Angola: Ulafi wa “Zedu” na makinda yake/ Raia Mwema, Novemba 13, 2019

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,239
BARAZANI

Na Ahmed Rajab

HII ni hadithi ya ubabe, uroho, ulafi, ufisadi na utumizi mbaya wa madaraka, utumizi wa nguvu za kisiasa kwa maslahi binafsi ya wahusika. Ni hadithi yenye kuonyesha jinsi mtu mmoja mwenye nguvu kubwa za kisiasa anavyoweza kuilaghai nchi iamini kwamba haiwezi kwenda bila ya yeye.

Ni hadithi yenye kuonyesha pia jinsi chama kikubwa cha kisiasa nchini kinachotumiwa na kiongozi wa kibabe kinavyoweza baadaye kumgeukia na kumtia adabu kiongozi huyo.

Mhusika mkuu wa hadithi hii ni “Zedu”, jina la utani la José Eduardo do Santos, Rais wa zamani wa Angola, nchi ambayo Jumatatu hii ya juzi iliadhimisha miaka 44 tangu iunyakue uhuru kutoka kwa wakoloni wa Kireno, walioitawala kwa takriban miaka 500.

Wahusika wengine wa hadithi hii ni wanawe “Zedu”. Kuna binti yake mkubwa Isabel, mwanawe mkubwa wa kiume José Filomeno “Zenu”, binti yake mwengine Welwitschia au “Tchizé”, kama ajulikanavyo mitaani, na mwanawe mwengine wa kiume José Eduardo Paulino, maarufu kwa jina la “Coréon Dú”.

Ni hadithi yenye kuonyesha jinsi “Zedu” na makinda yake walivyoila na kuinyonya nchi wakishirikiana na kupe wenzao.

Rais wa mwanzo wa Angola alikuwa Dk. Agostinho Neto, kiongozi wa kwanza wa chama cha ukombozi cha Movimento Popular de Libertação de Angola — Partido do Trabalho (MPLA). Chama hicho kilikabidhiwa uhuru na Wareno Novemba 11, 1975, kwa sababu wapiganaji wake ndio waliouteka mji mkuu wa Angola, Luanda, wakati wa mapigano dhidi ya Wareno.

Neto aliyehitimu udaktari Ureno alikuwa Mkomunisti, na mwanafasihi aliyepata umaarufu kwa utungaji wake wa mashairi kwa lugha ya Kireno.

Neto alikuwa mtu wa tafakuri nyingi. Alikuwa na usuhuba mkubwa na kina Che Guevara na Fidel Castro wa Cuba. Nchini Tanzania alikoishi kwa miaka mingi sehemu za Upanga, Dar es Salaam, wakati wa vita vya ukombozi wa nchi yake, Neto alikuwa karibu sana na Abdulrahman Babu, kiongozi wa chama cha Umma cha Zanzibar na baadaye waziri katika serikali ya Tanzania.

Neto na Babu walikuwa na usuhuba wa chanda na pete. Mara nyingi ilikuwa Babu aliyekuwa akimpangia Neto miadi yake ya kukutana na Rais Julius Nyerere. Hata wake zao, Maria na Ashura, walikuwa mashoga wakubwa. Familia hizo mbili zikiendeana majumbani mwao na mara kwa mara zikialikana kwa chakula.

Familia nyingine iliyokua karibu na kina Neto na Babu ilikuwa ya John Holness na mkewe, Marga. Holness, mzalia wa Jamaica, alikuwa mfuasi wa nadharia ya Kimarx aliyejuana na Babu walipokuwa wanafunzi London katika miaka ya 1950. Babu alimwalika ende kufanya kazi zake za usanifu majengo Tanzania. Huko alikutana na Neto na alisaidia harakati za MPLA.

Babu alikuwa karibu zaidi na Neto kushinda na Samora Machel wa Msumbiji ingawa kabla ya Samora kuongoza chama cha ukombozi wa Msumbiji, Frente de Libertação de Moçambique (Frelimo), Babu alikuwa akitembelewa sana kwake na Eduardo Chivambo Mondlane, aliyekuwa kiongozi wa awali wa Frelimo. Mondlane aliuliwa kwa bomu Dar es Salaam Februari 3, 1969.

Neto na Babu walishikimana hivyo licha ya kwamba walikuwa wakielemea pande tofauti katika vuguvugu la kimataifa la wafuasi wa Marx. Neto akielemea upande wa Moscow na Babu upande wa Beijing.

Neto akisisitiza kwamba lazima MPLA kiwe kinafuata itikadi ya Umarx na Ulenin. Hata hivyo, alipokuwa Rais wa nchi alishikilia Angola ifuate sera za kisoshalisti na si za kikomunisti. Msimamo huo ulizusha mtafaruku mkubwa ndani ya MPLA kati yake na Nito Alves, aliyekuwa waziri wake wa mambo ya ndani kwa muda mrefu.

Neto akitaka usoshalisti uendelezwe hatua kwa hatua, akipinga siasa za “ugozi” za kuwatenga wananchi wenzao waliochanganya damu na Wareno. Pia akitaka Angola isifungamane na upande wowote.

Alves aliupinga vikali msimamo wa Neto. Mwaka 1977 Alves na maelfu ya wafuasi wa chama cha Wakomunisti, Organizaçao dos Comunistas de Angola waliuliwa. Serikali ya Neto iliwashutumu kwa kujaribu kufanya mapinduzi. Kwa muda wa miaka miwili wafuasi wa Alves walisakwa na kuuliwa.

Neto alifariki dunia Septemba 10, 1979 jijini Moscow alikokuwa akitibiwa kwa ugonjwa wa saratani. Alikuwa na umri wa miaka 56.

Baada ya Neto kufariki ndipo uongozi wa MPLA na wa serikali ya Angola ulipomuangukia Eduardo do Santos. Aliitawala Angola tangu 1979 hadi alipostaafu 2017. Alikuwa rais wa pili barani Afrika aliyetawala kwa muda mrefu kushinda marais wote wengine. Alipitwa na Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo aliyeshika urais wa Equatorial Guinea kasoro ya miezi miwili tu kabla ya do Santos kuwa Rais.

Ingawa alikuwa waziri wa mwanzo wa mambo ya nje na mjumbe wa kamati kuu ya MPLA, dos Santos siye aliyedhaniwa na wengi kwamba angekuwa mrithi wa Neto.

Aliwapiku akina Iko Carreira na Lúcio Lara. Iko alikuwa waziri wa ulinzi na akionekana kuwa wa pili katika uongozi wa MPLA baada ya Neto. Lara alikuwa kwa miaka mingi katibu mkuu wa MPLA. Alipofariki Neto, alikuwa makamu rais wa chama.

Iko na Lara walikuwa “mulatto”, watu waliochanganya damu ya Kireno. Wote walikuwa na hofu kwamba serikali yenye kuongozwa na mmojawao isingedumu. Ingepinduliwa na “magozi” wa MPLA.

Kwa hakika, alipofariki Neto, Lara aliyashika kwa muda madaraka yote ya rais wa chama na vile vile wa nchi. Lakini mbio mbio Septemba 11, 1979 aliandaa mkutano mkuu wa pili wa MPLA na alifanya kampeni kubwa ya kutaka dos Santos achaguliwe Rais. Kuna waliomtaka Lara azishike yeye hatamu za uongozi. Alikataa.

Hivyo ndivyo dos Santos alivyochomoza kuongoza Angola. Mara tu baada ya kuyapata madaraka akaanza kubakuabakua na kujitajirisha. Alipokuwa akijidai kwamba taifa lake ni la kisoshalisti alijikusanyia utajiri usiosemeka.

Baadhi ya wenzake walimng’amua na hawakupendezewa na uroho wake. Asasi za kiraia zikaanza kuuanika ufisadi wake. Dos Santos akaota pembe na akazitumia kuwashambulia waliokuwa wakimtuhumu. Hakuna aliyesalimika. Si wapinzani, si wakosoaji, si vyombo vya habari.

Uroho wake ulikithiri serikali ilipokuwa inayauza mashirika ya umma. Alifungua makampuni yake binafsi na akanunua mashirika yaliyokuwa yanauzwa. Alipokuwa anafurutu ada Bunge likaingilia kati na likapitisha sheria za kumpiga marufuku Rais asiyanunue mashirika yaliyokuwa yakipigwa bei.

Dos Santos alianza kuliibia taifa kwa ustadi. Wizi ulipomkoloea alijifanyia mambo mchana kweupe bila ya kujali.

Dos Santos aliwapa wanawe na jamaa zake wengine, wakiwa pamoja na Fidel Kiluanje Araújo, nyadhifa nzito zinazohusika na uchumi na siasa. Mizengwe yake ndiyo yaliyomfanya binti yake mkubwa, Isabel, awe bilionea na atajike kuwa ni mwanamke tajiri kushinda wote barani Afrika. Utajiri wake unakisiwa kufika dola za Marekani bilioni tatu (US$3bn).

Mwaka 2016 Rais dos Santos alimteua Isabel awe mkuu wa shirika la mafuta la Angola, Sonangol. Alikuwa na mikono mithili ya pweza. Ilikuwa imo kwenye kila biashara na kwa vile alikuwa binti wa Rais yeye ndiye aliyekuwa akishinda kandarasi za serikali na aliyeruhusiwa kufanya biashara walizonyimwa wengine.

Hakuyadhibiti mafuta tu bali pia almasi, mitandao ya simu, benki, ujenzi wa barabara, mabwawa, upangaji upya wa jiji la Luanda na ujenzi wa bandari. Ilimradi hata ukikohoa na kikohozi chako kikawa cha kibiashara utaikuta kampuni yake, Niara, inasubiri ukiteme kikohozi iichukue biashara hiyo.

Hatuna nafasi hapa kuzitaja kandarasi zote alizopewa na serikali ya baba yake. Naitoshe tu tujue kwamba zilikuwa na thamani ya mabilioni ya dola za Marekani. Baadhi ya benki na mashirika makuu ya China yalihusishwa na kandarasi hizo.

Mwanawe Dos Santos wa kiume, Zenu ndiye aliyeanzisha benki ya kwanza ya uwekezaji yenye kumilikiwa na watu binafsi. Alifungua Benki Kwanza Invest mwaka 2008. Miaka michache baadaye akamteua asimamie Mfuko wa Utajiri wa Angola (FSDEA) wenye thamani inayokadiriwa kuwa ya dola za Marekani bilioni tano (US$5bn). Zenu akaanza kutajwatajwa kwamba huenda baadaye akamrithi baba yake katika kiti cha urais.

Kabla ya kuuacha urais, dos Santos alihakikisha kwamba anapewa ahadi madhubuti kwamba hatoshitakiwa milele kwa kosa lolote alilofanya alipokuwa Rais. Chama cha MPLA na wabunge wake walimkubalia.

Lakini baada ya kukaa sawa tu kwenye kiti cha urais, Rais mpya João Lourenço (JLo) akaanza kutimiza ahadi yake ya kuufyeka ufisadi. Alimuondoa Isabel kwenye uongozi wa shirika la mafuta la Sonangol na akaifuta mikataba kadhaa aliyoandikiana na serikali.

Zenu naye amekamatwa na kwa sasa anakabiliwa na mashtaka ya “kutumia vibaya” fedha za umma zipatazo dola za Marekani milioni 500 (US$500m).

Bunge pia limemchukulia hatua Tchize ambaye ni mbunge na mjumbe wa kamati kuu ya MPLA. Bunge limepiga kura kumfukuza bungeni kwa vile hakuhudhuria vikao vya bunge kwa siku 90 mfululizo. Tchize ana ushawishi mkubwa miongoni mwa wamiliki wa vyombo vya habari Angola. Ana kampuni kubwa ya kutangaza biashara. Amekimbilia London anakoishi akisema kwamba anahofia maisha yake nchini Angola.

Dos Santos aliyekuwa akiogopwa Angola hivi sasa ni yeye mwenye kuiogopa Angola. Hana imani na serikali wala na wenzake wanaoongoza MPLA.

Inasemekana kwamba Dos Santos amenuna na hakuzungumza kwa miezi kadhaa na mrithi wake Lourenço. Mara kadhaa alialikwa kuhudhuria sherehe rasmi za kiserikali na mara zote hizo alikataa kwenda.

Dos Santos si mtu wa maneno mengi. Hupendelea kuwa kimya na kufanya mambo yake bila ya ghasia. Si wanawe. Wako moto na wamekamia kupambana na Lourenço naliwe liwalo.

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab
 
Ipe nyama kidogo hii ya Santos Ni zaidi ya ufisadi
 
Back
Top Bottom