Hii nayo ni habari nzuri.
Wakiwa wengi wanatua Tanzania, bei zinaweza kushuka na hivyo kuvuta watalii wengi kuja kwani ikifika peak, bei zinakwenda juu hadi zinakatisha tamaa. I hope watakuja wengi au niseme watarudi wengi. Sijui LUFTHANSA wameishia wapi? Miaka hiyo ukienda DIA utawaona wengi sana wakitua na wakati wa Mwinyi wakakimbia karibu wote. Nafikiri Tanzania inarudi kidogokidogo kwenye barabara.
Egypt Air kurejesha safari zake nchini
Mwandishi Wetu
Daily News; Tuesday,March 03, 2009 @07:38
Kukua kwa sekta ya utalii na usafiri wa anga nchini kumelihamasisha Shirika la Ndege la Misri (Egypt Air) kuanza safari zake tena baada ya kuacha kuja nchini Aprili 2004. Akizungumza na wadau wa usafiri wa anga, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Meneja wa Shirika hilo nchini, Wael Eldemerdash, alisema shirika hilo limeamua kurudisha safari zake baada kubaini kuwa sekta ya utalii inakua kwa kasi na hivyo itachangia shirika lake kufanya biashara nzuri wakati huu.
"Kukua kwa sekta ya utalii na biashara nchini, kumetusukuma kuanzisha safari za ndege zetu nchini ili kuongeza kasi ya watalii kutoka Misri kuja Tanzania na wafanyabiashara kuja kuwekeza nchini," alisema Eldemerdash.
Katika utafiti waliofanya kwa mwaka mmoja, walibaini kuwa sekta ya utalii nchini inakua kwa kasi, hivyo shirika lake pamoja na kuanza safari, litaanzisha mpango wa ushirikiano na Shirika la Ndege la Tanzania ili kufanya biashara ya usafiri wa anga vizuri na kwa pamoja.
Shirika hilo ambalo litaanza safari zake Juni mwaka huu, limeboresha huduma zake kwa kuleta ndege kubwa na kuongeza safari kutoka moja ya wakati ule hadi nne ambazo zitakuwa Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumapili kila wiki. Kwa kuanzishwa safari hizo, meneja huyo anaamini litaongeza idadi ya watalii kutoka nchi za Mashariki ya Kati na za Kiarabu kuja nchini kwa gharama nafuu, ambapo awali watalii kutoka nchi hizo walihitaji ndege mbili au zaidi ili kutua katika ardhi ya
Tanzania kwenye Uwanja wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam. Balozi wa Misri nchini, Hael Adel Nass, alisema kuanzishwa kwa safari kati ya Cairo na Dar es Salaam, kutaongeza na kukuza biashara ya utalii kati ya nchi mbili hizi ambazo zitakuwa zikitembeleana mara kwa mara.
Kuanzishwa safari ya shirika la ndege hiyo nchini, kutaongeza pia kasi ya uwekezaji katika sekta ya utalii na katika sekta nyingine zikiwamo za biashara ambazo zitapatikana nchini. Naye mdau wa shirika hilo nchini, Mustafa Rajani alisema, Watanzania na Wamisri watapata fursa nyingine ya kutembeleana bila kuzunguka, kama ilivyokua nyakati zilizopita