Dr. Slaa avuliwa nguo, dili alilipanga Josephine. Alonga na Mwakyembe kabla hajaingia kwenye mkutano

amilyroley

JF-Expert Member
Jun 23, 2015
621
1,199
Hii ni kwa hisani ya magazeti ya Leo.... Siri ya mkutano wa Dr Slaa zinaanza kuvuja. Gazeti la Mawio linaripoti kuwa dili lote la kununulika kwa Dr Slaa liliratibiwa na mchumba wake aitwaye Josephine. Gazeti la Nipashe linalonga kuwa Makada Wa CCM walimpiga tafu kuandaa press.

Pia Dr Slaa alikuwa na private meeting na Dr Harrison Mwakyembe ndani Serena hotel saa chache kabla Dr Slaa hajaingia kufanya Press na wanahabari. Pia linasema nani alimlipia milioni 80 za kurusha matangazo hewani na kulipia ukumbi wakati anadai hana hela anakula mihogo.

Dr Slaa anadaiwa kumpaisha Lowassa kwa alichokifanya. Tusubiri tutajua mengi zaidi.

===========================


Nani alilipia mamilioni ya ukumbi hoteli? Nani alilipia matangazo �live� katika televisheni? Kwa nini atake makada CCM wamsaidie? Kulikoni Mwakyembe kuonekana hotelini kabla? Iweje amkomalie Lowassana kutomgusa Magufuli? Iweje maofisa serikali wamuandalie mkutano wake? Mkutano wake wagharimu milioni 80.

Dk. Willibrod Slaa.
Siku moja tu baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, kutangaza kujing'atua katika siasa huku akiwashushia tuhuma nzito viongozi mbalimbali akiwamo waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa, maswali kadhaa yameibuka juu ya hatua ya kiongozi huyo.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe jana ulibaini kuwa mijadala mbalimbali imeibuka kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na hatua hiyo ya Dk. Slaa, huku baadhi ya viongozi aliokuwa nao katika kambi ya upinzani wakihoji maswali kadhaa yasiyo na majibu ya wazi kuhusiana na mkutano wake wa juzi kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

Mkutano wa Dk. Slaa unakadiriwa kugharimu takribani shilingi milioni 80 kulingana na takwimu zilivyokusanywa na gazeti hili hapo jana.

Katika mkutano huo aliozungumza na waandishi wa habari kwa takriban masaa mawili, Slaa alitumia muda mwingi kumshambulia Lowassa aliyeteuliwa na Chadema kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwakilisha pia vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Mwenyekiti mwenza wa Ukawa unaoundwa na Chadema, Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na National League for Democracy(NLD), James Mbatia, ni miongoni mwa watu kadhaa walioibua maswali yasiyo na majibu ya wazi kuhusiana na mkutano wa Dk. Slaa.

Akizungumzia Dk. Slaa kumhusisha Lowassa na kashfa ya Richmond, Mbatia alisema hizo ni njama za kutaka kuwaondoa katika harakati kampeni za uchaguzi mkuu na kuhoji sababu za katibu huyo wa zamani wa Chadema kujitokeza juzi na kutoa tuhuma za kashfa hiyo ya mwaka 2008, huku akiacha baadhi ya kashfa kubwa za ufisadi zilizotikisa nchi.

Alitaja baadhi ya kashfa ambazo zilitikisa nchi kuwa ni pamoja na ile ya Tegeta Escrow ambayo kesi dhidi ya wahusika zilipelekwa kwenye vyombo vya sheria, Meremeta na ile ya wizi wa mabilioni ya shilingi toka benki kuu kupitia akaunti maalumu ya madeni ya nje (EPA).

Mbatia alishangaa Dk. Slaa kutozizungumzia kabisa kashfa hizo kama kweli ana ajenda ya kupambana na ufisadi na kusisitiza kwamba kulikuwa na njama ya kuwatoa kwenye ajenda ya kampeni za uchaguzi.

"Hawa wanataka kututoa kwenye reli ili tuanze kujibizana. Hatuna haja ya kumjadili," alisema Mbatia
Akieleza kuhusu kuwania urais kupitia Ukawa, alisema Dk. Slaa ambaye alipitishwa na Chadema kushindana na wenzake kutoka Cuf (Prof. Lipumba) na Dk. Kahangwa wa NCCR-Mageuzi, alikuwa akililia urais kwa kudai kuwa yeye ndiye bora kuliko wenzake na kufanya kikao kilichomalizika usiku Juni 17 mwaka huu kuvunjika, hivyo siyo sahihi kudai kwamba hakuwahi kuutaka urais.

Kwa mujibu wa Mbatia, Lowassa baada ya kujiuzulu akiwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kama alithibitika kuwa na kesi ya kujibu, angeweza kushtakiwa kwani Waziri Mkuu anapokuwa nje ya nafasi hiyo, hana kinga ya kumzuia kushtakiwa.

Alisema Waziri Mkuu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 33, anatekeleza na kuwajibika kwa majukumu yanayotolewa na Rais.

Pia alipinga madai ya Dk. Slaa kwamba Lowassa alisema angekuja na wenyeviti wa mikoa na wa wilaya wa CCM wakati wa kuhamia Chadema kuwa si ya kweli.

Alisema Dk. Slaa pamoja na wenyeviti wenza wa Ukawa akiwamo yeye mwenyewe (Mbatia) walishiriki bega kwa bega katika mchakato wote wa kumleta Lowassa.

Alisema Lowassa hakutoa kauli hiyo kwamba angekuja na viongozi hao wa CCM, bali alipokuwa bado katika chama hicho hao walikuwa ni miongoni mwa waliokuwa wanamuunga mkono.

Mbatia alisema Dk. Slaa alikuwa akililia urais na kusema kuwa yeye ndiye bora kuliko wenzake na kufanya kikao kilichomalizika usiku Juni 17 mwaka huu kuvunjika.

Alisema Dk. Slaa ndiye aliyesema asitangazwe kuwa mgombea kupitia Ukawa Julai 14 mwaka huu mpaka baada ya siku saba ili kulifanya tukio hilo kuwa la kihistoria.

Mbatia aliwataka wananchi kuepukana na hoja hizo ambazo ni nyepesi, kwani Ukawa wanasimamia uzalendo, utu, uadilifu, umoja na uwajibikaji.

Kuhusu wito wa mdahalo kuzungumzia suala la Richmond, alisema wapo tayari lakini hawawezi kumruhusu mgombea wao Lowassa kushiriki kwani hiyo ni mbinu ya kuwataka watoke kwenye reli ya kuendelea na kampeni za uchaguzi mkuu.

"Hawa wanataka kututoa kwenye reli ili tuanze kujibizana. Hatuna haja ya kumjadili," alisema Mbatia.
Aidha wachangiaji mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii nao waliibua maswali kadhaa kuhusiana na hatua hiyo ya Dk. Slaa.

Wakati maswali kadhaa yakiibuka, jana kulikuwa na taarifa ambazo Nipashe haikuweza kuzithibitisha moja kwa moja, kuhusu kutokweka kwa Dk. Slaa, ambaye inadaiwa aliondoka nchini jana.

Hata hivyo, Nipashe lilipojaribu kumtafuta Dk. Slaa kuhusiana na habari za kukimbilia nje, simu yake jana ilikuwa ikipokelewa na mwanamke ambaye alikana kwamba hiyo siyo namba ya Mwanasiasa huyo.

MASWALI YALIYOIBULIWA
Baadhi ya maswali yaliyoibua kizungumkuti kuhusiana na mkutano wa Dk. Slaa juzi ni pamoja na mlipaji wa gharama za ukumbi wenye hadhi ya juu wa hoteli ya Serena; mlipaji wa gharama za matangazo ya moja kwa moja kwenye televisheni tatu; kauli yake ya kutaka asaidiwe na makada wa CCM - Dk. Harrison Mwakyembe na Samuel Sitta katika kujenga hoja za kudhihirisha kuwa Lowassa alihusika na Richmond.

Kadhalika, maswali mengine kuhusiana na mkutano wa juzi wa Slaa ni pamoja na swali kwamba je, bni kwa nini alimshambulia zaidi mgombea wa Ukawa, Lowassa na kisha kutomgusa hata kidogo mgombea wa CCM, John Magufuli? Na kwamba je, ni iweje maandalizi ya mkutano wake yahusishe baadhi ya maafisa wa serikali waliokuwa wakitumia simu za ofisi ya umma kuwaalika waandishi wa habari?


MBOWE AJIBU KIAINA
"Safari ya Chadema ni sawa na treni, inayoanzia Dar es Salaam kwenda Kigoma. Njiani watu wakageuka, na wakaendelea kugeuka katika vituo vingine vya njiani. Sisi tunaendelea," alisema.

"Chadema siyo mali ya Mbowe wala kiongozi yeyote. Anayefikiri yeye ni mkubwa hana nafasi... Kamati Kuu (CC) iliamua, na Mkutano Mkuu uliamua vilevile kuwa Lowassa awe mgombea wa nafasi ya urais. Kama kuna watu wana mawazo tofauti watatukuta mbele ya safari," alisema Mbowe wakati akizungumza kwenye mkutano wa kampeni mjini Sumbawanga jana
.

Chanzo: Nipashe


Siri yafichuka mkutano wa Dk. Slaa



NA ELIZABETH HOMBO, DAR ES SALAAM
SIKU moja baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, kutangaza kuachana na siasa na kushusha tuhuma kwa chama chake, maaskofu wa Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), imebainika kuwa kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari alikutana na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwamo Dk. Harison Mwakyembe.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Dk. Slaa ambaye alimshambulia mgombea urais wa Chadema chini ya mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa, alikiri kukutana kwa takribani saa mbili na Dk. Mwakyembe akisema lengo lilikuwa ni kujikumbusha taarifa ya Richmond na ndipo alipopata ujasiri wa kutamka aliyoyasema.

"Hivi kukaa kwangu na Mwakyembe kuna kosa gani? Je, ni dhambi? Watanzania sijui kwanini huwa hawataki kuelewa mambo, mimi nilionana na Mwakyembe kabla ya kuanza mkutano wangu na waandishi wa habari, na tulikaa kuanzia saa nne asubuhi hadi sita mchana.

"Katika suala la Richmond hakuna ‘source ya information' (chanzo cha habari) zaidi ya Mwakyembe na ndiyo maana nilikaa naye…nilirudia kufanya utafiti.

"Sasa anayeshangaa Dk. Slaa kuongea na Mwakyembe nadhani kwa bahati mbaya akili yake haina upeo wa kutosha, kwa sababu unapofanya ‘research' (utafiti) lazima urudi kwenye ‘source' (chanzo) ya hilo jambo na ndiyo maana nilikuwa na jeuri ya kuzungumza kwa kujiamini," alisema Dk. Slaa.


USALAMA WA TAIFA
Dk. Slaa pia alikiri kusindikizwa na usalama wa taifa akisema alifanya hivyo kwa sababu tangu amejiuzulu ukatibu mkuu wa Chadema, amekuwa akitishwa hivyo alitoa taarifa polisi kwa ajili ya kulindwa.

"Nikiwa pale mkutanoni nilihoji kama polisi wapo ili tu watu wajue kuwa pale kuna usalama, nilisema kabisa kwamba hakuna kipindi nilichopata vitisho kama hiki, kuliko hata wakati nilipotangaza ‘list of shame' pale Mwembeyanga, hivyo nilitoa taarifa polisi ili nilindwe.

"Tangu nimejiuzulu ukatibu mkuu, nyumba yangu imekuwa ikilindwa na polisi. Polisi ni maadui zetu, lakini kuna wengine ni wazuri kwa ajili ya usalama," alisema Dk. Slaa.

Kabla ya kufanyika kwa mkutano huo, baadhi ya taarifa zilizokuwa zikizagaa zilidai kuwa umeandaliwa na watu wa CCM na Serikali.
MTANZANIA ilipomuuliza Dk. Slaa kuhusu suala hilo, hakuwa na jibu la moja kwa moja.

GHARAMA ZA MKUTANO

Alipoulizwa juu ya gharama alizotumia kufanya mkutano wake kwenye Hoteli ya Serena na kuurusha moja kwa moja kwenye vituo takribani vitano vya televisheni, wakati akisema yeye ni masikini, Dk. Slaa alihoji: "Hivi kwa uzito wa hotuba ile ulidhani ningefanyia Manzese?"

Gharama za kurusha matangazo ya moja kwa moja kwenye baadhi ya televisheni nchini, zinaanzia Sh milioni 6 kwa saa na mkutano wa Dk. Slaa ulirushwa kwa takribani saa moja na nusu.

Hivyo gharama za kurusha matangazo hayo kupitia televisheni hizo achilia mbali ukumbi, redio zilizorusha moja kwa moja, luninga mbili zilizorudia matangazo hayo juzi usiku na kampuni iliyoandaa mkutano huo ni takribani Sh milioni 45.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Dk. Slaa alisema yeye si mtu mwenye uwezo na hata fedha zake huwa zinatumiwa na mke wake kukijenga chama, hivyo yeye na familia yake huishi kwa kula mihogo.

Jana MTANZANIA ilipomtaka Dk. Slaa ataje gharama ya mkutano huo na nani amegharamia, alisema: "Bado nasubiri gharama za mkutano wangu na kampuni inayofanya kazi hiyo wakiniletea nitakwambia.

"Niliamua kufanya mkutano ule kwa kuwa Taifa limegawanyika katika sehemu mbili, wengine ni wale wanaounga mkono ufisadi ambapo ndiyo wanatumia fedha kufanya jambo lolote, kundi jingine ni lile ambalo linapinga, na ndiyo maana nikawatahadharisha Watanzania wawe makini na mafisadi," alisema Dk. Slaa.

PICHA NA LIPUMBA, MWIGULU
Akizungumzia kuhusu picha zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii akiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Rais wa Ujerumani, Joachim Gauck, alisema picha hiyo ni ya tangu rais huyo alipokuja nchini.

"(Anacheka) Yaani ninawashangaa sana Watanzania…hivi watu tukimbiane? Lakini bahati mbaya picha hiyo ni ya siku nyingi, tangu rais wa Ujerumani alipokuja nchini, na siku ile Mwigulu alikuja kuiwakilisha Serikali, mimi niliwakilisha chama changu na Lipumba aliwakilisha CUF," alisema Dk. Slaa.

AMJIBU LISSU

Pamoja na mambo mengine, alimtaka Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu afanye utafiti kabla ya kuzungumza chochote na vyombo vya habari.

"Lissu amekuwa mtu wa kukurupuka…hivi alijua mimi niko wapi, kwa anachofanya anapoteza ‘credibility' yake, na mtu makini anafanya tafiti kabla ya kutoa ‘press'. Sasa aende kwenye kumbukumbu ya chama na atoe vocha yoyote iliyosainiwa halafu aniambie kuwa nilichukua mshahara wa chama," alisema.

Akizungumzia kuhusu nyumba anayoishi, Dk. Slaa alisema alichangiwa na rafiki yake ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe hivyo alimtaka Lissu aweke hadharani uthibitisho wowote kama nyumba hiyo ni ya chama.

"Hivi mtu ukichangiwa nyumba ndiyo umelipiwa na chama? Nyumba yangu nilichangiwa na rafiki yangu Mbowe, sasa Lissu aweke hadharani kama nyumba ni ya chama," alisema.



Chanzo:
Gazeti la Mtanzania
 
Tutasikia mengi sana, la muhimu tunachepuka kwenye aina fulani za siasa ambazo hatukuwa nazo katika misimu yote ya uchaguzi zilizopita.
 
Ole ni wa wdhalimu wa nchi hii ambao wanajaribu kutumia watu wanaokubalika mfano.dr Slaa kwa malengo ya kuaminisha watu kuwa tatizo la nchi hii ni reachmond.Na etichadema imepotoka.Hebu tujiulize watu waliokuwa na tuhuma za wazi za wizi si wako jela mfano.Mramba na Yona.Watu wenye tuhuma ambazo si zao peke yao si wanapeta na tena wako wengi tena maelfu si wanagombea ubunge mfano mzuri tuna Chenge.ngeleja ambao wanatuhuma za kutisha na iliwapelekea hata kupoteza nafasi zao.Huo siyo wizi ila Lowassa ndiye.Ole ni wa hao wawapotoshao wasio na uelewa wa kutosha siku zinakuja na saa ipo ambapo kicheko cha maskini kitakuwa kilio na msiba wa kutisha wa walaghai wa nchi hii.
 
Mi maswali yangu ni matatu tu makubwa kwa Dr. Slaa kama kweli ana uchungu na watanzania:-
- Anasema EL ni mchafu hafai kuwa Rais, je watanzania malofa wamchague nani? Je tuichague tena CCM?
- Baada ya Press conference yake, kwanini anawakimbia watanzania? Je amechoka kula mihogo au anakimbia kujibu hoja za upande wa pili?
- Amekuwa akihimiza watu kupiga kura, haoni aibu yeye kukimbia nchi bila kupiga kura kipindi hiki muhimu cha kuleta mabadiliko ya kisiasa nchini? Ina maanahaelewi usemi wa "kura yako moja ni muhimu sana, kapige kura"
 
hii inadhihirisha wazi upinzani hawakujiandaa kuchukua dola maana kutangaza mgombea walisuasua hadi walipompata lowassa pili hata kampeni zao ni kama za kuvizia hivi wanasubiri ccm wapite ili wao waje kujisafisha na kote wanskopita hakuna hoja ya msingi inayotolewa,,
 
hii inadhihirisha wazi upinzani hawakujiandaa kuchukua dola maana kutangaza mgombea walisuasua hadi walipompata lowassa pili hata kampeni zao ni kama za kuvizia hivi wanasubiri ccm wapite ili wao waje kujisafisha na kote wanskopita hakuna hoja ya msingi inayotolewa,,

hoja ya msingi mtaiona kwenye sanduku la kura. Mtatafutana safari ihi.
 
Back
Top Bottom