Nililisoma ngumbaru, shairi langu sikia
Kijiji Nangurukuru,Mbaazi kupalilia,
Bila kusahau Masuguru, kwa bibi binti Rupia.
Lima Mkulima lima , lima upate mradi.
Lima lima mwana kwetu, lima mkulima lima,
Lima uupate utu, ukamilishe huduma
Lima bila gutugutu,njaa isipate dhima,
Lima lima mwana kwetu , lima Mkulima lima
lima Tanga na Tabora, lima Mbeya na Ruvuma
Lima tusije dorora, lima Singida mapema,
Morogoro na Mtwara , msichelewe kulima
Lima mkulima lima , lima upate mradi.
Lima Arusha Manyara,Iringa pia Tunduma.
Lima Mwanza na Kagera,Lima ulie Kigoma,
Limeni Mazao bora, Kilimanjaro Dodoma
Lima Mkulima lima ,lima upate mradi.
Lima Geita na Njombe,Lima mazao Mtama,
Simiyu shikeni Jembe,msidharau kulima.
Wa Pwani pia mtambe,kama Mzee Mwilima.
Lima lima mwana kwetu , lima mkulima lima.
Katavi Rukwa na Mara,acheni kurudi nyuma,
Kumbe hasira hasara,mmesahau kulima,
Msije pata hasara, Mvua itaja goma,
Lima mkulima lima, lima upate mradi.
Lima Mahindi Mpunga,chai Miwa Maharage,
Nyanya Matunda Karanga,Lima kahawa Mkonge,
Choroko Njegere panga, sokoni bei wapange.
Lima mkulima lima, lima upate mradi.
Kaditama na tamati, hapa ninamalizia,
Nalifunga langu Shati, Makobazi kuvalia,
Bila kusahau Koti,Babu aloniachia.
Lima mkulima lima, lima upate mradi.