CHADEMA Ianzishe mabadiliko ya Ndani, Vinginevyo kuiondoa CCM 2015 ni ndoto - Sehemu ya 1

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,478
40,000
chadema%2Bfurahisha.12.JPG

Na M. M. Mwanakijiji

Kama kuna vitu vya kusikitisha na wakati mwingine kukatisha tamaa ni mgongano ambao umekuwa ukifukuta kwa muda ndani ya CHADEMA kiasi cha kuwa kama doa chafu ambalo halipaswi kuvumilika. Mambo ambayo yametokea Arusha, Mwanza, Mbeya na sasa BAVICHA yanaashiria kuwa kama CHADEMA haitaamua kujiangalia ndani na kuanzisha mabadiliko ya mfumo na muundo wake basi kuiangusha CCM na kuiondoa madarakani mwaka 2015 itakuwa ni ndoto ya kutamania tu lakini kamwe haitatokea.

Migongano hii ambayo imeishia katika watu kutimuana na kutuhumiana imesababisa watu kuzungumzia migogoro ndani ya chama kuliko maono yake kwa taifa. Wiki hizi chache zilizopita zimesababisha mazungumzo mengi ndani ya CHADEMA na nje yake yawe ni kuhusiana na kundi la vijana ambao walituhumiwa kuendesha uasi ndani ya chama kuliko kuzungumzia mipango ya CHADEMA kushika dola. Tumeshuhudia kwa masikitiko makubwa wale wanaoitwa wapiganaji wakitumia muda mwingi kupigana wenyewe kwa wenyewe na sisi ambao tuko kwenye mitandao ya kijamii tumeshuhudia siyo tu kurushiana risasi bali mishale, visu, misumari, mawe na ndoana! Inaudhi, inasikitisha na inaacha maswali mengi kweli.


Tushukuru Mungu CHADEMA haikushinda uchaguzi mkuu wa 2010?

Jinsi ambavyo migogoro na milumbano ya chini kwa chini kati ya viongozi wa CHADEMA ambayo yamefikia mahali pa kulipuana kumenifanya nibakie na swali ambalo limenikaa kichwani kwa wiki sasa; je wale waliounga mkono CHADEMA washukuru Mungu kuwa haikushinda uchaguzi mkuu? Swali hili linakuja kwa sababu najiuliza kama CHADEMA wangeshinda mwaka 2010 wangeunda serikali ya namna gani? Je wangeweza kuaminiana?

Je wangeweza kuunda serikali ya namna gani? Je siyo kwamba wao kwa wao wangeanza kuhujumiana na kurushiana vijembe? Kwa wale ambao tulikuwa tunafuatilia siasa za ndani ya CCM hasa baada ya kujiuzulu kwa Lowassa Februari 2008 tunakumbuka jinsi ndani ya CCM kulivyozuka malumbano ya wao kwa wao, kunyemeleana, kuchimbana na hata – tukiamini maneno ya Rais Kikwete Butiama – ilifika mahali wao kwa wao CCM wanaogopa kuachiana glasi za maji mezani kwa kuhofia kutiliana sumu. Je hili ndilo ambalo nalo lingetokea ndani ya CHADEMA? Leo hii tunaona kuwa CCM chama chenye mifumo ya zamani na ambacho kina nyenzo nyingi za kushughulikia uasi imeshindwa kufanya hivyo je CHADEMA ingeweza?

Tumeshuhudia pamoja na majigambo yote ya "kujivua gamba" CCM imeshindwa kujisafisha na badala yake wameamua kuvumiliana, kubebana na kulindana huku wale waliokuwa ni watuhumiwa vitendo vya ufisadi wakijipanga vizuri zaidi kuweza kuendesha kampeni ya kufa mtu kuugombea urais. Sasa kama CCM pamoja na watu wake wote mashuhuri ambao walijipambanua kuwa ni wapinga ufisadi leo si wameshindwa? Wameshindwa si kwa sababu hawakuwa na nia bali kwa sababu mgawanyo ulioko ndani yake ni zaidi ya maslahi; ni mgongano wa binafsi (personal conflict) na hauaisha na naweza kusema hautaisha hadi ama Lowassa awe Rais mwaka 2015 au akataliwe. Na akiwa Rais nina uhakika wa kutosha tu kuwa mpasuko wa CCM utakuwa ni kamili!

Sasa leo CHADEMA ambao wanatarajiwa kuwa ndio wenye kuleta nuru mpya ya uongozi inapofika mahali wanachubuana wenyewe, hakuna nidhamu na kushindana kila siku kama wangeweza kuuchukua Urais kweli nchi ingekuwa salama? Je, kama mgongano huu ukiendelea kuvumliwa na kudharauliwa huku viongozi wakuu wa chama wakifunika vichwa vyao kama mbuni wakidai ati hakuna ‘mgongano' ni ‘demokrasia' kweli CHADEMA itaweza kupambana na CCM na kushinda uchaguzi mkuu? Kama leo kina Maige wananukuliwa wakimchimba vijembe Katibu wao wa Uenezi Nape si tunaweza kukuta hay ohayo yanatokea ndani ya CHADEMA kama ingeunda serikali ambapo baadhi ya wabunge wake au viongozi wake wangeanza kuirushia vijembe serikali yao au viongozi wao?


Mfumo wa CHADEMA wa sasa unalea mno uzembe na viongozi wanaosumbua!

Wengi wetu tumekuwa tukilalamika sana jinsi serikali ya CCM chini ya Rais Kikwete ilivyojenga mfumo wa kubebana, kulindana na kuvumiliana kiasi kwamba hadi mtu afukuzwe kazi au aondolewe kwenye naffasi yake basi ni lazima awe amevurunda mno – awe ameboronga. Na hata akiboronga bado kuna muda mrefu sana wa mtu huyo kupewa nafasi nyingine sehemu fulani. Mfumo huu wa CCM ndio uliozaa ufisadi na matokeo yake kwa taifa ni maangamizi.

Sasa mfumo kama huo huo ukiangalia kwa karibu unaona ukifanya kazi ndani ya CHADEMA. Ni mfumo wa kuvumiliana, kusubiriana na kutegeana. Ni mfumo ambao kwenye serikali ya CCM utasikia wanasema "mwenye ushahidi alete" wakati kwa CHADEMA ni mfumo "kutafuta ushahidi zaidi". Matokeo ya mifumo yote miwili ni kuwa serikali inalea viongozi wabovu, wabinafsi na hatari kwa taifa na CHADEMA inajikuta inavumilia viongozi wabovu, wabinafsi na hatari kwa maslahi ya chama. Matokeo yake ni kuwa CHADEMA itajikuta na yenyewe inazaa serikali dhaifu!


CDM ibadilike sasa vinginevyo ijiandae kuwa msindikizaji

Sasa ninachokisema hapa ni kuwa uongozi wa CHADEMA usijifanye wao Mbuni; wanafichwa kichwa mchangani. Tatizo la CCM ambalo limechelewesha chama hicho kujisafisha na kuweza kubadilika ni imani kuwa kinapendwa. Na kweli wapo watu wanaoipenda CCM kama mtoto anavyompenda mzazi wake. Wapo ambao wameapa kabisa kuwa liwalo na liwe wao na CCM milele. Mapenzi ya namna hii hayajali ubovu, mapenzi ya namna hii hayajali CCM inatawalaje au inaongoza vipi. NI mapenzi ambayo ‘hayaoni wala hayasikii'. Ni sawa na mapenzi ya wapendanao wawili ambapo licha ya mausia ya watu kuwa mmoja wao ni jambazi au ni kahaba wapenzi hao hawataki kusikia maneno hayo kwani wanaona ni ya watu wenye wivu, ambao hawataki mapenzi yao yafane. Hadi siku moja mmoja auawe kwenye matendo yake machafu ndio watu wanaanza kushangaa ‘mbona sikujua'!


Mabadiliko ya msingi ya CDM ni lazima yaanzie kwenye Katiba yake

Binafsi naamini kuwa mojawapo ya mambo yaliyochangia kwa kiasi kikubwa kwa CHADEMA kushindwa kwenda Ikulu mwaka 2010 ni Katiba yake ambayo imenakili kwa kiasi kikubwa mfumo ule ule wa CCM – yaani Chama kimejengwa kutoka makao makuu na kinaongozwa kutoka juu. Ni mfumo mbaya kwa sababu unategemea maamuzi ya juu kuweza kugusa uongozi wa chini kabisa na katika demokrasia mfumo huu ambao umetengenezwa kutoka juu kwenda chini ni mfumo mbaya. CHADEMA inajikuta inalazimika kujibu na kushughulikia mambo yanayotokea chini kutoka makao makuu.

Ipo mifano mingi ya kkuweza kuonesha hili likifanyika lakini miwili inatosha kuitaja hapa. Baada ya baadhi ya viongozi wa CHADEMA Karatu kuangaza kugongana ilimlazimu Mwenyekiti wa Taifa Mbowe kwenda Karatu na kujaribu kupatanisha pande mbili na kujaribu kkutafuta suluhisho. Na tumeambiwa suluhisho limepatikana. Jingine na suala la BAVICHA ambapo baadhi ya vijana wamejikuta wakitumuliwa toka BAVICHA na CDM kutokana na lundo la tuhuma dhidi yao. Uamuzi huo umechukuliwa na BAVICHA Taifa. Sasa baadhi ya watu wanaweza kuona ni jambo zuri lakini kwangu linathibitisha tu ubovu wa mfumo huo – huwezi kutatua kila kitu toka makao makuu! Ni lazima Chama kiwe na mifumo inayoweza kushughulikia matatizo ya chini au ya ngazi fulani na yakaishia huko huko bila kulazimika kwenda makao makuu.

Ili kuweza kuleta mabadiliko ambayo yataisaidia CHADEMA kujipanga naamini mabadiliko ya harakaya Katiba ya CHADEMA yanahitajika. Kama nilivyowahi kuandika nyuma kuhusu CCM kuwa ilihitaji Mkutano Mkuu Maalum wa Chama ili kijisafisha – hawakufanya hivyo – naamini CHADEMA nayo inahitaji Mkutano wake Mkuu (Baraza Kuu) kuweza kukaa chini na kupitisha mabadiliko ya msingi ya Katiba ili kuweza kukipanga chama. Mabadiliko hayo ni lazima –kwa maoni yangu – iweke mambo yafuatayo (pamoja na mengine mengi).


  • a. Viongozi wa juu wa Chama wa Kitaifa wasiwe wabunge – Wabunge wawe wabunge wasishike nafasi za uongozi makao makuu ya chama – hili nimuhimu kwa ajili ya kuweza kusimamiana (checks and balances).
  • b. Viongozi wa kitaifa wanaotaka kugombea nafasi yoyote ya kuchaguliwa (ubunge, udiwani au Urais) ni lazima waachie madaraka (wajiuzulu) nafasi zao mara wanapotangaza nia ya kugombea nafasi hizo. Hii itazuia viongozi wa kitaifa kutumia raslimali za chama kusaidia kampeni zao au za watu wao wa karibu.
  • c. Mgawanyo wa fedha za ruzuku uongozwe na kanuni zilizowekwa kikatiba ambapo kiasi kikubwa cha fedha kinaenda mikoani na ngazi zachini kujenga chama badala ya kutumika makao makuu. Makao makuu ipewe uwezo wa kubuni na kuendesha miradi ya chama kukipatia kipato.
  • d. CHADEMA irudishe chama kwenye majimbo kuonesha kuwa kinaamini kweli sera ya majimbo. CHADEMA imekuwa ikiuza sera kuwa wakishika madaraka wataongoza nchi wa kuweka madaraka katika majimbo zaidi. Sasa kama hili kweli wanaamini ni jambo zuri basi waanze nalo kwenye chama. Kwanini chama kiko too centralized? Naamini CHADEMA kitoe madaraka makubwa kwa chama mikoani au kwa kuunganisha mikoa na hivyo kuwa na makao makuu ya chama ya Kanda ambayo yatashughulikia shughuli zote za chama katika ngazi hizo. Kama majimbo ni mazuri kwa uendeshaji wa serikali bila shaka ni mazuri kwa uendeshaji wa chama! Hii pia itasaidia kuondoa watu wanaotaka kwenda kufanya kazi makao makuu ya taifa! Wengine waende kwenye kanda huko!
  • e. Mfumo wa nidhamu ubadilishwe ili masuala ya nidhamu yashughulikiwe katika mfumo mmoja, unaoeleweka na ambao unafanya kazi kwa haraka, kwa uwazi, na kwa uhuru. Mfumo unaosubiri miaka au miezi kushughulikia migongano kwenye majimbo au ngazi fulani ni mfumo mbaya. Ni muhimu mfumo uwepo ambao mara tatizo linapojitokeza linashughulikiwa mara moja na kumalizwa siyo kuachwa kiporo wiki baada ya wiki miezi baada ya miezi na hata inakuwa miaka baada ya miaka. Huo ni mfumo mbaya.
  • f. Kurasimisha M4C kama taasisi ya chama. Sasa hivi M4C sijui ni kitu gani ndani ya chama. Niliandika hili wiki chache zilizopita kuwa mojawapo ya matatizo mengine ni hili la M4C kutokuwekwa katika utaratibu unaoleweka ambao utaondoa hisia ya kuwa M4C inaendesha na makao makuu tu na itaweka utaratibu wa wazi kwa wanachama na mashabiki wa michango inayopatikana na inavyotumika. M4C ni lazima iwekwe kama taasisiya chama, uongozi wake utambulishwe rasmi ukiwa unajulikana majukumu yake na mipaka yake. Isije CHADEMA ikajikuta imetengeneza chama ndani ya chama

CHADEMA ikiamua kujipanga vizuri na kufanya maamuzi ya haraka, thabiti na kuharakisha maamuzi hayo – yakiwemo ya mabadiliko ya Katiba inaweza kujipa nafasi ya kushinda uchaguzi mkuu ujao. Sasa hivi baada ya kuupoteza mwaka 2012 sioni ni jinsi gani bila mabadiliko ya ndani ya chama tena makini, ya makusudi nay a haraka CHADEMA itaweza kushinda uchaguzi mkuu ujao. Na hili ni la kwanza hatujagusa suala la mabadiliko ya sera na maono.

Heri na fanaka za mwaka mpya mpendwa mzalendo


Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com
 
Umeandika uzi mrefu sana sijaumaliza wote maana sijaona umuhimu, ukiona changamoto ndani ya chama ujue chama kimekomaa we ulitaka CHADEMA wote wawe wasafi? Na ndio maana CHADEMA tuna katiba hiyo nikwaajiri ya muongozo na hakuna alie juu ya katiba ukitoka nje ya mstar usidhani utavumiliwa bila nidhamu hakuna jeshi lenye nguvu CHADEMA bana ni kama maji utayatumia tu, imeshakita mizizi nch nzima ziara za Dr hata Nyerere hajawahi kufika japo nusu yake.

Makamanda komaeni kwani ukaribiapo kufika wakatisha tamaa huongezeka jiulize chama kinachoongoza kujadiliwa mitandaoni na ndani ya jamii ni kipi? CHADEMA viva maoparetar anaecheza nje ya chaki tupilieni mbali maana kunavyama vilivyo jiandaa kupokea wafukuzwa kwani hawana jinsi.
 
Umesema kweli Mwanakijiji, inabidi CHADEMA wajipange na kufikiria kama leo hii wakikabidhiwa serikali watafanya nini, laa sivyo hata waki weza kuiangusha CCM 2015 wanaweza kushindwa pa kuanzia kwa sababu nguvu nyingi inatumika ku deal na migogoro isiyokwisha na ambayo haitaisha..
 
Manyi

Kwa mtazamo wangu wa siasa za Tanzania, uadui kati ya vyama ni mwingi sana na hasa pale kunakuwa na mambo yanayojifisha nyuma kama baadhi ya watu kutuhumiwa, kuhongwa ili watumikie chama kingine kwa usiri mkubwa sasa. Watanzania wengi elimu yetu ni ndogo sana ndiyo maana mtu anaweza kuangalia yale ya leo na kesho tu na akasahau kuwa na mtazamo wa zaidi ya hapo. Panapofika mahala hapa uongozi madhubuti unahitajika kutoka juu.

Kama ulivyosema mabadiliko ni ya lazima lakini ni wakati gani? Je, ni pale umejiimarisha na kueleweka vyema kwa watanzania? je CDM wamefikia hapo au la? Kwa maoni yangu msukumo wa mabadiliko ya msingi katika vyama utaanza pale serikali (Ofisi ya msajili wa vyama) itafanyiwa mabadiliko na kuwa taasisi huru ikiratibu shughuli za vyama (kuweka values and norms kwa mahitaji ya maendeleo ya Watanzania). Hili la Ofisi ya Msajili wa vyama ni muhimu sana na ndilo la kwanza kwa ajili ya maendeleo ya shughuli za kisiasa na kiuchumi nchini.
 
Last edited by a moderator:
Uzi huu umetulia na una point nzuri sana. Inahitajika hekima na utulivu. Mkjj asante kwa uzalendo Mungu wa mbinguni akukumbuke.
 
Bravo Mwanakijiji,

Nazani wamekusoma, ni ushauri mzuri sana.kama kweli cdm ina nia ya dhati kuleta ukombozi wa pili kwa injii hii. Basi huu ushauri waufanyie kazi kadri iwezekanavyo.

Kama mnapita mitaani nawambiieni wanainji wameanza kukatishwa tamaa kidogokidogo na mwenendo wenu cdm, kulikuwa kama na kanuru fulani kanakuja kupitia cdm ila watu wanaona ghafla kanaanza kutoweka.

Mfano watu kama shibuda na wengineo etc mmewalea wenyewe kama chama kwa muda mrefu na wkt vitendo vyao vya kudhoofisha chama viko wazi kabisa, haiingii akilini mtu umo dani ya nyumba yako mwenyewe halafu unamwaga petroli kwenye moto., mara CHADEMA cha wachaga, mara ukanda, mara udini, mara .....

Mpigeni chini bwanaaaa........
 
Ni mawazo mazuri sana naamini viongozi na wanachama wa chadema wanapita haya maeneo ni vizuri wakafata ushauri huu.. Binafsi nimekuelewa sana.
 
Ushauri mzuri sana hasa unapoongelea piramid na siku zote wakati ukiamini katika mfumo huu unahitaji maamuzi mengi yaanzie chini kuja juu na siyo juu kuja chini. Hii inanikumbusha hata kwenye sakata la madiwani wa Arusha Dr. Slaa kama katibu mkuu wa chama ndiye akiyekuwa akiratibu na kuongoza vikao vya kupendekeza madiwani wale wafukuzwe uanachama. Hapa unajiuliza kama Katibu mkuu anaratibu na kusimamia huku chini hawa wanachama watapata wapi haki hata ya rufaa yao?
 
  • a. Viongozi wa juu wa Chama wa Kitaifa wasiwe wabunge – Wabunge wawe wabunge wasishike nafasi za uongozi makao makuu ya chama – hili nimuhimu kwa ajili ya kuweza kusimamiana (checks and balances).
  • b. Viongozi wa kitaifa wanaotaka kugombea nafasi yoyote ya kuchaguliwa (ubunge, udiwani au Urais) ni lazima waachie madaraka (wajiuzulu) nafasi zao mara wanapotangaza nia ya kugombea nafasi hizo. Hii itazuia viongozi wa kitaifa kutumia raslimali za chama kusaidia kampeni zao au za watu wao wa karibu.
  • c. Mgawanyo wa fedha za ruzuku uongozwe na kanuni zilizowekwa kikatiba ambapo kiasi kikubwa cha fedha kinaenda mikoani na ngazi zachini kujenga chama badala ya kutumika makao makuu. Makao makuu ipewe uwezo wa kubuni na kuendesha miradi ya chama kukipatia kipato.
  • d. CDM irudishe chama kwenye majimbo kuonesha kuwa kinaamini kweli sera ya majimbo. CDM imekuwa ikiuza sera kuwa wakishika madaraka wataongoza nchi wa kuweka madaraka katika majimbo zaidi. Sasa kama hili kweli wanaamini ni jambo zuri basi waanze nalo kwenye chama. Kwanini chama kiko too centralized? Naamini CDM kitoe madaraka makubwa kwa chama mikoani au kwa kuunganisha mikoa na hivyo kuwa na makao makuu ya chama ya Kanda ambayo yatashughulikia shughuli zote za chama katika ngazi hizo. Kama majimbo ni mazuri kwa uendeshaji wa serikali bila shaka ni mazuri kwa uendeshaji wa chama! Hii pia itasaidia kuondoa watu wanaotaka kwenda kufanya kazi makao makuu ya taifa! Wengine waende kwenye kanda huko!
  • e. Mfumo wa nidhamu ubadilishwe ili masuala ya nidhamu yashughulikiwe katika mfumo mmoja, unaoeleweka na ambao unafanya kazi kwa haraka, kwa uwazi, na kwa uhuru. Mfumo unaosubiri miaka au miezi kushughulikia migongano kwenye majimbo au ngazi fulani ni mfumo mbaya. Ni muhimu mfumo uwepo ambao mara tatizo linapojitokeza linashughulikiwa mara moja na kumalizwa siyo kuachwa kiporo wiki baada ya wiki miezi baada ya miezi na hata inakuwa miaka baada ya miaka. Huo ni mfumo mbaya.
Hakika hapa umenena vyema!.

 
Umeandika uzi mrefu sana sijaumaliza wote maana sijaona umuhimu, ukiona changamoto ndani ya chama ujue chama kimekomaa we ulitaka cdm wote wawe wasafi?.

Siku nyingine upende kusoma uelewe jambo...acha uvivu ndugu yangu, aina ya watu kama wewe hamna muda wa kuread na kupata knowledge,mnaacha watu wengine wanasoma wanakuwa informed and as you know "if you got knowledge,una power" badaye mnazidiwa akili na watu unaanza kulalamika mara ukabila, wanapendeleana.. My Take: penda kusoma uzi uuelewe ndio uchangie wacha tabia za kiswahili!
 
Umeandika uzi mrefu sana sijaumaliza wote maana sijaona umuhimu, ukiona changamoto ndani ya chama ujue chama kimekomaa we ulitaka cdm wote wawe wasafi? Na ndio maana cdm tuna katiba hiyo nikwaajiri ya muongozo na hakuna alie juu ya katiba ukitoka nje ya mstar usidhani utavumiliwa bila nidhamu hakuna jeshi lenye nguvu chadema bana nikama maji utayatumia tu,imeshakita mizizi nch nzima ziara za Dr hata nyerere hajawahi kufika japo nusu yake.

Makamanda komaeni kwani ukaribiapo kufika wakatisha tamaa huongezeka jiulize chama kinachoongoza kujadiliwa mitandaoni na ndani ya jamii ni kipi? CHADEMA viva maoparetar anaecheza nje ya chaki tupilieni mbali maana kunavyama vilivyo jiandaa kupokea wafukuzwa kwani hawana jinsi.
Kama hukusoma wote na ukarukia kuchangia utumbo wako huu usiyo na kichwa wala miguu. Hatukulaumu sana kwani hata mikataba mibovu iliyoopo ilipatikana hivi hivi kwa uvivu wa kusoma. Dont judge a book by its cover, judge by its contents
 
Watakuita masaliii ..ngoja waje..mana cdm kinaonekana kama malaika vilee...... Ukiwa na akili sawasawa bila unazi wa kisiasa ukweli uko wazi chadema ni kama saccos si kama taasisi ambayo inaweza kupewa nchi na kuongoza .... Binafsi chadema kiendelea kujijenga na kuingiza watu makini sio hawa waliopo sasa hakuna hata mmoja ambaye yuko sawa kuongoza nchi .... Kuongoza nchi tujitambua watz sio kama familia yako...... Cdm inahitaji mfumo bora zaidi na sio kama ulioko sasa
 
NIMEIPENDA HII
"c. Mgawanyo wa fedha za ruzuku uongozwe na kanuni zilizowekwa kikatiba ambapo kiasi kikubwa cha fedha kinaenda mikoani na ngazi zachini kujenga chama badala ya kutumika makao makuu. Makao makuu ipewe uwezo wa kubuni na kuendesha miradi ya chama kukipatia kipato".

Pamoja na kwamba CHADEMA ni chama chenye uwezo mdogo wa kifedha kulinganisha na CCM yenye dola na resource lukuki.Kwa hicho kidogo wanachopata CHADEMA Walipashwa ku reform utaratibu mpya wa RESOURCE za chama utakaozingatia nidhamu ya matumizi na mgawanyo wa uwiano rasilimali za chama kwa mustakbali wa chama kwa nchi nzima. Badala ya wakuu wachache kutafuna rasilimali za chama na kutuingiza kwenye gharama kubwa za kuwatetea mitandaoni of which we cant afford.

CCM wanajua udhaifu wa CHADEMA ni rasilimali fedha, njaa za baadhi ya viongozi, na ndio maana inakuwa rahisi kwa CCM kuratibu migogoro mingi ndani ya CHADEMA (indirectly).

Siamini kwamba CHADEMA ingechukua nchi usaliti ungeendelea, kwa kawaida nidhamu kwa chama tawala chenye dola inakuwa kubwa kuliko kwenye chama cha upinzani.Hata wana ccm pia wanavumilianaga kinafiki kwasababu tuu ya kuendelea kulinda mkate, sio kwamba hawanaga tifu.
 
Manyi

Kwa mtazamo wangu wa siasa za Tanzania, uadui kati ya vyama ni mwingi sana na hasa pale kunakuwa na mambo yanayojifisha nyuma kama baadhi ya watu kutuhumiwa, kuhongwa ili watumikie chama kingine kwa usiri mkubwa sasa. Watanzania wengi elimu yetu ni ndogo sana ndiyo maana mtu anaweza kuangalia yale ya leo na kesho tu na akasahau kuwa na mtazamo wa zaidi ya hapo. Panapofika mahala hapa uongozi madhubuti unahitajika kutoka juu.

Kama ulivyosema mabadiliko ni ya lazima lakini ni wakati gani? Je, ni pale umejiimarisha na kueleweka vyema kwa watanzania? je CDM wamefikia hapo au la? Kwa maoni yangu msukumo wa mabadiliko ya msingi katika vyama utaanza pale serikali (Ofisi ya msajili wa vyama) itafanyiwa mabadiliko na kuwa taasisi huru ikiratibu shughuli za vyama (kuweka values and norms kwa mahitaji ya maendeleo ya Watanzania). Hili la Ofisi ya Msajili wa vyama ni muhimu sana na ndilo la kwanza kwa ajili ya maendeleo ya shughuli za kisiasa na kiuchumi nchini.
Humuhitaji Tendwa akufikishe kwenye ngazi ya msingi ya chama. Unachohitaji ni mfumo ndani ya chama ambayo ipo ila haifanyiwi kazi na hapa ndipo wazo la kupeleka rasilimari fedha katika ngazi ya mikoa, wilaya, kata na vijiji.

Kuimarisha chama huko ndiyo maana ya mwanakijiji alivyoshauri na akaongeza kuwa sasa umefika wakati chama kianze sasa kuonyesha mfano katika ngazi ya majimbo ili sera ya majimbo iweze kueleweka. Na huu ndiyo wakati wa sera ya majimbo kuanza kutekelezwa na Chama
 
Ndg Mwanakijiji,

Pamoja na hayo uliyoyaona kama matatizo ndani ya CHADEMA lakini ni chama ambacho kimekuwa kikipitia katika misukosuko mingi yenye dhuluma toka chama tawala.

Migongano ndani ya CHADEMA: Mf. Waziri anayelipwa kwa kodi za wananchi anasimama na kusema CHADEMA itasambaratika muda sio mrefu. Maana yake kuna yale anayoyafanya kuhakikisha chama hiki hakifiki popote kama vile NCCR mageuzi, CUF. MAwazo yako ni mazuri bali yalenge kuboresha chama na sio kulaumu tu bila kuangalia upande mwingine.

Mfano: Kipindi cha kampeni za urais 2010 CHADEMA walikuwa wananyimwa mpaka viwanja vya kufanyia mikutano na kuwekwa katika viwanja vya pembezoni na vidogo, Wanafunzi wa vyuo kunyimwa fursa ya kupiga kura, Wanajeshi kushikishwa bunduki siku ya kupiga kura ili wasipige kura, Msalala masanduku ya urais kupokwa. Migongano hii ndani ya CHADEMA kama tulivyoshuhudia pia ndani ya chama hiki hatarishi kwa Maccm ipo ya kupandikizwa na CCM na pia mitazamo,ufuatiliaji na utekelezaji. Chama hiki kimetokea kukua kwa kasi hasa kipindi cha Kampeni 2010 na leo ni miaka mitatu tu ya kukua kwake kwa kasi; hivyo zipo changamoto nyingi za kufanyia kazi na hasa hasa kupanga na kuratibu kwa pamoja kama ambavyo kamati zake zimekuwa zikikutana na kutoa maelekezo.

Mauaji: CHADEMA walitoa ratiba yao ya kuzunguka mikoani ili kuimarisha chama na kama unavyofahamu ile ratiba ilibidi isitishe maramoja kutokana na mauaji ya makusudi yaliyokuwa yanapangwa na Maccm na Polisi kwenye mikutano yao. Kama ilinyoona Morogoro ngome ya miaka mingi ya Maccm ilivyotekwa na Mikutano ile na hii iliashiria mwisho wa Maccm. Na laiti kama mikutano ile ingeendelea kufuatana na ratiba ile leo hii CCM ingekuwa taabani kabisa. Tunapojadiri kukwama kwa Chadema katika maeneo fulani tuangalie pia shida iliyopo kwa watawala wa nchi hii.

Kuwajibishana: Mimi binafsi nimeona kule kule kwenye jumuia zake wamekuwa wanawajibisha wale wasio na nidhamu; lakini pia lazima waombe ushauri kwa wakubwa wao nini cha kufanya. Katika uchanga huu huwezi kutoa maamuzi bila hata kuwepo juhudi za kushauriana kwanza. Tatizo kubwa na ma CCM kukingia mambo ya vyama vingine ambavyo ni tishio kwao.

M4c: Hii iangaliwe kwa mapana zaidi; lakini pia Chadema ina wanahazina wao kata, wilaya, mikoa na taifa. sasa sijui kama kuna audit ya kuangalia hayo. M4c imekuwa ikichangisha pesa za papo kwa papo na zinesaidia sana kuendesha mambo ya mahalia pale. sioni tatizo ilimradi kuwe na taarifa ya kila mwezi toka mikoani kwenda taifa juu ya mapato na matumizi. Kama sikosei Chadema walitoa taarifa kuwa itaajiri makatibu wakuu wa Wilaya au mikoa. Hao watasaidia sana katika suala hili maana ndo watendaji wakuu lakini pia wasiwe wabomoaji kama akina Matata(Mza).

CHADEMA MSINDIKIZAJI: Msindikizaji katika fair game au unfair game? Kama ulivyoona pia Mh.Lubuva katika maoni ya katiba amesema kuwe na fair game katika Maccm na vyama vingine. hapo ndo kwenye tatizo tu sio pengine. Ni ajabu ya kiafrica ( ngozi nyeusi) mtu kupiga kura eti ukae mita 100 ili mradi tu uzuie wenye ma-hotpot na makasha ya biskuti wasiingie na kura bandia na huo Maccm wakauona ujanja wa mwaka. Ni kweli kwa maccm chama kama Chadema watakuwa wasindikizaji tu maana kama Rais aliyeko madarakani ndo anaweza kuamua watu sasa waandikishe kupiga kura na daftari lenyewe la kupigia kura kuchezewa kwa makusudi kwa ushirikiano na viongozi wa mashina wa CCM.

CHADEMA chukuweni changamoto zote za mzifanyie kazi lakini Mungu ni wetu sote na sio wa Maccm tu.
 
Hoja ya MMK ni nzuri, ila kuna point moja labda nimeikosa au sikuielewa vyema.

Unaposema maamuzi ya kumfukuza mwanachama anayeshutumiwa au aliyekosewa yakafanywa moja kwa moja na uongozi wa chini hauni kuwa kuna wanachama ambao wanapenda kuwazushia viongozi wao tuhuma mwisho wa siku zinakuwa siyo za kweli ,akafukuzwa bila kuwa na kosa?

Na kitu kingine ni kuwa Watanzania wengi bado hatuna uelewa wa siasa ya vyama vingi,wengi wetu tumeweka mawazo kuwa wanaopenda vyama vya upinzani ni wahaini,na hili linakuja baada ya chama tawala chenyewe kutoelewa au kuridhia uwepo wa vyama vingi.Pili viongozi wengi waliomadarakani kwa sasa wanatumia mwanya wa umaskini wa vijana,ukosaji wa ajira kwa kuhonga pesa nyingi ili kuleta vurugu kwenye vyama vya siasa.

Hili halikuanza na CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi walipata pia vurugu hizi na mpaka leo vyama hivi vimeshindwa kusimama tena.
Na pia naunga mkono hoja yako kuwa mtu anapokuwa anatuhumiwa ajitahidi kujibu tuhuma ziele mapema ili kuondoa usiri unaokuwepo na watu kujiuliza je ni kweli? Na hasa kwa wale wenye uelewa mdogo.

Na mwisho napenda kuomba rai kwa wale wenye nia na uwezo wajaribu kuhamasisha elimi ya uraia ili japo kwa udogo watanzania tuweze kuelewa mbichi na mbivu.


Asante sana MMK
 
Makamanda komaeni kwani ukaribiapo kufika wakatisha tamaa huongezeka jiulize chama kinachoongoza kujadiliwa mitandaoni na ndani ya jamii ni kipi? CHADEMA viva maoparetar anaecheza nje ya chaki tupilieni mbali maana kunavyama vilivyo jiandaa kupokea wafukuzwa kwani hawana jinsi.

Wale wale kina zidumu fikra za mwenyekiti.
 
Back
Top Bottom