Ya Bamkwe yangalipo: Safari yangu ya gerezani bila kupitia polisi wala mahakamani

Jamhuri ya Zanzibar

Senior Member
Jul 17, 2012
126
195
Na; Ahmed Omar

UTANGULIZI

Kwa takriban miaka kumi hivi tokea kufanyika kwa Mapinduzi ya 1964 palikuwa pakifanywa uhalifu mkubwa hapa Zanzibar kwa jina la Mapinduzi hayo. Moja ya eneo maarufu ambalo lilikuwa limeshtadi kwa mateso na ukaltili ni gereza la Kwa Bamkwe. Huku gerezani Kwa Bmkwe, misamiati huruma na ubinadamu ilikuwa haifahamiki. Binadamu kama sisi walikuwa wanakatwakatwa, wananyongwa na kufukiwa wakiwa wazima. Wako wengi walionekana wakipelekwa Kwa Bamkwe lakini hawakuonekana tena wakirejea hadi leo.

Tokea kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa Tanzania, Zanzibar imekuwa ikikabiliwa na vitendo vya kihalifu, mateso, uwekaji watu vizuizini, ubakaji na mauwaji vinavyotekelezwa na vyombo vya Dola hususan kabla na baada ya kufanyika Uchaguzi Mkuu. Uhalifu huu wa kidola umekuwa ukizua taharuki kubwa ndani ya Zanzibar na kupelekea chuki, hasama na mifarakano baina ya watawala na raia kwa upande mmoja na baina ya kambi mbili za kisiasa zilizopo Zanzibar, kwa upande wa pili.

Mwaka 2010, viongozi wetu wapenzi, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dr. Amani Karume na Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, walidhamiria kwa dhati kabisa kupiga mstari mwekundu kwa siasa hizo za chuki, hasama, mifarakano, kuumizana na kuuwana, kupitia Maridhiano ya Novemba 5, 2009, ambayo pamoja na mambo mengine yalizaa Serkali ya Umoja wa Kitaifa. Azma hii hata hivyo haikudumu kwa muda mrefu kwani waliokabidhiwa hatamu za nchi yetu baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 walijali zaidi maslahi ya vyeo na matumbo yao badala ya maslahi mapana ya nchi yetu. Pamoja na msingi mizuri iliyowekwa kufuatia Maridhiano hayo, nchi yetu ilirejeshwa tena katika mkwamo mpya wa kisiasa baada ya kuvurugwa kwa makusudi kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Kama sote tunavyokumbuka, baina ya mwaka 2015 hadi mwaka 2020, hali ya kisiasa ilikuwa mbaya zaidi kote Bara na Zanzibar. Utawala wa kidikteta chini ya Hayati Magufuli uliweza kutamalaki nchini kuliko ilivyowahi kuwa tokea nchi yetu iingie katika ushindani wa vyama vingi vya siasa, na mara nyengine taswira ilikuwa ya kutisha hata kuliko tokea tupate uhuru. Utawala huo wa mkono wa chuma usiojali sheria, katiba wala ubinadamu uliweza kumdhibiti kila alietamani kuona haki, demokrasia na utawala bora vitamalaki ndani ya nchi yetu. Hivyo basi hali hiyo ikapelekea nchi kuingia katika giza nene lililopelekea Uchaguzi Mkuu wa 2020 kuwa wa kibabe zaidi, usiojali sheria zaidi na wa kihalifu zaidi uliojaa mateso na mauwaji.

Mimi ninaeandika makala hii ni mmoja tu kati ya mamia ya wahanga wa uhalifu uliofanywa na vyombo vya Dola kupitia jina la Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 hapa Zanzibar. Nimeona ipo haja ya kuhadithia kwa urefu ili kumbukumbu ziwekwe na kila mpenda haki za binadamu na demokrasia ndani ya nchi yetu na dunia kwa manufaa ya sasa na ya baadae. Nilikuwa mmoja wa vijana 40 waliokabidhiwa jukumu la kusimamia kituo cha kujumlisha na kuhakiki matokeo ya Uchaguzi Mkuu (Party Tallying Center) ya Mgombea wa Urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad. Tulikabidhiwa jukumu hilo na Chama cha ACT-Wazalendo na kituo chetu cha kufanyia kazi hiyo kilikuwa ni Hoteli ya Mazson iliyopo Shangani Zanzibar. Hoteli ya Mazson mara kadhaa hukodiwa na Chama hicho kwa ajili ya kufanya shuguli mbali mbali za Chama.

MAZSON.jpg
Tallying Center ya ACT-Wazalendo Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa 2020

MATESO WAKATI WA UVAMIZI

Usiku wa tarehe 28, Oktoba, 2020, hapo Mazson Hotel, kiasi cha saa 4 usiku, tukiwa tunakaribia kufunga jukumu tulilokabidhiwa la kujumlisha na kuhakiki matokeo ya Mgombea wa Urais wa Zanzibar wa ACT-Wazalendo, tulivamiwa na kundi kubwa la askari wanaokadiriwa kufikia mia moja waliokuwa wamevalia sare za JWTZ, wakiwa wameziba nyuso zao na wameshikilia silaha nzito za kivita mikononi, marungu, vipande vya nondo na nyenzo nyengine mbali mbali walizozitumia kwa ajili ya kutugeuza kuwa kama mateka wa kivita. Walituvamia kijeshi kwa kufyatua risari na kupiga mateke mlango mmoja baada ya mwengine hadi walipofika katika ukumbi tuliokuwa tukifanya kazi yetu.

Waliyotufanyia wanajeshi hao ni ya kusikitisha na kuhuzunisha. Bila ya kutueleza wametumwa na nani au kosa letu ni nini, walianza kututishia kifo, kuvunja vunja vifaa na miundombinu yote tuliyokuwa tunafanyia kazi, kutupiga, kutukatakata kwa visu na singe za bunduki zao, kutuvunja miguu, uti wa mgongo, kutupasua midomo, kututumbua macho n.k. Kwa upande wangu mateso ya uvamizi yaliniathiri uti wa mgongo kwa kupata maumivu makali na shida ya kuendelea hata kukaa kitako katika eneo hilo. Kwa namna nilivyokuwa nikijiskia maumivu kila mkao ninaokaa, sikutegemea kama nitaondoka nikiwa hai sehemu ile. Wakati tumelazwa kifudifudi, mwanajeshi mmoja aliekuwa karibu yangu aliniwekea buti lake juu ya shingo yangu na kuanza kunishindilia kwa nguvu zake shingoni. Nilipopiga kelele kwa maumivu na kukosa pumzi, aliniambia “wee gaidi nyamaza kimya”. Shingo yangu hadi sasa naandika makala hii haiwezi kugeuka kulia wala kushoto kwa ukamilifu pamoja na tiba ya muda mrefu. Tindi zinazofanya sehemu ya shingo zimepishana kusiko kawaida, nyengine zikizidi nyuma na nyengine zikizidi mbele.

Miongoni mwetu walikuwemo wanawake watano kati yao ni wadogo wasiozidi miaka 20. Hawa bila huruma au kujali jinsia yao, walivunjwa vunjwa na kukaa walemavu kwa zaidi ya mwaka mmoja. Pia walidhamiria kuwadhalilisha wanawake hao kijinsia mbele yetu wakati wa uvamizi pale Mazson Hotel. Askari mmoja alimfika mtoto mmoja wa kike na kumuagiza avue nguo kwa ajili ya kumuingilia. Kwa sababu walifyatulia risasi taa zote, na zogo la piga piga lilidumu kwa muda mrefu, na kila mmoja wetu alikuwa katika taharuki yake sikufahamu tena muendelezo wa kitendo cha kutaka kumbaka Yule mtot wa kike kama kilikamilishwa au laa.

Sakafu yote katika horofa tuliyofanyiwa uhalifu huu ilitapakaa damu zetu kila upande. Mateso ya Mazson Hotel yalidumu kwa takriban saa tano, kutanzia saa 4 usiku hadi kiasi saa 9 usiku. Mara baada ya kumaliza kutuadhibu kwa kiasi walichopenda pale Mazson Hotel, wakatufunga mikono nyuma na vitambaa vya macho. Wakatuamrisha tutoe kila kitu tulichokua nacho na tuwakabidhi ikiwa ni pamoja na simu za mikononi na fedha taslim. Binafsi nilikuwa na kiasi cha shilingi milioni moja na laki mbili mfukoni. Pesa hizi ni msahara wangu ambao nilikuwa nimetoka kuuchukua benki na pesa za malipo kwa baadhi ya shughuli za uchaguzi za Chama cha ACT-Wazalendo nilizokuwa nikizisimamia. Pesa hizi walizotupokonya pale Mazson Hotel hatukuziona tena hadi leo. Jeshi la kufanya uvamizi kama huu, kuwavunja vunja watu wasio na hatia, waliokuwa hawakugoma kukamatwa na baadae kuwapora, linaweza kuwa ni jeshi lenye upekee hapa duniani.

KUSAFIRSHWA KUELEKEA GEREZA LA HANYEGWA MCHANA

Baada ya kukamilika kwa mateso ya uvamizi pale Mazson Hotel, yalifuata mateso ya kutusafirisha kutupeleka katika gereza la Hanyegwa Mchana, Wilaya ya Kati, Unguja. Tukiwa hivyo tulilazimishwa kutembea kuelekea yalipo magari ya kijeshi ambayo hatuyaoni na kila aliekosea muelekeo alipigwa rungu moja baada jengine mpaka alipofankiwa kuligusa gari. Kazi ya kuyapanda magari makubwa ya kijeshi huku tukiwa hatuoni na tumefungwa mikono nayo ilikuwa sehemu muhimu katika mateso yetu. Unalazimishwa uruke na utue katika kingo za gari la kijeshi kwa tumbo lako au kifua na ujiingize katika gari kwa kujisukumiza na kujiviringisha.

Zoezi la kupanda gari la wafungwa lilikuwa gumu kwetu sote hivyo tulijikuta tunaruka na kuanguka chini mara kadhaa huku tukiangukiana vifuani na vichwani na kuumizana wenyewe kwa wenyewe. Halkadhalika kila alieshindwa kuingia katika gari wakati akiwa anahangaika kupanda au alikua anapigwa rungu ili kumhimiza kuingia katika gari. Wengi wetu tulijikuta tunaanguka chini ya gari na kunyanyuka mara kadhaa bila kufankiwa kupanda. Baadhi yetu mwishoe waliweza kujiingiza garini kwa mateso makubwa huku wengine wakikamatwa na wanajeshi na kulengwa katika gari kama viroba.

Ndani ya gari tulikaa mkao wa mateso na maumivu makubwa. Tulikuwa wengi na gari ilikuwa ndogo kwa mateka 40. Tulilaliana kama viroba vya viazi kila mmoja akimkalia mwenzake ama kichwani tumboni au kifuani. Kila mmoja alikuwa anapiga kelee za maumivu angalau aweze kupata msaada wa kubadili mkao ndani ya gari hilo lakini hakuna mwanajeshi aliejali. Ukipiga kele “afande naomba nisaidie amenikalia kichwani huyu”, afanye alikuwa anajibu, “wewe nyamaza”, huku anakupiga mkono wa bunduki.

Pamoja na kwamba Hanyegwa Mchana sio mbali sana kutoka Mjini lakini safari yetu ilichukua zaidi ya dakika 45. Nadhani njia zilizotumika zilikuwa za mzunguko sana ili kutufanya sisi tusiweze kujua sehemu halisi tunapopelekwa. Tukiwa ndani ya gari la wafungwa tuliendelea kufungwa mikono kwa nyuma na vitambaa vyeusi machoni katika safari yote ya kuelekea gerezani.

KUWASILI GEREZANI

Tulifika gerezani Hanyegwa Mchana kiasi cha saa 9 usiku. Hapo tulitenganishwa na wanawake na hatukuwaona tena hadi siku ya kuachiwa. Tulidhalilishwa kwa kulazwa kwa matumbo yetu sakafuni, ndani ya uzio wa gereza bado tukiwa na maumivu na vidonda vya mateso ya Mazson Hotel na bado tukiwa tumefungwa vitambaa vya macho na mikono ikiwa imefungwa kwa nyuma. Waliendelea kutupiga mateke na mikwaju. Hapa ndio kwa mara ya kwanza nilimuona Bwana Nassor Mazrui, Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Zanzibar, ambae tulikamatwa pamoja nae. Alikuwa pembeni yangu anapata mateso ya aina yake. Wanajeshi wanampandia mgongoni. Alikuwa anapiga mayoe anasema “wanangu basi tena, mtaniuwa, mimi ni mgonjwa”. Wale wanajeshi walikuwa wanamcheka na kumwambia “wewe si ulitwita wasenge pale katika uwanja wa Mnazi Mmoja, basi leo utatuona wasenge”. Katika chumba cha gereza alichoingizwa muda wote alikuwa akisikika akipiga mayoe na kulia kwa ukali wa mateso waliyokuwa wanampa mchana na usiku. Kwakweli siwezi kuyasimulia kwa ukamilifu mateso waliyompa Mazrui.

GEREZANI.jpg
Gereza Jipya la Watoto, Hanyegwa Mchana, Wilaya ya Kati, Unguja

Baada ya hapo walitufungulia mikono na kutuondolea vitambaa vya macho. Tulitakiwa tuvue nguo zote na tubakishe chupi tu. Baadae tukaingizwa katika vyumba vya gereza. Hatukujua tupo wapi kijeografia, ila tulifahamu tupo gerezani. Tulilala katika sakafu yenye baridi kali. Usiku mzima tulikuwa tunatetemeka kwa baridi kali kwa muda wa siku zote nane za maisha ya gerezani. Ndani ya chumba cha gereza tuliwakuta wenzetu kiasi thelathini hivi wakiwa wameshatangulizwa humo kutoka maeneno mbali mbali ya Unguja kutokana na visa vya uchaguzi. Baada ya kuchangayika na sisi, tulifikia idadi ya watu 65 hivi kwa jumla ndani ya chumba hicho kimoja cha gereza.

MAISHA NA MATESO YA GEREZANI

Tulikaa gerezani hapo kwa muda wa siku nane, yaani kuanzia siku ya Jumatano, tarehe 28 Oktoba, 2020, hadi Jumatano, tarehe 04 Novemba, 2020. Siku nane hizi tuliziona sawa na mika nane kutokana na umaaumu na ukubwa wa mateso tuliyokuwa tukipewa. Ni sawa tu na yale tunayoyasoma vitabuni ya Kwa Bamkwe katika zama za Mapinduzi. Tuliwekewa ratiba maalum ya kupigwa na kuadhibiwa kwa kila siku. Tulikuwa tunapigwa mara mbili kwa siku. Mara moja ni kabla ya kunywa chai ya asubuhi; na mara ya pili ni kiasi saa 9 hivi baada ya chakula cha mchana. Katika mara zote mbili, kiasi cha askari 20 wenye sare za aina tofauti za Vyombo vya ulinzi vya Jamhuri ya Muungano na vikosi vya SMZ huingia ndani ya chumba chetu cha gereza wakiwa na bunduki, marungu, waya, vipande vya mbao na vipande vya nondo. Hapo sote hutakiwa tukae mikao wanayotaka wao kama vile kulala kifudifudi na kusimama huku tukiegemea ukutani kwa tumbo kwa ajili ya kupigwa waya na marungu katika makalio na mgongoni. Mkao mwengine ni kitako na kunyoosha miguu na kusimama kuegemea ukuta kwa migongo kwa ajili ya kupigwa vipande vya mbao na vyuma katika vifundo vya miguu na mikono. Walitupiga sana walitupasuapasua kwa kadri walivyopenda bila huruma na chumba cha gereza kilitapaka damu ambazo tulikuwa tunazisafisha kila siku.

Walitaka watajiwe miongoni mwetu waiokuwa na dhamana ya kituo cha ujumlishaji matokeo pale Mazson Hotel. Wenzetu walitaka majina manne nikiwemo mimi. Sisi wane tulipata mateso maalum. Baada kipigo cha jumla kumalizika, tuikuwa tunaitwa sisi na kupigwa upya. Wakati wanatupiga, walikuwa wanasema“nyinyi ndio wakuu wa uchakachuaji wa uchaguzi wetu, sisi tunachagua Rais wetu, nyinyi mnabadilisha”.

KIPIGO.jpg
Kipigo Nilichopewa na Vyombo vya Dola Kufuatia Matukio ya Uchaguzi
Mkuu wa 2020, Zanzibar

MATESO KATIKA MAHOJIANO

Gerezani kuliendeshwa zoezi la mahojiano. Wakati wa kupelekwa na kurejeshawa katika chumba cha mahijiano tulifungwa vitambaa vya macho na mikono nyuma. Tulilazimishwa kutembea kichura tukiwa hatuoni mbele huku tunapigwa waya na marungu mpaka tunafika katika chumba cha mahojiano. Ndani ya chumba cha mahojiano tulukuwa tunatakiwa kukaa kikato na kunyoosha miguu kuwaelekea maafisa usalama kiasi ishirini hivi ambao ndio walikuwa wanatuhoji. Kabla ya mahojiano walitufunguwa kitambaa cha macho na kamba za mikono. Maafisa wa usalama ambao hawakuziba nyuso zao na ambao wengine tunawatambua walikuwa wanatuuliza maswali kwa kipindi kisichopungua saa moja.

Msawali yao ni mengi lakini ukiyatathmini maswali hayo utagundua walikuwa wanalenga kubaini mambo yafuatayo. Mosi, pamoja na uchaguzi wote kuharibiwa na mawakala wa upinzani kupigwa na kufukuzwa katika vituo vya kuhedabia kura, ni kwa vipi matokeo ya uchaguzi yaliweza kuwafikia ACT-Wzalendo? Pili, ni akina nani walioko ndani ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ambao wanashirikiana na ACT-Wazalendo wakati kwa uchaguzi huu hakuna afisa yoyote mwenye mafungamano na ACT ndani ya Tume? Tatu, matokeo ya uchaguzi ambayo Kigogo wa mtandaoni alikuwa anayatoa yalitokana na ACT-Wazalendo kupitia kituo chao cha kujumlishia? Na kama ndio ni akina nani ndani ya ACT-Wazalendo walikuwa wakifanya kazi na Kigogo? Nne, walikuwa na dhamira ya kutushawishi na kutulazimisha tukubali uongo kwamba pamoja kazi ya kujumlisha matokeo tuliokuwa tunaifanya, Mazson Hotel pia ilikuwa ni kituo cha ACT-Wazalendo cha kuhifadhia mabomu.

Wakati wa mahojiano, maafisa wa usalama walitulazimisha tutoe majibu wanayoyataka wao na kama hatukufanya hivyo tulikuwa tunapata mateso mwanzo hadi mwisho wa mahojiano. Wakati mahojiano yakiendelea, askari alievalia kijeshi, mwenye bunduki, rungu, alikuwa amesimama nyuma ya mhojiwa kwa ajili ya kupokea amri ya kupiga. Askari huyu alikuwa akitupiga mgongoni na katika nyayo za miguu huku marungu bila huruma. Baada ya mahojiano kumalizika tulikuwa tunalazimishwa kujaza fomu ya mashtaka ambamo tulipewa mashtaka ya uongo ya kukutwa mabomu.

KUTOKA GEREZANI

Baada ya CCM kumaliza kufanya walichokusudia kufanya na Rais kuapishwa, sisi mateka wa uchaguzi sote tulitolewa magerezani tukiwa hali zetu ni mbaya sana. Kwa juhudi za ACT-Wazalendo na familia zetu tulianza matibabu ya awali katika hospitali mbali mbali, Zanzibar na Bara. Kati yetu wapo waliopata athari za kudumu katika mili yao kama uti wa mgongo, macho, kichwa, miguu n.k. Baadhi yetu hadi sasa hatukupata matibabu ya uhakika ya kuondoa athari hizo kutokana na kushindwa kumudu gharama. Siku ya kuachiliwa huru, kuna maafisa wa usalama wa taifa walikuja katika chumba chetu cha gereza na kututisha. Walitueleza kuwa tusikubali kutumiwa na Marehemu Maaim Seif kwa sababu yeye hawezi kukamatwa analindwa na itifaki za kidiplomasia za kimataifa hivyo tutakaouliwa ni sisi. Walitusistiza kuwa baada ya kutoka gerezani tukae kimya na yeyote atakaethubutu kufungua mdomo wake atarejeshwa gerezani.

AHADI HEWA YA RAIS MWINYI KUTULIPA FIDIA

Baada ya uhuni ulioitwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kumalizika, sisi wahanga tukiwa bado vitandani na hospitalini tulipata taarifa kwamba Rais Mwinyi alimwita Marehemu Maalim Seif kuzungumza nae juu haja ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kutibu vidonda vilivyotokana na Uchaguzi Mkuu. Maalim Seif kwa uungwana wake, kwa kuweka maslahi ya nchi mbele na baada ya kushauriana na viongozi wenzake na wanachama waliridhia wito huo wa Rais Mwiny. Chama cha ACT kikafanya uwamuzii wa kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Hata hivyo Marehemu Maalim Seif aliwekeana makubaliano kadhaa na Rais Mwinyi kabla ya kukubali kuingia katika serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kuridhiana na kusameheana yaliyotokea na kusonga mbele. Baadhi ya makubaliano hayo ni yale yanayotuhusu moja kwa moja sisi wahanga wa mateso yaliyotokana na uchaguzi mkuu. Marehemu Maalim Seif na Rais Mwinyi waikubaliana wahanga wa mateso na udhalilishaji katika uchaguzi Mkuu wa 2020 walipwe fidia na serikali. Kwa masikitiko makubwa suala hilo la ulipaji fidia halikutekelezwa hadi sasa.

HITIMISHO

CCM wanapaswa kufahamu kuwa Watanzania hawapo mbali na dunia bali wanaona kila kinachoendelea duniani kote. Upole, ukimwa na uungwana wa Watanzania haumaanishi uzembe au woga bali una mshindo mkubwa. Utulivu na uvumilivu wa Watanzania haumaanishi wao ni wanyonge na ambao wanaweza kutawalika kwa mabavu milele. Ipo siku wanaweza kusema hapana na nchi yetu ikaingia katika maafa makubwa. Watawala hawana budi wajijitafakari kama bado wanahitaji kuendelea kuendesha nchi kwa kutumia gereza na mtutu wa bunduki. Dunia inabadilika kwa kasi katika kila Nyanja inayogusa maisha ya mwanadamu, hivyo na Tanzania inalazimika kufuata upepo wa mabadiliko hayo. Tanzania ijifunze kutoka hata kwa jirani zetu kama Kenya badala ya kubaki na kung’ang’ania ukiritimba na ubabe katika kuongoza nchi.

Tunapongeza juhudi za Rais Samia za kuanzisha mchakato wa mazungumzo na vyama vya siasa sambamba na kuanzisha mchakato wa kutafuta maoni yenye dhamira ya kufanya mabadiliko ya mifumo ya kiseria na kidemkrasia ndani ya nchi yetu. Tunaunga mkono juhudi hizi na tunaiomba sana serikali iweke udhati wa kutimiza dhamira hii ili tuweze kupata mabadiliko ya Katiba, sheria na mifumo ya kidemkrasia itakayoiweka nchi yetu pahala salama zaidi na kuepusha migogoro siku za usoni.​
 
Pole sana,nakusihi wewe na wenzako,muendelee kutafuta fidia na mtibiwe kikamilifu,athari mnazoziona saa hizi,nyingine zitajitokeza baadae msipotibiwa vilivyo.Poleni sana,mageuzi naona yafanyike kwenye vyombo vyote vya ulinzi na usalama,watu wasiishie kusema Polisi tu,kisa tuko nao muda mwingi uraiani,hata hao JW,Magereza na wengine,wangekua uraiani full,malalamiko yawezekana yangekua zaidi,siasa imepenyq kila mahali.
 
Lo, Aisee Hali Hii inasikitisha sana, CCM si Watu wema kamwe.
Kumbe watu hawa wanatabasamu machoni pa watu tuu na ni chuwi wakiwa katika mikakati yao ya kuiba kura na kunyakua madaraka kwa mabavu.
-Walaaniwe wahalifu wote wa kidola wanaotumia vyombo vya usalama vibaya.
-Bali walaaniwe wote walioingia Madarakani kwa kuwaumiza wengine huku wakijuwa na kudhamiria kuyafanya maovu hayo.
-Tunamshukuru Mungu kwa Kutuondoshea Kichawa cha Shetani Nchini petu,
-Tunamuomba Mungu akisambaratishe na Kiti chake kisiwepo tena Nchi hii.
Mungu Ibariki Zanzibar, Mungu Ibariki Tanganyika, Mungu Ibariki Tanzania.
Mungu wabariki Watanzania na uwapiganie dhidi ya kundi hili ovu la Manyangau wala damu za watu.
Amin Amin Amin
 
Mambo ya siasa karibu Dunia nzima yako hivyo. Kuna wengi wanaumia na pengine kufa kwaajili ya vigogo wachache. Pole Sana isee
 
Haiwezi kuwa ni uongo
Kama nchi tulikuwa kwenye kipindi kibaya sana.
Kuna mmoja alikuwa waziri wa mambo ya ndani
Katika kipindi chake watu ,waliuliwa,kutekwa n.k
Leo kawa waziri wa FEDHA.
Aiseee
Ni hatari kwa kweli, kama ni KWELI
 
Back
Top Bottom