CCM pumzikeni mtafakari namna ya kuanza upya

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,436
21,263
Pilipili: CCM pumzikeni mtafakari namna ya kuanza upya
broken-heart.jpg
Na Ayub Riyoba

KATIKA makala niliyoandika Agosti 16, mwaka huu nilizungumzia changamoto ambazo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilikuwa kinapambana nazo katika vikao vyake mjini Dodoma wiki hiyo.
Â
Yapo maneno niliyatumia kuelezea changamoto zile na yamejidhihirisha tena katika vikao vya Kamati ya Wazee wa CCM inayoongozwa na Rais Ali Hassan Mwinyi, iliyokutana na Wabunge huko Dodoma wiki hii.
Â
Katika makala ya Agosti 16, nilitoa udadisi wangu kama ifuatavyo, na ninanukuu aya kadhaa:
Â
“Kwamba leo CCM wanakutana Dodoma kwa ajili ya vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu huku chama kikiwa na viongozi wake wa ngazi za juu wanaohitilafiana katika misimamo na hata kifalsafa si jambo geni tena. Lakini kutofautiana tu huenda ni jambo la kawaida katika demokrasia iliyokomaa ndani ya taasisi au jamii yoyote.
Â
Kinachoongeza udadisi katika hili la kutofautiana baina ya vigogo wa CCM ni ukweli kwamba, leo hii wamefika pahala imedhihirika kuwa si wamoja tena kwa sababu tofauti baina ya baadhi ya vigogo zimegeuka kuwa uhasama wa kuwindana.

Hakuna atakayeshangaa kama ikiripotiwa kuwa katika vikao vyao kila mjumbe aliingia na maji yake ya kunywa akiwa ameyakumbatia kifuani! Naamini baadhi yao hata mikono hawatapeana!
Â
Wenyewe kwa wenyewe wamepeana majina. Wapo wanaitwa mafisadi na wapo wanaitwa walio mstari wa mbele katika vita dhidi ya ufisadi. Inawezekana tofauti hizo kweli zilitokana na mpasuko wa uchaguzi wa 2005. Inawezekana tofauti hizo zinatokana na kutofautiana malengo na maslahi baada ya uchaguzi wa 2005. Lakini pia inawezekana tofauti hizo zinatokana na kudhihirika kwa utashi wa kimrengo wa wanachama.
Â
Kwamba, katika chama wamo wabepari damu. Wamo wajamaa damu. Wamo waliberali. Wamo wahafidhina. Wamo wenye mrengo wa kati. Wamo wakulima. Wamo wafanyabiashara. Wamo wafanyakazi. Wamo ‘mission town’ n.k.
Â
Hivi sasa CCM wamejifungia Dodoma. Na kama kawaida yao, pamoja na tofauti zote hizo; pamoja na chuki na uhasama – wa kiwango cha juu - baina ya baadhi ya vigogo; bado CCM wanaweza kutoka Dodoma na umoja wa ajabu.

Wakapiga picha ya pamoja huku wakicheeeka. Tena wakawaonya wale wote wanaosema CCM si shwari. Uchaguzi umekaribia!” Mwisho wa kunukuu.
Â
Lakini nilikwishaandika pia makala nikieleza kwamba nilitarajia kuwa CCM yenye wanachama wanaohasimiana kiasi hicho, ingetafuta fursa kuwakutanisha wanachama wake viongozi ili wajadili kwa uwazi na kwa ukweli kiini cha uhasama wao.
Â
Japokuwa wapo Watanzania ambao hawakuona umuhimu wa Kamati ya Mzee Mwinyi, kwa mantiki kwamba, kiini na hata sura ya ugomvi ndani ya CCM vilikuwa dhahiri, bado kazi ya Kamati ile imekuwa na umuhimu wa aina yake. Kwanza imekuza utamaduni wa uwazi ambao ni nguzo ya msingi katika demokrasia.
Â
Pili kamati ile imedhihirisha kwamba, kweli wapo viongozi (wakiwamo wabunge) wa CCM ambao siyo tu wanahitilafiana, bali wana uhasama wa kiwango cha kutisha. Kwamba, kumbe yaliyokuwa yakizungumzwa na kuandikwa na vyombo vya habari hayakuwa majungu.
Â
Vikao vile pia vimedhihirisha kuwa, kumbe hitilafu zile na uhasama zilioutengeneza si lazima kwamba, vyote vinawakilisha maslahi ya Taifa na ya Watanzania kwa ujumla.
Â
Kwamba, kumbe kwa mujibu wa viongozi wa CCM wenyewe; kutokana na kupigana vikumbo vya wenyewe kwa wenyewe kutaka kushika madaraka, basi viongozi wa chama tawala wamejikuta wanaendesha nchi kivita ya wao kwa wao.

Na huenda kuna rasilimali nyingi za umma wanazitumia kugharamia vita vya wenyewe kwa wenyewe bila Watanzania -wenye nchi yao kujua.
Â
Wakati tumeendelea kutangazia ulimwengu kuwa Tanzania ni nchi ya upendo, umoja na amani na kwamba, vyote hivyo vimeletwa na TANU na baadaye kuendelezwa na CCM; kumbe mambo yamebadilika.

Kumbe tayari CCM wale wale ambao walipaswa kuwa nguzo ya upendo, umoja na amani ya Tanzania, leo wanapigana vita vya wenyewe kwa wenyewe kama ilivyo Somalia.
Â
Hivi kuna upendo gani, umoja gani na amani gani katika kauli tulizozisikia katika malumbano ya viongozi na wabunge wa CCM huko Dodoma katika vikao vya Mzee Mwinyi? Hivi kama viongozi wa CCM wenyewe kwa wenyewe wamefikia hatua hiyo hizo ni dalili gani kwa mustakabali wa Taifa?
Â
Na kama kweli viongozi wale waliokuwa wakizungumza vile kule Dodoma wanaamini kuwa katika kauli zao; hawaoni umefika wakati wakubaliane kama chama kwamba, sasa wawaombe wanachama wao na Watanzania kuwa wawaruhusu wapumzike kidogo (waondoke madarakani) ili watafakari upya misingi ya chama chao na watathmini ni wapi walipojikwaa kidhamira hadi kufikia viwango vya siasa za chini na za uhasama wa kienyeji, ambao hata Mwenyekiti wa chama Rais Jakaya Kikwete alikiri kusikitishwa nao siku alipozungumza na wananchi kupitia televisheni na redio hivi karibuni.
Â
CCM itakayoomba kupumzishwa leo, itaweza kurudi madarakani hata baada ya kipindi kimoja tu. Lakini CCM itakayotaka kuendelea kutawala hivi hivi ilivyo, siku ikiondoka madarakani itaangukia pua. Na itaambatana na UNIP, KANU na vyama tawala vyengine katika safari ya kuzimu kisiasa na itabaki tu katika maandishi yaliyofifia ndani ya vitabu vya historia visomwavyo na mende tu.
Â
Vinginevyo, kama wanataka waendelee kutawala, viongozi wa CCM watatakiwa kutafuta namna ya kumaliza uhasama wao. Na uhasama hautaisha tu kwa mahasimu kulazimishwa wachekeane na wakumbatiane kisha wapigwe picha ya pamoja kwa ajili ya umma kushuhudia. Uhasama uliofikiwa utaisha kwa chama kuamua kuinua juu misingi inayodumu na kushusha kiburi cha umimi.
 Wakishamaliza uhasama wao waje wawaambie Watanzania kwamba, kiini hasa cha ugomvi wao kimeshughulikiwa na waliokubali kutubu makosa ni kina nani na wote waliovunja sheria, misingi ya utu na utaifa wetu wawajibike (au wawajibishwe), halafu watuahidi kuwa wanaanza upya na watahakikisha wanapigania maslahi ya umma na misingi ya umoja wa taifa letu na si kukanyagana kuhusu namna ya kushinda chaguzi zijazo.  Â
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom