Kutoka
Victorious Life Ministries
UNAFAHAMU JINA LAKO LINAVYOWEZA KUINUA AU KUHARIBU MAISHA YAKO? – Dr Lawi Mshana
Katika wakati wetu tunapenda kuwapa watoto majina kwa sababu mbalimbali. Kama vile kumtofautisha na wengine, kudumisha mila, kuendeleza ukoo, kumpenda mtu fulani maarufu, kukumbuka tukio lililotokea wakati wa ujauzito au uchungu wakati wa kuzaa nk.
Katika kipindi cha Biblia majina yalitolewa kwa sababu zinazofanana na za kwetu. Lakini jambo la kipekee katika kipindi cha Biblia ni kwamba jina lilibeba maana kubwa zaidi. Jina lilibeba utambulisho wa mtu na kazi atakayoifanya. Mfano, Jina la YESU au ambalo kwa kiebrania ni YESHUA lina maana sawa na neno WOKOVU ndiyo sababu Biblia ikasema “Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye ATAKAYEWAOKOA watu wake na dhambi zao.” (Mt 1:21). Kwa hiyo YESU sio tu jina bali ni wadhifa (title).
UMUHIMU WA JINA KIROHO
1. Kujulikana kwa Mungu.
Kut 33:17 “Bwana akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako.” Kuna watu ni maarufu sana hapa duniani lakini mbingu haiwajui. Na kama hawatamgeukia Mungu kuna siku watajikuta wako kwenye aibu na kudharauliwa milele.
2. Kupata heshima
Mit 22:1 “Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi; Na neema kuliko fedha na dhahabu.” Isaya 58:12 “Na watu wako watapajenga mahali palipokuwa ukiwa; utaiinua misingi ya vizazi vingi; nawe utaitwa, Mwenye kutengeneza mahali palipobomoka; na, Mwenye kurejeza njia za kukalia.” Jina zuri linatatua shida za watu.
3. Kutimiza malengo na maono ya Mungu
Mwanzo 17:5 “wala jina lako hutaitwa tena Abramu, lakini jina lako litakuwa Ibrahimu, kwani nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi.” Abramu (baba aliyeinuliwa) akabadilishwa na kuitwa Ibrahimu (baba wa makusanyiko) ili aweze kutimiza misheni mpya ya Mungu.
Yohana 1:42 “Akampeleka kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama, akasema, Wewe u Simoni, mwana wa Yohana; nawe utaitwa Kefa (tafsiri yake Petro, au Jiwe).”
4. Kutolewa katika matatizo
Isaya 62:4 “Hutaitwa tena Aliyeachwa, wala nchi yako haitaitwa tena, Ukiwa; bali utaitwa Hefsiba; na nchi yako Beula; kwa kuwa Bwana anakufurahia ,na nchi yako itaolewa.” Mungu anaweza kumpa mtu jina jipya ili apokee uponyaji wa kudumu.
5. Kumgusa Mungu kipekee
Mwanzo 32:28 “Akamwambia, Jina lako hutaitwa tena Yakobo, ila Israeli, maana umeshindana na Mungu, na watu, nawe umeshinda.” Yakobo (mshika kisigino au mdanganyifu) akaitwa Israeli (kukabiliana na Mungu). Ukifuatilia vizuri utagundua kwamba Yakobo alimdanganya kaka yake Esau akachukua haki yake ya mzaliwa wa kwanza na akamdanganya baba yake na kuchukua baraka za Esau. Ila Yakobo alipomng’ang’ania malaika akabarikiwa na kupewa jina jipya. Mungu anaguswa na juhudi katika kumtafuta.
Isaya 62:2 “Na mataifa wataiona haki yako, na wafalme wote watauona utukufu wako; nawe utaitwa jina jipya, litakalotajwa na kinywa cha Bwana.”
Ufu 2:17 “Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa, nami nitampa jiwe jeupe, na juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye anayelipokea.”
MADHARA YA MAJINA MABAYA AU MAJINA YENYE CHANZO KIBAYA
1. Unaweza kurithi matatizo ya mtu aliyekuwa na jina hilo.
Nimewahi kuombea watu kadhaa ambao walipewa majina ya bibi zao wenye magonjwa nao wakayarithi. Mmojawapo nilipomuongoza maombi ya kulikataa jina hilo mapepo yalilipuka na kutoka. Sio lazima mtu arithi tu magonjwa. Anaweza pia kurithi matatizo kama kutozaa, kutoaa/kutoolewa, kutofanikiwa, kukataliwa nk.
2. Unaweza kulazimika kurithi kazi za mapepo alizokuwa anazifanya mwenye jina hilo
Roho chafu zilizokuwa zinamtumikisha mtu kv mganga wa kienyeji zinalazimika kumtafuta mwenye jina hilo pale anapofariki. Hasa pale anapokuwa hakupata mrithi wa uganga katika uhai wake. Mapepo hayo yatamtesa mpaka akubali uganga kwa vile yanahitaji huduma ya damu za wanyama na za watu. Kuna mtu ilikuwa vigumu kufunguliwa mpaka nilipombadili jina. Bibi yake yuko hai na ni mganga wa kienyeji hivyo kila tukimuombea baada ya muda fulani anayarudisha mapepo. Ilibidi kumbadili jina ili kumbukumbu zake zifutike kwenye madhabahu ya bibi huyo.
3. Unaweza kuingizwa katika maagano ya mwenye jina kwa njia ya ndoto
Yupo ambaye alikuwa analishwa vyakula vya mapepo kwenye ndoto mpaka alipokubali kubadilisha jina la bibi yake. Alilibadili akiwa tayari mtu mzima ambaye ameolewa ndipo matatizo hayo yakaisha. Kulishwa vyakula kwenye ndoto maana yake ni kwamba mtu anashiriki vikao vya wachawi kama mjumbe halali hata kama hataki.
4. Unaweza kuishi maisha yanayoendana na maana ya jina hilo
Kwa mfano unapoitwa taabu au shida, unaweza kufuatiliwa na matatizo fulani yasiyopata ufumbuzi. Unaweza kuwa na mafanikio upande mmoja lakini eneo fulani uwe na shida sana hata kama kwa nje huonekani hivyo. Ndiyo maana unaweza kukuta mtu ni tajiri lakini shetani amemfunga asizae au asiolewe au asiwe na ndoa ya furaha.
5. Unaweza kukosa baraka za Mungu ulizokusudiwa
Ni vigumu Mungu kumbariki mtu ambaye jina lake anaitwa Hasara au Laana. Ndiyo maana mtu akiokoka kama jina lake lina utata inafaa kulibadilisha. Sio rahisi Mungu kuandika jina baya kwenye kitabu chake cha uzima. Yapo majina hayaandikiki kwenye kitabu cha uzima. Najua unaweza kusema nitalitakasa kwa Jina la Bwana. Inawezekana kutakasa chombo kichafu lakini sio uchafu wenyewe. Hivi kama jina lina maana ya ‘kinyesi’ utalitakasaje ili lifae? Au kama jina lako ni la jinni hivi kweli Mungu ataliandika wakati shetani na malaika zake walishafukuzwa mbinguni? Usipobadili jina baya utakuwa ukisimama na kuanguka kila wakati hata kama una bidii ya kumcha Mungu.
6. Unaweza kuvamiwa na mapepo ambayo hayakutumwa rasmi kwako
Biblia inasema pepo anapomtoka mtu anazungukazunguka akitafuta mahali pa kupumzika (rest house). Akikosa anarudi kwenye nyumba yake ya kwanza aangalie kama kuna mlango wazi au nafasi tupu (empty space). Kwa hiyo wakati pepo anazunguka zunguka akikuta mtu mwenye jina linalomualika anaweza kumuingia apate makao mapya. Lk 11: 24,45 “Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika; asipoona, husema, Nitairudia nyumba yangu niliyotoka.” Kuna siku tulikemea pepo limtoke mtu likasema halikutumwa rasmi kwake bali liliamua kumuingia tu njiani. Mfano, kama jina lako lina maana ya ZINAA lazima mapepo ya zinaa yatakuvaa bila kuyakaribisha. Utajikuta unawakwa tamaa ovyo, hutosheki na mwenzi wako mpaka litakapokuaibisha kwa fumanizi, ugonjwa au mauti. Shetani hatoi kitu bure. Lazima kuna siku utalipia tena kwa gharama kubwa.
7. Unaweza kuchukuliwa na wachawi au waabudu shetani kwa wepesi
Shetani amekuwa mjanja sana kwa kuhakikisha kama unakataa majina yake anakupa nguo yenye jina lake au nembo yake ili siku wakihitaji damu au nyama wakuchukue kirahisi. Unaweza kusema mimi nalindwa na Mungu hivyo nitavaa chochote. Sijui utatakasa vipi fulani yenye nembo ya kanisa la shetani au iliyoandikwa kwa lugha usiyoijua ambayo tafsiri yake ni ‘MIMI NAMWABUDU SHETANI’. Nguo kama hiyo haina tofauti na hirizi lazima ichomwe moto isiwepo ndani ya nyumba yako. Kumbuka hata katika Biblia walibadili nguo na mitindo isiyokubalika ndipo wakawa na utisho wa Mungu (wakaogopwa na kuheshimiwa). Mwa 35:2-5 “Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake, na wote waliokuwa pamoja naye, Ondoeni miungu migeni iliyoko kwenu, mjisafishe mkabadili nguo zenu. Tuondoke, tupande kwenda Betheli, nami nitamfanyia Mungu madhabahu huko; yeye aliyenisikia siku ya shida yangu, akawa pamoja nami katika njia yote niliyoiendea. Nao wakampa Yakobo miungu migeni yote iliyokuwa mikononi mwao, na pete zilizokuwa masikioni mwao, naye Yakobo akazificha chini ya mwaloni ulioko Shekemu. Wakashika njia, hofu ya Mungu ikaishika miji iliyowazunguka, wala hawakuwafuata wana wa Yakobo.”
NINI CHA KUFANYA?
1. Fanya uchunguzi au utafiti ujue maana ya jina lako.
Yapo majina ya makabila yenye maana nzuri kuliko majina yaliyotoka kwenye Biblia. Kumbuka hata jina shetani lipo kwenye Biblia! Sio majina yote yameandikwa kwenye Biblia ili tuyachukue na kuyatumia. Hata majina mengi ya kingereza yana maana mbaya ila tu hatufuatilii kwa vile tunadhani wazungu wameendelea kuliko sisi.
2. Fanya utafiti ujue kwa nini wazazi wako walikupa jina hilo.
Kama walikupa kwa maana mbaya unaweza kuvunja kusudi ambalo liko nyuma ya jina hilo. 1 Mambo ya Nyakati 4:9,10 “Naye Yabesi alikuwa mwenye heshima kuliko nduguze; na mamaye akamwita jina lake Yabesi, akisema, Ni kwa sababu nalimzaa kwa huzuni. Huyo Yabesi akamlingana Mungu wa Israeli, akisema, Lau kwamba ungenibarikia kweli kweli, na kunizidishia hozi yangu, na mkono wako ungekuwa pamoja nami, nawe ungenilinda na uovu, ili usiwe kwa huzuni yangu! Naye Mungu akamjalia hayo aliyoyaomba.”
3. Fanya utafiti ujue tabia na maisha ya mtu uliyepewa jina lake kisha linganisha na maisha yako
Kama utaona kuna dalili za kufanana na maisha yake mabaya, chukua hatua ya maombi na ikibidi badili jina hilo. Hakuna faida yoyote unayopata kwa kuendeleza ukoo wakati unateseka. Kumbuka kipindi cha Biblia wapo waliobadili majina yao wakiwa watu wazima. Unaweza kupata shida sana kushinda dhambi kwa sababu ya ngome ya mtu uliyepewa jina lake.
4. Ukihitaji jina jipya au kumpa jina mtoto wako, mpe jina lenye maana nzuri
Usichukue na kutumia tu jina bila kujua maana yake. Unaweza kutengeneza mlango wa mapepo kwenye maisha yako au ya mtoto wako bila kujua. Wewe ni nabii wa familia yako. Ukiona ndugu au wazazi hawakuelewi waambie hata wewe mwenyewe hutaki mtu achukue jina lako. Itokee tu lifanane na lako lakini asichukue jina lako. Niliwahi kumkatalia muumini wangu aliyetaka kumpa mtoto jina langu. Nilimwambia ampe mtoto jina lenye maana anayoipenda na sio jina langu kwa kuniheshimu tu. Kwa hiyo nilichomsaidia ni kumpa majina yenye maana mbalimbali achague linalomfaa mtoto wake. Wewe unataka uwe nani au mwanao awe nani? Pata jina sahihi!
Hata hivyo usifanye maamuzi yoyote kwa kukukurupuka. Muombe Mungu akupe hekima ya jinsi ya kufanyia kazi mambo haya ili usieleweke vibaya wala kugombana na ndugu zako.
USHUHUDA KUHUSU JINA LANGU
Namshukuru Mungu wazazi wangu walinipa jina ambalo Mungu amelitumia sana katika wito niliopewa na Mungu. Wazazi wangu waliniambia kwamba walishatosheka na watoto tisa waliowahitaji hivyo bila kutarajia baada ya miaka takriban mitano mama akashangaa mtoto anaruka tumboni. Alilia sana kwa vile alishatahadharishwa kwamba kizazi kimechoka kwa kuzaa watoto wengi na umri wake umesogea. Baba aliwahi kuniambia kwamba kwa watoto wengine walipata muda wa kuandaa majina mengi yakiwa ni ya kingereza. Kwa vile nilikuja bila matarajio ikabidi watafute kwenye Biblia na kuchagua Lawi. Hawakujua maana yake lakini maana ya Lawi ni ‘joined’ au ‘attached’ yaani ‘kuunganishwa’. Lea alimuita mtoto wa tatu Lawi ili mumewe aungane naye maana alijua mumewe anampenda Raheli kuliko yeye. Mwanzo 29:34 “Akapata mimba tena, akazaa mwana, akasema, Basi wakati huu mume wangu ataungana nami, kwa sababu nimemzalia wana watatu. Kwa hiyo akamwita jina lake Lawi.” Baadaye Mungu alilitumia kabila la Walawi. Namshukuru kwamba kwa neema yake nimeweza kuwaunganisha watu wengi na Mungu tangu aliponiokoa nikiwa na umri wa miaka 16. Katika familia yetu nilikuwa wa kwanza kuokoka na wengi wakamgeukia Bwana kupitia kwangu wakiwemo wazazi wangu. Sasa mimi ni mtu mzima na familia yangu lakini bado mama yangu hapati amani kukaa muda mrefu bila kuniona. Nadhani hili jina limesababisha pia. Nimekupa historia hii ili ufuatilie maisha yako yaliyopita na kuyahusianisha na ya sasa. Mungu ana mpango mkubwa na wewe kuliko unavyofahamu.
Mtu anaweza kuwa na jina lenye maana nzuri lakini asinufaike nalo kwa vile hajamjua Mungu, amelirithi tu, amelipewa kienyeji tu, hajui maana yake au anaishi maisha yasiyompendeza Mungu.
Fil 2:9-11 “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.” Jina la Yesu ni jina linalopita majina yote. Hata majina ya magonjwa uliyo nayo hayana nguvu yanapokutana na Jina hili. Yesu anaweza kurudisha jina lako lililoharibiwa na shetani au maadui zako. Pokea jina jipya lenye upenyo halisi wa maisha yako!
TANGAZO MAALUM:
Nimekuwa na safari za kimisheni katika mikoa mbalimbali hapa nchini. Nashukuru kwamba kupitia mtandao kuna watumishi wa Mungu wamenialika siku moja niwatembelee. Kwa hiyo:
1. Kwa mtumishi wa Mungu ambaye angependa siku moja nikiwa maeneo ya karibu na kwake nimtembelee, naomba aniandikie KIBINAFSI anijulishe majina yake, kanisa lake, wadhifa wake, mkoa/wilaya/mji au kijiji na eneo dogo kv kitongoji kanisa lilipo na simu yake.
2. Kwa muumini ambaye ana hitaji ambalo anaona ushauri na maombezi kwa mtandao havitoshi bali angependa kushiriki kipindi cha maombezi moja kwa moja kinapofanyika karibu na eneo lake, atanijulisha majina yake, mkoa/wilaya/mji au kijiji, mahitaji makuu, simu yake na whatsapp kama anayo. Kwa vile napita Dar mara kwa mara na nimeona uhitaji huo, nitakuwa nakodi ukumbi kwa siku 1 au 2 na kuhudumia watu kabla ya kuendelea na safari zangu. Kuna watu kama watapewa tu ushauri na maelekezo sahihi wanaweza kupiga hatua kubwa katika maisha yao.
Naamini kwamba Mungu anawapenda watu wote bila kujali dini, madhehebu wala dhambi walizozifanya. Ndiyo maana anawaangazia jua lake wema na wabaya bila ubaguzi wowote. Mt 5:44,45 “lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.”