Adhabu bungeni zinachochea mpasuko nchini

Return Of Undertaker

JF-Expert Member
Jun 12, 2012
4,572
26,868
Adhabu bungeni zinazochochea mpasuko




adhabu_pic.jpg

Matarajio ya wageni wanaotembelea Bunge kama hawa na watu wengine nje ya Bunge ni kuona haki na usawa vikitawala ili kukidhi matarajio yao. Picha ya Maktaba

Kwa ufupi
MSIMAMO WA BUNGE

> Uongozi wa Bunge haujakaa mkimya. Naibu Spika, Dk Tulia Ackson anajibu malalamiko akisema ndani ya Bunge hakuna anayebaguliwa.

“Wabunge humu wana hadhi na wengine. Wote wako sawa kwa mujibu wa kanuni, sheria na Katiba na ndicho ambacho kinapaswa kukumbukwa. Ndiyo maana wote huwa wanapewa fursa zinazofanana na hakuna anayependelewa wala anayeonewa.

Mbali na msimamo wa Naibu Spika, Spika wa Bunge, Job Ndugai anaeleza kukerwa na wapinzani kususia futari iliyoandaliwa na Waziri Mkuu kutokana na mpasuko uliopo na hivyo kuja na suluhisho.

“Lakini nimejifunza kitu kimoja ambacho sikupenda kukisema ila nikiseme hapa kidogo. Kuna wenzetu wamekatazana rasmi kuhudhuria shughuli kama hizi.”

By Sharon Sauwa, Mwananchi; ssauwa@mwananchi.co.tz
Mtindo wa kuitwa mbele ya Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kwa wabunge wa upinzani, hasa Chadema katika Mkutano wa Saba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeacha vidonda katika uhusiano wa kisiasa wa pande mbili ndani ya mhimili huo.

Vidonda vya chuki, uhasama na kukamiana vilijidhihirisha wazi katika mijadala mbalimbali ndani ya Bunge na hata kwenye uhusiano nje ya Bunge, jambo ambalo kama halitafanyiwa kazi huko tuendako hali inaweza kuwa mbaya zaidi.

Mathalan, halikuwa jambo la kawaida kwa wapinzani kususia futari iliyoandaliwa na Waziri Mkuu (kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni) na iliyoandaliwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai kutokana na kile wanachodai “mambo wanayofanyiwa bungeni”.

Achana na hilo, kutokana na hali iliyopo kuna wabunge lukuki walioonja chungu ya adhabu za Bunge baada ya kufikishwa katika kamati hiyo, miongoni mwao ni Halima Mdee (Kawe) na Ester Bulaya (Bunda Mjini) wanaotumikia ‘kifungo’ cha mwaka mzima cha kutohudhuria vikao. Wengine ni Joshua Nassari (Arumeru Mashariki), Severina Mwijage (Viti Maalumu) na John Mnyika (Ubungo) wote kutoka Chadema.

Mbali na ‘kifungo’ cha mwaka mmoja kwa Mdee hivi sasa ana mashtaka mapya kutokana na mkutano wake na wanahabari alioufanya hivi karibuni. Wabunge wengine wanane wa Chadema wanapelekwa kwenye kamati hiyo wakituhumiwa kutaka kumshambulia Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Juliana Shonza.

Wabunge hao ni Saed Kubenea (Ubungo), Pauline Gekul (Babati Mjini), Cecil Mwambe (Ndanda), Joseph Selasini (Rombo), Cecilia Pareso (Viti Maalumu), Suzan Kiwanga (Mlimba) na Frank Mwakajoka (Tunduma).

Adhabu na mpasuko

Kutokana na michango hiyo na hali ilivyo bungeni, ni vigumu kutenganisha mpasuko unaoanza kujijenga ndani ya chombo hicho na adhabu zinazotolewa kwa wabunge wa upinzani. Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara amewahi kueleza wazi katika majadiliano bungeni kwamba kuna mpasuko baina ya wabunge wa CCM na upinzani.

Akichangia Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa Mwaka 2017, Waitara anasema kuna mtindo umeanza kuzoeleka kwa wabunge wa CCM kujibu hoja za wabunge wa upinzani kama vile wao ndiyo Serikali.

“Tunapotoa hoja tunatarajia aliyeleta hoja ajibu, wabunge wa CCM nyie mmejigeuza wasemaji wa Serikali,” anasema.

Hata pale Bunge lilipokaa kama Kamati ya Bunge kupitisha muswada huo, mbunge huyo aliamua kuondoa marekebisho aliyokuwa amewasilisha akidai hayatapita kutokana na ubaguzi uliopo.

“Mapendekezo yangu yote nayafuta, najua hayatapita kutokana na mambo yanayoendelea humu ndani ya kiubaguzi kwa kutowasikiliza wabunge wa upinzani,” anasema.

Makosa vs kanuni

Makosa yanayoonekana kuwaponza wabunge wengi wa upinzani ni ya kusema uongo bungeni na kudharau kiti cha Spika ambayo yameelezwa katika kanuni za Bunge na adhabu za kuchukua.

Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ndiyo iliyopewa madaraka ya kusikiliza mashauri ya wabunge na kutoa mapendekezo yake kisha kuwasilisha ndani ya Bunge zima kwa ajili ya kutolewa uamuzi.

Hata hivyo, kuna kanuni zinazompa madaraka Spika kutoa adhabu bila kupitia katika kamati, ikiwamo kanuni ya 63(8).

Kanuni hiyo inasema mbunge aliyepewa muda wa kuthibitisha jambo alilolisema bungeni hadi mwisho wa siku (aliyopewa) hajafanya hivyo, atashindwa ama atakataa kutoa uthibitisho kwa kiwango cha kuliridhisha Bunge na kama atakataa kufuta kauli yake, basi Spika atamwadhibu kwa kumsimamisha kuhudhuria vikao visivyozidi vitano.

Pamoja na adhabu ya kamati, kanuni ya 63(9) inampa nafasi mbunge mwingine yeyote atakayeona uongo uliosemwa na mbunge bungeni ni mkubwa kiasi cha kuathiri heshima ya Bunge, kutoa hoja kwamba mbunge huyo ikiwa ni kosa lake la kwanza basi asihudhurie vikao visivyozidi 10.

Pia, mbunge anaweza kutoa hoja na ikiwa ni kosa lake la pili asihudhurie vikao visivyozidi 20 au achukuliwe hatua nyingine za kinidhamu zitakazotajwa katika hoja yake.

Kanuni zinaelezea kuhusu amani na utulivu bungeni wakati shughuli zinazoendelea zimetoa mwongozo kwa ajili ya kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri.

Kanuni ya 72(1) inatamka kuwa Spika atakuwa na wajibu wa kuhakikisha kuwa utaratibu bora unafuatwa bungeni na uamuzi wa Spika kuhusu jambo lolote kuhusu utaratibu utakuwa ni wa mwisho.

Kanuni 74 (1) inasema Spika anaweza kutaja jina la mbunge kwamba amedharau mamlaka ya Spika na kisha kupeleka jina hilo kwenye kamati ya haki, maadili na madaraka ya Bunge.

Adhabu zinazotajwa chini ya kanuni hiyo iwapo mbunge amethibitika kufanya kosa kwa mara ya kwanza ni kutohudhuria vikao vya Bunge visivyozidi 10 na ikiwa ni kosa lake la pili au zaidi mbunge huyo asihudhurie vikao vya Bunge visivyozidi 20.

Kanuni zina tija?

Mbunge wa Vwawa (CCM), Japheth Asunga anasema kanuni zinasaidia kwa kiwango kikubwa isipokuwa hazitoshelezi na kinachohitajika ni vyama kuzingatia mafundisho na maadili.

“Kwa sababu vyama vinatakiwa vitoe elimu kwa wabunge wao namna ya kuzingatia maadili kufuata taratibu, jinsi ya kuenenda kwa upinzani jinsi ya kujenga hoja, kuheshimu mawazo ya mtu na vitu vinginevyo,” anasema.

“Kumejitokeza wabunge wengine ambao wameanza kuwashambulia watu binafsi. Hakuna sababu ya kushambulia watu, wewe jenga hoja yako, elezea kama umefanya utafiti na kikubwa ambacho mimi nakiona ni kwamba wabunge tulio wengi hatufanyi utafiti wa kutosha ilikuwa na taarifa kamili.”

Anasema suala hilo linawafanya wabunge wanapoongea wanafanya kwa kubahatisha na bila kuzingatia kanuni, hapo ndiyo tunasababisha matatizo.

Kuhusu adhabu, anasema, “Adhabu zinazotolewa zinaenda kikanuni, unajua kanuni zetu ziko wazi zinasema ukifanya kosa la kwanza, ukifanya kosa la pili na la tatu. Sasa unapokuwa umemaliza zile adhabu zote zimekwisha ambazo zimewekwa kikanuni hapo ndiyo shida,” anasema.

Kuhusu adhabu hizo kujenga mpasuko baina ya wabunge na jamii, Asunga anasema ni kweli zinaleta mpasuko lakini kuna haja vyama vya siasa kusimamia zaidi maadili.

“Kule tunakuwa na wasimamizi wetu hao sasa ndiyo wasimamie zaidi maadili ya vyama kwa wabunge, bila kufanya hivyo licha ya kuwapo kwa kanuni bado kukiuka kutaendelea kuwepo. Lakini chama kikisema hiki msifanye hiki mfanye watu wengi watazingatia haya,” anasema.

Anazungumziaje malalamiko kuwa wabunge wa CCM hawaadhibiwi pale wanapofanya makosa sawa na wenzao? “Hili halina ukweli, sijawahi kuona mbunge wa CCM akiambiwa akae chini anapofanya jambo linaloenda kinyume anakiuka maadili, yeye anakataa.

Mbunge wa Vunjo (NCCR Mageuzi), James Mbatia anasema wakati wanaanza vikao vya Bunge wamekuwa wakianza na dua wakimuomba Mungu awape hekima na busara za kufanya uamuzi.

“Hatumwambii ee Mwenyezi Mungu utujalie Katiba wala kanuni za kufanya uamuzi, hatujaomba tutumie kanuni wala katiba kufanya uamuzi, tunasema hekima na busara. Kwa hiyo hekima ndiyo pekee itakayoleta utukufu wa Mungu na linaitwa Bunge tukufu,” anasema.

Mbatia anasema hekima na busara inazidi sheria, kanuni na Katiba lakini kuna mambo mengine badala ya kutumia hekima na busara wanakimbilia katika kanuni.

“Ndiyo maana kanuni, sheria na Katiba inatungwa kila leo lakini zinavunjwa, lakini hekima na busara zinaleta watu pamoja. Hekima na busara zinasababisha watu kuaminiana.”

“Hata tukibadilisha kanuni zinafaa au hazifai, utaratibu wetu hivi sasa ili mbunge aingie bungeni lazima apitie chama cha siasa. Ninashauri meza ya mazungumzo kwa vyama vya siasa vilivyo na uwakilishi bungeni vione namna bora ya kuzungumza na wale wanaowawakilisha bungeni ili kuleta muafaka.”

Mbatia anasema jukwaa la mazungumzo ni muhimu na litaleta maridhiano na kwamba hilo si jambo geni, liliwahi kufanywa katika Bunge la 10 chini ya Spika Anne Makinda. Tutumie TCD kuleta maridhiano Bungeni,” anasema.
 
Back
Top Bottom