Wakurugenzi wa Hospitali wakanusha kulalamikia kelele za tamasha la Fiesta viwanja vya Leaders Club

chakii

JF-Expert Member
Sep 15, 2013
19,696
22,733
Mwandishi alifika katika Hospitali ya Ubalozi Medical Clinic iliyopo mita 200 kutoka vilipo viwanja vya Leaders na kukutana na Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Aneth Rwebembela ambaye alisema hakuna mgonjwa aliwalalamikia wala kuzimia kutokana na muziki.

=====

Tamasha la Fiesta laacha simanzi, maswali lukuki
Kwa ufupi
  • Tamasha hilo lililotarajia kufanyika Jumamosi lilifutwa wakati maandalizi yakiwa yamefanyika kwa kiasi kikubwa na kuibua simanzi kwa mashabiki huku sababu ya kufutwa tamasha hilo ikidaiwa kuwa ni barua kutoka Manispaa ya Kinondoni ikidai wagonjwa walio karibu na eneo hilo wanabughudhiwa kwa uwapo wa tamasha hilo.
Siku ambayo ilitarajiwa kuwa sherehe ilibadilika kuwa ya fadhaa. Asubuhi ya jana, kila aliyekuwapo katika Viwanja vya Leaders, Kinondoni jijini Dar es Salaam alionekana kupigwa na butwaa na hii ni baada ya kutangazwa kuwa Tamasha la Tigo Fiesta halitafanyika.

Hiyo ilitokana na barua ya Manispaa ya Kinondoni iliyotolewa juzi ikisema imepokea malalamiko kutoka kwa wagonjwa walio karibu na eneo hilo kubughudhiwa.

Kwa uamuzi huo, burudani iliyosubiriwa kwa mwaka mzima iliyeyuka ghafla ikiwa tayari jukwaa limeshasimikwa, muziki umefungwa na nguo zimeshanyooshwa.

Katika viwanja hivyo makundi ya vijana waliokuwa na huzuni wengi wao wakiwa wameshika mikono viunoni yalitawala.

Mbali ya vikundi hivyo, kibanda kilichopo karibu na mlango wa kuingilia upande wa mashariki mwa viwanja hivyo ambao wachuuzi walikuwa wamejipanga kuuza vinywaji baridi walionekana kujawa na simanzi huku wakiwa nje ya eneo lao la biashara.

Maagizo hayo yameibua maswali mengi kuhusiana na mwenendo mzima na mtiririko wa matukio hadi kusitishwa kwa tamasha hilo ambalo lilitanguliwa na mengine katika miji 14 tangu lilipozinduliwa miezi miwili iliyopita.

Baadhi ya maswali hayo ni kwa nini kibali kilitolewa wakati ikifahamika kuwa kuna hospitali jirani na eneo hilo? Je, hospitali hiyo ni mpya kwa ni tamasha hilo limekuwa likifanyika hapo miaka ya nyuma. Je, baaada ya ‘figisu’ zilizojitokeza katika tamasha la mwaka jana, kwa nini pande mbili hazikukutana kupata mwafaka? Maswali mengine yaliyokuwa yakiulizwa ni iwapo uamuzi huo umemtazama mfanyabiashara aliyewekeza, Kampuni ya Tigo iliyotumia mamilioni katika udhamini, mjasiriamali mdogo aliyetarajia kubadili maisha yake usiku wa jana kwa biashara ya vyakula, vinywaji au usafiri wa bodaboda.
Usumbufu kwa wagonjwa

Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kinondoni, Aaron Kagulumjuli aliiambia Mwananchi jana kuwa tamasha hilo lingesababisha usumbufu kwa wagonjwa ingawa hakutaja jina la hospitali husika.

“Tumelizuia tamasha kufanyika hapo kwani uhai wa watu ni muhimu kuliko hicho kinachotaka kufanyika.Jana tu walipokuwa wakitangaza hapo Leaders maeneo ya karibu kuna hospitali na watu wawili walizimia, sasa hatuwezi kuruhusu furaha ya watu wengi ikawa majonzi kwa wengine,” alisema.

Mwandishi wa Mwananchi alifika katika Hospitali ya Ubalozi Medical Clinic iliyopo barabara ya Kilimani, mita 200 kutoka vilipo viwanja vya Leaders na kukutana na Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Aneth Rwebembela ambaye alisema hakuna mgonjwa aliwalalamikia wala kuzimia kutokana na muziki.
“Sisi tunafunga saa 2:00 usiku na tukiwa huku ndani hatusikii muziki ukipigwa huko uwanjani kwa sababu ya madirisha ya vioo.”
Mwananchi pia ilifika hospitali ya Besta iliyopo Mtaa wa Tunisia, mita 300 kutoka vilipo viwanja hiyo ambako meneja wake,Leon Lee alisema kuwa hawalazi wagonjwa na wanashughulika na vipimo pekee. Pia alisema hawajalalamika kuhusu kelele na hawajui chochote kuhusu tamasha hilo.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi wanaozunguka eneo hilo walisema hupata usumbufu wa kelele panapokuwa na matamasha au bendi.

Kijana aliyejitambulisha kwa jina moja la Mudy alisema raia mmoja wa kigeni anayeishi maeneo ya St Peters ndiye ambaye amekuwa akipinga muziki kupigwa usiku eneo hilo.

Clouds wagoma kuhamisha
Barua iliyoandikwa juzi na ofisa utamaduni manispaa hiyo kwenda kwa waandaaji, Clouds Media Group inasema, “Hivyo kwa barua hii nafuta kibali kilichotolewa Novemba 22, 2018 cha kufanya Fiesta Uwanja wa Leaders na kuihamishia Uwanja wa TTanganyika Packers, Kawe.”

Hata hivyo, badala ya kulihamishia Tanganyika Packers kama ilivyoelekezwa, waandaaji walitangaza kulifuta kabisa na kuahidi kuwarudishia viingilio mashabiki ambao walikuwa wamekwisha nunua tiketi.

“Kwa masikitiko makubwa tunatangaza kusitisha tukio la kilele cha msimu wa Tigo Fiesta 2018 lililopaswa kufanyika leo Novemba 24, 2018 katika viwanja vya Leaders Kinondoni Dar es Salaam. Sababu za kusitishwa kwa tamasha hili zipo nje ya uwezo wetu,” alieleza mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, Sebastian Maganga.



Chanzo: Mwananchi
 
Mambo yale yale ya mtu mweusi na weusi wake mpaka rohoni mwake. Huyo afisa aliyezuia fiesta alishindwa vipi kuwaambia clouds tangu jumatatu ili wajipange?.

Uzembe wa aina hii unaweza kupuuziwa lakini ni tabia ambayo inaweza hata kufukuza wawekezaji. Maana yake ni kwamba hatujipangi, tunajiendea tu kama gari bovu.
 
Back
Top Bottom