Usalama Barabarani ni jukumu letu sote, lakini wewe ndio KAMANDA.
Naomba nianze kwa kupongeza juhudi zilizowahi kuoneshwa na kikosi chako kipindi fulani hapo nyuma, ambazo sasa zimefifia na zinatoweka. Askari wa Usalama Barabarani kwa kushirikiana na Road Safety Ambassadors waliibuka na utaratibu mujarab wa kiutendaji wa kunyoosha tabia za wahuni wachache wasiopenda kufuata sheria za matumizi ya barabara kwa kuwapiga picha, kuwakamata na kuwachukulia hatua madereva wasio na nidhamu. Nilifarijika na utaratibu ule, na kero ya watanuaji ilianza kupungua lakini sasa TUMERUDI NYUMA.
Kamanda Mpinga, tambua kuwa wakati madereva wahuni wakisherekea kufanya uhuni wao na kujiona wajanja, kuna kundi kubwa sana la Watanzania raia wema, walipa kodi wa nchi hii wanaumizwa na kukerwa na tabia hizi chafu ambazo zinafanyika barabarani.
Nitaitolea mfano Nyerere Road.
Quality Centre hadi Sigara hapa watanuaji wanapita kwenye service roads na kuja kuchomekea kwa mbele. Watiifu wa sheria wanabakia kukaa kwenye foleni isiyotembea wakiambulia vumbi kali linalotimuliwa na dala dala zinazopita pembezoni mwa barabara zikiaribu kingo za barabara na kuhatarisha maisha ya wachuuzi wanaojitafutia riziki. Hivi ni kweli wale askari wanaorundikana pale kibandani Tazara hawawezi kudhibiti hawa wahuni wachache?
Vingunguti hadi Tazara (Bosch) daladala zinatimua vumbi kwenye kingo za barabara huku gari ndogo zikipita kwenye service road na kuja kuchomekea kwa mbele. Kwenye hizi vurugu ndiko wananchi huambulia michubuko kwenye magari yao na kucheleweshwa kazini.
Labda Kamanda nikumbushe kwamba, hii ndio njia inayoenda airport.
1. Tunawaonesha wageni ustaarabu wa namna gani? Siku za karibuni nimeanza kuona magari ya ubalozi nayo yanatanua, ndio sasa uvumilivu umekwisha nao sasa wameweka nidhamu pembeni wanatanua.
2. Uharibifu wa kingo za barabara ni mkubwa na mashimo yanajitokeza.
3. Hawa wanaobaki njia kuu, uvumilivu unapowaisha na wao wanaongeza idadi ya wahuni
Yapo mabaya mengi sana ukiachilia mbali kero za kucheleweshwa na kuchubuliwa magari yetu, lakini kuna la ziada hapa. Hawa wavunja sheria hawa, mbona ni wengi kila napopita njia hii kiasi najiuliza ni kiasi gani cha mapato serikali inakosa kutoka kwa waharibifu hawa wa barabara?
Kila napopita toka airport kwenda city centre, si chini ya gari 40 zitanipita zikitanua na kwenda kuingilia mbele. Ikiwa askari wale wanaojirundika pale kibandani Tazara wakikamata KIRIKUU na BODABODA wakivamia ghafla hii misafara ya wavunja sheria, si kwamba kuna 30,000 x 40 =1,200,000 serikali ingaliweza kufidia uharibifu wa barabara wanaoufanya wahuni hawa?
Mimi naamini inawezekana. Siku zile chache za kampeni za RSA na Askari wa Barabarani niliona foleni kubwa za magari kama ilivyo siku zote, lakini zilikuwa zinatembea. Nikuombe Kamanda Mpinga urudishe zoezi lile na liwe la kudumu. Hatupaswi kuwa na taifa la watu wa hovyo wasiofuata utaratibu kiasi tufanane na wanyama pori.
Zile pikipiki ziachane na bodaboda, hapa kuna wahuni wakubwa wanaofanya uhuni wao wazi wazi wakiwakejeli wanaofuata sheria. Hili likifanyiwa kazi, serikali itapata mapato stahiki kutoka kwa waharibu barabara na raia wema watapunguziwa kero ya kucheleweshwa kazini na magari yao kuchubuliwa rangi na DCM.