‼️WAKILI UCHWARA

CHAGOSI GERALD

Senior Member
Joined
Jan 25, 2020
Posts
162
Reaction score
284
Katika jamii yoyote inayojitambua, wakili ni zaidi ya mtaalamu wa sheria—ni mhimili wa maadili, sauti ya wanyonge, na mlinzi wa utu. Lakini leo, mbele yetu amesimama kiumbe mpya: wakili msomi, mfanyabiashara wa haki. Ni msomi aliyeapa kulitumikia taifa kwa uadilifu, lakini ameigeuza taaluma yake kuwa soko la maneno ya kifahari, vifungu vya sheria na vifungu vya benki.

Wakili huyu hana tofauti na mfanyabiashara wa sokoni. Tofauti ni kuwa bidhaa yake ni haki. Yuko tayari kuipima haki kwa bei. Haki ya masikini ina thamani ya kidogo, haki ya tajiri inaweza kupindisha sheria nzima. Siyo tena juu ya usahihi wa hoja, bali uwezo wa mteja wake kulipa vizuri. Anaweza kuigeuza dhambi kuwa uhalali, na kosa kuwa ushindi wa kisheria—mradi tu malipo yawe mazuri.

Wapo waliopata elimu ya sheria kwa jasho la walala hoi, wakasomeshwa ili siku moja wawe walinzi wa utu. Lakini sasa wamekuwa mawakala wa mabwanyenye, wakitumia ujuzi wao kuwanyonya waliowalisha. Wanapokea kesi, si kwa nia ya kusaidia, bali kama zabuni ya biashara: “Nani analipa zaidi, ndiye mwenye haki.”

Kwao, dhana ya "kumtetea asiye na sauti" ni hadithi nzuri ya kuandika kwenye wasifu, si mazoea ya maisha. Wanaweza kushawishi jaji kuipinda sheria, mradi malipo ya ‘consultation’ yapite milioni moja.

Mawaziri wanavunja sheria hadharani. Wakuu wa taasisi wanawabana raia bila msingi wa kisheria. Lakini cha kushangaza, mawakili na wasomi wa sheria wapo kimya. Au wakiongea, ni kwa lugha ya kuficha maovu kwa istilahi tata na hoja zenye kupindisha mantiki. Wakili msomi leo si mwalimu wa taifa, bali mpambe wa watawala.

✔️Sheria Bila Maadili ni Upofu.
Sheria inayotumika bila dhamira ya kiutu siyo sheria bali ni chombo cha mateso. Taaluma ya sheria ni kama upanga—ikishikiliwa na mwenye dhamira safi, inaleta haki; ikishikiliwa na mwenye tamaa, inaleta maafa. Wakili msomi anapogeuka kuwa mfanyabiashara wa haki, anageuza upanga huo kuwa chombo cha kukata maisha ya watu.

Katika mahakama zetu leo, haki haipatikani kwa ushahidi, bali kwa uwezo wa kumudu huduma ya wakili anayejua "namna ya kuzungumza na mfumo." Mtuhumiwa maskini ataendelea kuozea rumande bila kesi kusikilizwa, ilhali mfanyabiashara mwenye kosa kubwa anatembea huru kwa kuwa na wakili ‘mahiri’. Na ni nani huyo? Ni msomi aliyetarajiwa kuwa mkombozi wa taifa, lakini amejiuza kwa bei ya soko.

Wakili msomi aliyepoteza dhamira ni hatari zaidi kuliko jambazi wa mtaani. Jambazi huiba kwa siri, lakini wakili huyu huiba kwa kisingizio cha sheria. Tunahitaji kizazi kipya cha mawakili watakaothubutu kuwa sauti ya waliopokwa, watakaochagua njaa kuliko hongo, na ambao wataona haki si bidhaa bali ni wajibu mtakatifu.

Kwa sababu katika dunia ya sasa—wakati mwingine, haki inalia si kwa kukosekana kwa sheria, bali kwa sababu msomi aliyepaswa kuilinda, ameigeuza kuwa biashara ya kifahari.
 

Attachments

  • @Chagosi Gerald_20250522_151441_0000.png
    2.4 MB · Views: 17
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…