Waziri wa Ulinzi, Bashungwa akagua zoezi la usafirishaji misaada kwa Malawi

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,814
11,991

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Lugha Bashungwa (Mb) ametembelea Ofisi za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Kanda ya Dodoma, kwa lengo la kujionea utekelezaji mzima wa zoezi la usafirishaji wa msaada wa chakula kwenda nchini Malawi. Zoezi hili linatekelezwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kutumia magari pamoja helikopta.

Utekelezaji huu, ulioanza tangu tarehe 18 Machi, 2023 unatokana na Agizo la Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, linaloitaka Wizara ya Ulinzi na JKT kupitia JWTZ kusafirisha misaada iliyotolewa na Serikali ya Tanzania kwa wananchi wa Malawi. Misaada hiyo inajumuisha Chakula tani 1000, mahema, mablanketi pamoja na misaada mingine ya kibidamu, kufuatia maafa yaliyosababishwa na kimbunga cha kitropiki kiitwacho Freddy.

1.JPG

Akiongea mara baada ya kukagua zoezi hilo, Bashungwa amempongeza Rais na Amiri Jeshi Mkuu, kwa kutimiza miaka miwili ya kuliongoza vyema Taifa letu, na akatoa wito kwa watanzania kumuunga mkono, katika harakati zake katika kuwaletea maendeleo.

Aidha, amesema kuwa Wizara ya Ulinzi na JKT itaendelea kujituma na kutekeleza maagizo na maelekezo yake kila wakati.
2.JPG

3.JPG

Vilevile, amesema kuwa kwenye maelekezo ya Rais aliyoyatoa kwa Wizara kuhusu msaada unaoenda kwa jirani zetu, ndugu zetu wananchi wa Malawi. Rais alielekeza vifaa (logistics) kupelekwa na kusimamiwa na JWTZ, kuhakikisha kuwa misaada inafika kwenye vituo ambavyo vinapokea misaada hiyo, kwa ajili ya kusafirishwa kwenda kwa ndugu zetu wa Malawi.

Aidha, ameahidi kuwa maelekezo hayo ya Rais na Amiri Jeshi Mkuu ataendelea kuyasimamia kwa weledi mkubwa.

Ametumia fursa hiyo pia, kumpongeza Mkuu wa Majeshi, Jenerali Jacob John Mkunda pamoja na Makamanda wote wanaomsaidia katika JWTZ , kwa namna ambavyo wamepokea maelekezo ya Mheshimiwa Rais na kuyasimamia vizuri na ndani ya muda alioelekeza kwa ndugu zetu, itapeleka kwa wakati kama alivyoelekeza Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu.

Amewashukuru pia, Wizara ya Kilimo chini ya Hussein Bashe (Mb) pamoja na timu yake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb), kwa namna wanavyoendelea kushirikiana katika kutekeleza jukumu hili.

Kwa uratibu mzima wa kiserikali, amemshukuru Waziri Mkuu, Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa kwa kuendelea kuratibu zoezi hili, kwa ukaribu.

Aidha, amemshukuru Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene (Mb) anayeratibu Wizara zote kuhakikisha maagizo yanatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati. Kwa maana hiyo, amempongeza kwa namna anavyoendelea kushirikiana nao kwa pamoja katika kutekeleza maagizo ya Mheshimiwa Rais.
4.JPG

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Utawala kutoka Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Dkt. Saneslaus Boniface Chandaruba amemshukuru Waziri kwa kutenga muda wake na kutembelea Wakala huyo kwa lengo la kukagua utekelezaji wa maagizo hayo, unaofanywa kwa ushirikiano Mzuri na kwa nidhamu wa hali ya juu ya Wanajeshi wetu.

Aidha, Dkt. Chandaruba amesema kuwa mpaka sasa tani zipatazo 380 zimeshasafirihwa kuelekea Malawi, kutoka kwenye kituo cha Kanda ya Dodoma ambayo imetoa tani 180 na tani zingine 200 kutoka kituo cha Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Kilichopo Iringa.

Athari za kimbunga kilichozikumba nchi ya Malawi, zimesababisha mamia ya watu kupoteza maisha, wengine kujeruhiwa, upotevu wa mali pamoja na uharibika kwa miundombinu. Kufuatia athari hizo imemlazimu Rais wa Malawi, Mheshimiwa Lazarus Chakwera kuziomba Taasisi za Kimataifa kutoa misaada ya kibinadamu, ili kuwawezesha kukabiliana na maafa yaliyotokana na Kimbunga pamoja na Mafuriko.
 
Back
Top Bottom