YAH:Mgodi Kiwira watafuna mabilioni fedha za umma

kupelwa

JF-Expert Member
Aug 24, 2011
1,087
450
mkono%20nimrod.jpg
Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono​
Mwandishi Wetu
LICHA ya kusababisha hasara ya Sh61 bilioni, mgodi wa makaa ya mawe Kiwira uliopo mkoani Mbeya umetengewa tena kiasi cha Sh40 bilioni katika bajeti ya Serikali ya 2012/2013 iliyopitishwa jana na Bunge mjini Dodoma.Mgodi wa Kiwira ukijulikana kwa jina la Kiwira Coal & Power Limited (KCPL) ni kampuni iliyokuwa ikiundwa kwa pamoja baina ya Serikali ya Tanzania na Tan Power Resources (TPR) ikiwa na malengo ya kufufua uendeshaji wa mgodi huo na kuuwezesha kuzalisha umeme ambao ulitarajiwa kuingizwa kwenye gridi ya Taifa.

Licha ya kwamba TPR walikuwa wabia katika ulimiki wa mgodi huo kwa kuwa na asilimia 70 ya hisa na Serikali ikiwa asilimia 30, pia wao ndio waliochukua jukumu la uendeshaji wake kinyume cha makubaliano kwamba wangetakiwa kutafuta manejimenti nyingine.

Taarifa za Serikali zinaonyesha kuwa mgodi huo chini ya menejimenti ya Kampuni ya Tan Power Resources Ltd hadi kufikia Desemba 31, 2010 umelimbikiza hasara ya zaidi Sh61 bilioni wakati madeni yake (liabilities) yanafikia Sh56 bilioni.

Kulingana na ukaguzi uliofanywa na Kampuni ya Kimataifa ya Ukaguzi wa Hesabu ya PKF, madeni hayo yanatokana na mikopo kutoka benki na taasisi za fedha ambazo jumla yake ni Sh32.19 bilioni kutoka Benki ya CRDB inayodai kiasi cha Sh4.65 bilioni, Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF) Sh11.09 bilioni na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Sh16.5 bilioni.

Kadhalika, taarifa hizo za hesabu, zinathibitisha kwamba Sh23.81 bilioni ni madeni ya yanayohusiana na wafanyakazi na wadai wengine.

Kutokana na hali hiyo, nyaraka mbalimbali ambazo Mwananchi limeziona, zinathibitisha kuwa Serikali ilishauriwa na timu ya wataalamu kutoilipa kampuni hiyo kiasi chochote baada ya kufanyika kwa uamuzi wa kurejeshwa kwake serikalini baada ya kushindwa kutekeleza kazi zake.

Kurejeshwa serikalini

Uamuzi wa kurejeshwa kwa Serikalini ulitangazwa bungeni na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja Julai 23, 2009 baada ya kuwapo shinikizo kutoka kwa wabunge kadhaa hasa kutoka mkoani Mbeya ambao walidai kwamba imeshindwa kutimiza sababu za kuwapo kwake.

Kabla ya kutangazwa rasmi kwa uamuzi huo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliliambia Bunge kwamba Serikali iliamua kufanya mazungumzo na TPR ili kurejesha hisa zake serikalini kama moja ya hatua za kuepusha kutajwa kila mara jina la Rais Mstaafu Benjamin Mkapa.

Mkapa na aliyekuwa Waziri wake wa Nishati na Madini, Daniel Yona ndio wamiliki wa kampuni ya TPR, hivyo tuhuma nyingi zilielekezwa kwao kwamba walijiuzia mali ya umma wakiwa viongozi wa umma.

Hadi uamuzi wa kuurejesha Serikali ulipofanyika, KCPL ilikuwa haijaweza kujiendesha hivyo kushindwa kutimiza malengo yake ya kuwezesha nchi kunufaika na uzalishaji wa umeme kama ilivyokuwa imetarajiwa awali, licha ya kupewa mkopo kwa dhamana ya Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Miongoni mwa nyaraka ambazo Mwananchi limeziona ni barua kutoka Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC) kwenda kwa uongozi wa TPR ya Novemba 18, 2011 ambayo sehemu yake inasomeka:

“Imethibitika kwamba Kampuni ya KCPL imekuwa ikijiendesha kwa hasara kwa miaka yote chini ya uongozi wa TPR. Mali (asset book value) za KCPL zilikuwa na thamani ya Shilingi bilioni 19…nakisi ya mtaji (capital deficit) ya shilingi bilioni 37, na hivyo kufanya kampuni hiyo kuwa mufilisi,”inaeleza sehemu ya waraka huo wa CHC.

Kadhalika sehemu ya taarifa ya watalaamu wa CHC iliyotumwa Serikali ambayo pia gazeti hili limeiona inasomeka kuwa: “Utendaji wa KCPL tangu ubinafsishwe umekuwa hauendani na matarajio Serikali kutokana na kampuni hiyo kushindwa kuendeleza mradi wa makaa ya mawe na uzalishaji wa umeme wa Kiwira kwa wakati uliopangwa. Aidha, KCPL ilishindwa kuwalipa wafanyakazi mishahara yao ya miezi 15, kiasi cha takribani Sh2bilioni ”.

Kutokana na hali hiyo kiasi cha Sh40 bilioni kilichotengwa na Serikali ndicho kilichozua mvutano bungeni wakati wa mjadala wa bajeti ambapo Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrodi Mkono alihoji sababu za kupelekwa fedha hizo hali mgodi huo ukiwa umeishaisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya fedha.

Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo jana alisema hawezi kujibu hoja ya Mkono kwa maelezo kwamba Mbunge huyo ana maslahi katika mgogoro huo kutokana na kuwa mwakilishi wa Kampuni moja nchini Dubai.

Taarifa ya hesabu
Taarifa ya hesabu inathibitisha kwamba KCPL fedha ambazo kampuni hiyo ilipewa kwa dhamana ya BoT matumizi yake hayana maelezo na kwamba kinachoonekana katika taarifa ya mkaguzi, ni hasara pamoja na malimbikizo ya madeni.

Kwa kuzingatia taarifa hiyo, kikao cha wataalamu kilichoratibiwa na CHC katika taarifa yake ya Novemba 10, 2011 ilibainisha kwamba mwekezaji Tan Power hakutumiza wajibu kulingana na mkataba wa ubia ulioingia kati yake na Serikali.

“Mwekezaji hakuwa anaendesha mgodi kwa misingi ya utawala bora. Hili linathibitishwa na kushindwa kwake kutunza kumbukumbu za hesabu za Kampuni kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2008,”ilieleza sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza:

“Pia menejimenti ya KCPL imeshindwa kumpatia mtaalamu, kumbukumbu za vikao vya Bodi za Wakurugenzi ili kuthibitisha utendaji na uamuzi mbalimbali uliokuwa ukifanywa na Bodi kwa madai kuwa katika kipindi chote kampuni ikiwa chini yao hakukuwa na kikao chochote kilichoitishwa wala kukaa kujadili masuala ya KCPL”.

Kamati hiyo katika mapendekezo yake kwa Serikali ilitaka majadiliano ya kuurejesha mgodi huo kwake yazingatie kushindwa kwa TPR kukidhi matarajio ya kufufua mgodi na kuendeleza mradi wa uchimbaji wa makaa ya mawe kwa kujenga kituo cha kuzalisha Megawati 200 za umeme na njia ya kusafirisha umeme huo kutoka KCPL hadi kwenye gridi ya taifa mjini Mbeya, umbali wa kilometa 70.

“Utendaji wa KCPL baada ya kubinafsishwa umedorora na kusimama kabisa. KCPL ipo katika hali mbaya kifedha na imeshindwa kujiendesha ikiwa ni pamoja na kushindwa kuwalipa wafanyakazi mishahara kuanzia Agosti 2008 hadi hivi sasa,”ilieleza taarifa hiyo na kuongeza:

“Ni maoni yetu kwamba TPR hawastahili kulipwa pesa yoyote na Serikali kwani KCPL ni kampuni mufilisi na hivyo hisa zao hazina thamani yoyote. Vilevile Serikali katika kuchukua umiliki wote wa kampuni inamaanisha pia kuchukua madeni ya kampuni yanayofikia Shilingi bilioni 56”.

Msimamo wa wabunge
Mkono alilitaka Bunge kuunda Kamati Teule kwenda kuchunguza ufisadi huo, huku akihoji sababu za Serikali kutengea mabilioni ya shilingi wakati ikifahamu uhalisia wa mgodi huo.

Hata hivyo jana, mara baada ya Profesa Muhongo, kumtupia kombora hilo, Mbunge Mkono ambaye ni Mwanasheria, aliomba Mwongozo kwa Spika Anna Makinda ili kutaka ufafanuzi wa kauli ya Waziri Muhongo kuwa yeye ana maslahi na mgogoro huo.

“Namheshimu sana Profesa Muhongo, lakini mimi jana nilipochangia nilitumia kanuni ya 61 kueleza maslahi yangu katika mgodi huu,”alisema Mkono.

Hata hivyo hivyo, Spika Makinda alisema kama Mbunge huyo alitangaza maslahi yake sawa na hata kama aliandika kwa maandishi lakini waziri wakati anajibu hoja hakumtaja.

Hata hivyo, Mbunge wa jimbo la Ubungo, John Mnyika kwa kutumia kanuni ya 68 kifungu kidogo cha 7, alimtaka Waziri Profesa Muhongo atoe majibu ya hoja ya Kiwira kama ilivyochangiwa.


Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Kabwe Zitto pia, alisimama kwenye kiti na kutaka mwongozo juu ya jambo hilo, lakini hata hivyo naye hakupewa fursa.


Spika Makinda alizima hoja hiyo kwa alisema hajui alichokuwa akisema waziri na kufunga mjadala huo kwa kumpa fursa Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Godluck Ole Medeye kuendelea kujibu hoja za wabunge.


Hata hivyo, nje ya Bunge, akizungumza na Mwananchi, Mkono alisema anaamini Profesa Muhongo, amepotoshwa alipokuwa akitaka kujibu hoja zake juu ya ufisadi wa Mauzo ya Mgodi wa Kiwira.


“Tayari nimewasiliana na Waziri na naamini atatoa taarifa nyingine bungeni kuhusiana na alichokisema kwani ukweli unabaki pale pale kuna ufisadi katika mauzo ya mgodi wa Kiwira,”alisema Mkono.
 
jana baadaya prof muhongo kuchangia bajeti, kuna thread nyingi sana za kumpongeza kama aliwasilisha vizuri na mwanzo mwema na kuhusu tatizo la kiwira alisema hivi,"Hata hivyo jana, mara baada ya Profesa Muhongo, kumtupia kombora hilo, Mbunge Mkono ambaye ni Mwanasheria, aliomba Mwongozo kwa Spika Anna Makinda ili kutaka ufafanuzi wa kauli ya Waziri Muhongo kuwa yeye ana maslahi na mgogoro huo."
Kimsingi maana na dhana ya kuitwa prof, maanake mchambuzi mwenze kuwa na data zenye uthibitisho.Kwa msitakabari huu majibu ya muhongo yalikuwa ya kisiasa, na naamini tatizo hili nalijua ila angejibu itakiwavyo angechochea bajeti iwe na maswali mengi hata yeye wakati wa kuwasilisha , angepata usumbufu sana.
nachela kusema, dhana ya uwazi hapa ni ngumu na serikali inaficha mambo ya msingi kuhusu tatizo hili, na majibu yake ni kiCCM mno huku huku mrad huo si WA CCM bali ni mali ya wapiga kura na walipa kodi
wote.
kwa hili nafikiri mtendaji mkuu nape wa mnawiye labda analijua vizuri
 
Kutengewa kwa mwaka TZS40bil karibu sawa na USD25mil ni wizi mkubwa - wanaendesha nini? Za mishahara ama nini? Hii ni pesa nyingi sana. Pale ufundi na uzoefu kidogo, sululu na spedi vinatosha kuchimba mkaa.

Mgodi wa Kiwira ni mdogo sana na uneconomical kuendeshwa na serikali, binafsi naona bora wangekodishiwa artisan miners ama wachimbaji-vibarua wangechimba kwa vipande na kuuza mkaa kwa wazalishaji umeme - kama kweli kuna mtambo mpya wa kufua umeme. Hivi kweli pesa hiyo itapelekwa Kiwira ama on papers tu - mimi nadhani inaishia Swiss Banks. Hakuna mtu mwenye akili timamu anaweza toa pesa bwelele kiasi kikubwa hivyo kupelekwa kwenye kamradi kama KIWIRA. Haya yote ni matatizo ya kuamuliwa mambo na watu irresponsible waliopo Dar ambao hawajuai chochote kuhusu site ama uchimbaji mkaa bali wanachojua ni matumbo yao tu na uzembe.
 
Back
Top Bottom