Dhihaka ya "wrong or right my counry first"

Foum Jnr

JF-Expert Member
Joined
Jul 27, 2012
Posts
272
Reaction score
132
Tanzania tumekuwa na mizozo katika kila sehemu tunayokuwa nayo karibu, msururu wa migogoro unazidi kuongezeka, heshima baina yetu haipo na hata umoja tunaoupigia kelele na kuunadi kama ndio urithi wa Mwalimu haupo.

Ndani ya nchi hatutendeani haki, hatuheshimiani, wala hatuna ustaarabu wa kuvumiliana. Uongozi wa sasa uko shaghla baghla, hauna miadi ya kuaminika, kauli za viongozi wakuu haziendani na hata misimamo katika safu ya uongozi iko zigzag. Tumekuwa na taifa kama la fisi, kutegeana namna ya mmoja kumla mwenziwe. Hakuna "urge" kwa uongozi ya kutanabahi tulipo katika hasara ya aina gani, tumebeba uongozi mkubwa usio na manufaa kwa nchi, hawajakosoa wanaposema vijana "tupo tupo tu".

Tazama jinsi majirani zetu wanavyosonga mbele, itazame Rwanda ya leo na namna inavyopiga hatua madhubuti wakati sisi tupo tukichekacheka na kuumbuana. Tulikuwa wa mwanzo kuwa na shirika la ndege la ndani, lakini sera potofu tulizozikumbatia pamoja na ujinga tunaorithishana tumekuwa wa mwisho katika kila la maendeleo. Rwanda ndogo mara kumi ya Tanzania, leo ukitazama "in real terms" iko mbele ukusanyaji wa mapato yao, pamoja na matumizi yenye lengo la maendeleo. Shirika la ndege lao limekuwa kiasi ya kutambulikana kwa usanifu wake na weledi wa kutekeleza ahadi kwa watumizi. Sisi tulikodi ndege ikakatika tairi njiani, tulikodi ndege ambazo mbovu na hadi hii tunalipa mamilioni ya pesa za kigeni kwa ndege hewa.

Mbali ya kujaaliwa ardhi kubwa, mali asili ya kutosha, na wingi wa watu bado hatujaweza kutambua umuhimu wa kujiendeleza wenyewe. Tumejaaliwa uongozi wenye ubunifu wa kuomba misaada, lakini zero katika sera za kujikomboa na kujinufaisha na mazingira mazuri tulio nayo. Mungu katupa utulivu, si amani. Amani husimama pale penye mazingira ya haki, usawa na uadilifu. Lakini utulivu unasimama kutokana na akhlaki za wananchi, na ndio maana ukakuta polisi wakitesa raia, mahakama dhaifu kiutendaji na mihimili ya nchi ikiyumba kwa kuendekeza uonevu, ubaguzi na kukosa insafu pamoja na uadilifu. Lakini nchi tulivu, kwa vile wananchi walilelewa katika mazingira ya utulivu hata pale wanaponyimwa fursa na haki zao muhimu. Bado hakuna kiongozi anaetambua umuhimu wa utulivu katika masuala ya maendeleo. Na ndio maana tuko pale pale au nyuma zaidi ukilinganisha na wakati wa mihula ya marais waliotangulia. Sisi hatujengi "legacy" ya uongozi uliopo ila tunahakikisha tunarudi nyuma zaidi kuupa nafasi nzuri ya kusifiwa uongozi wa nyuma. Na ndio maana leo hii Mwalimu anaonekana kama kioo cha taifa, kwa vile hakuna aliemtangulia akaweza kumpiku katika maendeleo, haki, heshima na ustaarabu wa wakati wake. Utashangaa akisifiwa kama si binaadamu na kupuuza makosa yake? Nchi iliokosa "legacy" ya sasa haitathubutu kutazama makosa ya waliotangulia.

Lengo la maandishi ya leo ni kujitathmini sisi wenyewe muelekeo wetu uko wapi? Tukumbuke maneno ya Kolimba kwamba chama kimekosa dira. Haya ni maneno yaliotamkwa nyuma lakini ishara zote zinaelekea katika usahihi wake kwa sasa. Leo urais umekuwa ndio azma ya kila mmoja akijiamini kabisa kwamba anafaa. Tumegeuka nyumba ya juha kalulu, maana fikiri mtu kama Shamsi Nahodha kwa miaka kumi akiwa Waziri Kiongozi Zanzibar, ni ipi legacy yake? Na hata muda wake alipokuwa bara kama Waziri wa Jeshi ameacha historia gani wizarani mbali ya kashfa ya jeshi kupiga na kutesa raia ikabidi hata nae afukuzwe kazi? Lakini msikilize katika mahojiano yake siku aliojitangaza, anasema yeye anafaa na hakufanya kosa na alipendwa na jeshi zima. Uongozi wa juha kalulu hauona kipimo cha kufeli, bali ni mafanikio matupu. Watazame waheshimiwa wengine waliojitokeza, hakuna anaefaa kwa vile wote ni wale wale ambao hawana legacy yoyote katika nafasi wanazoziongoza. Wazuri wa kujipamba kwa maneno mengi, lakini vitendo wote ni wale wale. Tunahitaji kiongozi jasiri atakaekuja na kufuta kila kitu na kuanza upya. Leo mgombea urais hata vifungo vya koti hajui kufunga.

Mwengine akitomaza vyombo vya ulinzi kupiga tu wananchi, bila ya kikomo au hata utu kwa anaowaongoza, majuzi tu kinyume na sheria za nchi anarudia kauli ya "mtoto wa nyoka ni nyoka" kuhalalisha amri iliowataka wanafunzi kuhudhuria sherehe za chama tena katika mfumo wa vyama vingi. Hio ndio "cream" ya utawala wa sasa unaotaka kuendelea kututawala kwa miaka mitano mengine huku nchi ikizidi kudidimia.

Mtazame Lowasa, hadi hii leo ameshindwa kujibu tuhuma za wizi wa EPA, RICHMOND na mengine hayasemeki. Ni nani anaemlinda hasa ashindwe kutueleza wananchi kama kweli hahusiki? Ikiwa wanalindana hivi sasa tutegemee nini katika uongozi wao? Mtazame Membe, analalamikiwa na waziri wenzake visiwani kwa jeuri na kibri, ameongoza wizara bila ya mafanikio katika mashaka baina yetu na majirani, hata ukitazama usuluhishi wa sudan ya Kaskazini, utamkuta Kinana na uongozi wa CCM mbele kuliko yeye mwenye mamlaka. Tutegemee nini kwa kiongozi alielelewa na safu hii hii ya ESCROW? Nyalandu majuzi tu katajwa kwa uzembe wa kulikosesha taifa mabilioni leo na yeye anasema Mungu ndie aliemtoa kujinadi nafasi kubwa nchini. Kila mmoja hukimbilia kwa Mungu na mitume ya utabiri kwa vile hakuna atakaenyanyuka na heshima ya legacy nzuri.

Taifa letu limekuwa na migogoro na nchi washirika, lakini nia thabit ya kutatua matatizo imekuwa ikididimizwa kwa woga tu wa kusimama na haki. Imeanza migogoro na Malawi, Rwanda, leo UN imeitaja pia katika mgogoro wa DRC, na hata Kenya nayo tuko katika mikwaruzano. Na tazama wananchi tulivyo na giza la mawazo, sote tumeivamia Kenya na kufika hadi kumtaja mkuu wa nchi jirani kwa lugha ya ufedhuli. Tukiulizwa tunajibu "wrong or right my country first". Tukumbuke maneno kama haya ndio yalioanzisha vita ya pili ya dunia. Hitler aliwafanya wajarumani waiweke nchi yao kwanza hata ikiwa na makosa. Na akaona bado akaenda mbali zaidi na ile concept yake ya "Die Herrerace" kwamba wajarumani nio Master Race. Hawakuwa na kosa, na kwa majirani zao tumeona namna ilivyowashughulikia.

Tunajisahau kwamba haya yote yanatokana na uongozi dhaifu wa sasa usiojitambua na usiojuwa maana ya miadi. Tumezowea kurefusha mambo, na kuyawekea uporo tukifikiri na majirani zetu wana akili kama zetu. Nasema haya kwa ushahidi wa nchi zetu wenyewe. Mara ngapi Zanzibar imelalamika kwamba upande wa pili hauna nia thabit ya kutatua kero zilizopo. Mara ngapi tume zimeundwa, mara ngapi uongozi wa juu umekaa kuzungumzia kero, mara ngapi ahadi hutolewa na kuishia hewani, jee haiwezekani kuwa ndio sababu ya Kenya kujilinda na udhaifu wa maamuzi yetu? Sisi si wa kugombana na Uongozi wa Kenya, bali ni kuwabana uongozi wetu tuliowachagua na kushindwa kutafuta suluhu madhubuti katika masuala muhimu ya nchi. Tunashindwa kutumia ukomavu wa kisiasa kwa masulaa ya magari tu kuingia katika viwanja vya usafiri Kenya, jee tukishaamua kujiunga na sarafu ya pamoja itakuwaje?

Uongozi uliopo ni imara katika kuhakikisha demokrasia haikuwi, ni imara katika kuhakikisha udini unazidi kuwagawa wananchi, si umeyaona matamshi ya Lukuvi, ni imara katika kuhakikisha haki za binaadamu zinakiukwa, ni imara katika kuhakikisha wananchi wanapigwa tu bila ya kikomo, ni imara katika kuzuia haki kutendeka kwa watuhumiwa kwa kutowafikisha mahakamani na kuwadhalilisha kuendeleza uimara wa uimla tuliorithi.

Unaposikia taarifa kwamba wizi wa mabilioni umefanyika kweupe, hadi watu wakabeba pesa kwa mapolo tena mchana ujuwe tuko katika hali ngumu sana. Unaposikia taarifa za bunge zinataja ufisadi na uzembe kwa asilimia 80 na bado hakuna anaechukuliwa hatua ujuwe tuko katika hasara isiorekebishika. Unapokuta msururu wa wagombea wa urais kwa kigezo cha ukulima, na wabunge kwa kigezo cha kusoma na kuandika na wagombea kuhalalisha matumizi ya nguvu kwa raia, wakitamani udikteta na wakuu wakichekelea ujue tutakuwa katika majuto makubwa kwa ujinga wa kujitakia.

Tutajilaumu kwamba nchi imekosa maadili, kwamba "role model" wa leo ni waimbaji mchiriku na bongo flavour? Iko wapi ile ari ya wananchi wa kila rika iliotamani uhuru wa kujiendesha? Tutavuna mema gani katika mfumo usiojali haki, uadilifu na usawa? Tutavuna nini ikiwa mkuu wa nchi amezungukwa na mafisadi wanaompaka mafuta na akasahau malengo yake ya kutuongoza? Tunahitaji kiongozi atakeweza kurejesha heshima ya serikali kwa wananchi tena kwa amani sio utulivu tu. Atakaeunda serikali ya watendaji sio ya itikadi , atakaekuwa na ari ya vitendo katika kusimamisha taifa lenye mafahamiano na kuaminiana, linalokumbatia kuwapo kwa nchi mbili na kujifaharisha kwa umoja wa ushirikiano unaounda taifa. Atakaekuwa tayari kuwaongoza wananchi kwa hiyari katika kurasa mpya za ujenzi wa taifa kwa uadilifu, haki, heshima na usawa. Viongozi wasanii iwe ndio mwisho kwa taifa hili.

Aluta continua.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…