Busara zitumike kutatua sakata hili la madaktari

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,320
33,125
katuni(7).jpg

Maoni ya katuni


Sakata la mgomo wa madaktari wanafunzi limezidi kutikisa ambapo sasa Chama cha Madaktari Nchini(MAT) kimetoa tamko linalotoa saa 72 kwa serikali iwarejeshe madaktari wanafunzi 229 waliotimuliwa wiki moja iliyopita.
Aidha katika tamko hilo kimemvua uanachama Mganga Mkuu wa Serikali pamoja na kutaka Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Blandina Nyoni awajibishwe kutokana na sakata hilo.

Kabla ya hatua hii, Wizara ya Afya ilieleza kuwa imewapa mkataba mpya madaktari hao wenye kipengele cha adhabu kwa watakaoenda kinyume na mkataba.

Katika mkataba huo kipo kifungu kinachoeleza kuwa Wizara ya Afya itakuwa na mamlaka ya kumpa adhabu ya kumfukuza au kumhamisha daktari ambaye atakuwa ameenda kinyume na mkataba kulingana na taratibu za wizara.
Madaktari wanafunzi 229 katika hospitali ya Muhimbili waliondolewa wiki iliyopita na kurudishwa Wizarani kutokana na mgomo wa kushinikiza posho ambazo ni stahili yao.

Mgomo mara zote huleta madhara. Na kwa mantiki hiyo ni busara mgomo ukaepukwa ili athari ambazo zimekuwa zinasababishwa na mgomo zikaepukwa. Mgomo siku zote hufanyika baada ya rai kutolewa kuhusu madai ya msingi lakini yakapuuzwa.
Posho ya madaktari wanafunzi ilikuwa ni stahili yao ya msingi na hivyo chombo kinachosimamia malipo hayo iwe ni hospitali ya

Muhimbili au serikali yenyewe vilipaswa kujipanga na kuandaa malipo hayo mapema kwa kuwa yanafahamika.
Madaktari ni miongoni mwa wanataaluma wanaohitajika sana katika maendeleo na ukuaji wa taifa letu. Sekta ya afya inakabiliwa na changamoto lukuki ikiwa ni pamoja na uhaba wa madaktari.

Waziri wa Afya, Haji Mponda katika moja ya vipindi cha Dakika 45 vinavyorushwa na Kituo cha ITV alikiri hilo hivi karibuni. Akasema; “ Tumeapa na tumewaahidi Watanzania kwamba changamoto mojawapo katika sekta ya afya ni watumishi.
Akaongeza kwa kusema kwamba wizara yake imejipanga katika kuzalisha madaktari wengi zaidi na kwamba hadi mwaka jana, wizara imeweza kuzalisha madaktari 700 kwa mwaka.

Kwa mantiki hiyo, busara zaidi zinahitajika katika kutatua mtatatizo yanayochipua migomo ambayo inaleta athari kwa wengine wasio na hatia. Hata hiyo hatua ya kuwaondoa pale Muhimbili baada ya kuwalipa haikuwa sahihi. Pale ni mahali muhimu pa

kujifunzia kwa sababu wapo mabingwa wengi wa kuwasaidia kufikia azma zao. Kuwahamishia hospitali za chini ni kuwadhoofisha. Waanzie mazoezi kwenye hospitali za rufaa ndipo wakafanye kazi hospitali za ngazi za chini.

Isitoshe, mgomo ule wa madaktari umeathiri pia huduma kwa wagonjwa wengi. Kama wanaoshughulikia malipo ya posho za madaktari hao wanafunzi wangetekeleza wajibu huo, adha waliopata wagonjwa isingekuwepo.

Madaktari hawa walikuwa na madai ya msingi kwa ajili ya kujikimu ikiwa ni pamoja na nauli na mahitaji mengine. Hivyo hata wao waliathirika kwa kucheleweshewa malipo yale. Ni kweli uvumilivu ni muhimu, lakini uwe katika mazingira rafiki pasipo vitisho.

Pia tunadhani kwamba mvutano kati ya madaktari hao, uongozi wa hospitali ya Muhimbili na serikali ndio uliowatesa wagonjwa wasio na hatia. Busara zingetumika zaidi katika kutatua tatizo hilo kwa malipo kufanyika kwa wakati ili huduma ziendelee bila kukwama.

Kama posho za viongozi katika sekta mbalimbali zinatolewa haraka kama vile za wabunge na watendaji wengine serikalini, kwanini hizi za wataalamu wetu zitafutwe kwa mbinde? Bajeti iandaliwe mapema siyo kushtukiza.

Tusiwapoteze wataalam ambao tayari wameshomeshwa kwa fedha nyingi za umma na tayari wako katika hatua ya kutoa huduma. Kama kweli tunawahitaji wanataaluma wengi katika sekta nyeti kama hiyo ya afya, basi ziwekwe taratibu nzuri na zisizo na usumbufu katika kushughulikia stahili zao.

Ni imani yetu kwamba tamko hilo la MAT litatizamwa kwa mapana na hatimaye serikali ipate ufumbuzi wa kudumu kuhusu wanataaluma hao. Hiyo ni moja ya siri ya utawala bora.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
 
thank you, hakika busara inahitajika la sivyo madaktari inabidi washikamane kudai haki yao
 
Kumsimamisha uanachama Mganga mkuu wa Serikali ya Muungano Tz ni suala kubwa sana kisheria. Ni lazima Mganga huyo ajiuzuru na kuachia madaraka mpaka hapo atakapokuwa mwanachama wa kutambuliwa na chama cha madaktari nchini kwake.

Kazi ipo.
 
hapa mkuu serikali imeshaamua kuwatimulia mbali madaktari maana yenyewe ndio 'imeshika mpini'. We acha tu!
 
Back
Top Bottom