Rare Sapphire

JF-Expert Member
Jul 24, 2021
576
1,626
Wajukuu zangu leo nataka niwaeleze mambo fulani, fundo ambalo limenikaa kooni mpaka nashindwa kuhema. Aliyewaroga kafa na katupa gunia chini ya bahari kukiwa na chuma kizito ndani yake kusiwe hata na chembe ya matumaini kuwa ipo siku litaonekana na kufunguliwa mkawa huru. Mmefungwa akili, ama niseme vizuri bongo zimekatwa na madini yote yakatupwa halafu ngozi ikarudishwa na kufunika kama hakuna kilichotokea. Maana kama zingekua zimefungwa na kulala tu walau kungekua na matumaini kwamba tungepiga shoti zikaamshwa na kuanza kufanya kazi. Vitu vinafanyika mbele yenu mchana kweupe lakini hakuna mnachofanya. Mnaishia kukenua na kupiga makofi, sauti zinawakauka kwa kuachia vigelegele vya furaha. Siyo kwamba nataka kuwatukana au kuwasema vibaya, ila kiukweli ni kama mnafikiria na miguu mpaka muinyanyue ndio vichwa vyenu vinaanza kufanya kazi. Mmefunga macho na kuziba masikio, wote mnaongozwa kwa kushika kamba na kuifatisha kama mazuzu ambayo hayawezi kuhoji chochote. Mnajua fika mnayoyafumbia macho hayaondoki eti kisa tu mmeamua kuangalia pembeni. Uozo huu mnaoacha kusafisha unaharibu vya kwenu na hata kesho kwa wajukuu zenu.

Nakwambia wajukuu zangu ningekuwa na uwezo ningetembeza bakora kote ili tuamke kutoka katika usingizi huu mzito. Msafishe macho yenu yaliyozibwa na ukungu mzito unaowafanya msione, na kuzibua masikio msikie vizuri kelele na vilio mlivyovigeuza kuwa nyimbo za kunengulia wakati wanasesere ni nyie wenyewe. Wajukuu zangu yowe hili napiga nataka muamke hapa kijijini, na siyo tu kuamka bali kuyafatilia na kuhakikisha haturuhusu kuuziwa mbuzi kwenye gunia. wajukuu zangu nakwambia wale walishawasoma akili zenu, wanajua fika mnavyofikira. Wanawachezesha wanavyotaka kama vikaragosi. Watoto wa sasa mnasema hawapoi hawaboi yaani wakitoa hilo wanaweka lile na nyinyi kama bendera mnavalia njuga kila linalozuka, mnapiga soga weeee halafu mnaliacha hapo hapo mkisubiri panapofuka moshi pawake moto mchezo uwe ule ule.

Wajukuu zangu tukianza na vibanda vya wale wanaohakikisha kuna usalama tukiwa tunaenda kusaka michuzi sasa hivi vimegeuka kuwa sehemu za kutoa michango. Kuhakikisha taratibu zinafatwa na kuwa kuna usalama kwao sio kipaumbele, tena sasa hivi wameanzisha mtindo mpya. Wanakodi vijana wao wa kutosha, hawa wapo mahsusi kuhakikisha lile kapu lao linanona vilivyo. Vijana hawa wanakua tayari kusubiri ndiga zikiwa zinakaribia kukatisha kwenye mistari ya myama pundamilia, wewe utakua huna habari sababu macho yako yamehakikisha hakuna mtu anakatisha na pako salama wewe kuendelea na safari zako. Sasa ukikaribia tu kijana mmoja atakatisha ghafla mbele yako, mwenye jezi yake nyeupe atakuja haraka kukusimamisha na kukwambia bwana ulitaka kupoteza nguvu ya taifa. Mazingira ya kuchangia kapu lao yanakuwa yashatengenezwa unaambiwa “sasa sikia mi najua una mambo mengi we changia kapu tu na uende zako”. Wao wala hawataki mambo mengi, shida yao na lengo lao kuu ni uchangie kapu lao tu. Kinachosikitisha ukitaka kufata sheria hawa bwana watakwambia “acha ujinga wewe nipe buku 5 tu nikuache uendelee na safari yako, we huoni kukundikia risiti unaenda kutupa tu michuzi yako bure? We nitoe ya vocha tu nikuache uwahi kwenye shughuli zako”. Ukitia ngumu zaidi wanakutafutia sababu na kukukomoa zaidi mwisho wa siku unalainika na kuwa mchangia kikapu.

Tukija kwenye elimu yetu yaani ndio nashindwa hata kuongea kwa hii hasira ninayopata kila nikifikiria jambo hili. Hivi wajukuu zangu kuna kitu kimeoza hapa uanjani kwetu kama mfumo wetu wa maarifa?! Mbaya zaidi kila siku tunapiga kelele lakini hakuna kinachofanyika. Inasikitisha yaani mpaka leo hii bado mnameza vile vitu vya enzi zangu. Hivi kwani hawaoni kama mambo yamebadirika na sisi inabidi twende na kasi hiyo hiyo tuweze kukimbizana na wenzetu? Na kinachofurahisha sasa, kwa jinsi wanavyojua wanavyowalisha ni uozo wakiwa wanataka watu mahiri kujenga hapa kijijini kwetu wala hawahangaiki na sisi, wanaenda kuchukuwa watu kutoka vijiji vingine vya wale watu walioshiba vizuri na si tu bora kushiba bali wameshiba chakula che virutubisho. wajukuu zangu yaani mpaka huwa najifikiria kweli kuna haja ya kuwapeleka wadogo zako shule tena, au niwafundishe kusoma na kuandika vingine ulimwengu utawafunza? Tulipoharibu ni pale tulipochukua walivyoviacha bilia kuchuja, tukaendelea kuwekeza kwenye hadhi, ukishapata madini yakajaa basi ukakae kwenye kiti cha kuzunguka upigwe na kiyoyozi yaishe, huna maajabu! Ubunifu ukawa msamiati mpya, kazi za mikono zikapuuzwa tukasahau hata hizo ni muhimu pia kwa maendeleo ya kikiji chetu, kama tunavyotia nguvu kwenye hadhi basi na kwenye ujuzi wa mikono tututie nguvu zaidi, kwa pamoja tutakuwa na kitu chenye nguvu kitakachoweza kutusimamisha popote pale kwa kujiamini. Lini tutawekeza kwenye utafiti na tathmini ili kujenga vilivyo wakombozi wetu wa baadae?! Kwa kufanya hivi tutajua nini kinahitajika, wapi tuweke nguvu zaidi na wapi kunahitajika msaada zaidi ili hata wasiomudu wasiachwe nyuma, nini kinatufaa twende nacho,nini hakitufai tuache na nini kipya cha kuongeza. Inasikitisha kwamba mbali na haya madudu yote kuna watu wamejaliwa vipawa na wanapambana kweli kweli Kijiji koine uwezo wao, lakini leo wako wapi?! Utasikia siku mbili tatu wanapiga nao picha halafu basi kila kitu kinakuwa kimeishia hapo. Hakuna juhudi zozote za makusudi zinazofanywa kuwanyanyua wanakikijiji hawa ili tuongeze nguvu na uwezo wa kijiji chetu lakini pia iwe chachu ya vijana wengine kufanya mambo makubwa zaidi. Nimekumbuka ule msemo wenu mnapenda kutumia vijana siku hizi "kusoma hamuwezi basi hata picha hamuoni?" Amkeni wajukuu zangu kijiji chetu kinawahitaji sana.

Wajukuu zangu, kuna mtu amepewa filimbi hapa kijijini kwetu ambaye kila mwaka anatoa ripoti ya mwenendo wa kijiji chetu ili tuweze kujitathmini tumefikia wapi, wapi tumeweza na wapi tunahitaji nguvu zaidi lakini pia ni nani anachangia kuzamisha meli yetu tusifike kule tunapotaka. Kila mda unapofika mkeka hutolewa uwanjani na waliofanya madudu wanatajwa, kinachofata wajukuu zangu mtavalia njuga tuliyojuzwa weee, mtapiga zogo kila kona mpaka mishipa inawasimama na mara nyingi hata waliopewa vijiti wakiongozwa na kiranja mkuu nao wanaungana na sisi na wanakuwa wanakemea kweli kweli uharibifu huo wa meli yetu baada ya hapo kelele zinazima tunaenda kulala kama hakuna kilichotokea. Sasa wajukuu zangu nini maana ya kutuletea mkeka huu kama mwisho wa siku mnachofanya ni kusikiliza tu na kupiga kelele?! Kwani wajukuu zangu hamna uchungu na huu ubadhirifu unaofanyika uwanjani kwetu?! Hamjui wasiposhughulikiwa wale wachache wenye kutia doa nguo zetu nyeupe basi wote tutaishia kuwa wachafu na tutaendelea kutafunwa na uchafu huu hadi siku tuamke?! Nawauliza nyie mjukuu zangu kweli kaa hili la moto mnalolikumbatia waliwaunguzi hata kidogo?!

Leo nimewaamulia wajukuu zangu, yaani ni bandika bandua mpaka bongo zenu zianze kufanya kazi. Hapa kijijini kwetu tumebarikiwa bwana, na moja ya vitu ambavyo tumebarikiwa na tunajivunia ni hivi viazi vyetu adhimu, viazi ambavyo vinapatikana kutoka katika kijiji chetu tu. Unajua wajukuu zangu mnachukulia mchezo mchezo kuhusu hivi viazi vyetu na hamuoni ni jinsi gani tulivyobarikiwa na utajiri huu. Embu fikiria katika vijiji vyotee vya karibu na mbali ambavo idadi ya wanakikijiji wote ni zaidi ya bilioni saba na katika idadi hii ni sisi tu ndio tumebahatika kuwa na viazi hivi vyenye thamani kubwa. Swali langu kubwa wajukuu zangu na maumivu niliyonayo inakuwaje vijiji vingine wanaanza kumiliki viazi vyetu na kuviuza kwa watu wengine bila ya sisi wamiliki kuwa na taarifa yoyote?! Lakini pia sio viazi tu, kuna vingine vya thamani kubwa vinafika katika vijiji vya mbali vinauzwa kwa michuzi mingi kwelikweli kwa mabwenyenye, habari zinatembe kote na sisi kama kawaida yetu tunakuwa wa mwisho kujua. Mnatoa macho mnashangaa, ni kweli hamjui yanayofanyika au ndio mnafunika kombe mwanaharamu apite, kila mtu ale kwa urefu wa kamba yake?!

wajukuu zangu yaani inashangaza kwelikweli ile habari nimesikia kwenye redio mbao yangu hapa, eti mmetengeneza bustani yetu adhimu, baada ya kujiridhisha mambo yapo safi msimamizi wa bustani yetu akaenda kule Kijiji cha ng’ambo kuonyesha maua yetu mazuri tuliyokua nayo. Lengo si baya ni zuri kabisa, kwamba wakiona jinsi maua yetu yalivyo mazuri yananukia na kupendeza basi tutajaza maelfu kwa maelfu ya watu waje kwetu kuyaangalia. Kile cha kushangaza sasa, baada ya watu kuhamasika kuja kuyaona maua yetu tumekuja na mpango kabambe au niseme kashambe wa kuuza haya maua yetu adhimu wawe wanayaona huko huko walipo. Hapa uwanjani wote tukabaki hoi, ilikua mpango mzuri wa kuwashawishi waje kuona bustani yetu hapa tujiongezee na michuzi leo tukiwapelekea bustani yetu huko huko walipo, kwetu watafata nini tena?! Labda kutuuzia ya kwetu yakinyauka na mengine kutoweka kabisa! Naona kelele zenu zilisaidia kidogo tukasikia mpango umesitishwa kwa muda, japokuwa kuna mlevi mmoja alikua akipayuka eti kuuza maua yetu hatujaanza leo sema sasa hivi wino mwekundu utapita ili ifanyike wazi wazi.

Wajukuu zangu nna uchungu, kijiji chetu kimeoza, kinanuka na kutoa harufu mbaya. Kila iendayo leo wenye vijiti wako bize kumega uwanja wetu, japokuwa kwenye hili siyo wale tuliowapa vijiti au nyinyi wajukuu zangu wote mnahatiai. Inasasikitisha sana kwamba kijijini kwetu ukitaka mambo yaenda basi ni lazima uwe na michuzi ya kutosha kusukuma jambo lako la sivyo kila siku utakuwa wa kupewa ahadi za kuku; kesho kifaranga kitanyonya. Hapa sizungumzii kutoa makaratasi pekee, wengine wanaenda mbali zaidi hadi kudai vipande vya nyama ndio watie wino mambo yaanze kusoga. Ikitokea jambo lako limeenda bila kuambiwa uzame mfukoni inakua kama maajabu, yaani wewe mwenyewe unapata mshangao na kujiuliza mara mbilimbili kweli umemaliza kila kitu bila kutolewa michuzi hata lepe?! Wajukuu zangu kweli ndio tunaelekea huku kufanya haramu iwe halali na halali tuone kama kaa la moto? Hamuoni kwa kufanya hivi mnawanyima wanakijiji wengine kupata stahiki zao na kuruhusu mambo ya hovyo yaendelee?! Lini mtakaa na kusema sasa basi, kuanzia leo tutasimamia kijiji chetu ili kiendelee, na wale wote watakaokuwa wakimega kijiji chetu kidogo kidogo kuwawajibisha ili tusije kupotea kabisa tukabaki kwenye vitabu tu kwamba tulitokea tukatafuna kijiji mpaka tukapotea?! Wajukuu zangu sisi wakati wetu umeisha, nyinyi mkisimama kwa nguvu moja hakuna ujinga utakatiza mbele yenu bila kushughulikiwa. Embu uchungu huu uwaingie mpaka kwenye mifupa na uwakasirishe kweli kweli mpaka mseme sasa basi.

Wajukuu zangu kuna jambo lingine pia ambalo sielewi kwanini bado liko hivi. Tunaelewa sasa hivi hali si nzuri baada ya kua wenzetu wa ng'ambo mambo hayapo vizuri na wote tunaathirika na hili. Lakini kwanini mzigo mkubwa wanashushiwa wanaochechemea waubebe peke yao? Yaani kila suhulisho linaloletwa basi ni kutia kaa la moto pale pale ambako kuna kidonda kibichi. Mimi sitaki kuamini kwamba katika vitu vyote vya kufanya basi macho yao yameishia kuona vilivyopo chini tu, hakuna anaefikiria kugeuza shingo kuangalia nyuma, pembeni, kushoto na kulia kuna kuna kipi kinaweza kutoa njia nyingine itakayoongezea nguvu huku ili hawa wa chini wapate kupumua. Kuna mlevi mmoja alipayuka akiwa anarudi nyumbani kwake asubuhi, "yaani ingeguswa mifuko ya hata kiduchu mngeona jinsi tungepata mapendekezo mazuri mpaka tuchoke wenyewe, ya jinsi ya kukabiliana na hili bila kumega mkate wao". Hali ni mbaya kote lakini wanafanya nini ili huyu anaechechema aweze kupona na kutembea na sio kumkata mguu kabisa arudi kutambaa.

Wajukuu zangu kuna kitu kingine kibaya sana kinafanyika ambacho sasa muda si mrefu kitaonekana ni kawaida na mzunguko utakuwa ni ule ule kupiga kelele mkimaliza mnasubiri mwingine aje afanye hivyo hivyo mpige tena kelele bila kuchukua hatua yoyote. Taratibu jambo hili linashika mizizi na itakuja kuwa ngumu sana kuling'oa. Hawa watu tuliowapa vijiti wakimbie kwa niaba yetu, wakati wakiwa na nguvu za kukimbia huku wameshikilia vijiti barabara huwa hawaoni baya wakati huo. Yaani wakati huo kila wanachofanya kiko sawa, hata wakivurunda wanasimama kwa nguvu zote kusimamia wanachokisema na wanamaanisha kwamba yao ndio sahihi na sawia. Sio kiranja mkuu wala wasaidizi wake yaani hakuna utakachowaambia wakasikia. Sasa subiri muda wakuachia vijiti na kukabidhi watu wengine waanze mbio ufike, hakuna rangi hutaacha kuona. Kila mmoja anaanza kuwa msafi, kila mmoja anataka apewe muda asikilizwe kusema "ukweli wake” na karibu wote huwarushia lawama watu wengine kwamba wenyewe walikua wanasukumwa tu lakini mpanga mchezo wote ni mwafulani. Eti wakishaachia viti ndio wanapata fahamu, roho zinawasuta kwa kukaa kwao kimya na kuacha kusema ukweli kwa kipindi chote walichokuwa na nafasi ya kufanya hivyo. Kweli ukistaajabu ya Musa ya Firauni ndio yatafanya uzimie kabisa. Wewe ufuje mali zetu siku zote hizo hapa kijijini kwetu ukijua fika unadhulumu maendeleo ya kijiji chetu lakini pia ukijua ni kosa kisheria leo ghafla tu kwakua umeachia kijiti basi macho yako yamefunguka na masikio yamezibuka sasa umegundua yaliyofanyika yalikua ni udhalimu wa hali juu na hukuwa sahihi?! Nani atalipia muda huo wote uliotudhulumu kwa makusudi tena ukijigamba kwa uliyoyafanya?! Utarudisha vyote ulivyodhulumu?! Nini lengo la wewe kukiri ubadhirifu huo leo hii?! Haya ni baadhi ya maswali inabidi muwe mnajiuliza wajukuu zangu, lakini cha kushangaza siku wakiachia vijiti na kuvuta vipasa sauti ndio kwanza mnaanza kuwaona wema, eti wamewasaidia kubainisha nyeusi na nyeupe, mkiendelea na mwenendo huu mtakuja kushtuka kila kitu kimeisha hakuna tena cha kulinda, watakula na kuharibu wakijua mtawasikiliza tuna kuwashukuru kwa “ujasiri wao” wa kutueleza “tusiyoyajua”

Wajukuu zangu kwa sehemu kubwa mnatuangusha, wanakijiji mnawapa vijiti wenyewe huku mkiwa mnajua fika walikotoka na waliyofanya, yaani mpo na mikoba yote iliyojaa taarifa zao lakini mwisho wa siku mnawapa vijiti hao hao kwa vijizawad vya hapa na pale na kusahau udhalimu wote waliyoufanya. Halafu bila aibu mnapata nguvu za kuja kulalamika eti mliowapa vijiti wamewatenda na kuwasaliti, wajukuu zangu hamna haya wala hamjisikii vibaya kwa hili?! Kwanini msisimame kidete na kuweka tamaa pembeni tukapata watu wa maana na wakujivunia, watu wenye uchungu na kijiji chetu, wanaojua tulipotoka, wapi tupo na nini tunahitaji, wapi tumesimama vizuri na wapi tunahitaji kukaza mkanda? Mbali na kupiga kelele kila siku mnafanya nini kuhakikisha mnaboresha pale tunapochechemea? Siwaambii mkafanye vurugu na kufanya mambo ya hovyo kwa kisingizio eti mna uchungu na yanayofanywa, hapa mtakuwa hamna tofauti na wahalifu wengine mnaopaswa kuadhibiwa kutokana na makosa mtakayokuwa mmefanya. Hatua mtakazozichukuwa kuboresha mambo hapa kijijini kwetu yawe ya kujenga na kuweka heshima hapa uwanjani kwetu, sio viwe vya kubomoa zaidi na kufanya tuzidi kuonekana hatuna maana zaidi ya ambavyo tulivyo sasa. Haya ni machache tu katika mambo mengi ambayo yanahitaji wajukuu zangu muamke kama mnataka Kijiji chetu kiendelee na kifike kule mnapotamani kifike, kila mmoja awe mwangalizi wa mwingine kuhakikisha mambo yanaenda sawa, muwe na uchungu na mkemee maovu yanayofanyika mkijua kwamba yanayofanyika yanatuathiri wote, usipoguswa wewe leo basi litamuathiri mtoto wako kesho au mjukuu wako keshokutwa.​
 
"Hili nalo muende mkalitizame"
Babu tumepigwa kichwani na kitu kizito chenye ncha kali!

 
Babu wajukuu hawana walijualo zaidi ya uchwa na ushabiki wa kipumbafu wa simba yanga mondi na alikiba..kwa akili hizo sahau kupata wajukuu aggressive kwaajili ya nchi yao.

Wajinga wengi sana nchi hii.

#MaendeleoHayanaChama
 
Back
Top Bottom