Ujengelele
JF-Expert Member
- Jan 14, 2008
- 1,253
- 22
Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko;
Tarehe: 22nd September 2010
BAADA ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukataa kushiriki midahalo ya wazi, mdahalo mwingine umeandaliwa ukilenga baadhi ya wagombea vijana kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) na Chama Cha Wananchi (CUF).
Baadhi ya wagombea ambao watakuwa katika mdahalo huo, ni pamoja na Mbunge wa Kuteuliwa anayemaliza muda wake, Ismail Jussa Ladhu, anayegombea uwakilishi wa Mji Mkongwe kupitia CUF.
Wengine ni mgombea ubunge wa Chadema Ubungo, John Mnyika na mgombea ubunge wa CUF katika jimbo hilo, Julius Mtatiro, mgombea wa Chadema Kilombero, Regia Mtema na wa Chadema Vunjo, John Mrema.
Mdahalo huo maalumu kwa wagombea vijana, utarushwa moja kwa moja na kituo cha Televisheni cha ITV keshokutwa saa moja usiku na utahudhuriwa na waalikwa 200.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa Mdahalo huo, Rosemary Mwakitwange, alisema kaulimbiu ya mdahalo huo ni ‘Tanzania Tunayoitaka' na Mwenyekiti wake atakuwa mwanaharakati na mwandishi aliyebobea, Jenerali Ulimwengu.
Alisema mdahalo huo ulioandaliwa na taasisi za East African Business and Media Training na Vox Media Center Limited, ulikuwa na nia ya kushirikisha vijana wa vyama vitatu vilivyokuwa na wabunge katika awamu iliyopita, ikiwamo CCM, lakini walipowasiliana na Kamati ya Kampeni ya Chama hicho tawala, ilikataa kushiriki.
Akizungumzia vyama vingine vyenye wagombea, alisema imekuwa vigumu kushirikisha wagombea wote, kwa sababu ya muda , kwani wangezungumza kwa muda mfupi huku wengine wakikosa muda huo hivyo walitaka vyama vishiriki kutoa idadi ndogo ya wagombea.
Alisema, lengo la mdahalo huo ni kutoa nafasi kwa wapiga kura kuwafahamu na kusikiliza hoja za vijana wanaoomba ridhaa ya kuingia bungeni kwa miaka mitano ijayo, huku wakiwahamasisha vijana wengine kwa kuwapa ujasiri wa kushiriki siasa.
"Mdahalo huu umemlenga kijana anayetafuta ridhaa ya wapiga kura ya kuingia katika chombo cha kutunga sheria zitakazowaathiri Watanzania wote, hata wasiokuwa ndani ya jimbo lake au chama.
"Utatoa nafasi kwa wapiga kura kuwaona ili kupima matarajio ya Watanzania ndani ya miaka mitano na zaidi, kwani vijana wa sasa wanaweza kukaa ndani ya Bunge kwa muda mrefu," alisema Mwakitwange.
Alisema, mdahalo huo hautagusa maisha binafsi ya wagombea kwa lengo la kuwadhalilisha au kuwachafua, hautatoka nje ya majadiliano yenye malengo ya kutoa majibu kwa wananchi na wapiga kura juu ya mustakabali wa Taifa.
"Utazingatia ujenzi wa demokrasia kuliko itikadi za vyama, ingawa washiriki wana nafasi ya kurejea hadidu kadhaa za ilani za vyama vyao katika kujenga hoja," alisema.