Dar, Zanzibar: Hofu Maiti 15 zikikutwa kwenye viroba

Ghazwat

JF-Expert Member
Oct 4, 2015
23,718
66,262
Wavuvi na wafanyabiashara katika masoko na minada ya samaki ya Kunduchi, Ununio na Feri jijini Dar es salaam wanaishi kwa hofu baada ya kuwepo kwa taarifa za kuopolewa miili 15 ya watu baharini ikiwa imewekwa katika mifuko maalumu kama viroba, Bara na Zanzibar.

Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika kilichozungumza na Nipashe, miili hiyo iliokotwa kwa nyakati tofauti na wavuvi ambao waliwajulisha polisi, waliofika kuichukua.

Kuwepo kwa idadi kubwa ya miili inayoopolewa kutoka baharini au kukutwa fukweni ikiwa imefungwa kama mzigo kumefanya wavuvi na wafanyabiashara wa samaki kuingiwa na hofu ya kuja kutakiwa kuisaidia polisi katika uchunguzi wa mauaji hayo, pindi wanapogundua na kutoa taarifa za maiti hizo.

Hofu hiyo imesababisha baadhi ya wavuvi kunyamaza wanapoona miili zaidi ikielea baharini.

"Polisi tunawajulisha, wanakuja, wanabeba maiti, lakini hakuna siku wametueleza ni za kina nani"alisema mvuvi mmoja wa Kunduchi aliyezungumza na Nipashe kwa sharti la kutotajwa jina gazetini akihofia usalama wake.

"Wavuvi tunafahamiana na ikitokea mwenzetu amekufa au chombo kimezama majini tunafahamu.

"Lakini tangu Agosti mwanzoni tunaokota miili ikiwa imeandaliwa (imefungwa) kabisa na siyo ya wenzetu".

Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Lucas Mkondya, aliiambia Nipashe kwa njia ya simu jana kuwa miili iliyookotwa ni mitatu na haikuwa kwenye viroba.

"Hadi sasa taarifa za miili mingi kama hiyo kuokotwa nazisikia kwako", alisema Kamanda Mkondya. "Hao watu watueleze nasi tutachukua hatua, hatuna taarifa za miili iliyofungwa kwenye viroba au sandarusi.

"Miili mitatu iliyookotwa Kunduchi iko Hospitali ya Taifa ya Muhimbili MNH na haijatambuliwa, wananchi wafike kuitambua".

Lakini wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti kwenye maeneo ya uvuvi hayo jana, wavuvi walisema wamepokea taarifa kutoka wenzao wa eneo la Kizimbani, Zanzibar, kwamba huko pia zimeokotwa maiti tano.

Mvuvi mmoja wa Kunduchi alisema siku mbili zilizopita ziliokotwa maiti tano katika eneo Bongoyo na nne nyuma ya kisiwa cha Mbudya, jijini Dar es salaam.

Alisema kati ya maiti tisa hizo, moja ilikuwa ya mwanamke na kwamba zilikuwa zimefungwa kamba mguuni, kichwani na tumboni.

"Zote zilikuwa zimeharibika na sura hazitambuliki", alisema na zinachukuliwa na polisi baada ya kutaarifiwa.

Alisema polisi waliochukua miili hiyo ni wa mkoa wa Kinondoni kutoka vituo vya Kawe ambayo ni wilaya ya kipolisi na Wazo Hill.

"Hawajawahi kusema mtu huyo alifia wapi na chanzo cha kifo, (hivyo) wengi tuna wasiwasi tu", alisema mvuvi mwingine ambaye pia jina lake lihifadhiwe.

"Ukiangalia umri ni miaka 25 hadi 50.

"Jamaa zetu wa Feri waliokota maiti sita wiki mbili zilizopita na kati ya mbili zimefungwa pamoja na katika hizo moja ni mwanamke.

"Tulichozoea wavuvi ni kuokota maiti za wavuvi wenzetu ambao wanazama au kupotea, na zinakuwa na nguo zake za kawaida, lakini hizi ni za kuandaliwa".


Chanzo: Nipashe
 
Hao itakuwa ni wakosoaji wa silikari yetu....
Tuwe makini huyu bwana anakotupeleka sio..
Kma kipindi cha nyerere hii ilotokeaga and ilikuwa ni big issue..
Lkn sikuhz eti ni kawaida tu kuskia mambo kma hayo
 
Back
Top Bottom