Dhana 10 potofu kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar - sehemu ya kwanza

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,531
Na Mwandishi maalum

KUNA tishio kubwa dhidi ya Muungano wetu. Tishio hilo liko zaidi kwenye dhana kuliko udhaifu wa dhamira ya Muungano wenyewe. Tishio hilo limedhihirika katika kipindi hiki cha mchakato wa kuandaa Katiba Mpya ya nchi yetu.


Mjadala wa rasimu ya Katiba mpya umetawaliwa kwa kiasi kikubwa na ajenda ya Muungano. Yamejitokeza makundi yenye mitazamo tofauti juu ya Muungano. Wako wanaoutaka uendelee, wako wasioutaka, wako wanaotaka urekebishwe, ilihali kuna kugongana kifikra. Kinachowaunganisha wote ni mjadala wa Muungano huo huo.


Mgongano wa maoni juu ya Muungano ni jambo jema na la kujivunia. Mgongano huu unadhihirisha jinsi ambavyo Muungano uko hai maana Muungano usiokuwa hai haujadiliwi. Mgongano huu wa fikra umetufunulia kile ambacho hatukuwa tukikijua au tukikipuuza.Mara zote tumekuwa tukiamini kuwa ni Wazanzibari pekee wenye ulalamishi juu ya Muungano, lakini mjadala unavyokwenda tumeona pia kwamba hata wabara nao wana malalamiko yao. Hivyo, ni sahihi kusema kuwa mjadala wa Muungano na mgongano wa fikra juu ya Muungano wenyewe vinatupa fursa ya kuuboresha Muungano kuliko kuuvunja.


Sio sahihi kuogopa watu kuujadili Muungano wao, wala hatuwezi kuujenga Muungano wenyewe kwa kuukinga dhidi ya mjadala. Ikiwa sababu na dhamira ya kuungana ni njema, busara ile ile iliyochochea kuungana itaendelea kutawala na hatimaye kushinda jaribio lolote la kuuvunja. Muungano wa hila ndio Muungano pekee ambao unapaswa kukingwa dhidi ya mjadala na kuhojiwa. Muungano wetu sio Muungano wa hila, hivyo unapaswa kujadiliwa na kuhojiwa. Wananchi wanayo haki ya kuutathmini ikiwa umetimiza malengo na matarajio yao, maana tatizo laweza kuwa ni kubadilika kwa matarajio ya wananchi kuliko kufeli kwa Muungano wenyewe.
Tatizo tulilo nalo ni kuwa wenye dhamana ya kurithisha Muungano huu kwa vizazi vilivyofuatia wanagwaya kufanya hivyo. Kugwaya kwao, kwa maoni yangu hakutokani na Muungano wenyewe kuwa wa hila, bali udhaifu wa viongozi hao katika kuuelezea na kujenga hoja. Kuusimamia ukweli daima huhitaji ujasiri, wakati mwingine, ujasiri pekee hautoshi, ujasiri huo hutakiwa kuambatana na uadilifu. Maadam baadhi ya viongozi wetu wamekengeuka kimaadili, wanakosa ujasiri wa kusema na kuusimamia ukweli wanaouamini. Huusema ukweli huu pembeni tu lakini sio mbele ya jamii. Upungufu huu hufanya kusiwepo na watetezi wa Muungano mbele ya jamii.


Silaumu hata kidogo wale wanaohoji Muungano wetu hasa muundo na umuhimu wake leo. Ukiwasikiliza wanazo hoja, tena hoja nzuri na za kimantiki. Hili linadhihirisha kuwa hawana tatizo la uelewa, na wakipatiwa hoja mbadala wanaweza kuelewa. Wengi wa hawa hawana taarifa za kutosha juu ya Muungano wenyewe, hivyo wanauhoji kwa taarifa chache za kuokoteza. Nimewahi kuwa mwathirika wa hilo hadi nilipofanikiwa kudadisi na kupata taarifa zaidi kwa njia ya mapokeo, kwa kuwa nyingi ya taarifa hizi hazijahifadhiwa kwenye maandiko. Haiyumkini, hali hii inatokana na utamaduni wetu wa kutokuandika historia na matukio.


Kutokana na pengo la taarifa juu ya Muungano, kumeibuka dhana mbalimbali nyingi zikiwa potofu. Uwepo wa dhana potofu ni kielelezo cha ombwe, na kawaida, ombwe huvutia ghasia na mwangwi. Katika mwangwi huo, dhana potofu hupata uhalali na huweza kuzaa nadharia. Katika mjadala unaoendelea kuhusu Muungano hivi sasa, zipo walau dhana 10 potofu ambazo zimetamalaki maoni ya wengi kuhusu Muungano. Dhana hizi potofu zinaainishwa na kuchambuliwa katika aya zinazofutia.


I. Tatizo muundo, suluhisho serikali tatu
Imejengeka dhana kwa muda mrefu kwamba tatizo la Muungano wetu ni muundo wake wa serikali mbili. Dhana hii inatuaminisha kuwa mwarobaini wa tatizo hilo ni serikali moja au tatu. Ajabu zaidi, serikali moja haipigiwi sana upatu kama serikali tatu.Hapa tatizo linasemekana ni Tanzania Bara kukosa serikali yake. Wengine huenda mbele na kusema kitendo cha Serikali ya Muungano kuwa ni hiyo hiyo inayoshughulikia masuala ya Tanganyika, kunaifanya Tanganyika kutumia rasilimali za Muungano kujinufaisha.


Aidha, upande mwingine unasema, Serikali ya Muungano kuwa ndio hiyo hiyo ya Tanganyika inayoifaidisha Zanzibar kwa mapato yatokanayo na uzalishaji ndani ya Tanganyika. Hivyo, serikali tatu zitasaidia kutenganisha shughuli za Muungano na shughuli za Tanganyika na Zanzibar, hivyo, kuepusha kupunjana. Ni wazi, kila upande una shaka juu ya upande mwingine. Hivyo, msingi wa kutaka serikali tatu unatokana na kutokuaminiana. Kutokuaminiana huku hakutatuliwi kwa kuongeza idadi ya serikali.


Hoja ya Serikali tatu sio mpya, ilikuwapo mezani wakati waasisi wa Muungano walipokubaliana kuwa na serikali mbili badala ya tatu au moja. Busara ya waasisi ilitawala katika kutafuta msawazo kati ya gharama za uendeshaji wa Serikali ya Muungano na utaifa wa Mzanzibari. Muundo wa serikali tatu ulionekana ungekuwa wa gharama kubwa hasa kwa Serikali ya Tanganyika ambayo ndio ingelazimika kubeba gharama kubwa. Hali kadhalika, serikali moja ilihofiwa ingeufuta utaifa wa Mzanzibari kwa kuzingatia udogo wa kisiwa chenyewe ikilinganishwa na Tanganyika na idadi ndogo ya watu ambayo wakati huo ilikuwa inakadiriwa kuwa laki tatu. Utaifa wa Mtanganyika na utamaduni wake usingeweza kutishiwa kumezwa na Uzanzibari.


Maumbile ya Tanganyika na Zanzibar hayajabadilika kwa miaka 49 kiasi cha kuifanya hoja ya serikali tatu kuwa na nguvu sasa. Tanganyika ina kilometa za mraba 942,553 na Zanzibar ina kilometa za mraba 2650 (Eneo la Zanzibar linaingia mara 355 katika eneo la Tanganyika). Tangayika na Zanzibar kwa pamoja zina jumla ya kilometa za mraba 945,203.
Tanganyika ina idadi ya watu milioni 43,625,354 na Zanzibar ina watu 1,303,569 kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya 2012. Tanganyika ina kaya milioni 9,109,150 na Zanzibar 253,608. Ujazo wa idadi ya watu Zanzibar ni watu 530 kwa kilometa moja ya mraba wakati Tanganyika ni watu 49 kwa kilometa ya mraba. Takwimu hizi zingali zinahalalisha hoja ya serikali mbili ya Waasisi wa Muungano.



Tukienda na maelezo aliyotoa Jaji Warioba kuwa gharama za kuendesha mambo saba ya Muungano yanayopendekezwa katika mfumo wa serikali ya tatu ni trilioni tatu, hoja ya serikali mbili inaimarika. Tukiwa na serikali tatu, mantiki itataka nchi washirika wa Muungano waongeze michango ya gharama za uendeshaji wa serikali hiyo ya tatu.


Aidha, kutokana na ukweli kuwa serikali ya tatu inazaliwa katika mazingira ya kutoaminiana, hisia mbaya na dhamira ovu, utayari wa kila upande kuchangia gharama utabeba hulka hizo hizo. Bajeti ya Tanzania kwa mwaka wa fedha 2013/2014 ni shilingi trilioni 18.2 na bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa 2013/2014 ni shilingi bilioni 658.5. Ikiwa tutaondoa masuala ya Muungano, bajeti ya Tanganyika itakuwa ni Sh trilioni 15.2. Ndani ya mfumo wa serikali mbili, kuna unafuu mkubwa wa gharama kwa kuwa gharama za kiuendeshaji zinapungua kwa sababu Serikali ya Muungano kwa kutumia nguvu kazi na vitendea kazi hivyo hivyo inatekeleza pia shughuli za Tanganyika.

Inaendelea


Mwandishi Maalum
Rai Mwema
Toleo la 310
 
Back
Top Bottom