Wanafunzi kuweweseka, kuanguka.Ni ugonjwa wa kisaikolojia, sio ushirikina

jamadari

JF-Expert Member
Feb 13, 2010
295
92


kuanguka.jpg
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Kitopeni iliyoko Korogwe mkoani Tanga, wakiwa nje ya chumba cha darasa. Mahudhurio ya wanafunzi wa kike katika shule hii yamedorora, kutokana na hofu ya kupatwa na ugonjwa wa , kuweweseka, kulia na kuanguka./Picha na Kizitto Noya​

Na Kizitto Noya
"KIWANGO cha taaluma nchini kitaporomoka kwa kasi kama hakutafanyika jitihada za makusudi kutafiti tatizo la wanafunzi kuweweseka, kuanguka darasani na kukimbia hovyo na kisha ikatolewa elimu stahiki kwa jamii,"

Hivi ndivyo anavyoonya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ulanga, Alfred Luanda kufuatia wanafunzi wa Shule ya Msingi Chirombola iliyoko wilayani humo, kukumbwa na tatizo hilo kiasi cha kusababisha mtafaruku mkubwa baina ya wazazi, walimu, wanafunzi na viongozi wa Serikali.

"Kimsingi hili ni tatizo na kuna haja kwa serikali na wadau wote wa elimu, kuunganisha nguvu ili kulitafutia ufumbuzi wa kudumu,"anaongeza kusema.

Kwa muda mrefu, tatizo la wanafunzi kuweweseka, kupiga kelele ovyo na hatimaye kuanguka, limekuwa likizikabili shule nyingi nchini hasa zile za msingi, na mara nyingi limekuwa likinasibishwa na vitendo vya ushirikina.

Sio Shule ya Msingi Chirombola pekee, matukio ya aina yameshatokea katika shule za msingi Kitopeni (Korogwe), na sekondari ya Hale (Korogwe). Kama haitoshi, kumbukumbu zinaonyesha tatizo hilo limekuwa maarufu miaka ya karibuni.

Yako matukio kadhaa kuanzia mwaka 2005 ambayo yamewahi kuripotiwa katika vyombo vya habari yakihusisha wanafunzi kuanguka, kupiga kelele ovyo au kupoteza fahamu.Kwa mfano, Agosti 2005, wanafunzi 24 wa Shule ya Msingi Uwanja wa ndege ya jijini Dar es Salaam, walikumbwa na hali hiyo ambayo haikuweza kuelezeka chanzo chake na hatimaye kuanguka.

Novemba 2006, wanafunzi 15 wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Mbuyuni pia ya jijini Dar es Salaam, walianguka na kupoteza fahamu wakati mwalimu wao akifundisha darasani.

Machi 2007, tukio kama hili likajirudia tena kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Lewa iliyopo wilaya ya Korogwe mkoani Tanga. Hawa walikumbwa na hali ya ajabu zaidi, kwani walikuwa wakikodoa macho, kucheka, kukimbia hovyo, kuanguka na hatimaye kupoteza fahamu.
Mei 2008 , wanafunzi 50 na mwalimu wao walikumbwa na ugonjwa wa kuanguka mkoani Dodoma kabla ya tukio hilo hilo kuwakumba

wanafunzi 30 wa Shule ya Msingi Mang’ula ya mkoani Morogoro mwaka 2009.
Mwaka 2010 ulibidi usubiri hadi Agosti 14 ambapo wanafunzi wa kike zaidi ya 100 wa Shule ya Kanda mjini Sumbawanga Rukwa walipokuwa wakipepesuka na kisha kupoteza fahamu.

Siku tano baadaye, wanafunzi zaidi ya 20 wa Shule ya Msingi Tumaini iliyopo Tabata jijini Dar es Salaam nao wakakumbwa na kizaizai cha kuweweseka na hatimaye kuanguka. Haya ni baadhi tu ya matukio ambayo watu wengi hasa wazazi wamekuwa wakiyahusisha na imani za kishirikina.

Katika Shule ya Msingi Kitopeni, tatizo hili linatajwa kusababisha kifo cha mwanafunzi mmoja aliyefariki Agosti 12 mwaka huu, baada ya kuanguka ghafla na kupoteza fahamu akiwa darasani.
Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Theodolph Karigita, mara nyingi tatizo hilo limekuwa likiwakumba wanafunzi wa kike wanaosoma kuanzia darasa la tano hadi la saba.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, katika Shule ya Sekondari Hale iliyoko wilayani Korogwe, tatizo hilo hutokea siku maalumu ambazo ni Jumanne na Ijumaa.

Mkuu wa shule hiyo, Ntuli Mwakabungu, anasema wanafunzi wanaopatwa na tatizo hilo huanguka na kupoteza fahamu kwa muda kisha hupona na kuendelea na masomo.

Mwakabungu anahusisha tatizo hilo na mazingira wanayoishi wanafunzi hao kwa kusema:"Mazingira wanayoishi pia nadhani yanachangia. Wengine wanakesha kwenye disko na hata kwenye ngoma za mashetani."

Anaongeza kusema kuwa tatizo la wanafunzi kuanguka ovyo shuleni hapo, sasa limekuwa la kawaida na mara kadhaa wanafunzi wenyewe wamekuwa wakilimaliza kwa kupepeana vichochoroni.

Watalaamu wanasemaje?

Wataalamu kadhaa wa afya, wanasema kuwa tatizo hilo linatokana na matatizo ya kisaikolojia na tiba yake inapaswa kuwa ya kisaikolojia pia .

"Hili sio tatizo geni katika jamii, ni ugonjwa wa akili unaomtokea mtu kwa muda na unajulikana kitalaamu, kama 'Mass neurosis' au 'mass psychosis'," anasema Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Eddy Mjungu na kuongeza:

"Ni ugonjwa unaowapata zaidi watoto wa kike, tafiti zinaonyesha kuwa hili ni tatizo la kisaikolojia linalotokana na conflict (mvutano) kwenye ubongo wa mtu,"

"Ugonjwa huu unaambukiza kisaikolojia. Mtu anayepatwa na tatizo hilo, anaweza kupiga kelele au kuanguka. Kimsingi anachohitaji, ni watu kumjali, na attention (uangalizi wa karibu)."

Chanzo cha ugonjwa

Kwa mujibu wa Dk Mjungu , Mass Psychosis/Neurosis, ni ugonjwa unaotokana na mvutano wa mawazo kwenye ubongo wa mtu unaosababishwa na mambo mengi, ikiwemo uhusiano wa mtu huyo na jamii.

"Hii inaweza kuwa watoto kutolelewa vizuri, uhusiano wao na wazazi, walimu na hata migogoro ya kimapenzi," anasema na kuongeza:

"Ndiyo maana wengine wanapopatwa na ugonjwa huo wanawataja watu kama walimu, wazazi, wapenzi au hata kitu kilichofanya mawazo yake yagongane. Sasa tiba sahihi zaidi ni kuibua tatizo linalomsumbua."

Tiba yake

Dk Mjungu anasema Mass psychosis/ neurosis sio ugonjwa unaotibika kwa kidonge wala dawa ya hospitalini, unatibika kisaikolojia. Anaeleza:

"Unapotokea, daktari anapaswa kwenda katika eneo la tukio na kuwafanyia cancelling (kuwapa ushauri) wagonjwa na sio kuwapeleka wagonjwa hospitali. Cha kwanza muhimu baada ya daktari kufika kwenye eneo la tukio, ni kupunguza msongamano wa watu wanaomzunguka mgonjwa.’’

"Kwa kuwa ugonjwa huo unaambukiza kisaikolojia, kupunguza umati wa watu kunasaidia wengine kutojua kinachoendelea. Baadaye ifuate huduma ya ushauri.’’

Anaendelea kusema kuwa kinga ya ugonjwa huo kuwa ni wanafunzi kutopewa muda wa kufikiri mambo yao na badala yake wapangiwe ratiba ya mambo maalumu ya kufanya yanayoratibiwa na walimu, wazazi au walezi.

Kwa upande wake, Ofisa Elimu Sayansi Kimu na Afya shuleni wa Korogwe, Kinangwede Fadhili, anasema tatizo la wanafunzi kuanguka, kuweweseka na kukimbia hovyo shuleni, ni ugonjwa unaojulikana Kiingereza kwa jina la “Hysteria”

"Ugonjwa huo unatokana na vurugu za maono. Hysteria inamtokea mtu na kutoweka yenyewe bila tiba na zamani ilikuwa ikiwatokea zaidi wanafunzi katika shule za bweni."anafafanua.

Sababu za Hysteria?

Kwa mujibu wa Fadhili, ugonjwa huo mara nyingi huwapata watoto ambao tayari wameanza kupevuka na mara nyingi huwakumba wanafunzi kuanzia darasa la tano hadi la saba.

"Zamani, wagonjwa wengi walikuwa ni wasichana waliokuwa na umri wa kuanzia miaka 15, lakini siku hizi hysteria inawapata wanafunzi wasichana wenye umri wa miaka tisa," anasema na kuendelea:

"Hysteria ni matokeo ya sensory disturbance (mvurugiko wa akili). Watoto wa kike waliopevuka na kupata maudhi kwa wazazi, walezi, walimu au wenzi wao, wanaweza kupata tatizo hilo."

Mbali na umri wa kupevuka, Fadhili anataja mambo mengine yanayochangia ugonjwa huo kuwa ni pamoja na matumizi ya dawa za kulevya na ulevi wa pombe.

"Pia hofu ya mitihani au hofu ya jambo lolote ni mambo mengine yanayoweza kuharibu ubongo na kumsababishia mtu hysteria, "anaongeza.

Mganga Mkuu wa mji wa Korogwe, Jerry Mwakanyamale anataja dalili za ugonjwa huo kuwa ni pamoja na mgonjwa kunyong'onyea mwili na kulegea.

"Dalili zingine ni blicking (kupepesa macho), kulia sana na kupiga kelele. Mgonjwa pia anaweza kuwa na ukimya mzito, kuanguka chini bila kutoa povu, moyo kwenda mbio, upweke na hata kucheka bila sababu za msingi,"anasema.

Kuhusu matibabu, Dk Mwakanyamale anasema ugonjwa huo unatibika kwa ushauri na watoto kuwa karibu na wazazi, walezi au walimu, ili kujua matatizo yao na kisha kuyapatia ufumbuzi kwa haraka.

Aidha, anatoa wito kwa jamii kutoingiza imani za kishirikina kwenye tatizo hilo, badala yake anasema watoto wanaopatwa na tatizo hilo, wanapaswa kupelekwa hospitali kwa ajili ya vipimo vya awali na matibabu ya haraka.


chanzo: Gazeti la Mwananchi
 
Back
Top Bottom