UENDESHAJI wa shughuli za vikao vya Bunge kwa mwaka 2011, uliongozwa zaidi na msukumo wa kisiasa na uliolenga kulinda na kutetea masilahi ya upande mmoja badala ya kuzingatia mambo muhimu ya kitaifa.
Wakielezea maoni yao katika utendaji wa Bunge, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Mkuu, Jude Thadaeus Ruwa'ichi, pamoja na Askofu Mkuu wa Anglikana Tanzania, Dk. Valentino Mokiwa, walisema Bunge lilishindwa kufanya vizuri zaidi kutokana na kukosa uongozi wenye uelewa mpana wa kutambua mahitaji ya taifa.
Ruwa'ichi ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Kuu la Mwanza, alisema Bunge la Jamhuri ya Muungano lingeweza kufanya vizuri zaidi kutokana na kuwa na mchanganyiko wa wabunge kutoka vyama tofauti wenye uwezo mkubwa lakini uongozi wake umekuwa ukishughulikia mambo mbalimbali kwa mtazamo wa siasa za chama kimoja.
"Bunge kama lingeongozwa na uelewa mpana wenye kutambua historia ya nchi yetu ilikopitia na wapi tulipo, ni wazi lingeweza kufanya vizuri zaidi kwa kuwa lina watu wenye uwezo mkubwa wa kujenga hoja lakini uongozi uliyashughulikia mambo ya msingi visivyo," alisema Ruwa'ichi.
Alisema bado kuna kigugumizi cha watawala kukubali kwamba nchi iko kwenye mfumo wa vyama vingi, ikiwa ni kukabiliana na changamoto ya hoja zinazoibuliwa kama mbadala wa maendeleo, badala yake kilichofanyika ni kujaribu kuwaziba midomo wapinzani.
Naye Dk. Mokiwa alionesha kushangazwa kwake na namna Bunge lilivyoacha kujadili mambo ya msingi, na kuanza kuwajadili wabunge wa upande mwingine, jambao alilosema halikuwa kipaumbele kwa wananchi.
"Bunge lilikuwa na changamoto kubwa katika baadhi ya matatizo yakiwamo kujadili hoja nzito kwa kufuata masilahi ya chama na kufumbia macho mambo muhimu ya kitaifa," alisema Dk. Mokiwa.
Akizungumzia juu ya mhimili huo wa nchi, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema Bunge lilionesha udhaifu mkubwa pale Spika Anne Makinda na Katibu wake, Dk. Thomas Kashilillah walipopingana waziwazi kuhusu suala la ongezeko la posho.
Alidai kuwa kusigana huko kulitoa kielelezo cha wazi jinsi wakuu hao wa Bunge wanavyoendesha chombo hicho kwa namna ya utengano na pasipo masikilizano.
Pamoja na hayo, alisema idadi kubwa ya wabunge ni mzigo kwa serikali kutokana na kutumia rasilimali nyingi kuwahudumia wao, badala ya kutatua kero za wananchi.
"Hali hii inasabaishwa na mfumo wa muungano wa kuwa na serikali mbili, lakini tungeweza kuwa na Bunge dogo la Muungano lenye wabunge wachache ambalo lingekuwa bora zaidi," alisema.
Hata hivyo, Mwenyekiti Mwenza wa Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) na Mkuu wa Kitivo cha Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisifu uendeshaji wa Bunge akidai lilionesha ukomavu wa kisiasa.
"Tulishuhudia mbwembwe na vitimbi na vilikuwa vizuri vikiashiria kukomaa kwa demokrasia.
"Tulishuhudia wabunge wakitoka nje wakiashiria kwamba kila chama kina wajibu wa kudai haki yake kwa stahili yake," alisema Dk. Bana.
Jambo jingine ambalo alilipongeza ni hatua ya wabunge kuikataa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, hatua iliyosababisha wizara hiyo kuifanyia marekebisho ya hali ya juu kabla ya kupelekwa tena bungeni.
Alisifu pia hatua ya Bunge kulilipua sakata la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, hali iliyosababisha Bunge kuunda kamati ya kuyachunguza.
"Kwa ujumla mambo hayo na mengine yaliibua changamoto kubwa bungeni hivyo kulifanya kutimiza wajibu wake wa kuidhibiti serikali kikamilifu," amesema.
Mbali na viongozi hao, wananchi wengi waliohojiwa na Tanzania Daima, walisema hawakuridhishwa na namna Bunge lilivyojadili mambo mengi ya msingi ya kitaifa.
Suleiman Nassoro, mkazi wa Temeke jijini Dar es Salaam, alisema kuwa wingi wa wabunge wa Chama cha Mapinduzi, ulitumika vibaya kukidhi mahitaji na malengo ya chama hicho na kusahau kuwa walitakiwa kuwakilisha masilahi ya Watanzania wote.
"Hata kama mimi ni mwanachama wa CCM, napenda niseme wazi kuwa wabunge wangu hawakutenda vema kwa mwaka huu. Kwanza kulikuwa kama kuna namna ya kukomoana baina yao, hasa baada ya kuteuliwa kwa spika mpya na kuachwa yule wa zamani, lakini baadaye ikawa vita kati ya wabunge wa upinzani na wa CCM," alisema.
|