Badala ya kumshangilia Magufuli tuna wajibu wa kufanya

Shayu

Platinum Member
May 24, 2011
608
1,653
Nadhani badala ya kumshangilia Raisi Magufuli kwa hatua anazochukua katika ukusanyaji na udhibiti wa kodi na matumizi yasiyo ya lazima katika serikali. Ambalo ni jambo la kimsingi . Tujue kwamba na sisi wananchi wote tuna wajibu. Na sisi tuna wajibu wa kufanya.

Na jambo la msingi ni kwetu sisi kufanya kazi kwa bidii. Nchi hii haiwezi kuendelea pasipo watu wote kushiriki katika ujenzi wa nchi yetu. .Mungu ametupatia sisi binadamu maarifa na vipaji tofauti ni wajibu wetu kutumia vipaji hivyo kwa maendeleo ya taifa letu.

Kama nilivyowahi kusema hapo awali nchi yetu haiwezi kuendelea pasipo watu wetu kujibidiisha katika kutafuta maarifa.Tujue kwamba Magufuli hawezi kufanya kazi peke yake. Ni wajibu wetu pia kufanya kazi. Na kutenda yale ambayo tunawajibika nayo kama raia.

Hili ni jambo la msingi kama raia. Nadhani ni wajibu wa kila raia mwema kutimiza wajibu wake bila kusukumwa. Kwahiyo uwajibikaji huu hautakiwi kuwa wa upande mmoja tu bali na kwa raia pia kuwajibika kwa yale yanayowahusu kama raia.

Kushangilia peke yake hakusaidii taifa hili. Tusiwe washangiliaji tuwe wachezaji. Tutimize wajibu wetu. Tutumie muda wetu vizuri kwa mambo yanayojenga na yenye manufaa. Ni muhimu pia kujiangalia kama raia. Kila raia ana nafasi yake katika kulifikisha taifa hapa lilipo kwa namna moja au nyingine. Matendo yetu na tabia zetu yamechangia kwa kiwango fulani kulifikisha taifa hili hapa lilipo. Baadhi ya matendo tumeyafanya kwa kujua na mengine pasipo kujua. Kwa kujenga tabia zenye madhara kwa taifa letu badala ya faida.

Nadhani ni wakati wa mabadiliko ya kimtizamo. Pamoja na udhibiti wa matumizi mabaya ya serikali na uwajibikaji na ukusanyaji wa kodi. Nchi yetu inahitaji great social reforms. Nadhani huu ndio utakuwa msingi imara. Kujenga kujitambua kwa wananchi wetu kuhusu wajibu wao kama raia.

Kuwafanya kuwa wananchi wanaowajibika kwa mambo yanayowahusu. Na kujenga misingi imara ya familia zetu na mahusiano ya kijamii.Kuweka ''moral values''. Na kubadili mitazamo ya watu kuhusu taifa lao. Na kujenga tabia za watu wetu kutumikia. Kujenga nidhamu kwa watu wetu na elimu bora yenye misingi imara ya kimaadili. Nadhani wakati umefika sasa wa kubadilika kifikra. Na kubadili matendo yetu na tabia zetu.

Hii kazi Magufuli hawezi kufanya peke yake kama wananchi wao wenyewe hawatojenga tabia kufikiri na kufanya kazi. Pasipo watu wetu wote kuacha uzembe na kujua wana wajibu kwa taifa lao.Ili taifa hili liendelee watu wote lazima wawajibike. Lazima wafanye kazi.

Unaweza usiwe mzuri katika kazi za nguvu lakini ukawa mzuri katika kufikiri.

Binafsi harakati zangu ni kuleta mapinduzi katika fikra naamini maendeleo ya nchi hii yatapatikana kutakapokuwa na mapinduzi ya kifikra. Watu wetu wote watakapojihusisha katika kutafuta maarifa kuliko kitu chochote kile na kutakapo kuwepo uhuru wa maoni na wa fikra. Tumaini letu liko hapo. Liko kwenye nidhamu, uwajibikaji wa watu wetu na katika kutafuta maarifa bila kuchoka.

Ni muhimu kujenga misingi sasa , ambao kizazi chetu kijacho watakuja kuinua kile tulichokiwekea msingi. Tunahitaji watu wetu wawe wanye skills na wajuzi wa mambo mengi.

Maarifa ndio msingi wa taifa lolote kuendelea.Kuwajengea watu wetu kulipenda taifa lao na kuwa tayari kulitetea na kulilinda. Kutumia muda wao mwingi kutafuta maarifa yatakayosaidia taifa hili.

Tutadhibiti wezi wanaoibia nchi sawa lakini hatua zaidi ya hizo zinatakiwa kuchukuliwa kwa kutoa elimu yenye misingi imara ya kimaadili na nidhamu na kwa malezi yaliyo bora kwa watoto.

Ni muhimu kujenga tabia za watu katika hatua ya awali, kuwa raia wanaowajibika, waaminifu na wenye nidhamu. Kujua malengo na dira ya taifa lao ni ipi na kuwa tayari kutumikia ili malengo na dira hiyo ifikiwe. Nadhani tukifanikiwa katika kujenga tabia za watu wetu kupitia elimu tutakuwa tumepiga hatua kubwa katika kujenga raia wanaowajibika na tutakuwa msingi imara.Kwahiyo katika jambo hili la ufisadi na kutokuwajibika kwa watu wetu nguvu pekee haitoshi. Utakapodhibiti watu, watatafuta mbinu nyingine za kuiba. Utawajengea uoga tu bali sio tabia ya kuwa wawajibikaji, waaminifu na wenye nidhamu.

Mambo haya mawili lazima yaendane elimu na udhibiti wa dola.Kwahiyo Magufuli anaweza kudhibiti kwa kipindi chake cha miaka mitano au hata kumi lakini kama hakutakuwa na misingi imara mambo yale yale yatajirudia akitoka madarakani. Nadhani elimu bora ni muhimu sana kwa watu wetu wote.

Ni katika elimu ambapo tabia mbaya hujitokeza. Watu au serikali inaposahau nidhamu. Nakudhani kwamba hakutakuwa na madhara yeyote kutozingatia nidhamu na maadili katika elimu. Hivyo tabia mbaya na utovu wa nidhamu huingia.

Na taratibu utovu wa nidhamu na maadili mabaya huingia katika mifumo ya kiserikali na kwenye masuala ya kibiashara. Maadili ya taifa hushuka na watu kuwa sio waaminifu.

Huingia kwenye sheria na kwenye katiba, Watu huingiza maslahi yao binafsi na sio yale ya taifa. Na mwisho wa siku hujenga watu wasio na fikra sahihi bali matapeli ambao huongozwa na tamaa binafsi ya mali na sio fikra. Na busara huwa haipo miongoni mwao. Na watu walioelimika badala ya kuwa chachu ya mapinduzi ya kifikra katika jamii kwa kuleta mwanga wa maarifa wanakuwa mwanzo wa giza nene . Wanaharibu kabisa maadili na misingi ya utaifa na kijamii. Na taifa hukosa dira..
 
Back
Top Bottom