SoC02 Adhabu za viboko na athari zake

Stories of Change - 2022 Competition

ilapfasha

New Member
Aug 22, 2022
3
1
Ni kwa muda sasa adhabu za viboko zimekuwa zikitumika mashuleni kama njia ya kuwa-adabisha wanafunzi, huku ikiaminika kuwa kupitia kuwa adhibu watoto kwa kuwachapa fimbo husaidia kuongeza utii mashuleni hali inayofanya makosa ya utovu wa nidhamu kupungua na kuongezeka kwa nidhamu darasani. Jambo linalopelekea mwalimu kuwa na muda wa kutosha wa kujikita katika kumfundisha mtoto.

Lakini licha ya hayo yote, utafiti wa zaidi ya miaka hamsini sasa uliyo fanywa na endcorporalpunishment.org unaonyesha kuwa matumizi ya viboko kwa watoto yana madhara makubwa kuliko faida hivyo inatupasa sisi kama watanzania tubadilike na kuachana na njia hii ya kuwa adhibu watoto.

Moja kati ya sababu kubwa inayofanya njia hii ya kuwa-adhibu watoto kwa kutumia viboko kuonekana kutofaa ni kwasababu njia hii inajenga hofu mioyoni mwa wanafunzi.

Ikiwa mara kwa mara walimu wanatumia adhabu ya viboko kama njia ya kujenga nidhamu kwa wanafunzi itawafanya watoto kuingiwa na uoga kwani watahisi kuwa wapo katika hatari ya kuadhibiwa. Kama tujuavyo kuwa watoto ni taifa la kesho na wanapaswa kuandaliwa vyema katika mazingira salama na rafiki ili kuwa na taifa imara katika siku za usoni.

Kutoa adhabu ya viboko kwa wanafunzi kuna wajengea uoga, jambo linalo punguza morali ya wanafunzi kwenda shule. Baadhi ya wanafunzi huenda wakakataa kuhudhuria shule au hata kukwepa baadhi ya vipindi kwa kuwa tu wanaogopa kuchapwa hali inayosababisha ongezeko la kesi za utoro na wanafunzi kuacha shule. Badala ya kujenga nidhamu binafsi adhabu ya viboko inajenga nidhamu ya uoga jambo ambalo halimsaidii mtoto.

Ukiachana na hiyo adhabu ya viboko inazuia mawasiliano ya wazi baina ya mwalimu na mwanafunzi. Hii ni kwasababu adhabu ya viboko huathiri mtazamo wa wanafunzi kwa walimu wao na kuwafanya wawaone walimu wao kama ‘wakoloni’ ambao wapo tayari kumuadhibu vikali mwanafunzi yoyote anaye kosea. Mbaya Zaidi baadhi ya wanafunzi wanaogopa kutoa maoni yao katika majadiliano mbalimbali ya darasani, na wakati mwingine wanafunzi huofia kunyosha mikono yao na kujibu maswali darasani kwa kuhofia kuchapwa pale watakapokosea. Hali inayopunguza uwezo wa mwanafunzi kujiamini na hata kuathiri matokeo yake ya darasani. Wanafunzi wanahitaji kujihisi wapo salama ili waweze kujifunza kwa amani na matumizi ya viboko hayata fanya jambo hili kutokea.

Pili adhabu ya viboko husababisha athari za kisaikolojia, Wanafunzi wanaopata adhabu ya viboko mara kwa mara wata hukumbwa na athari msongo wa mawazo. Hii ni kwa sababu watahisi kudhalilishwa na sifa zao miongoni mwa wanafunzi wengine zitaathirika.

Kama tujuavyo wanafunzi wengi wanasoma mashuleni bado wako kwenye hatua ambayo mitazamo ya wenzao juu yao inawa athiri, na Wanahitaji kujisikia vizuri juu yao wenyewe. Kwa wale wanafunzi ambao huwa wanachapwa viboko kila mara huonekana kuwa watukutu na mara nyingi huonekana kutengwa na wanafunzi wenzao hiyo hali ya kutengwa na wanafunzi wenzao huathri hali yao ya kujiamini na kujithamini, jambo linalopelekea wajione kuwa kama watu wasiofaa.

Kwa kuongezea kutokana na adhabu za viboko baadhi ya wanafunzi hupatwa na dalili za wasiwasi kwasababu wanaogopa sana kuchapwa viboko.

Kesi ya mtoto John yaweza kuwa mfano mzuri kwenye hili. John amekuwa akiogopa sana kwenda shule kwani ni kwa muda sasa amekuwa akishuhudia marafiki zake wengi wakichapwa na walimu wao yeye binafisi ni mtoto mwema sana na ni ngumu mno kumkuta akiwa kwenye makosa. Hata hivyo kitendo cha kuwaona marafiki zake wakiadhibiwa kwa viboko kimemsababishia athari kubwa akilini mwake. Anapokuwa shuleni, John hawezi kuzingatia darasani kwasababu tu anamuogopa mwalimu.

Hii inamaana kwamba watoto wadogo wanaweza kuwa na aina Fulani ya ‘athari ya kiwewe’ wanapoona marafiki zao waki-adhibiwa kwa viboko. Athari hizi za kisaikolojia zinapelekea kuwa na ufaulu mdogo miongoni mwa wanafunzi waliyoadhibiwa pamoja na wale walio shuhudia adhabu ikitolewa.

Licha ya hayo matumizi ya viboko mashuleni hujenga chuki kati ya wanafunzi na walimu wao kwa wale wanafunzi wakorofi huwenda wakawa wakorofi Zaidi na kumchukia aliyewaadhibu jambo ambalo linaweza kuwasukuma wanafunzi waanze kuonyesha tabia zisizofaa ikiwa ni pamoja na kutosikiliza darasani na kuwa sumbua wenzao wakati masomo yakiendelea kama njia ya kulipiza kisasi kwa walimu hao.Jambo linaloathiri ufaulu wa wanafunzi.

Licha ya athari zote mbaya zilizotajwa hapo juu bado kuna watu ambao wanataka adhabu ya viboko itumike mashuleni wanadai kuwa adhabu ya viboko husaidia kupunguza tabia mbaya za wanafunzi. Wanasema kuwa kwa kumuadhibu mtoto kwa fimbo humsaidia kugundua athari za makosa yake na hivyo hivyo hatarudia utovu wake wa nidhamu. Na mwishowe atajifunza kutenda ipasavyo. Na ikiwa ni kweli kwamba adabu ya viboko ni mbaya kwa wanafunzi inakuwaje inaendelea kutumika?

Kabla ya kujibu maswali haya naomba itambulike kuwa mpaka sasa kuna nchi zaidi ya 130 ambazo zimepiga marufuku matumizi ya viboko shuleni, hii inaonyesha kuwa kadiri ambavyo watu wanazidi kuelimika ndivyo ambavyo wana achana na mazoea haya ya kuwa-adhibu watoto kwa viboko na hii ni kutokana na athari zinazo tokana na njia hii ya kuwa-adhibu wanafunzi. Na kama kweli lengo ni kujenga nidhamu ya wanafunzi kuna njia nyingi za kulishugulikia jambo hilo fimbo sio njia pekee ya kujenga nidhamu kwa wanafunzi na kama haitoshi matumizi ya fimbo yatawafanya wanafunzi wafuate sheria kwa sababu tu wanaona adhabu kama tishio na si kwa utashi wao wenyewe.

Kwa kumalizia, kama lengo la kuwadhibu mototo kwa kutumia fimbo ni kumjengea nidhamu basi njia hii haifai kutumika kwani ina madhara mengi kuzidi faida na mbaya Zaidi inamjengea mtoto nidhamu ya uoga badala ya kumjengea nidhamu binafsi hali inayokuja kuriadhiri taifa badaye hasa kwenye soko la ajira kwani kupitia njia hii tunajenga taifa la watu ambao hawawezi kujiongoza na kujisimamia hata linapokuja kwenye swala la ajira tunatoa watu wanofanya kazi pale tu ambpo bosi akiwepo asipokuwepo kazi haziendi jambo linalofanya tusiajirike.

Licha ya hayo, matumizi ya viboko yataunda mazingira yasiyofaa ya kujifunzia. Hali inayosababisha athari za kisaikolojia kwa wanafunzi, na kuongeza tabia ya ukatili ya wanafunzi. Inapotosha kabisa madhumuni ya mwanafunzi kwenda shule ambayo ni kupata elimu katika mazingira rafiki na yenye afya bila kuhisi tishio.

Adhabu ya viboko haifai hata katika kupunguza tabia mbaya za wanafunzi. Kwa hivyo, inapaswa kupigwa marufuku kwani athari zake mbaya ni nyingi kuliko faida. Aidha, adhabu ya viboko sio njia pekee ya kushughulikia matatizo ya kinidhamu. Hivyo walimu wetu wanapaswa kujifunza kwa nchi zilizo jikomboa na janga hili.
 

Attachments

  • to send jf.pdf
    437.4 KB · Views: 15
  • to send jf.docx
    67.5 KB · Views: 5
Ila kuna wanafunzi bila viboko hawatulii, ila pia viboko vimewasaidia wanafunzi wengi kufaulu, kuliko kuondoa kabisa ni bora kuweka njia bora ya kutoa adhabu hii bila kuleta madhara kwa mwanafunzi
 
Ila kuna wanafunzi bila viboko hawatulii, ila pia viboko vimewasaidia wanafunzi wengi kufaulu, kuliko kuondoa kabisa ni bora kuweka njia bora ya kutoa adhabu hii bila kuleta madhara kwa mwanafunzi
ni kweli ila kuna inchi kama southafrica ambayo yenyewe haitumii adhabu za vipoko kujenga nidhamu kwa wanafunzi na bado inafanya vizuri kielimu na kinidhamu so kama watanzania tunamengi ya kujifunza
ila hata hilo wazo lako linafaa kwa kuanzia
 
Back
Top Bottom