Linah tena nimerudi,ule ujumbe nakazia,
Vipi nimebisha hodi, bado waninyamazia,
Kumbuka niliahidi, sitolishusha pazia, Linah nakukumbushia, ujumbe nilokutumia
Ngoja nijitambulishe,kidogo unifahamu,
Walau nikujulishe, vile niko hendisamu,
Sio mtu wa kasheshe,kutwa ninatabasamu, Linah nakukumbushia, ujumbe nilokutumia.
Linah ninakuja Dar, unipe dawa nipone,
Nipo ninajiandaa,naja huko nikuone,
Usidhani ni hadaa,sitanii hata tone, Linah nakukumbushia,ujumbe nilokutumia
Si utani wa Masudi, kipanya nakichukia,
Usifanye makusudi, majanga wanitakia,
Ndio maana nimerudi, ongea nitasikia, Linah nakukumbushia, ujumbe nilokutumia.
Kuitwa ndege mnana, wamekupatia dia,
Leo ndio nakuchana, sautiyo bomba dia,
iwe usiku mchana, nacheza kwa kurudia, Linah nakukumbushia, ujumbe nilokutumia
Moyo umenipa ufa, hutaki kuja kuziba,
Ni nani huyo mshefa, nafasi ananiziba,
Basi hata nikikufa, usije kwenye msiba, Linah nakukumbushia,ujumbe nilokutumia.
Ukizidi nichunia,jiandae kwa lolote,
Jinsi nimekupania, nitakusaka kokote,
Jukwaa nitavamia, nikubusu kotekote, Linah nakukumbushia, ujumbe nilokutumia.
Basi sema nisikie,maoni yako nipate,
Imani inibakie,nitakuja nikupate,
Usiache nichukie,mwenzio nije nidate, Linah nakukumbushia, ujumbe nilokutumia.