Boniface Meena,Gazeti la Mwananchi;August 18/2010
SUALA la uraia limezidi kuwa mwiba mchungu kwa CCM baada ya mgombea aliyepitishwa na halmashauri kuu ya chama hicho kuwania ubunge wa jimbo la Nzega, Dk Hamis Andrea Kigwangala kukamatwa na maofisa wa idara ya uhamiaji na kuhojiwa dhidi ya tuhuma kuwa ni raia wa Burundi.
Dk Kigwangala, ambaye alizua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya mawasiliano ya kompyuta baada ya kutangaza nia ya kuwania jimbo hilo, alishika nafasi ya tatu kwenye kura za maoni za jimbo la Nzega, lakini akapitishwa kuwania kiti hicho baada ya mshindi wa kura za maoni, Hussein Bashe kudaiwa kuwa ni Msomali huku mshindi wa pili, Lucas Selelii akidaiwa kuwa amepoteza mvuto.
Lakini wakati akiwa kwenye maandalizi ya mikikimikiki ya ubunge, Dk Kigwangala alijikuta akitakiwa amalizane kwanza na tatizo la uraia wake, ikiwa siku mbili kabla ya siku ya mwisho ya kuchukua na kurejesha fomu kwenye Tume ya Uchaguzi (Nec).
Mbali na uraia, mtaalamu huyo wa afya ya jamii pia anadaiwa kuwa hatumii jina halisi na kwamba jina lake ni Said Bagaile ambaye alimaliza elimu yake ya msingi mwaka 1990 kwenye Shule ya Msingi ya Kitongo iliyo wilayani Nzega.
Habari zinasema kuwa maofisa wa Idara ya Uhamiaji walimchukua Kigwangala kwenye ofisi za CCM wilayani Nzega ambako alikuwa akisaka udhamini kabla ya kwenda kuchukua fomu na kurejesha tayari kwa pilikapilika za kugombea ubunge.
Huku tuhuma za kufanyiana njama kwa kutumia uraia na umri zikizidi kushamiri ndani ya CCM, Dk Kigwangala hakuwa mbali na hisia hizo wakati alipohojiwa na Mwananchi kuhusu uraia wake.
"Hizo ni fitina za Bashe ili anichafue kwa kuwa tayari ana matatizo ya uraia," alisema Dk Kigwangala alipoongea na Mwananchi kwa njia ya simu jana.
"Ni kweli nimehojiwa na Uhamiaji kuhusu uraia wangu... mimi ni mzaliwa wa Tabora na sijawahi kufika wala kukanyaga ardhi ya Burundi.
"Mpaka hivi sasa ninavyoongea na wewe nahojiwa na nimetoa nyaraka zangu zote kuthibitisha kuwa mimi ni Mtanzania halisi na zinafanyiwa uchunguzi."
Alisema kuwa uhamiaji wanaendelea na uchunguzi wa taarifa zake na kwa kuwa fitina hizo zinafanywa na Bashe atamshtaki kutokana na kumchafua.
"Bashe ananichafulia na nitamshitaki kwa kufanya haya ambayo yananichafulia jina langu," alisema Dk Kigwangala.
Alisema kuwa jina lake kamili ni Hamis Kigwangala na amekuwa akilitumia siku zote tangu akiwa shuleni.
Alipotafutwa kuzungumzia tuhuma zilizotolewa na Dk Kigwangala kuwa ndiye anayemchafua, Bashe hakupatikana.
Wakati Dk Kigwangalla akijitetea kuhusu urai wake, sakata la jina limeibukia kwenye chama cha upinzani cha NCCR-Mageuzi ambako mwenyekiti wake, James Mbatia ameeleza kuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho kwenye jimbo la Nzega anaitwa Hamis Andrew.
Mbatia alidai kuwa Dk Kigwangala alikuwa akitumia jina la Hamis Andrea ili aendelee na elimu na kwamba jina lake halisi ni Said Nassor Bagaile.
Mbatia alidai kuwa Kigwangala alichukua jina la Hamisi Andreaw Kigwangala baada ya kutopata nafasi ya kuendelea na elimu ya sekondari wakati Hamisi Andrew alikuwa amefaulu na hivyo kukubaliana atumie jina hilo.
Mgombea huyo wa NCCR-Mageuzi anatarajiwa kuchukua fomu kupambana na Dk Kigwangala.
Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Florence Horombe hakuweza kupatikana kuzungumzia taarifa hizo za kukamatwa kwa mmoja wa wagombea wa ubunge wilayani kwake.
Taarifa tulizopatikana jana usiku zilisema kwamba Kigwangala alienda juzi Mahakama ya Wilaya Nzega kula kiapo kwa jina hilo lenye utata. Habari zaidi zinasema maofisa wa Uhamiaji walimwita Dk Kigwangala juzi kwa ajili ya mahojiano, lakini hakutokea na ndipo walipoomba polisi kumkamata wakati akitafuta wadhamini kwenye ofisi ya chama.
Chanzo cha habari kutoka Nzega kinasema kwamba Dk Kigwangala aliruhusiwa jioni kwenda kufuturu na baadaye alitakiwa kurejea ofisi za Uhamiaji kwa mahojiano.
Hii si mara ya kwanza kwa wanachama wa CCM kujikuta kwenye tuhuma za kutokana uraia wao wa zamani, hasa inapofikia wakati wa uchaguzi.
Akiwa mbunge wa Ilala kati ya mwaka 200-2005, waziri wa zamani wa Viwanda na Biashara, Idd Simba alijikuta akifurumushiwa tuhuma kwamba si raia wa Tanzania wakati wa kesi ya kupinga matokeo ya ubunge wa jimbo hilo.
Simba alituhumiwa kuwa ni raia wa Burundi, lakini baadaye mahakama ilithibitishiwa na hati kutoka nchini Burundi kuwa mbunge huyo wa zamani ni raia wa Tanzania.
Mbunge wa zamani wa CCM wa jimbo la Kigoma Mjini, Azim Premji pia aliwahi kuvuliwa ubunge kwa tuhuma za kutokuwa raia wa Tanzania.