Bibi Titi Festival Ikwiriri Rufiji 27 November hadi 2 December 2023

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,920
30,263

View: https://youtu.be/EGlJS8PwzoA

DONDOO KATIKA MAISHA YA BIBI TITI​

Msukumo mkubwa nchini Kenya ilikuwa kufanya kampeni ya nchi nzima kuwashinikiza Waingereza wamwachie huru Kenyatta aliyekuwa akichukuliwa na wananchi wote kama kiongozi na nguvu ya umoja wa Waafrika wa Kenya.

Jomo Kenyatta na wenzake walikuwa kifungoni Kapenguria.
Hawa walikuwa Peter Mbiu Koinange, Bildad Kaggia, Achieng Oneko, Kungu Karumba na Fred Kubai.

Katika wimbi hili la kutaka Kenyatta afunguliwe kutoka gerazani, Tom Mboya alimdokeza kijana mmoja kutoka Tanganyika jina lake Ismail Bayumi kuwa TANU ingeweza kusaidia katika kampeni hii ya kuwashinikiza Waingereza kumtoa Kenyatta na wenzake kifungoni.

Ismail alikuwa kijana kutoka Moshi akifanyakazi Mombasa Municipal Council na mmoja wa viongozi wa TANU Club pale mjini.

TANU Club ilikuwa mfano wa tawi la TANU Mombasa kwa kuwa isingewezekana kwa chama cha siasa cha Tanganyika kupewa tasjila Kenya.

Ismail alifikisha wazo hili makao makuu ya TANU mjini Dar es Salaam kwa kupitia mtu maalum aliyekuwa akiwasiliana na Tom Mboya na Nyerere kwa siri.

Historia hii nimeisikia kutoka kwa Bi. Titi mwenyewe na kwa Ismail Bayumi.
TANU ilimtuma Bibi Titi Mohamed kwenda Kenya kuzitia shime harakati za kufunguliwa Kenyatta.

Wazalendo nchini Kenya walikuwa wameshindwa kabisa kuwaingiza wanawake ndani ya KANU hivyo kuzinyima harakati za uhuru nguvu kubwa sana na ya kutegemewa ya akinamama.

Huko Mombasa TANU Club ilifikiria kuwa kumleta Bibi Titi kuja Kenya kuifanyia kampeni KANU ilikuwa ni kitu kipya cha kuwahamasisha wanawake ndani ya KANU na kwa hiyo kuongeza nguvu mpya na kutia ari ya utaifa katika Kenya.

Bibi Titi alikuja Mombasa na kufanya mkutano Ukumbi wa Tononoka.

Kwa kawaida kwa madhumuni ya kupata kibali mikutano hii ilikuwa inahesabiwa kama ni mikusanyiko ya kufanya sherehe siyo mikutano ya siasa na ilikuwa ikifanyika ndani.

Lakini mkutano huu ulikuwa na umuhimu wake kwa sababu ya kuwako Bibi Titi Mohamed mjini Mombasa.

Wengi walikuwa wamemsikia Bibi Titi lakini hawakuwa wamepata kumuona.

Watu walijaa ndani ya ule ukumbi hadi nje kuzunguka viwanja vya Ukumbi wa Tononoka.

Kwa kweli kwa hali yoyote mkutano ule usingeweza kuitwa kuwa ni mkutano wa wanachama wa TANU Club mjini Mombasa, au hata mkutano wa TANU Club Kenya nzima, kwa sababu wanachama wa KANU waliwazidi wanachama wa TANU Club kutoka Tanganyika.

Kenya ilikuwa bado haijaweza kumtoa hata mwanamke mmoja wa kiwango cha Bibi Titi.

Kwa wakati ule kumwona mwanamke wa Kiislamu amesimama bila baibui akihutubia halaiki ya wanaume ilikuwa ni jambo la kushangaza sehemu za pwani, ambako wanawake walitembea huku wamejifunika mabaibui na hawakutakiwa hata kufanya kazi maofisini.

Bibi Titi alifanya mikutano Mombasa na Nairobi akiwasisitizia watu wasikate tamaa wasimame pamoja hadi Kenyatta amefunguliwa kutoka gerezani.

Habari za mikutano hii iliandikwa kwa mapana na marefu na magazeti ya Mombasa Times na Taifa Leo.

Kenyatta alipotoka jela alikuja Dar-es-Salaam akahutubia mkutano mkubwa Viwanja Vya Janwani kutoa shukurani zake na za watu wa Kenya kwa TANU na kwa Bibi Titi kwa msaada wake wa kumtoa kifungoni.

Haya ni machache sana katika historia ya siasa ya Bibi Titi Mohamed.
 
Back
Top Bottom