Mheshimiwa Spika, Rushwa hii imekuwa ikiwaumiza sana wananchi wa kawaida ambao wamekuwa wakikosa huduma na hasa kwa kuwa hawana fedha za kuwahonga maafisa wa polisi. Hali hii imepelekea hata baadhi ya wananchi kubambikiwa kesi mbalimbali kwa makusudi kwasababu tu wanakuwa hawana fedha za hongo kwa polisi na hata wengine wamekuwa wakijichukulia sheria mkononi kwa kujua jeshi la polisi haliwezi kuwatendea haki. Hivi sasa kuna msemo maarufu, "kuingia kituo cha polisi ni bure, ila kutoka ni pochi". Hii ni aibu kubwa kwa Jeshi la Polisi na Serikali. Badala ya kuwa Jeshi la kulinda usalama wa raia na mali zao, sasa vituo vya polisi vimekuwa ni pango la kufanyia biashara ya rushwa na hongo.
Mheshimiwa Spika, rushwa pia imekithiri ndani ya vitengo vyote vya Wizara ya Mambo ya Ndani kama vile Idara ya Magereza, Kikosi cha Zimamoto, na Polisi Usalama Barabarani (Traffic). Kibaya ni kuwa rushwa hii ni ya kitaasisi, kwani hata raia wema wanapopenda kutoa taarifa kuhusiana na kuombwa rushwa hujikuta wakiwa kwenye wakati mgumu zaidi badala ya kupatiwa msaada.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kuwa vipato vidogo, maslahi duni na maisha ya umaskini ya askari wetu wakiwemo wale wa Idara ya Magereza, vinachangia kwa kiasi kikubwa cha rushwa ndani ya Jeshi la Polisi. Pia, ukiukwaji mkubwa wa utawala wa sheria na maadili ya jeshi polisi ndio vinavyosababisha kushamiri matendo maovu na usaliti wa kweli, haki na utu ndani ya vikosi vya Jeshi la Polisi na idara zake zote.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Kambi rasmi ya Upinzani, inaitaka serikali na Bunge lako tukufu kuhakikisha maslahi ya walinzi hawa wa usalama wa raia na mali zao, yanaboreshwa kwa kiwango cha kuwafanya waone kwamba raslimali wanazolinda na raia wanaowalinda, wanathamini mchango na wajibu wao. Kwa kuzingatia umuhimu wa majeshi yetu ya Usalama wa Raia, Kambi rasmi ya Upinzani inataka mishahara ya askari wetu ipandishwe ili waweze kumudu gharama zote za msingi za kimaisha.
Mheshimiwa Spika, njia nyingine ni kuhakikisha utawala wa sheria ndani ya Jeshi la Polisi unaheshimiwa kikamilifu. Badala ya kuwahamisha vituo polisi wanaotuhumiwa na makosa mbalimbali ikiwemo kujihusisha na vitendo vya rushwa, Kambi rasmi ya Upinzani, inasisitiza kuwa ni lazima utawala wa sheria uheshimiwe kikamilifu. Yeyote anayebainika kujihusisha na rushwa achukuliwe hatua kali za kinidhamu na kisheria, ili kukomesha uhalifu huu.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inawataka Askari polisi wote wa nchi hii, wasikubali kutumiwa vibaya kukandamiza demokrasia na haki za wananchi, kwa maslahi ya kukibeba chama fulani cha siasa na badala yake watende haki kwa manufaa ya Watanzania wenzao. Wajue kuwa Watanzania wanaowafyatulia risasi, mabomu ya machozi na kuwapiga virungu, ni Watanzania wenzao. Ni sawa na Baba zao, Mama zao, Kaka zao au wadogo zao, kwa hiyo wasikubali kutumika vibaya kuua au kukandamiza ndugu zao. Badala ya kufanya hivyo, tunawashauri waishinikize serikali hii inayowatumia vibaya, iboreshe mishahara na maslahi yao.
Mheshimiwa Spika, Askari mmoja mwenye hekima wa nchini Ujerumani, wakati wa utawala wa Dikteta Adolf Hitler, aliwahi kusema, "Nilifarijika pale nilipofukuzwa kazi kwa kutokutii amri dhalimu inayokiuka haki na utu wa mwanadamu.... kwa sababu nilijua siku moja nitakufa na nitakuwa na wajibu mbele ya Mwenyezi Mungu. Nilikataa kuheshimu amri katili za wakuu wangu kazini, kwani Mwenyezi Mungu ni mkubwa kuliko wao". Kambi rasmi ya Upinzani, inawasihi polisi wote nchini wasikubali tena maagizo yote katili ya makamanda wao.
Mheshimiwa Spika, ili kuondoa malalamiko mbalimbali kuhusu ajira za polisi na maslahi yao mengine, Kambi rasmi ya Upinzani, inashauri serikali kufanya yafuatayo;i) Kuondoa utaratibu wa Askari polisi kuthibitishwa ajira yake baada ya kipindi cha miaka 12 ya sasa, na kuhakikisha ajira ya polisi inathibitishwa angalau ndani ya miaka 3.ii) Askari polisi wapandishwe vyeo kutokana na utumishi wao jeshini na vigezo viwe vya wazi, ili kuondoa malalamiko ya upendeleo.iii) Viwepo vigezo vya wazi katika kuwapanga Askari wetu kwenye vitengo mbalimbali, kwani hili linalalamikiwa sana kuwa sasa baadhi ya vitengo ni kwa ajili ya kundi fulani, huku wengine wakiwa wao ni kukaa vitengo hivyo hivyo mpaka wastaafu.iv) Ngazi za kupanda mishahara ziwe kama kwa watumishi wengine wa umma badala ya polisi wao kuwa na utaratibu wa kupanda vyeo. Pawe na vigezo ambavyo Askari akivifikia basi hata kama hajapanda cheo, basi ngazi yake ya mshahara nayo iongezeke.
Mheshimiwa Spika, hii itasaidia kuhakikisha kuwa Askari waliokaa muda mrefu wanakuwa na mishahara iliyoboreka na hata wakistaafu wanaweza kupata pensheni nzuri na hivyo kuweza kukabiliana na ukali wa maisha pindi wanapostaafu.
Mheshimiwa Spika, ili kuboresha zaidi utendaji wa Jeshi la Polisi na kuwatendea haki askari wetu, Kambi rasmi ya Upinzani inapendekeza kuwa utaratibu wa sasa wa polisi wa ngazi za chini kukatwa shilingi 5,000 kila mwezi kwenye mishahara yao, kwa ajili kugharamia mazishi yao na wategemezi wao, ufutwe mara moja, kwani hilo si jukumu lao, ni jukumu la serikali. Kambi rasmi ya Upinzani tunatoa msimamo wa kuitaka serikali ihakikishe inawarudishia askari polisi fedha zote ilizowakata kila mwezi kwa ajili ya mazishi, kwani haikuwa halali kufanyiwa hivyo.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inasisitiza, iwapo serikali haitawarudishia askari polisi pesa zao zote ilizowakata kila mwezi kwa madai ya kugharamia mazishi yao pindi wanapofariki, na iwapo utaratibu huu utaendelea; Kambi rasmi ya Upinzani inatangaza rasmi kwamba tutapanua ajenda yetu ya maandamano na kufanya pia maandamano nchi nzima ya kushinikiza pesa zote walizokatwa askari polisi warudishiwe na utaratibu huo ukome.
JESHI LA MAGEREZA
Mheshimiwa Spika, Mwezi Mei mwaka 2010, Chama cha wanasheria wa Tanganyika (Tanganyika Law Society) walichapisha ripoti ya matokeo ya ukaguzi katika Magereza waliyoifanya katika magereza 24 mwaka 2009. Ripoti hiyo inaeleza kuwa wafungwa walifanyiwa ukatili na kuteswa wakati wakiwa mahabusu, na pia kulikuwa na msongamano mkubwa katika magereza ya Dar es Salaam, Tabora, Arusha, Mara, Mwanza, na Tanga.
Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo pia ilidokeza kuwa katika gereza la Segerea kulikuwa na wafungwa 170 katika vyumba vya jela ambavyo vilijengwa kwa ajili ya watu 50, na katika Gereza la Ilagala mkoani Kigoma, wafungwa walilazimika kutembea zaidi ya maili 4 kwenda kuchota maji kwa sababu ya matatizo ya usafiri. Ripoti ilielezea kushindwa kwa gereza kuwapatia wafungwa huduma ya msingi ya usafi pamoja na chakula cha kutosha.
Mheshimiwa Spika, katika ripoti yake ya nusu-mwaka (2010), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, kimeeleza kuwa Idara ya Magereza imetumia takriban shilingi 650 kwa siku kwa ajili ya chakula kwa wafungwa, badala ya shilingi 2,420 ambayo ilikuwa imeidhinishwa na serikali. Kwa mantiki hiyo, uhaba wa chakula magerezani hautokani na uhaba wa fedha, bali unasababishwa na ufisadi wa fedha za chakula zinazoidhinishwa na Bunge hili. Kiasi kinachoidhinishwa sicho kinachotumika, fedha nyingi inabanwa na kuingia kwenye mifuko ya watu wachache.
Mheshimiwa Spika, serikali isiyojali wafungwa ni serikali katili. Kambi rasmi ya Upinzani haiko tayari kuvumilia ufisadi na ukatili huu unaofanywa dhidi ya wanadamu wafungwa. Tunataka kujua; Je, mpaka sasa ni Watumishi wangapi wachechukuliwa hatua ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Jeshi la Polisi na ndani ya Idara ya Magereza, kwa kufanya mchezo huu mchafu wa kutafuna fedha za chakula cha wafungwa? Pia, tunataka kujua serikali imejizatiti vipi kuhakikisha hali hii haijirudii tena.
MRADI WA VITAMBULISHO VYA TAIFA
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, uamuzi wa kuwa na vitambulisho vya taifa ulifikiwa kwa mara ya kwanza mwaka 1968, katika kikao cha Kamati ya Usalama cha Wakuu wa nchi za Afrika Mashariki na Kati, kilichohusisha Kenya, Uganda, Zambia na Tanzania. Kwa mantiki hiyo, imepita takribani miaka 43, tangu nchi hii iamue kuwa na vitambulisho vya taifa lakini hadi leo bado havijaanza kutolewa.
Mheshimiwa Spika, hakuna lugha yoyote nzuri ya kuuzungumzia ucheleweja huu isipokuwa kusema tu, serikali yetu imefanya uzembe na haina dhamira ya dhati ya kuhakikisha Watanzania wanapata vitambulisho vya taifa mapema.Pia ni vema ikazingatiwa kuwaMradi hu umechukua muda wa mwaka mmoja tangu tarehe ambayo Bodi ya Zabuni ya Wizara ilitoa idhini kwa ajili ya kazi ya ushauri na kusainiwa kwa mkataba wenyewe. Ucheleweshwaji wote huu, una athari katika kufikia na kutimiza malengo ya shughuli za mradi.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inashauri kwamba menejimenti ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa iongeze juhudi katika kuongeza kasi ya Mradi wa Vitambulisho vya Taifa kwa manufaa ya Taifa, angalau viwe tayari ifikapo mwaka 2014, ili pamoja na mambo mengine, Tume Huru ya Uchaguzi itakayoundwa, iangalie uwezekano wa kuvitumia kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ambalo katika uchaguzi mkuu uliopita lilionekana kuwa na dosari kubwa.
IDARA YA ZIMA MOTO NA UOKOAJI
Mheshimiwa Spika, Idara ya zima moto ni muhimu sana kwa usalama wa raia na mali zao, pindi majanga mbalimbali yanapotokea. Hata hivyo, taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali katika ukurasa wa 82, inathibitisha serikali haina sera ya usimamizi wa vihatarishi na namna ya kuvidhibiti. Kambi rasmi ya Upinzani inahoji, serikali inawezaje kunusuru maisha ya wananchi dhidi ya majanga kwa ufanisi, ikiwa hata sera yenyewe haipo?Kambi rasmi ya Upinzani inataka hatua za haraka zichukuliwe kuhakikisha vikosi hivi ambavyo vipo kwa ajili ya kusaidia jamii vinakuwepo katika kila sehemu ya nchi ili kushughulikia majanga mbalimbali yanayotokea wakati wa dharura kwa ufanisi.
Mheshimiwa Spika, wakati hakuna ufanisi wa kutosha katika kudhibiti na kushughulikia majanga, ripoti ya Mdhibiti naMkaguzi na Mkuu wa serikali, imegundua upotevu mkubwa wa fedha za umma, kiasi cha shilingi1,441,689,620 ambazo hazina maelezo ya kutosheleza na hivyo kusababisha hasara. Kambi ya upinzani tunaitaka serikali kuimarisha idara hii na pia kuwachukulia hatua waliohusika na ufisadi huu.
IDARA YA UHAMIAJI
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na ongezeko la wageni wengi kutoka nchi za nje na limekuwa jambo la kawaida, kiasi cha kujiuliza kama nchi hii ina utaratibu wowote wa kuratibu na kudhibiti uingiaji wa wageni hapa nchini. Imeripotiwa hata kwenye vyombo vya habari kuwa Mkoani Morogoro, katika kipindi cha Desemba 2009 hadi Februari 2010, raia wa Somalia 80 wanaoishi nchini kinyume cha sheria walikamatwa na Idara ya Uhamiaji.
Mheshimiwa Spika, kukamatwa kwa wageni hao ni uthibitisho wa namna tatizo la wahamiaji haramu lilivyo sugu na kubwa, kwani hao ni idadi ndogo tu kulingana na watu wanaoingia nchini bila kufuata taratibu za uhamiaji, na kuishia mitaani wakiishi na kufanya shughuli zao kama vile ni raia nchi hii. Mbali ya raia hao wa Somalia, pia wamo raia wa nchi zingine zikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda, Pakistan, Nigeria na China, India, Bangladesh, ambao wanaishi Tanzania kwa mfumo usio rasmi, bila ya kuwa na hati zinazowaruhusu kufanya hivyo.
Mheshimiwa Spika[FONT=Georgia], utaratibu wa kuachia kila mgeni kuingia Tanzania na kuishi atakavyo bila ya vyombo husika kujua kuwepo kwake, kiusalama ni hatari, hasa katika zama hizi za kusambaa kwa tatizo la ugaidi na uharamia wa kimataifa katika masuala ya fedha, biashara za binadamu na hata ulaghai na utapeli. Kambi rasmi ya Upinzani inasisitiza hoja yake ya kutaka mchakato wa kupata vitambulisho vya taifa uharakishwe, kwani pia vitasaidia kuwabaini kwa urahisi wageni ambao wataingia nchini bila kuzingatia taratibu zilizopo.[/FONT]
[FONT=Georgia][/FONT]
[FONT=Georgia][/FONT][B]WAKIMBIZI
[B]
[B][FONT=Georgia][B]Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu yameripotiwa matukio yanayotishia usalama wa raia wetu pamoja na mali zao hasa maeneo yenye wakimbizi. Kambi ya upinzani tunaitaka serikali kutoa taarifa ya kina juu ya usalama wa mipaka yetu na watu wake katika maeneo hayo.Pia serikali itupe taarifa kuhusu makambi yaliyofungwa, Je, yatatumika kufanyia shughuli gani baada ya kambi hizo kufungwa?[/FONT]
MAPENDEKEZO YA JUMLA YA KAMBI RASMI YA UPINZANI.
[B]
[B][FONT=Georgia][B]Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani, tunapenda kutoa mapendekezo yafuatayo ili kuweza kuliboresha Jeshi la Polisi, Magereza na Uhamiaji na kuyafanya yawe ya kisasa zaidi na kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali na za kisasa ambazo zimetokea na zinaendelea kutokea.Tunapendekeza mambo yafuatayo yaweze kufanywa kikamilifu;[/FONT]
(i) Ijengwe maabara ya kitaifa ya masuala ya Uhalifu ([B]National
Crime Laboratory). Hii itasaidia kupata vipimo vya kubaini uhalifu na hivyo itarahisishia kazi jeshi la polisi katika kuchunguza na kupambana na uhalifu.
(ii) Vyuo vya polisi vya Moshi, Dar Es Salaam na vile vya Magereza kama vya Ukonga na Tukuyu viimarishwe ili kuhakikisha maofisa wanaohitimu kwenye vyuo hivi wanakuwa na weledi wa kutosha katika kupambana na uhalifu unaotumia mbinu mpya na za kisasa.
(iii) Kikosi cha Uokoaji kiboreshwe kwa kupatiwa nyenzo na vifaa vya kisasa, ili kiweza kukabiliana vizuri na majanga.
(iv) Sheria ya Uhamiaji irekebishwe ili kuhakikisha kuwa Mamlaka za Mikoa zinakuwa na uwezo wa kutoa hati za kusafiria (Passport). Hati hizo ziwe zinapatikana kwa haraka mara baada ya maombi badala ya hali ilivyo sasa ambapo huchukua muda mrefu hadi mtu kupata Passport.
(v) Zitengwe fedha za kutosha kwa ajili ya kununulia fulana za kuzuia risasi ([I]bullet proof vest[/I]), ili Askari polisi wote nchini waweze kukabiliana vizuri na uhalifu mkubwa hasa ujambazi wa kutumia silaha.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, Kambi rasmi ya Upinzani inasisitiza kwamba ukandamizaji na ukiukwaji wa utu na haki za binadamu, hautavumiliwa kamwe. Na ieleweke kwamba, tishio la Usalama na Amani ya Nchi hii si Maandamano ya Amani yanayofanywa na CHADEMA, kupinga uovu, bali ni ukiukwaji wa haki na utu wa Mtanzania, unaofanywa na serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
..............................
Godbless Lema (Mb)
Jimbo la Arusha MjiniMsemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani,
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
28/07/2011