Dk Slaa ampasha IGP Mwema

JOHN MADIBA

JF-Expert Member
Jan 30, 2011
251
155
KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa amelitaka Jeshi la polisi nchini kutoingilia masuala ya vyama vya siasa kwa kuwa kufanya hivyo ni kukiuka wajibu wake.

Kadhalika Dk alisitiza kuwa Chadema wataendeleza maandamano kudai haki za raia na kwamba kamwe hawatalala na kwamba kinachoweza kuwanyamazisha ni iwapo serikali ya CCM na Polisi watatekeleza wajibu wao kwa kuondoa kero za wananchi na ikiwa ni pamoja na kuwafikisha watuhumiwa wote wa ufisadi mahakamani.

“Sisi Chadema tunalitimiza hilo kwa vitendo na kamwe hatutalala na wala hatuogopi polisi, tutaendelea kutimiza wajibu wetu, kama serikali ya CCM na Jeshi la Polisi wanataka Slaa anyamaze, watekeleze wajibu wao kwa kuondoa kero za wananchi na kuwafikisha watuhumiwa wote wa ufisadi mahakamani,”alisema.

Dk Slaa ambaye alikuwa akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kisarawe Mkoani Pwani, alisema kazi ya polisi si kutisha na kuzuia kazi ya vyama vya siasa bali ni kulinda raia na mali zake.

"Polisi na usalama wa Taifa mpo nataka mumpelekee taarifa IGP Mwema kuwa kazi ya polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao, hawa ni watumishi wa wananchi na si mabosi wao, siyo hizi za kujiingiza kwenye masuala ya kisiasa na kusahau majukumu yenu,”alisema Slaa na kuongeza

“Mwambieni Mwema kama hawezi avue magwanda apande majukwaani ili tupambane kwa hoja, vitisho mnavyovifanya mtawafanyia hao wasiojua haki zao lakini sio mimi Dk Slaa ambaye nazijua sheria na haki zangu za msingi,"alisema.

Alisema kuzuia shughuli za vyama vya siasa kwa kisingizio cha kuhatarisha amani na utulivu si kwamba ni kinyume na katiba tu bali pia ni ukandamizaji wa maksudi wa demokrasia.

Maandamano na mikutano
Slaa katika mkutano huo alitetea maandamano na mikutano inayofanywa na chama chake kuwa siyo chanzo cha kutoweka kwa amani hapa nchini, bali Chadema wanatimiza wajibu wao wa kikatiba na kwamba “amani inalindwa na haki dhidi ya wananchi wote”.

“Polisi mpo,….. naomba mpige picha na mnakili hili vizuri na kumfikishia IGP Mwema; ghasia katika nchi yoyote haitokani na maandamano bali inatokana na kukiukwa kwa haki, kama wananchi hawapati haki zao za msingi hiyo siyo amani na utulivu tunayoihubiri,”alisema Slaa.

Slaa alitetea maandamano na mikutano inayofanywa na chama chake inalenga kuamsha uelewa wa wananchi na kusisitiza kuwa kwa kufanya hivyo, Chadema wanatimiza wajibu wa msingi kama chama cha siasa kwa mjibu wa katiba.

“Naomba niwaambie Polisi, kazi ya chama cha upinzani si kupigia makofi serikali iliyoko madarakani, bali ni kuikosoa na kuwaleleza wananchi juu ya kushindwa kwake kutatua kero za wananchi ili unapofika uchaguzi wananchi kwa pamoja wachukue hatua kwa kukiondosha madarakani kwa njia ya kura,”alisema Slaa.
Upotevu wa fedha
Katika mkutano huo Slaa alidai kuwa tangu Tanzania ipate uhuru 1961 hadi June 30 mwaka jana, ilikuwa imepoteza Sh 1.3 trilioni sawa na asilimi 10 ya pato la Taifa kwa matumizi yasiyofahamika.

Alisema fedha hizo ambazo zimeishia mikononi mwa watu wachache zingeweza kujenga barabara za lami kilomita 500.

"Tulipoanza kuzungumza kuhusu EPA (Fedha za kulipa madeni ya nje), Kikwete (Rais Jakaya) alisema kelele za akina Slaa hazininyimi usingizi lakini leo hii halali usingizi kwasababu ya EPA,"alisema Slaa.

Alisema Chadema kitaendelea kupiga kelele hadi watuhumiwa wote wa mali za umma watakapokamatwa na kufilisiwa kwa fedha zao kurejeshwa ili zitumike kujenga shule na Zahanati kwa ajili ya Watanzania.

Kauli ya Mpendazoe
Naye kada maarufu wa Chadema, Fred Mpendazoe aliwataka wakazi wa Kisarawe kubadilika na kukihama CCM kwa maelezo kwamba chama hicho kimetengeneza matabaka ya masikini na majiri.

Alisema wakati wa utawala wa Rais wa kwanza, Hayati Julius Nyerere, CCM ilisimamia haki kwa wote, matajiri na maskini hivyo kujenga heshima ya Watanzania ndani na nje ya nchi.

“Wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere maadili ya uongozi yalizingatiwa, mtu aliyetaka kugombea aliulizwa fedha amezipata wapi, lakini leo uongozi ndani ya CCM ni biashara na mtu akitaka kugombea nafasi yoyote anaulizwa una shilingi ngapi?”alisema Mpendazoe.

Alisema viongozi wa aina hiyo hawawezi kuhoji sababu za umasikini wa wananchi na badala yake wanawaza jinsi ya kurejesha fedha walizotumia kwenye kampeni.
 
Back
Top Bottom