Wanaharakati wakamwatwa

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,322
33,126
Analelia.jpg

Polisi akimkamata Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Ananilea Nkya katikati katika hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam jana.


Wanaharakati 16 wanaotetea haki za binadamu nchini, wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Ananilea Nkya na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Kijo Bisimba, jana walikamatwa na Jeshi la Polisi na kuhojiwa kwa zaidi ya saa tatu.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema wanaharakati hao walikamatwa baada ya kuwepo kwa taarifa za uvunjifu wa amani kutoka kwa wanaharakati hao.
Kenyela alisema baadhi ya wanaharakati walikamatwa wakielekea katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na wengine sehemu tofautitofauti jijini Dar es Salaam, wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe mbalimbali kwenye magari yao.
“Jeshi la Polisi ni taasisi inayojitegemea, hawa wanaharakati wamefanya kosa la jinai, na sisi tumefanya kazi yetu ya kulinda uvunjifu wa amani,” alisema.
Hata hivyo, baada ya kuhojiwa kwa muda mrefu, jeshi la polisi liliwaachia huru wanaharakati hao, baada ya kupewa dhamana.
Akizungumza baada ya kuachiwa huru, Nkya alisema kitendo walichokifanya askari polisi ni cha unyanyasaji na kwamba hawatakata tamaa kupambana na kupigania haki za Watanzania.
“Kitendo kilichofanywa na Jeshi la Polisi ni cha unyanyasaji, kwa sababu sisi hatukuandamana leo (jana), tulikuwa katika magari yetu kwenda kuangalia serikali imetekeleza vipi maagizo yetu baada ya sisi kufanya maandamano hapo juzi,” alisema.
Aliongeza: “Sisi hatutakata tamaa, tutaendelea kupambana pale tunapoona haki haitendeki hasa kwa maslahi ya Watanzania.”
Pia aliwataka wale wote waliochangia kupotea kwa maisha ya Watanzania kwa kushindwa kuyatafutia ufumbuzi madai ya madaktari kuwajibishwa mara moja.
Hata hivyo Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), ambao walipiga kambi katika kituo cha Polisi cha Oysterbay kusubiri mwafaka wa wanaharakati hao, walilaani kitendo cha serikali kuchelewa kuyatafutia ufumbuzi madai ya madaktari na kusababisha kupoteza maisha ya Watanzania.
“Tuko hapa kwa ajili ya kuangalia mwafaka wa wenzetu wanaharakati waliokamatwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kutetea haki za Watanzania, hatutatoka hapa mpaka tuhakikishe wanatolewa bila masharti yoyote la sivyo tutafanya uamuzi mwingine,” alisema Mwenyekiti wa Bavicha, John Heche.
Heche alisema kitendo cha serikali kushindwa kufanya maamuzi ya haraka ni cha kulaaniwa kwa sababu itafika mahali nchi itakwenda pabaya.

Juzi wanaharakati hao waliandamana na kufunga barabara katika eneo la daraja la Salender na kuzuia magari kwa saa kadhaa, wakishinikiza serikali kukutana na madaktari waliokuwa katika mgomo.




CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom