Dar es Salaam. Hali si shwari ndani ya
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
kumebainika kuwa mgogoro baina ya
watendaji wa shirikisho hilo.
Habari za ndani zinaeleza, rais wa TFF,
Jamal Malinzi amewekwa kiti moto baada ya
kudaiwa kuwabadilisha watia saini wa benki
huku Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) ikianza kuwahoji baadhi
ya viongozi wa shirikisho hilo.
Ingawa Takukuru haikuwa tayari
kulizungumzia suala hilo, lakini habari zaidi
zinasema viongozi kadhaa wa TFF
wamehojiwa na Taasisi hiyo wakihusishwa
na matumizi mabaya ya fedha za shirikisho
hilo.
Mbali na Takukuru, pia imeelezwa kuwepo
kwa maelewano mabaya baina ya viongozi
wa Kamati ya Utendaji ya TFF huku kikao
cha Machi 26 kikipangwa kutumika kumuhoji
Malinzi juu ya madai ya kughushi muhtasari
na kubadili watia saini.
Baadhi ya wajumbe katika kikao hicho
wameeleza kutojua ajenda ingawa tayari
wamepokea barua za wito wa kikao.
Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas ilisema
jana kuwa kikao kitafanyika Dar es Salaam
na ajenda kuu itakuwa kupanga tarehe ya
uchaguzi mkuu wa shirikisho utakaofanyika
baadaye Oktoba.
“Wataanza kufungua kikao, kisha mengineyo
na baadaye kufunga kikao, masuala mengine
yanayosemwa ni siasa hakuna chochote,”
alisema Lucas.
Makamu wa rais wa TFF, Walence Karia
alikiri kupewa taarifa za kikao, lakini
akasisitiza masuala mengine aulizwe katibu
mkuu, Celestine Mwesigwa.
“Habari za kughushi muhtasari na kubadili
watia saini wa benki mimi siwezi
kulizungumzia, hilo ni suala la Katibu Mkuu
kwanza silifahamu,” alisema Karia kwa
kifupi.
Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa
alipotafuwa alisema yuko na majukumu
mengine hawezi kuzungumza chochote.