April 13, 2016
Turiani Morogoro
Tanzania
Matokeo mechi ligi ya VPL (Vodacom Premier League) Mtibwa 0 - Azam FC 1
By ppkahemele
Azam FC, imezidi kufufua matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kuichapa Mtibwa Sugar bao 1-0 katika Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro jioni ya leo.
Ushindi huo wa Azam FC umekuja wakati ikitoka kupata sare mbili mfululizo kwenye mechi zilizopita za ligi dhidi ya Toto Africans (1-1) na Ndanda (2-2).
Shukrani za kipekee ziende kwa nahodha John Bocco ‘Adebayor’ aliyefunga bao hilo pekee kwa njia ya mkwaju wa penalti na kuihakikishia Azam FC pointi zote tatu muhimu ugenini. Ushindi wa Azam umeifanya kufikisha jumla ya pointi 55 katika nafasi ya tatu, ikizidiwa pointi mbili na Simba inayoongoza kileleni na pointi moja dhidi ya Yanga, ambayo ipo nyuma mchezo mmoja.
Kikosi cha Azam FC kwa mara ya kwanza kwenye ligi, leo kilikuwa bila beki kisiki Pascal Wawa, ambaye amekusanya kadi tatu za njano na akiwa katika programu ya kuwekwa fiti kwa ajili mchezo ujao dhidi ya Esperance, nafasi yake ilichukuliwa na Racine Diouf.
Dakika ya 16 beki wa Mtibwa Sugar, Andrew Vincent ‘Dante’ alifanya kazi ya ziada kuinyima bao Azam FC baada ya kuokoa mpira kwenye mstari kufuatia kichwa kilichopigwa na Bocco, aliyetumia uzembe wa kipa wa Mtibwa Sugar, Said Mohamed aliyeuokoa vibaya mpira wakati akiruka naye juu.
Azam FC wangeweza kuondoka na mabao mawili kipindi cha kwanza kama wachezaji wake Kipre Tchetche na beki Racine Diouf wangekuwa makini kutumia nafasi walizopata na hivyo .
Hadi mapumziko timu hizo zilikuwa hazijafungana Kipindi cha pili kilianza kwa benchi la ufundi la Azam FC chini ya Stewart Hall, kufanya mabadiliko ya kutoka Diouf na nafasi yake kuchukuliwa na Abdallah Kheri, lengo likiwa ni kuimarisha eneo la ulinzi.
Dakika ya 61 Tchetche alifanya kazi ya ziada kumkimbiza Andrew Vincent ‘Dante’ wa Mtibwa Sugar na kupiga krosi ya hatari pembeni kidogo ya eneo la 18 na beki huyo alijikuta akiunawa mpira huo katika harakati za kuokoa na mwamuzi Alex Mahagi kutoka Mwanza kuamuru penalty ipigwe langoni mwa Wakata miwa hao.
Dakika ya 90 mwamuzi Mahagi alimuonyesha kadi nyekundu kiungo wa Azam FC, Himid Mao.baada ya kumuonyesha mwamuzi kutokukubaliana na namna alivyofanyiwa na watu wa huduma ya kwanza waliompandisha vibaya kwenye machela kufuatia kudondoka chini kufuatia kupigwa usoni na mchezaji wa Mtibwa Sugar.
Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitaanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam kesho saa 1 asubuhi na mara moja kitafikia kambini kwa ajili ya kujiandaa na mchezo ujao wa marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika CAF CF dhidi ya Esperance Sportive de Tunis utakaofanyika jijini Tunis,Tunisia Aprili 19 mwaka huu.
Kikosi cha Azam FC leo:
Aishi Manula, Wazir Salum, David Mwantika, Aggrey Morris, Racine Diouf/Abdallah Kheri dk 46, Himid Mao, Michael Bolou/Jean Mugiraneza dk 82, Frank Domayo, Ramadhan Singano, John Bocco, Kipre Tchetche/Allan Wanga dk 79
Source:
Azam FC yaibwaga Mtibwa Manungu | The Official Website of Azam Football Club