Walioua ndugu kwa Viboko, Wafungwa miaka 6, baba yao anusurika

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,120
Mahakama Kuu imewaadhibu mzee wa miaka 91, Leshoo Kishoki Mollel na wanawe wawili, waliomuua bila kukusudia mwanafamilia mwenzao aliyekwenda kwa wakwe katika kikao cha usuluhishi akiwa amelewa chakari.

Katika hukumu hiyo iliyosomwa Juni 23 mwaka huu na nakala kupatikana jana, Mahakama Kuu Kanda ya Moshi imehukumu mzee huyo kifungo cha nje cha miezi 12, huku wanawe Saimon Leshoo (31) na Baraka Leshoo (39) wakitupwa jela miaka sita.

Tukio hilo la mauaji ya Simon Leshoo Mollel (35) lilitokea asubuhi ya Oktoba 24, 2022 katika Kijiji cha Munge Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, ambapo kwa mila na tamaduni za Wamasai, familia ilimwadhibu ndugu yao kutokana kuwa mlevi kupindukia na kutia aibu ukweni.

Hili si tukio la kwanza kwa jamii ya Wamasai, kwani Januari mosi, 2023, mkazi wa Sanawari, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Nelson Mollel (32), alifariki dunia baada ya kudaiwa kupewa adhabu ya kuchapwa viboko 280 kwa tuhuma za kumtukana mama yake mzazi.

Katika tukio hilo, ilielezwa wazee wa jamii ya Kimaasai na Kimeru, wamekuwa wakitoa adhabu ya kuwachapa viboko vijana wanaobainika kufanya matendo ambayo ni kinyume cha maadili kwa jamii ya makabila hayo. Yapo matukio mengi yanayofanana na hayo na baadhi ya waliochapwa walinusurika kifo.

Hukumu ya mzee Mollel

Akisoma hukumu ya mzee Mollel na wanawe, Jaji Kilimi alisema ingawa walikuwa na dhamira njema ya kumbadili tabia mwanafamilia mwenzao aliyekuwa na tabia ya ulevi uliokithiri, njia waliyoitumia haikuwa sahihi.

“Katika kesi hii washtakiwa walikuwa na lengo la kumwadhibu marehemu (Simon) kwa lengo la kumbadili tabia, lakini nadhani walichagua njia mbaya ambayo kwa maoni yangu haikuwa ya kumbadili.

“Hata hivyo, nimezingatia umri wa mtuhumiwa wa kwanza ni mzee sana, naona ushiriki wake katika zoezi la kuadhibu haliwezi kulinganishwa na watuhumiwa wengine wawili ambao ni watoto wake,” alisema Jaji Kilimi na kuongeza:

“Kwa kweli alitakiwa kuwazuia wanawe kufanya hivyo, kwa hiyo ile kuwepo kwenye eneo la tukio ilikuwa uzembe wa kutotumia busara za ubaba wake wakati kosa likitendeka.”

Jaji Kilimi alisema katika mazingira hayo na kwa mujibu wa miongozo ya hukumu Tanzania ya mwaka 2023, kosa lililotendwa linaangukia katika mauaji ya bila kukusudia ya kiwango cha juu kwa mshtakiwa wa pili, Saimon na wa tatu, Baraka.

“Hii ni kwa sababu walisababisha majeraha mengi mabaya yaliyochochewa na genge lao huku mshtakiwa wa kwanza (mzee Leshoo) akianguka katika kiwango cha chini mauaji kwa sababu ya uzembe wake,” alisisitiza Jaji Kilimi.

Jaji alisema kutokana na mazingira ya mauaji hayo, kifungo cha miaka 10 kinatosha kuanzia kutoa haki kwa mshtakiwa wa pili na wa tatu, lakini kwa kuwa walikiri kosa, moja ya tatu ya miaka hiyo inapunguzwa na kuwa miaka sita na miezi nane.

Kulingana na Jaji Kilimi, mahakama inawapunguzia kifungo hicho kutokana na muda waliokaa gerezani ambao ni miezi nane kuanzia siku ya kwanza walipofikishwa mahakamani, hivyo washitakiwa watatumikia kifungo cha miezi sita gerezani.

Kuhusu mshtakiwa wa kwanza, mzee Leshoo, Jaji Kilimi alisema kulingana kifungu namba 38(1) cha Kanuni ya Adhabu kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002, anamwachia kwa masharti ya kutotenda kosa lolote la jinai ndani ya miezi 12.

Mauaji yalivyofanyika

Kulingana na maelezo yaliyosomwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Clara Charwe akisaidiana na wakili Edithi Msenga ni kwamba marehemu aliingia katika mgogoro na mkewe, Mariam Lataro kutokana na tabia ya ulevi.

Tabia hiyo ilimfanya marehemu atengane na mke wake huyo wa pili na Oktoba 23,2022 saa 2:00 asubuhi, marehemu akiwa ameongozana na washtakiwa walikwenda kwa wakwe, ili kutafuta suluhu ya mgogoro huo.

Hata hivyo, usuluhishi huo uligonga mwamba baada ya baba mkwe kukataa mazungumzo hayo yasifanyike kwa kuwa marehemu aliendelea na tabia yake ya kunywa pombe nyingi na siku hiyo ya kikao alifika akiwa amelewa.

Siku iliyofuata saa 12:00 asubuhi, washtakiwa wakiwa wameongozana na ndugu wengine saba wa familia ya mzee Mollel walifika nyumbani kwa marehemu wakiwa wamebeba fimbo nyingi, ili kumwadhibu kutokana na tabia ya ulevi.

Walimvamia ambapo baadhi walimchapa hadi akapoteza fahamu na ilipofika saa 2:47 asubuhi, balozi wa nyumba kumi, William Matayo alipita na kuwakuta washtakiwa wamemzunguka ndugu yao akiwa amekufa.

Taarifa ilitolewa kituo cha polisi ambapo washukiwa wote walikamatwa na mshtakiwa wa pili na wa tatu waliandika maelezo ya kukiri kumuua ndugu yao na uchunguzi wa daktari ulionyesha alipasuka bandama na pingili za uti wa mgongo.

Maombi ya mawakili

Ingawa wakili wa Serikali, Msenga aliyeiwakilisha Jamhuri alisema hana kumbukumbu za makosa ya jinai ya nyuma ya washtakiwa, aliomba mahakama kuwaadhibu kulingana na muongozo wa utoaji hukumu wa mwaka 2023.

Pia akaiomba mahakama izingatie kuwa ingawa lengo la washtakiwa ilikuwa kumwadhibu marehemu, lakini walitumia nguvu kubwa wakati mshtakiwa alikuwa mtu dhaifu kutokana na unywaji pombe wa kupindukia.

Wakili Deogratious Matata aliyemtetea mzee Mollel, aliiomba mahakama kuzingatia umri wa mzee huyo, ni mgonjwa na ndiye anayehudumia familia iliyoachwa na marehemu na pia izingatie kuwa alikiri kosa hilo mapema.

Kwa upande wake, wakili Martin Kilasara aliyewatetea mshtakiwa wa pili na wa tatu, aliiomba mahakama izingatie kuwa washtakiwa hawakuwa na dhamira ya kumuua ndugu yao, bali kumuonya ili arudi kuwa mtu mwenye tabia njema.

Wakili huyo alienda mbali na kusema adhabu hiyo ni sehemu ya mila na utamaduni wa washtakiwa ambao ni wa kabila la wamasai na pia walikiri kosa mapema, hivyo kutoisumbua mahakama wala kuingiza gharama.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom