NIAJE aisee, wanasemaje waungwana hapo, pole kwa starehe za hapa na pale, wape hi ‘kakaz' na ‘dadaz', waambie tupo pamoja kama kawaida, kama vipi ‘nitawaibukia' kimtindo tuzungumze yanayotuhusu.
Mungu ni mwema, ninamshukuru kwa zawadi ya uhai, maisha yanaendelea, mwaka ndiyo huooo, ilikuwa Januari sasa Septemba.
Hongera wote mliohitimu elimu ya msingi, nashawishika kuamini kuwa, mlichokipata kinafanana na hiyo inayoitwa elimu ya msingi, kwamba mmepata msingi wa kuwawezesha kujitegemea na si ufahamu wa ‘kupiga mizinga', kushinda vijiweni na kuwa mzigo kwa ndugu, jamaa na marafiki.
Kama wewe ni miongoni mwa hao tambua kwamba, umefungua ukurasa mpya wa maisha yako, itumieni vizuri likizo ya JK kufikiria itakuwaje baada ya matokeo kama hautajiunga na shule ya sekondari, wakati ni huu, biashara asubuhi, jioni mahesabu.
Nafahamu ni kipindi chenye changamoto nyingi hasa kwa walio vijijini kwa kuwa baadhi yao wanalazimika kupambana na changamoto za familia zinazothamini mali badala ya elimu, kiasi cha kuuliza mabinti zao kuwa wanasoma ili iweje, darasa la saba linatosha, waolewe.
Ni bahati mbaya sana, wasichana wenye wazazi kama hao wanaishi kwenye mazingira yasiyowezesha kupanua upeo wao wa kuelewa madhara ya kuolewa utotoni, elimu wanayopata wenzao wa mijini kupitia vyombo vya habari kwao ni anasa.
Mabinti mjini wana upeo fulani unaowawezesha japo kuthubutu kuuliza hiki na kile, na wengine wanaweza kujenga hoja kutetea kile wanachoamini kuwa ni sahihi hata kama wanachemka.
Mliohitimu mnapaswa kutambua kuwa, mlikuwa kule sasa mnahamia huku kwenye gari kubwa liitwalo Mtaani Kwetu, linalobeba walionacho na fukara, wenye vijisenti na ombaomba, waajiriwa, vibarua, wanaotafuta kazi, wezi, majambazi, matapeli, vibaka, na wengine wanaoishi kiujanja ujanja.
Jamaa aliongea na Ridhiwani kufikisha ujumbe kwa ‘mshua', kwamba mtaani ‘kimenuka', na mfumo wa maisha yako ni ujumbe tosha kwa wenye kuthamini uwepo wa kundi kubwa la wenye umri kama wako, wenye kuamini kuwa vijana ni taifa la leo, si kesho.
Tafuta namna ya kupeleka ujumbe chanya kwenye jamii kwamba, elimu uliyoipata imekuwezesha kupanua upeo wako wa kufikiri, ni raia mwema, nguvu kazi muhimu kwa Taifa la Tanzania.
La mwisho lakini si kwa umuhimu, dada zangu mliohitimu elimu ya msingi, mnapaswa kutambua namna mlivyo kwenye hatari ya kuangamia kwa sababu ya umri wenu, wanaotamani wamejaa mitaani, chondechonde, ngono nomaa, ukilegeza utanasa.
Dunia ‘imechafuka' na ni bahati mbaya sana kwenu kwa kuwa hata wenye umri sawa na baba zenu wajiita ‘bebi', wanaukataa uzee, nao wanataka ‘kupiga shoo' a.k.a mechi za kirafiki.
Mabinti mnapaswa kuelewa kuwa, wengi wanawataka ni mafataki, ni chovya chovya tu, hawana upendo wa dhati kwenu, wanawatamani kwa sababu mpo kwenye ' mvuto time', wanataka waonje wasepe.
Chanzo:Habari Leo