Balozi Karume amechokonoa ustaarabu wa kidemokrasia

Oldmantz

JF-Expert Member
Jan 24, 2023
430
996
Kihistoria, Afrika baada ya ukoloni, karibu kila nchi ilipitia hatua tatu. Hili limewekwa sawia na mwanazuoni mzawa wa Ghana, anayeishi Afrika Kusini, Profesa Kwesi Prah.

Andiko la Profesa Prah “Multi-Party Democracy and It’s Relevance in Africa” – “Demokrasia ya Vyama Vingi na Uhusika wake Afrika", linachambua maisha baada ya ukoloni Afrika, zama za Waafrika kupumua hewa safi ya uhuru, kisha udikteta na nyakati za mapinduzi.
Hata hivyo, kwa uchambuzi wa matukio ya zama hadi zama Afrika, nitasogea mbele ya Prof Prah kwa kuonesha kuwa nchi za Kiafrika, kwa wingi wake, hivi sasa zipo hatua ya tano. Ndoto ni kuifikia ya sita ili demokrasia ya kweli itamalaki.
Ufafanuzi, karibu kila nchi, baada ya kumwondosha mkoloni, wananchi walifurahia uhuru wao, shangwe mitaani zilipambwa na demokrasia. Vyombo vya habari vilifanya kazi bila bughudha wala masharti. Uhuru wa maoni ulikuwa wa mfano.
Katikati ya kipindi hicho cha uhuru wa vyombo vya habari na maoni, watawala walioshika mamlaka za nchi baada ya ukoloni, walianza kuona kero. Haraka sana walipiga marufuku vyama vingi. Nchi zikawa za chama kimoja. Uhuru wa habari ukaminywa.
Kuminya demokrasia ni hatua ya pili baada ya furaha ya upumuaji wa hewa safi ya demokrasia. Bahati mbaya zaidi, kipindi cha uminyaji demokrasia kilisababisha Afrika itengeneze madikteta hatari mithili ya watawala wa zamani wa Latini Amerika.
Hatua ya tatu ikafuata. Ilikuwa kudai demokrasia. Naam, Waafrika walishaonja utamu wa hewa safi, ghafla madirisha yakafungwa. Walihitaji kupumua kwa mara nyingine. Zikaibuka vuguvugu za kimapinduzi.
Kutoka nchi moja hadi nyingine Afrika, ama mapinduzi yalifanyika au majaribio yalifeli. Zilikuwa nyakati za kuuana au kufungana jela. Wapo watawala waliuawa, vilevile wapinzani wengi walinyongwa. Yapo mauaji yalifanyika hadharani. Mbele ya kadamnasi.
Hatua ya nne ni karoti au bakora. Taasisi viranja wa sarafu duniani, Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), zilitoa chaguo kwa watawala wa Afrika. Wafungulie demokrasia ya vyama vingi wamegewe karoti au wagome wachapwe bakora ya kiuchumi.
Taratibu, kwa shingo upande, watawala wengi walikimbilia karoti. Vyama vingi vikafunguliwa mwenye nchi nyingi Afrika. Waliovimba kuwa hawakutaka karoti, sio tu walipigwa bakora za kiuchumi, bali pia mataifa ya Magharibi yalifadhili uasi dhidi yao.
Hatua ya tano, ndipo nchi zote za Afrika zilipo. Madirisha ya demokrasia yalifunguliwa kwa ushawishi wa karoti na kwingine baada ya machafuko, hivyo kulazimisha zama mpya za kisiasa.
Kilichotokea, madirisha ya demokrasia yalifunguliwa nusu. Watawala wengi waliruhusu vyama vingi, wakiwa na fikra pamoja na mitazamo ya chama kimoja.
Hoja ya Balozi Karume
Balozi Ali Karume, mmoja wa watoto wa Kiongozi wa Mapinduzi Zanzibar, Abeid Aman Karume, amekuwa maudhui ya siasa za Zanzibar, hasa mitandaoni katika siku za karibuni.
Balozi Karume amekuwa akizungumzia masuala mbalimbali ya siasa za Zanzibar. Misuagano ndani ya chama chake, CCM. Uteuzi wa wagombea urais Zanzibar kuamuliwa Dodoma, kisha uchaguzi na uhalali wake.
Tuweke kando yote, tushike la uchaguzi na uhalali. Balozi Karume anasema kuwa CCM, chama chake, huwa hakishindi uchaguzi. Kwamba mabadiliko ya Katiba yaliyoleta muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, ulikuwa mpango wa kung’ang’ania madaraka.
Balozi Karume ni mdogo wa Rais wa Sita wa Zanzibar, Aman Abeid Karume. Balozi Karume alidai kwamba kaka yake hakushinda uchaguzi wowote, hivyo alibadili Katiba kumsaidia Rais ambaye angemrithi kutoka CCM.
Ubelgiji, Ujerumani na Italia ni nchi ambazo Balozi Karume alizitumikia kama balozi, kabla ya hapo, alipata kuwa balozi mwenye hadhi ya waziri (Minister Plenipotentiary), Brussels, Ubelgiji. Vilevile Naibu Balozi wa Marekani, akawa pia Balozi na Mkurugenzi wa Wizara ya Mambo ya Nje, Idara ya Ulaya na Amerika.
Balozi Karume pia alishajitokeza kuwania tiketi ya kuwa mgombea urais Zanzibar kwa tiketi ya CCM mara tatu; mwaka 2000, 2010 na 2020. Majaribio yake hayo yote yaligonga mwamba.
Sasa, mtu huyo na wasifu wake huo uliosheheni, ndiye anasema CCM hawajawahi kushinda urais Zanzibar. Na sababu aliyotoa ni mtindo wa mgombea kupatikana Dodoma kwa namna ambayo huwa sio ya kidemokrasia.
Tuchukue la kuwa CCM huwa haishindi Zanzibar. Tuunganishe na malalamiko ya vyama vya CUF na ACT-Wazalendo kuwa mgombea wao, Seif Sharif Hamad, alishinda kila uchaguzi wa urais Zanzibar ila aliporwa.
Seif aligombea urais kwa CUF mara tano, mwaka 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015, kisha ACT-Wazalendo mwaka 2020. Kwa kuyaelewa maelezo ya Balozi Karume ni kuwa Seif alishinda kila uchaguzi ila alidhulumiwa.
Changamoto ya demokrasia
Ujumbe ambao Balozi Karume anaufikisha japo anaonekana yupo zigzaga, iwe kwa ukweli au uongo wake, ndio matokeo ya demokrasia kufunguliwa dirisha nusu Afrika.
Aprili 1991, Mathieu Kerekou, alimshangaza kila mtawala Afrika, alipokubali kushindwa kiti cha urais Benin na aliyekuwa mpinzani wake, Nicephore Soglo. Ni baada ya kuiongoza nchi hiyo ambayo zamani iliitwa Jamhuri ya Dahomey kwa miaka 19 kasoro miezi sita.

Kenneth Kaunda, alifuata mkondo wa Kerekou kwa kukubali kushindwa uchaguzi na kukabidhi nchi kwa mpinzani wake, Frederick Chiluba. Watawala wa Afrika walistaajabu na walimwona mjinga.
Angalau Kerekou aliweza kurudi madarakani, aliposhinda uchaguzi Benin mwaka 1996. Kaunda alipoachia kiti, kila alipojaribu kugombea tena urais, Chiluba alimwekea vizingiti, ikiwemo kumfunga jela.
Hilo ndio tatizo la demokrasia nusu dirisha Afrika. Hata viongozi walioingia madarakani kidemokrasia, wakishakalia kiti hugeuka madikteta. Hung'ang'ania ofisi, hujaribu mpaka kubadili Katiba wabaki ofisini.
Uchaguzi unakuwa mchakato wa kitapeli. Wananchi wanapanga foleni kujiandikisha na hata kupiga kura. Wanayaacha mashuka alfajiri na baridi kali. Wanasimama kwenye mistari mchana wa jua kali. Halafu uamuzi wao unapindishwa. Asiyeshinda ndiye anashinda.
Afrika ilivyo, madaraka ni matamu kuliko uamuzi wa wananchi. Ndio sababu uchaguzi hauishiwi manung’uniko ya wizi mpaka machafuko. Hali ni hiyohiyo kutoka nchi moja hadi nyingine.
Katiba zinaandikwa. Zipo ambazo zinatungwa kwa hila za kuwalinda watawala, lakini hata zile ambazo maudhui yake ni bora kwa nchi, bado huwa hazifuatwi. Uhuni unakuwa mwingi. Ustaarabu wa kidemokrasia ni kitendawili.
Kenya ilifanya Uchaguzi Mkuu Agosti 9, 2022. Mifumo ya kidemokrasia, iwe kwa kuichezea au uimara wake, ndio iliwezesha William Ruto, kushinda kiti dhidi ya Raila Odinga, aliyekuwa anapigiwa chapuo na Rais aliyekuwa madarakani, Uhuru Kenyatta.
Baada ya Ruto kula kiapo cha kuwa Rais wa Tano wa Kenya, kazi ya kwanza ikawa kununua wabunge wa upinzani ili kujihakikishia nguvu za kutosha kwenye Bunge.

Tafsiri ni hii, heshima ya demokrasia ni changamoto. Watawala dhidi ya wapinzani wao wa kisiasa, wanatazamana kwa macho ya uadui kuliko kujenga taifa moja. Ruto aliona dhahiri kuwa wapinzani kubaki na nguvu zao, wangemkwamisha.
Hata jinsi alivyoingia madarakani, makamishna wanne kati ya saba wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Kenya, waligomea matokeo. Hiyo inakupa picha kuwa demokrasia ya vyama vingi ilipokelewa ila ilifunguliwa nusu dirisha.

Hatua ya sita
Ndoto zinashawishi matumaini ya demokrasia kamili. Ile iliyosemwa na Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln kuwa “Serikali ya watu, iliyowekwa na watu, na kwa ajili ya watu.” Wananchi waamue na uamuzi wao uheshimiwe.
Uchaguzi uwe huru na haki. Karatasi ya kupigia kura iwe na thamani. Endapo wananchi watafanya uchaguzi mbaya, ni wao watakaoumia. Alisema pia Lincoln: “Uchaguzi ni mali ya watu. Ni uamuzi wao. Kama wataamua kugeuza migongo na kujiunguza kwa nyuma, ni wao watalazimika kuketi kwa makalio yenye majeraha ya moto.”
Ndoto ya demokrasia kamili ni kuona watawala Afrika wanatambua kuwa madaraka ni utumishi. Watumikie watu kwa mujibu wa Katiba na sheria. Kiongozi anapobadili Katiba au sheria ili asibanwe au kudhibitiwa na mifumo, huyo ni adui wa demokrasia.
Balozi Karume amechokonoa ndoto ya nchi kuwa na demokrasia kamili. Sio ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ambayo wanaounda Serikali na wanaoshirikishwa, kila upande unadai kushinda uchaguzi.
Serikali za umoja wa kitaifa mithili ya Kenya mwaka 2008 mpaka 2013, ambayo Wakenya huiita nusu mkate au Zimbabwe Februari 2009 hadi Septemba 2013. Marais Mwai Kibaki (Kenya) na Robert Mugabe (Zimbabwe), baada ya presha ya ghasia za kisiasa, wakalazimika kugawana madaraka na wapinzani.

Kibaki na Raila, Mugabe na Morgan Tsvangirai, ilikuwa baada ya machafuko, marais madarakani wakidaiwa kupoteza ushindi dhidi ya wapinzani wao. Mazungumzo yakakaribisha maridhiano. Waliodaiwa kushinda wakabaki viongozi wakuu, ‘walioshinda', wakapewa nusu mkate. Hiyo sio demokrasia.
Demokrasia ya mfano ni ile ya Kerekou na Kaunda. Ikatekelezwa na Goodluck Jonathan, Nigeria, alipokubali kushindwa urais Machi 2015, kisha akamkabidhi madaraka mpinzani wake, Muhammadu Buhari, kwa amani, Mei 2015.
Sio demokrasia ya hofu kama Gambia Desemba 2016. Rais Yahya Jammeh alikubali matokeo ya kushindwa urais, akampigia mpinzani wake Adama Barrow, akampongeza. Baadaye akashituka, akataka kugoma kutoka, mpaka alipolazimishwa na jeshi la nchi za Afrika Magharibi, Januari 27, 2017.

CREDIT:LUQMAN MALOTO - MWANANCHI
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom