenye rangi nyeusi lisilokuwa na namba za usajili.

"Watu hao walikuja mpaka mahali tulipokuwa na kujitambulisha kuwa ni askari polisi na wanamhitaji Dk. Ulimboka Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Dar es Salaam.

"Baada ya askari hao kumchukua Dk. Ulimboka na kuondoka naye, sisi tulikwenda kituo hicho cha polisi ili kujua kwa nini wamemchukua, lakini tulipofika hatukumkuta na badala yake tulitoa maelezo na kuondoka.

"Pamoja na kutomkuta, tuliendelea kumtafuta kwa njia ya simu lakini hakupatikana hadi tulipopigiwa simu leo asubuhi na msamaria mwema akitueleza kuwa Dk. Ulimboka yupo Mabwepande ametelekezwa na amejeruhiwa vibaya.

"Nilipopokea taarifa hiyo, niliwatafuta watu wengine, tukaondoka kwenda Mabwepande na kumkuta Dk. Ulimboka akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake na meno yote pamoja na kucha zikiwa zimeng'olewa na inaonekana walitumia ‘plaizi' na tulipomchunguza vizuri, tuligundua pamoja na kung'olewa meno na kucha pia amevunjwa taya.

"Nilipomuona sikuamini kama yule ni Dk. Ulimboka, alikuwa uchi na mwili mzima ulikuwa na majeraha makubwa, nilizungumza naye akawa anaongea kwa shida, lakini nilimuelewa.

"Kwa mujibu wa Dk, Ulimboka, anieleza kuwa baada ya kuchukuliwa pale walianza kumpiga sehemu mbalimbali za mwili na kuishiwa nguvu na walipoona yuko hoi walianza kushauriana.

"Walikuwa wanashauriana kwamba wampige risasi, wengine wanakataa, wakapendekeza wamweke barabarani na kumgonga na gari ili ionekane amegongwa na gari, mwingine akakataa, akasema wamdunge sindano yenye sumu na kumuua lakini pia hawakukubaliana.

"Dk Ulimboka alinieleza kwamba, baada ya kutafakari yote walifikia uamuzi wa kumpeleka msitu wa Mabwepande baada ya kuonekana muda wowote anaweza kufariki na kumvua nguo zote na kuchukua simu zake zote," alisema Dk. Deo.

Kutokana na hali hiyo, alisema walitoa taarifa Kituo cha Polisi Bunju na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ili kupata gari la wagonjwa.

"Jambo la ajabu ni kwamba, Muhimbili waligoma kabisa kutoa gari la wagonjwa, hivyo tukalazimika kukodi gari jingine la wagonjwa kutoka Kampuni ya AAR," alisema.

Alisema kampuni hiyo iliwapatia gari lenye namba za usajili T 151 AVD na kumleta Hospitali ya Taifa Muhimbili ili kupata matibabu.

Hata hivyo alisema hali yake wakati anafikishwa ilikuwa mbaya na alilazwa katika Chumba cha Wagonjwa mahututi (ICU).

Hali ilivyokuwa Muhimbili

Dk. Ulimboka alifikishwa hospitalini hapo jana saa nne asubuhi huku akisindikizwa na wanaharakati mbalimbali, wakiwamo Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Haki za Binadamu, Dk. Hellen Kijo Bisimba, Mkurugenzi wa Taasisi ya Sikika, Irenei Kiria na wengine wengi.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo waliangua vilio baada ya kumuona Dk. Ulimboka akiwa hoi na mwili wake ukiwa unavuja damu kutokana na majeraha mbalimbali.

Vilio hivyo vilizua taharuki kubwa kwa wagonjwa na kusababisha huduma zote hata za dharura zilizokuwa zikitolewa hospitalini hapo kusimama, huku kila mmoja akitaka kumuona daktari huyo.

Madaktari hao na wauguzi walipositisha huduma nyingine, walielekeza nguvu na utaalam wao katika kuokoa maisha ya mwenzao huyo, ingawa wengine walisikika wakilia kwa chini chini.

Katika hospitali hiyo, waandishi wa habari waliokuwapo walizuiwa kufika katika baadhi ya maeneo kutokana na sababu ambazo hazikuwa wazi.

Wakati hayo yakiendelea, madaktari na wauguzi jana walionyesha umoja wa hali ya juu, kwani walifurika hospitalini hapo kutoka katika hospitali mbalimbali, zikiwamo Amana, Mwanyamala kwa ajili ya kuongeza nguvu za kitabibu.

Kutokana na wingi wa watu waliokuwa mahali hapo, ilifika wakati waandishi wa habari wakajikuta wamefungiwa ndani ya moja ya korido za Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI).

Waandishi hao walipofungiwa katika eneo hilo, Dk. Ulimboka alitoroshwa kupitia mlango wa nyuma na kupelekwa kitengo cha maabara na X-ray.

Askari apigwa na madaktari

Wakati Dk. Ulimboka akiwa MOI ili kupatiwa matibabu, katika hali isiyo ya kawaida, mtu mmoja aliyekuwa ndani ya chumba cha matibabu alitoka na kuingia chooni na kusikika akizungumza na simu ya mkononi.

Mtu huyo ambaye alionekana kuhusika moja kwa moja kutekwa kwa daktari huyo, alisikika akisema kuwa ‘Kumbe hajafariki, bado ni mzima, mimi niliwaambia tumchome sindano ya sumu nyie mkakataa, sasa bado yuko hai'.

Mtu huyo bila kujijua kwamba alichokuwa akikisema kilikuwa kikisikika kwa madaktari, alijikuta akivamiwa na kundi la madaktari ambao walimhoji kisha wakampiga na kuvunja simu yake ya mkononi na simu yake ya upepo (radio call) aliyokuwa nayo.

Kuna taarifa zinasema kuwa, mtu huyo alipoteza bastola aliyokuwa nayo.

Kutokana na kichapo hicho, mtu huyo ambaye alikuwa amevalia suti nyeusi aliokolewa na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na kufungiwa kwenye kibanda cha walinzi wa getini na kufanyiwa mahojiano na kubainika ni Mkuu wa Upelelezi Kituo cha Polisi, Salender Bridge, ASP Mokiri.

Baada ya mahojiano hayo, askari huyo alitoroshwa na askari wenzake kwa kutumia gari la kukodi yenye namba za usajili T 716 BKZ, huku akisindikizwa na gari la polisi lenye namba T 220 AMV lililokuwa na askari wenye silaha na mabomu ya machozi.

Wakati wa tukio la kumtorosha askari huyo, waandishi wa habari walikuwa wakizuiwa kupiga picha, huku wengine wakitishiwa kupasuliwa kamera zao na baadhi ya waandishi walipigwa makofi na kusukumwa.

Katika tukio hilo, askari huyo alichaniwa nguo na kutafutiwa nguo nyingine za kuvaa kwa kuwa zile suti zilichanwa na madaktari wakati wanampiga.

Madaktari waandamana

Wakati Dk. Ulimboka akipelekwa katika vyumba mbalimbali kwa ajili ya matibabu, madaktari walikuwa wakilisukuma gari alilokuwamo huku wakiimba nyimbo za mshikamano.

Baada ya muda mfupi madaktari hao walikutana wenyewe na kuandaa tamko lao lililojumuisha Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) na Jumuiya ya Madaktari na kulitoa mbele ya waandishi hao wa habari.

Akizungumza na waandishi hao, Rais wa MAT, Dk Namala Mkopi, alisema wamesikitishwa na unyama huo aliofanyiwa Dk. Ulimboka.

"Kutokana na kitendo hiki cha unyama, tumeamua kuungana pamoja na kupigania maisha ya Dk. Ulimboka na si wengine tena, tunapenda kuwaambia Watanzania tunalaani kitendo hiki cha unyama na tukio hili limetuhamasisha kuwa imara zaidi.

"Tumegundua hii ni mbinu maalum iliyoundwa na Serikali ya kumuangamiza Dk. Ulimboka na hii imedhihirika katika sura mbili, moja Muhimbili wamekataa kutoa ushirikiano wa kutoa gari la wagonjwa, pili tumempata askari akitoa taarifa kwa wenzake kwamba Dk. Ulimboka hajafariki na alitakiwa kuchomwa sindano ya sumu.

"Kutokana na haya, sasa natangaza kuwa mgomo uko pale pale, kwani sasa umechochewa zaidi," alisema Dk. Mkopi.

Pinda: Liwalo na liwe

Wakati hayo yakiendelea jijini Dar es Salaam, bungeni Mjini Dodoma, jana asubuhi, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliliambia Bunge, kuwa mgomo wa madaktari ulipofikia sasa ni pabaya na sasa bora litakalokuwa na liwe kuliko kuacha hali hiyo ikiendelea kinyume cha sheria.

Alisema kuwa, leo Serikali itatoa kauli bungeni kuhusu mgomo huo kwa kuwa Serikali iliamua kukaa kimya ili kuona utekelezaji wa amri ya Mahakama ukitekelezwa.

Pinda alitoa kauli hiyo baada ya Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM), kuomba Mwongozo wa Spika kuhusu mgomo wa madaktari unaoendelea nchini.

Baada ya mbunge huyo kuomba mwongozo huo, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alimuomba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, atoe kauli ya Serikali bungeni hapo.

Akizungumzia mgomo huo, Waziri Mkuu Pinda alisema Serikali imefanya jitihada kubwa, lakini dhamira kwa madaktari imeondoka na kwamba jana (juzi), serikali ilikutana na kutafakari jambo hilo na leo itatoa kauli yake.

Dk. Nchimbi alaani tukio

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, amelaani tukio hilo, huku akisema hivi sasa Jeshi la Polisi linaendesha msako mkali kuhusu tukio hilo.

Dk. Nchimbi aliyasema hayo Mjini Dodoma, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

"Jana asubuhi katika Kituo Kidogo cha Polisi Bunju, liliripotiwa tukio la mtu kupigwa katika Msitu wa Pande na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Juma Mgaza ambaye alikuwa amembeba Dk. Ulimboka katika gari yake.

"Baada ya mahojiano ya muda Mgaza, alisema alikuwa akipita katika njia na kumkuta Dk. Ulimboka akiwa amepigwa na kumuomba msaada.

"Baada ya kupokelewa hatua iliyofuata ni kuhakikisha anakimbizwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu.

"Katu Serikali haiwezi kuvumilia vitendo hivi vya utekaji watu ambavyo ni kinyume cha sheria zetu za nchi na tunalaani tukio hili na hivi sasa tayari Jeshi la Polisi lipo katika msako mkali wa kuwatafuta wahusika wote wa tukio hili," alisema Dk. Nchimbi.

Akizungumzia tukio la kupigwa mtu ambaye alidhaniwa ni moja ya watekaji nyara wa Dk. Ulimboka, Waziri Nchimbi, alisema ni kweli mtu huyo alikuwa ni Ofisa wa Jeshi la Polisi na siyo kati ya waliokuwa wamemteka Dk. Ulimboka.

"Yule ni Ofisa wa Jeshi la Polisi ambaye ni Mkuu wa Upelelezi wa Kituo cha Polisi Salender Bridge, yule ni ASP Mokiri ambaye alitumwa na mkuu wake wa kazi kwa ajili ya kufuatilia tukio hilo.

"Kwa mujibu wa tarifa, alipofika pale na kuonekana ana radio call, baadhi ya madaktari walimvamia na kuanza kumpiga kwa kumtuhumu ni moja kati ya watu waliomteka Dk. Ulimboka," alisema Dk. Nchimbi.

Zitto Kabwe anena

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana jioni, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), alisema kwanza amepokea ujumbe mfupi wa simu.

"Nimetumiwa ujumbe na daktari mmoja yupo pale MOI akisema hivi, kaka Zitto, hali ya Dk. Ulimboka yuko unconscious, multiple ribs fracture na kwenye mikono pia amevunjika pamoja na taya, yuko ICU wanamstabilise kwanza kwa sababu hapumui vizuri, the situation here is really bad, I agree with you this is outright outrageous," ulisema ujumbe huo wa Zitto kutoka kwa daktari huyo.

Pamoja na hayo, Zitto alisema amechukizwa na habari za kutekwa, kupigwa na kuumizwa vibaya kwa Dk. Ulimboka ambaye ni Kiongozi wa Madaktari Nchini.

"Mambo kama haya tumezoea kuyasikia kwenye nchi za kidikteta na kuongozwa kiimla ambapo watawala badala ya kutumia njia ya kidemokrasia na kisheria, kushughulikia wanaoamini ni maadui zao katika utawala, hutumia wahuni katika taasisi za usalama kuteka raia, kuwatesa, kuwafunga na hata kuwaua.

"Sitaki kuamini kwamba Tanzania imefikia huko, nimezungumza na baadhi ya madaktari walio karibu na Dk. Ulimboka na kujulishwa kwamba, majeruhi huyu alikamatwa jana usiku mnamo saa sita na watu wasiojulikana na kupelekwa katika msitu wa Mabwepande na kujeruhiwa vibaya. Habari hizi bado hazijathibitishwa na vyanzo huru lakini ndio zilizopo hadi hivi sasa.

"Serikali inawajibika kueleza kama sasa imeamua kutumia njia za kihuni kumaliza matatizo na wananchi wake.

"Nimemuomba Waziri kivuli wa Afya wa CHADEMA kufuatilia suala hili kwa karibu sana ili kuhakikisha kwamba ukweli wote na ukweli mtupu unafahamika. Kamwe hatuwezi kuacha Mtanzania yeyote aonewe, anyanyaswe au akandamizwe eti kwa sababu ya kudai haki yake na za wenzake, an injury to one, injuries to all.

"Naomba madaktari wamwangalie kwa karibu daktari mwenzao ili aweze kupata nafuu. Ulinzi uimarishwe ili kuhakikisha usalama wake," alisema Zitto katika taarifa hiyo.



Wanaharakati walaani
Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo Bisimba, alisema wanaharakati wote wamelaani kitendo hicho na kusema kuwa huo ulikuwa ni mpango wa Serikali kwa ajili ya kuwanyamazisha wananchi.

"Nilipokea simu saa 12 asubuhi kutoka Kituo cha Polisi Bunju, tulipofika tuliishiwa nguvu baada ya kumuona Dk. Ulimboka namna alivyokuwa amepigwa vibaya.

"Huu unaonekana kuwa ulikuwa ni mpango wa Serikali kwa sababu hata Dk. Ulimboka alipohojiwa na kuzungumza kwa shida alithibitisha kuwa alimtambua mmoja wa watu waliokuwa wakimpiga kwani alimuona Ikulu wakati alipofika katika awamu ya kwanza ya mgomo wao.

"Kwa sababu Dk. Ulimboka alisema kuna mtu aliyemtaja kwa jina la Abel ambaye alikuwa akimpigia simu mfululizo kwa muda wa siku tatu akitaka waonane ana kwa ana kabla ya kuitikia wito juzi na kutendewa unyama huo.

"Kiujumla hiki ni kitendo cha kinyama ambacho hatuwezi kukivumilia, kwani Serikali imethibitisha kuwa kweli haiwajali wananchi," alisema Bisimba.

Alisema kutokana na hali hiyo wanaitaka serikali kuunda tume huru kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo kwa sababu mazingira yake yana utata.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa taasisi ya SIKIKA, Irenei Kiria, alisema serikali imeonesha kushindwa kutatua matatizo yaliyopo katika sekta ya afya na badala yake imeamua kutumia mabavu.


KOVA: Tumeunda tume
Kutokana na uzito wa tukio hilo, Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limewaomba wananchi Kutoa ushirikiano utakaofanikisha kupatikana kwa watu waliomteka Dk. Ulimboka.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Suleiman Kova, alisema jeshi hilo limeunda jopo la wapelelezi linaloongozwa na Mkuu wa Upelelezi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Ahmed Msangi.

Alisema kuwa, tukio hilo ni la kipekee na Jeshi la Polisi limejiandaa kukabiliana nalo na wahusika kufikishwa katika vyombo vya sheria.

"Siku ya tukio walikuja watu akiwa kwenye club moja pale Leaders Club, wakamchukua kwamba wao ni polisi na wanampeleka Kituo cha Polisi.

"Wakati wanaondoka, kwa mujibu wa maelezo yake, ndani ya gari kulikuwa na watu sita pamoja na yeye ambapo walianza kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili.

"Dk Ulimboka aliendelea kueleza kwamba, walipofika eneo la Mwenge walimvisha fulana nyeusi usoni na kwamba hakujua tena walikokuwa wakielekea na hatimaye alijikuta yuko Msitu wa Pande.

"Alisema kuwa, mmoja wa watekaji wake alimwambia watamuua na wakaendelea kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kutumia ngumi na mateke na mwishoni walimuacha hapo na kisha wakaondoka zao.

"Dk Ulimboka alieleza kuwa, baada ya kuwa ameachwa hapo, alijivuta na kufika barabarani na ilipofika majira ya asubuhi, ndipo huyo raia mwema alipomuokoa akiwa amefungwa kamba miguuni na mikononi na kumpeleka hadi Kituo Kidogo cha Polisi Bunju," alisema Kova akimkariri Dk. Ulimboka.

Habari hii imeandaliwa na Gabriel Mushi na Benjamini Masese, Dar es Salaam na Bakari Kimwanga, Dodoma.

 
Nami nimesikia hivyo..sura imemkaa akilini kwasabb cku ya kikao na mkulu magogoni alikuwepo pia.
Kamanda msangi aliyehusika kumtesa Dr. Ulimboka na mmoja kati ya watu wanaounda tume ya kuchunguza unyama aliofanyiwa Dr. Ulimboka ameaibika mara alipoingia chumba alicholazwa Dr. Ulimboka aliweza kumtambua na kumwambia "Nirudishie simu na wallet yangu".

Kamanda Msangi alitoka wodini kainamisha kichwa.

Source (Mimi mwenyewe-nilikuwepo)
 
Kamanda Msangi aliyemkamata na kumtesa Dr Ulimboka yupo katika jopo la kuchunguza nini kilimtokea Dr Ulimboka. Alipofika kumuhoji Dr Ulimboka alimwambia 'Nirudishie simu na waleti yangu'. Kamanda Msangi taratibu akatoka wodini kichwa chini.

Huu ni ushahidi tosha

anza kunoa mapang
 
Chini ya ulinzi upi sasa?hapa nikujichukulia sheria mkononi nyonga wote waliohusika.
Kama police ndo wanalinda uasalama wa raia kwa nn wasichukue hatua?? kama ndo hao hao wamehusika bas hatunabudi kujichukulia sheria mkononi,piga kama mwizi,choma moto!!!
 
Du huyu Msangi, Mpare aliyetoka Dodoma akaenda Moro baadae Dar hii kali naona Dr atawatambua wote wauaji wake na nani kawatuma kwa Dau gani
Dr Ulu ugua pole
 
Du huyu Msangi, Mpare aliyetoka Dodoma akaenda Moro baadae Dar hii kali naona Dr atawatambua wote wauaji wake na nani kawatuma kwa Dau gani
Dr Ulli ugua pole
 
Hii ni hatari ama kasingiziwa? ana ujasiri gani- ama kweli siku nyani anakufa miti yote huteleza.
 
Madaktari na manesi wanaomhudumia wawe makini wasiruhusu watu ovyo kwenda kumwona wengine sio wazuri wasije wakammaliza kijana wa watu. Ningekuwa mzazi wake au nduguye wa karibu nisingetoka kando ya kitanda chake nikimlinda! Duniani kuna majitu yana roho mbaya kuliko wanyama. Sijui wamepata nini sasa baada ya kufanya walichokifanya.
 
Back
Top Bottom