Simulizi : Hatia Takatifu

Mjusi Sharobalo

JF-Expert Member
Joined
Sep 4, 2025
Posts
7,572
Reaction score
12,989
SIMULIZI: HATIA TAKATIFU

Mtunzi: Kedmund Mtembezi
Mwamdishi: Kedmund Mtembezi

Email: kedmund742@gmail.com

WhatsApp: +255 672 229 424

SEHEMU YA 1

Jua lilikuwa linachoma kama kawaida ya mchana wa Dar es Salaam. Vumbi lilikuwa likipaa kila gari lilipopita kwenye barabara ya udongo ya mtaani, na kelele za wauza chips, mama lishe na boda boda zilichanganyika kama muziki wa maisha ya kila siku.

Kijana mmoja aitwaye Kedmund alikaa juu ya jiwe lililochakaa pembeni ya nyumba yao ya mabati. Alikuwa na fulana iliyochuja na suruali iliyopauka, macho yake yakiwa yamejaa mawazo mazito kuliko umri wake ulivyokuwa.

“Maisha haya siyo rahisi…” alijisemea taratibu huku akiangalia watoto wadogo wakicheza bila kujali kesho.
Alikuwa mtoto wa mwisho kwenye familia ya watoto watatu. Baba yao alifariki miaka mitano iliyopita kwa ugonjwa, na tangu hapo mama yao, Mama Asha, ndiye aliyebeba mzigo wa familia. Kila siku alikuwa anaamka alfajiri kwenda kuuza maandazi na chai ili angalau wapate kula.
Lakini pesa haikutosha.

Usiku mwingi walilala na njaa, na siku nyingine Kedmund aliamua kusema uongo kwa mama yake kuwa ameshiba ilhali tumbo lilikuwa linamnguruma.
Siku hiyo, rafiki yake wa karibu, Juma, alikuja akiwa na tabasamu la ajabu.
“Vipi Kedmund, bado uko hapa unafikiria maisha?” Juma aliuliza huku akikaa karibu yake.
“Na nifanye nini sasa… kila siku ni ile ile. Nimechoka kuwa maskini bro,” Kedmund alijibu kwa sauti ya chini.
Juma alitabasamu kidogo, kisha akasogea karibu zaidi.
“Kuna mchongo nimeusikia… unaweza kututoa hapa.”
Kedmund aligeuza kichwa kwa haraka. “Mchongo gani?”
Juma aliangalia kushoto na kulia kuhakikisha hakuna anayesikiliza.
“Kuna jamaa mmoja anahitaji vijana wa kusafirisha mizigo… siyo kazi ngumu, pesa yake ni nzuri sana.”
Kedmund alinyamaza kwa sekunde chache. Moyoni alihisi kitu si sawa, lakini njaa na hali ya maisha vilianza kumshawishi.
“Ni mizigo gani?” aliuliza kwa tahadhari.
Juma alicheka kidogo. “Usiulize sana bro… cha muhimu ni pesa. Hapa mtaani ukitaka kutoka, lazima ujitoe mhanga kidogo.”
Maneno hayo yaligonga kichwa cha Kedmund kama nyundo.
Alijua kabisa hii inaweza kuwa njia ya hatari. Lakini pia alijua hakuna njia rahisi ya kutoka kwenye umaskini waliokuwa nao.
Usiku huo, Kedmund alikaa kimya ndani ya nyumba yao ndogo ya mabati. Mama yake alikuwa amechoka sana, amelala mapema. Kaka yake mkubwa alikuwa hajapata kazi kwa miezi mingi, na dada yake alikuwa ameacha shule kwa sababu ya ada.
Alimtazama mama yake aliyelala.
“Mama anastahili maisha mazuri…” alijisemea.
Ndani ya moyo wake, vita ilikuwa inaendelea.
Upande mmoja ulimwambia: kaa mbali na mambo ya hatari.
Upande mwingine ulikuwa unapiga kelele: hii ndiyo nafasi yako ya kubadilisha maisha.
Asubuhi iliyofuata, aliamka mapema kuliko kawaida.
Alitoka nje, upepo wa asubuhi ukimpiga usoni. Alihisi kama maisha yanampa mtihani mkubwa.
Juma tayari alikuwa anamsubiri kona ya barabara.
“Umefikiria?” aliuliza haraka.
Kedmund alinyamaza kwa sekunde chache, kisha akavuta pumzi ndefu.
“Twende… lakini nataka kujua tunaingia kwenye nini.”
Juma alitabasamu kwa ushindi.
“Hapo sasa… umekuwa mwanaume.”
Walitembea pamoja kuelekea sehemu ambayo Kedmund hakuwahi kufika. Moyo wake ulikuwa unapiga kwa kasi, lakini hakurudi nyuma.
Walifika kwenye nyumba moja ya kifahari kidogo, tofauti kabisa na mazingira ya mtaani.
Mlango ulifunguliwa na mwanaume mmoja mwenye mwili mkubwa na macho makali.
“Ndiyo hawa?” aliuliza kwa sauti nzito.
Juma alikubali kwa kichwa.
Mwanaume huyo alimwangalia Kedmund kwa makini, kama mtu anayepima kitu cha thamani.
“Unaonekana mdogo… lakini macho yako yana njaa. Napenda watu wenye njaa ya maisha.”
Kedmund hakujibu. Alisimama tu kimya.
“Ukifanya kazi vizuri, utapata pesa nyingi. Ukicheza mchezo, utajuta,” mwanaume huyo alisema kwa sauti tulivu lakini yenye vitisho.
Kedmund alihisi baridi ikipita mgongoni.
Lakini hakusema chochote.
Ndani ya sekunde chache, alijua maisha yake hayatarudi kuwa yale yale tena.
Hapo ndipo safari yake ilianza.
Safari ya kutoka kwenye vumbi… kwenda kwenye ndoto ambazo hata yeye mwenyewe hakuwahi kuamini.
Lakini hakujua kuwa kila hatua aliyokuwa anachukua… ilikuwa inaenda kumpeleka karibu zaidi na hatari kubwa kuliko alivyowahi kufikiria.

Mwisho wa Sehemu ya 1

#LIKE_COMMENT Tuendelee sehemu ya 2.
 
SIMULIZI: HATIA TAKATIFU

Mwandishi: Kedmund Mtembezi

SEHEMU YA 2

Ndani ya ile nyumba ya kifahari, hali ya hewa ilikuwa nzito kama vile kuna jambo kubwa linaenda kutokea.
Kedmund na Juma waliongozwa hadi sebuleni. Sofa zilikuwa za gharama, televisheni kubwa ukutani, na kila kitu kilionyesha pesa — pesa ambayo Kedmund hakuwahi kuiona hata kwa ndoto.
Mwanaume yule aliyewakaribisha aliketi mbele yao, akawatazama tena kwa macho ya kupima.
“Mimi naitwa Rashid,” alisema kwa utulivu. “Na hapa hakuna mchezo wa kitoto.”
Kedmund alikaa kimya, lakini moyo wake ulikuwa unadunda kwa kasi.
Rashid aliweka begi dogo mezani.
“Hii ndiyo kazi yenu ya kwanza.”
Juma alitabasamu, kama vile tayari alijua kinachoendelea. Lakini Kedmund bado alikuwa na wasiwasi.
“Kazi gani hasa?” aliuliza.
Rashid alimwangalia moja kwa moja.
“Mtasafirisha mzigo kutoka hapa hadi Mbagala. Hakuna maswali. Hakuna kufungua. Hakuna kuchelewa.”
Kimya kilitanda.
Kedmund alihisi koo lake likikauka.
“Na kama tukikamatwa?” aliuliza kwa tahadhari.
Rashid alitabasamu kidogo… tabasamu la kutisha.
“Msikamatwe.”
Maneno hayo yalikuwa mafupi, lakini yalibeba uzito mkubwa.
Kabla Kedmund hajafikiria zaidi, Rashid aliweka bahasha mezani.
“Advance.”
Juma aliichukua haraka, akaifungua kidogo… macho yake yakang’aa.
“Bro… hii ni pesa ya kweli,” alinong’ona kwa furaha.
Kedmund aliangalia zile pesa — zilikuwa nyingi kuliko alivyowahi kushika maishani mwake.
Ndani ya sekunde ile ile, alihisi akili yake inaanza kubadilika.
Hii inaweza kubadilisha maisha yetu…
Lakini pia, sauti nyingine ilimnong’oneza:
Hii inaweza kukuangamiza…
Dakika chache baadaye, walikuwa njiani.
Jua lilikuwa limeanza kupungua, lakini joto la mchana bado lilikuwa linaonekana ardhini. Walipanda daladala, begi lile likiwa mikononi mwa Kedmund.
Alikuwa amelishika kwa nguvu, kama mtu anayebeba kitu kisichoeleweka.
“Kuwa kawaida tu,” Juma alisema. “Usionyeshe hofu.”
Lakini haikuwa rahisi.
Kila mtu aliyekuwa ndani ya daladala alionekana kama polisi kwake.
Kila macho yaliyomwangalia yalimfanya ajisikie kama ameshikwa tayari.
Moyo wake ulikuwa unapiga du-du-du bila kupumzika.
Walipofika maeneo ya katikati ya jiji, ghafla daladala ilisimama.
“Simamisha! Ukaguzi!” sauti ilisikika nje.
Kedmund alihisi damu ikiganda.
Polisi wawili walipanda ndani.
“Vitambulisho!” mmoja wao alipaza sauti.
Juma alijifanya mtulivu, lakini Kedmund alikuwa karibu kupoteza fahamu.
Mikono yake ilianza kutetemeka.
Hii ndiyo mwisho wangu… alifikiria.
Polisi mmoja alianza kukagua watu mmoja mmoja.
Alikuwa anakaribia.
Karibu zaidi.
Mpaka alipofika mbele yao.
“Nyie wawili… mnatoka wapi?” aliuliza.
Juma alijibu haraka: “Tunaenda kwa ndugu yetu Mbagala, bwana.”
Polisi alimwangalia Kedmund.
“Wewe mbona unaonekana na hofu?”
Kedmund alimeza mate.
“Ni… ni joto tu mkuu,” alisema kwa sauti iliyokatika.
Kulikuwa na ukimya mfupi.
Dakika chache zilionekana kama saa.
Kisha polisi akacheka kidogo.
“Hamna shida… lakini kuwa makini.”
Walishuka.
Daladala ikaendelea.
Kedmund alikaa kimya kwa muda mrefu, kisha akavuta pumzi ndefu kama mtu aliyenusurika ajali.
“Nilidhani tumekwisha…” alisema kwa sauti ya chini.
Juma alicheka.
“Hii ndiyo game bro… ukizoea, utaona kawaida tu.”
Lakini Kedmund hakuhisi kawaida hata kidogo.
Alihisi kama ameanza kuingia kwenye dunia ambayo haina kurudi nyuma.
Walipofika Mbagala, walipeleka lile begi kwa mtu mwingine aliyekuwa anawasubiri kwenye kona ya giza.
Hakukuwa na mazungumzo mengi.
Walikabidhi mzigo… wakapewa pesa nyingine.
Safari ya kurudi ilikuwa tofauti kabisa.
Kedmund alikuwa kimya, lakini kichwani mwake kulikuwa na mawazo mengi.
Alipofika nyumbani, alimkuta mama yake akipika kwa shida, akichochea sufuria iliyokuwa na chakula kidogo.
“Mwanangu… leo umechelewa,” mama alisema kwa sauti ya upole.
Kedmund alisimama kimya kwa sekunde chache… kisha akatoa sehemu ya pesa na kumpa.
Mama yake alishangaa.
“Hizi pesa zote umetoka wapi?”
Kedmund alisita… kisha akasema:
“Nimepata kazi, mama.”
Mama yake alitabasamu kwa furaha… macho yake yakajaa matumaini mapya.
“Asante Mungu…”
Lakini Kedmund alihisi moyo wake ukiuma kidogo.
Kwa sababu alijua…
Hii “kazi” haikuwa ya kawaida.
Na hii ilikuwa ni mwanzo tu.
Usiku huo, alilala kitandani akitazama paa la bati.
Pesa zilikuwa mfukoni.
Lakini amani haikuwepo moyoni.
Na ndani kabisa ya nafsi yake, alijua kitu kimoja:
👉 Hatua ya kwanza imechukuliwa… na kurudi nyuma haitakuwa rahisi tena.

Mwisho wa Sehemu ya 2

#Like_comment Tuendelee sehemu ya 3.
 
 
SIMULIZI: HATIA TAKATIFU

Mwandishi: Kedmund Mtembezi
Email kedmund742@gmail.com
WhatsApp+255 672 229 424

SEHEMU YA 3:

Siku chache zilipita tangu ile kazi ya kwanza.
Maisha ya Kedmund yalianza kubadilika… taratibu, lakini kwa namna ya hatari.
Mfukoni kulikuwa na pesa. Sio nyingi sana, lakini za kutosha kubadilisha hali ya nyumbani. Mama yake alianza kupika vizuri zaidi, na hata tabasamu lake lilianza kurudi.
Lakini kwa Kedmund…
Amani ilizidi kupotea.
Kila usiku alipolala, akili yake ilirudia ile tukio ya polisi. Ile hofu haikuisha. Ilibaki ndani yake kama kivuli kinachomfuata.
Siku moja jioni, akiwa amekaa na Juma pale pale kwenye jiwe lao la kawaida, simu ya Juma iliita.
Alipokea, akasikiliza kwa sekunde chache, kisha akakata.
“Rashid anakuita,” alisema.
Kedmund alinyanyua macho polepole.
“Leo tena?”
Juma alitabasamu kwa maana nzito.
“Hii sio kazi ya mara moja bro… umeingia game sasa.”
Walipofika tena kwenye ile nyumba, hali ilikuwa tofauti.
Safari hii, kulikuwa na watu wengine ndani. Wanaume wawili wenye sura ngumu, na mwanamke mmoja aliyekaa kimya kona akicheza na simu yake.
Macho yao yote yalikuwa na kitu kimoja — ukali.
Rashid aliingia akiwa na simu mkononi, akawaangalia Kedmund na Juma kwa utulivu.
“Mlifanya kazi safi,” alisema.
Juma alitabasamu. Kedmund alibaki kimya.
Rashid alimsogelea Kedmund.
“Lakini wewe…” alisema, “bado unaogopa.”
Kedmund hakujibu.
“Usiogope pesa,” Rashid aliendelea. “Oga hofu.”
Kila mtu ndani ya chumba alicheka kidogo.
Kedmund alihisi kama anazidi kushinikizwa kuingia ndani zaidi ya kitu ambacho hakielewi kikamilifu.
Safari hii, hawakupewa begi.
Walipata kitu tofauti.
Bahasha.
Ndogo.
Nyepesi.
Lakini Rashid alisisitiza:
“Hii ni muhimu zaidi ya ile mzigo wa jana. Hii haipaswi kupotea. Ukipoteza… maisha yako yanaweza kupotea pia.”
Moyo wa Kedmund uliruka.
“Hii ina nini?” aliuliza.
Rashid alimsogelea karibu sana, macho kwa macho.
“Usiulize vitu visivyokuhusu.”
Kimya kilitanda.
Safari hii hawakupanda daladala.
Walichukua bodaboda.
Walikuwa wanapita mitaani kwa kasi, upepo ukipiga uso wa Kedmund, lakini akili yake ilikuwa mbali kabisa.
Alihisi kama anazama polepole kwenye maji marefu.
Walipofika sehemu ya makaburi yaliyotelekezwa kidogo pembeni ya mji, Kedmund alishangaa.
“Tunafanya nini huku?” aliuliza.
Juma hakujibu.
Walikutana na mtu mwingine — kijana mdogo, lakini macho yake yalikuwa makali kuliko hata ya Rashid.
Alipokea ile bahasha bila kusema neno.
Lakini kabla hajaondoka, alimwangalia Kedmund kwa sekunde kadhaa.
Halafu akasema:
“Karibu kwenye mchezo wa kweli.”
Maneno hayo yalimfanya Kedmund atetemeke.
Wakiwa njiani kurudi, Kedmund hakuvumilia tena.
“Juma… hii ni kazi gani hasa?” aliuliza kwa hasira kidogo.
Juma alikaa kimya kwa muda, kisha akasema:
“Ni biashara bro… biashara ya watu wakubwa.”
“Biashara gani? Dawa za kulevya? Uhalifu?” Kedmund aliuliza moja kwa moja.
Juma alimtazama.
“Unataka kujua sana au unataka pesa?”
Swali hilo lilimchoma.
Kedmund alikaa kimya.
Ndani ya moyo wake, alijua jibu.
Lakini hakupenda ukweli huo.
Usiku huo, alipofika nyumbani, alimkuta dada yake akitabasamu.
“Kedmund! Leo nimepata nafasi ya kurudi shule!” alisema kwa furaha.
Kedmund alishangaa.
“Vipi?”
Mama yake alitoka jikoni.
“Hizi pesa ulizotuletea zimeanza kusaidia mwanangu… Mungu akubariki.”
Maneno hayo yalimchoma moyo.
Kwa sababu alijua…
Pesa hizo zina harufu ya hatari.
Lakini pia…
Zinaanza kubadilisha maisha yao.
Siku zilivyopita, Kedmund alianza kuzoea.
Hofu ilipungua kidogo.
Confidence ikaongezeka.
Pesa zikawa nyingi zaidi.
Lakini pia…
Alianza kuona vitu ambavyo hakutakiwa kuona.
Usiku mmoja, alipokuwa anarudi peke yake baada ya kazi, aliona gari likisimama ghafla karibu yake.
Mlango ukafunguliwa.
Wanaume wawili wakashuka.
“Mzee anataka kukuona sasa hivi,” mmoja alisema.
Hakukuwa na chaguo.
Aliingia kwenye gari.
Moyo wake ukianza kupiga tena kwa kasi ile ile ya mwanzo.
Safari hii, alihisi wazi kabisa:
👉 Anaingia ndani zaidi ya kitu kisicho na njia ya kutoka.
Na safari hii…
Hakuwa na uhakika kama ataweza kutoka salama.

Mwisho wa Sehemu ya 3

#Like_comment Tuendelee sehemu ya 4.

Kwa wenye haraka link hiyo hapo wahi ukasome sehemu ya nne na kuendelea 👇
 
SIMULIZI: HATIA TAKATIFU

Mwandishi: Kedmund Mtembezi

Email kedmund742@gmail.com
WhatsApp+255 672 229 424

SEHEMU YA 4

Gari lilikuwa linatembea kwa kasi usiku wa manane. Taa za barabarani zilikuwa zinapita kama mistari ya mwanga kwenye macho ya Kedmund.
Hakuna aliyekuwa anaongea.
Moyo wake ulikuwa unapiga kwa nguvu, lakini safari hii haikuwa hofu ya polisi… ilikuwa hofu ya kitu kisichojulikana.
Walifika kwenye jengo moja la kifahari zaidi kuliko lile la Rashid. Hapa kulikuwa na ulinzi mkali — walinzi, kamera, kila kitu kilionyesha hii ni level nyingine.
“Mshuke,” mmoja wa wale wanaume alisema.
Kedmund alishuka taratibu, macho yake yakizunguka kila kona.
Alipelekwa ndani… hadi kwenye chumba kikubwa kilichokuwa na taa za rangi laini.
Ndipo alipomwona.
Alikuwa amekaa kwenye sofa, akivuta pumzi polepole kama mtu asiye na wasiwasi wowote duniani.
Msichana.
Mzuri kuliko yeyote ambaye Kedmund alikuwa amewahi kuona.
Ngozi yake iling’aa chini ya mwanga, macho yake yalikuwa makali lakini yenye mvuto, na tabasamu lake lilikuwa la hatari.
“Karibu,” alisema kwa sauti laini.
Kedmund alisimama kimya kwa sekunde chache.
“Mimi naitwa Amina.”
Jina hilo lilikaa kichwani mwake.
“Kedmund,” alijibu kwa tabu kidogo.
Amina alisimama, akamkaribia taratibu. Alikuwa anatembea kwa kujiamini kama mtu anayejua nguvu yake.
“Nilikuwa nasikia habari zako…” alisema huku akimzunguka kama anamsoma.
“Unaanza vizuri kwenye mchezo.”
Kedmund alishangaa.
“Wewe ni nani hapa?” aliuliza.
Amina alitabasamu kidogo.
“Mimi ni sehemu ya mchezo huu… lakini siyo mtu mdogo kama unavyofikiria.”
Kabla hajaendelea kusema, mlango ulifunguliwa.
Rashid akaingia.
Safari hii, hakuwa peke yake. Alikuwa na mwanaume mwingine mwenye sura kali zaidi — macho yake yalikuwa baridi kama barafu.
“Huyu,” Rashid alisema, “ndiye mtu mkubwa hapa. Tunamwita Mzee.”
Kedmund alihisi presha ikipanda.
Mzee alimwangalia kwa makini.
“Wewe ndiye kijana mpya?” aliuliza kwa sauti nzito.
“Ndiyo,” Kedmund alijibu.
Mzee alikaa chini polepole.
“Ninapenda vijana wenye njaa ya maisha… lakini sipendi wasaliti.”
Chumba kilinyamaza.
Kedmund alihisi uzito wa maneno hayo.
Baada ya mazungumzo mafupi, Kedmund aliruhusiwa kuondoka.
Lakini kabla hajaenda, Amina alimfuata nje.
“Subiri,” alimwita.
Kedmund alisimama.
Amina alimsogelea karibu sana… karibu kiasi kwamba aliweza kuhisi pumzi yake.
“Usiwaamini sana hawa watu,” alisema kwa sauti ya chini.
Kedmund alishangaa.
“Kwanini?”
Amina alimtazama moja kwa moja machoni.
“Kwa sababu kila mtu hapa anacheza mchezo wake mwenyewe.”
Maneno hayo yalimchanganya.
Lakini kabla hajauliza zaidi, Amina alitabasamu tena kama hakuna kilichotokea.
“Tutaonana tena,” alisema, kisha akaondoka.
Siku zilizofuata, Kedmund alijikuta akimfikiria Amina mara kwa mara.
Si tu kwa uzuri wake…
Bali kwa maneno yake.
Kulikuwa na kitu ndani yake kilichovutia — lakini pia kilitisha.
Siku moja usiku, simu yake iliita.
Namba mpya.
Alipokea.
“Sauti hii utaikumbuka?” ilikuwa ni Amina.
Moyo wake uliruka kidogo.
“Amina?”
Alitabasamu upande wa pili.
“Good… hujasahau.”
Waliongea kwa muda mrefu usiku huo.
Mazungumzo ya kawaida yakageuka kuwa ya karibu zaidi.
Kedmund alihisi kitu kipya — kitu ambacho hakikuhusiana na pesa wala hatari.
Alianza kumpenda.
Lakini…
Hakujua kuwa Amina alikuwa na siri kubwa.
Usiku mwingine, mbali na macho ya kila mtu, Amina alikutana na mtu kwenye gari.
Mwanaume aliyekuwa tofauti kabisa na wale wa Rashid.
“Huyo kijana anaingia sana kwenye mfumo,” mwanaume alisema.
Amina alinyamaza kwa sekunde chache.
“Kazi yangu ni kumuweka karibu… siyo kumuonea huruma,” alijibu.
Mwanaume alitabasamu kidogo.
“Usisahau lengo letu.”
Amina aliangalia mbali… macho yake yakionyesha mgongano wa hisia.
Wakati huo huo, Kedmund alikuwa anaingia ndani zaidi ya penzi hilo.
Hakujua kuwa kila tabasamu la Amina…
Kila simu…
Kila neno la karibu…
Likuwa linaweza kuwa sehemu ya mchezo mkubwa zaidi.
Mchezo wa usaliti.
Usiku mmoja, walikutana.
Walikaa pamoja, wakiongea, wakicheka.
Kedmund alimshika mkono Amina.
“Kuna kitu nakuhisi… siwezi kuelezea,” alisema kwa ukweli.
Amina alimtazama kwa muda mrefu.
Kwa mara ya kwanza…
Tabasamu lake lilionekana la kweli.
Lakini ndani yake, kulikuwa na vita.
Kwa sababu alijua ukweli mmoja:
👉 Moyo wake unaanza kuingia… lakini kazi yake ni kumuangamiza Kedmund.
Mwisho wa Sehemu ya 4

#Like_comment Tuendelee sehemu ya 5.
 
Kwa mwenye haraka Link hiyo hapo inaendelea huko.

 

Similar Discussions

Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…