Wakubwa wapagawa; Mabadiliko ya Baraza la Mawaziri hayakwepeki

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797


Waandishi Wetu

Toleo la236
25 Apr 2012


236_pinda.jpg



  • Mabadiliko ya mawaziri dhahiri
  • Pinda kupeleka ‘ripoti' zao za utetezi Ikulu
  • Pinda kupeleka ‘ripoti' zao za utetezi Ikulu
  • Ni kama ya Nyerere mwaka 1978

MABADILIKO ya Baraza la Mawaziri hayakwepeki, vyanzo vya habari kutoka Ikulu ya Magogoni, vimesema.

Vimethibitisha kwamba sasa, pengine kuliko wakati mwingine wowote, mabadiliko yatakuja, yakichangiwa na shinikizo la Bunge, hususan wabunge wa CCM katika vikao vyao, lakini pia msingi wake ukiwa ni baadhi ya mawaziri na manaibu wao kuhujumiana katika utendaji, kiasi cha ‘kuombeana mabaya', Raia Mwema limeelezwa.

Baadhi ya maofisa wa Ikulu wamelithibitishia gazeti hili kwamba, baada ya miezi mingi kupita tangu Rais Jakaya Kikwete kuwakutanisha mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu na manaibu wao, pamoja na baadhi ya watendaji wengine wakuu serikalini, katika semina elekezi katika ukumbi wa St. Gaspar mjini Dodoma, udhaifu mkubwa umebainika wa kutozingatia maadili ya kiuongozi kwa mujibu wa sheria na hata kwa mujibu wa mada zilizowasilishwa kwenye semina hiyo elekezi.


"Mabadiliko hayakwepeki licha ya kwamba kuna jukumu zito la maandalizi ya bajeti za wizara na kwa hiyo ni changamoto kubwa kuingiza watu wapya kwa maana ya nafasi za mawaziri, lakini hata hivyo, hao wapya itabidi wategemee zaidi mihtasari ya watendaji watakaokuwapo katika kila wizara husika itakayoguswa na mabadiliko," kinaeleza chanzo chetu cha habari kutoka Ikulu.


Mabadiliko hayo ya Baraza la Mawaziri pia yanatarajiwa kujitokeza baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye naye ni majeruhi wa ‘hasira' za wabunge, kuwasilisha ripoti za utetezi za kila waziri kwa kadiri walivyotuhumiwa na wabunge wa CCM, katika kikao chao kilichoketi faragha mwishoni mwa wiki iliyopita.


Inaelezwa kuwa Pinda anatarajiwa kushauriana na Rais Jakaya Kikwete, pamoja na Makamu wa Rais, Dk. Gharib Bilal kuhusu mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na hatimaye Baraza jipya kutangazwa wakati wowote.


Lakini wakati hayo yakiendelea, sasa ni dhahiri kuwa Baraza la Mawaziri linaloundwa na mawaziri 31, akiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na naibu mawaziri 21, linalotarajiwa kuvunjwa limethibitisha udhaifu mkubwa katika eneo la utawala wa kisiasa kiasi cha kudhoofisha mno mfumo wa jumla wa kiutawala nchini.


Kwa kiasi kikubwa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebeba tafsiri kwamba, ufisadi unaofanywa na baadhi ya mawaziri na watendaji katika wizara mbalimbali unaigusa mamlaka yao, ambayo ni Rais Kikwete ambaye alipaswa kufanya mabadiliko ya kiuongozi kabla hata CAG hajatoa ripoti yake.


Inaaminika kuwa, Rais Kikwete alikuwa na uwezo wa kubaini kupitia vyombo vya usalama namna baadhi ya viongozi wanavyoiba mali za umma na angeweza kuchukua hatua kali, kama alivyowahi kufanya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.


Mwaka 1978, Mwalimu Nyerere akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alimfukuza kazi aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano na uchukuzi, Augustine Mwingira na aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Ndege (ATC), Laurance Mmasi, katika tukio ambalo linaweza kufananishwa na tukio lililoibuliwa na ripoti ya CAG kuhusu ufisadi katika Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).


Katika tukio hilo la Mwalimu Nyerere, Shirika la Air Tanzania (ATC) lilikodi ndege kutoka kwa raia wa Lebanon, George Hallack, ndege ambayo ilikuwa mbovu, ikiwa ‘imeruka' kwa saa ambazo ni pungufu ya zile zilizohitajika kwa mujibu wa utaalamu wa ripoti za watalaamu.


Ilibainika kuwapo kwa njama katika mkataba huo ambao ndege iliyokodiwa iliishia kuegeshwa katika uwanja wa ndege na ‘kuoza.' Ni kutokana na hali hiyo, Mwalimu akawafuta kazi Waziri na Mkurugenzi wa ATC.


Tukio hilo linafanana na hili la sasa. Katika tukio la sasa, menejimenti ya Shirika la Ndege (ATCL) imekodi ndege aina ya Airbus, namba A320214 kutoka Shirika la Wales Trading la Lebanon, Oktoba, mwaka 2007, nchini Lebanon ambayo ripoti za watalaamu zilibainisha kuwa ni ndege mbovu lakini shirika lilikodi bila kuzingatia maslahi ya taifa.


Akizungumzia tukio hilo, Mbunge Amina Mohamed Mwidau ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), anasema: "...kwa kweli katika mashirika ambayo tumeyapitia (kuyakagua) shirika ambalo lilinifanya nikaumwa kichwa na kusikia kizunguzungu na nikalala na homa ni ATCL."


Mwidau ambaye alizungumza maneno hayo bungeni na mbunge mwenzake kuingilia kwa kuropoka "kwa nini asianguke kutokanana na kizunguzungu hicho, alisema menejimenti ya ATCL ilionyesha kiburi kikubwa kwa kuingia mkataba na Wales Trading bila ridhaa wala dhamana ya Serikali.


"Waliingia mkataba kwa miezi takriban saba bila ya dhamana ya Serikali. Mbali ya hilo, lakini pia ilinisikitisha sana kwa sababu kulikuwa na timu ya wataalamu ambayo ilitoa taarifa kuwa si jambo la busara kukodi ndege ile kwa sababu baada ya miezi takriban sita itaenda tena matengenezo makubwa kwa kitaalamu ni 12 years checks ambayo najua Waziri Nundu pale anafahamu.


"Ni matengenezo makubwa ambayo ndege hiyo inatakiwa ibadilishwe vitu vingi, lakini wao walidharau, walidharau ushauri wa wataalamu wale ambao wako kwa ajili ya kushauri shirika na wanalipwa, wakaweza kusaini mkataba ule ambao ni wa miaka sita, ni takribani ni miezi 72.


"Lakini pia kilichonisikitisha zaidi ni pale walipokubaliana katika mkataba ule, rate ya kukodisha ndege ile itakuwa ni dola 374,000 kwa mwezi, kama imeruka au haijaruka na ndege ile ilikaa miezi takribani 48 katika mikono ya ATCL. Katika miezi hiyo 48 ni miezi saba tu ambapo ndege ile iliweza kuruka lakini miezi 41 ilikuwa chini.


"Kwa ujumla mpaka kufikia tarehe 30 Januari, 2010 Shirika la Wales Trading lilileta hesabu yake kwa ATCL inaonyesha kuwa deni lile lilikuwa limesimama kwenye takriban pesa za Kitanzania bilioni 323 ambayo ni sawa sawa na dola milioni 200...pesa inayoweza kununua ndege mbili ambazo ni aina hiyo hiyo ya Airbus 320 ambayo ukiangalia kwenye website ya Airbus utakuta bei ya ndege moja mpya (a brand new aircraft) ya aina hiyo imesimama kwenye dola milioni 88.3.


"Kwa hiyo, tungeweza kupata ndege mbili mpya na chenji ikabakia, lakini manejementi hii imeonyesha dharau kwa sababu timu ya wataalamu ime-prove ni kweli ndege ile imeruka miezi saba na ikaenda matengenezo. Imenisikitisha sana kwa sababu watendaji wale walionyesha dharau na inaonyesha kuwa hawapo peke yao lazima wana mashiko sehemu wanayoyategemea na ndiyo maana wakafanya kiburi kile cha hali ya juu."


Shinikizo dhidi ya Waziri Mkuu

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, ni kama vile ndiye ‘nyota' wa mkutano uliopita wa Bunge na hasa baada ya kuwataka wabunge kutia saini zao kwa lengo la kutaka kumpigia kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutokana na ripoti za CAG kuonyesha ufisadi unaojirudia kila mwaka miongoni mwa taasisi za umma.

Zitto ambaye ameshikilia rekodi yake ya kuwa kinara wa mkutano miwili mfululizo ya Bunge, akiibuka na pingamizi la posho kwa wabunge katika mkutano Februari, mwaka huu na sasa, akiibuka na ajenda ya ‘kumng'oa' Waziri Mkuu, hoja zote zikipata ushabiki ndani na nje ya Bunge, amelifanya Bunge kuwa na rekodi ya kipekee lakini pia, hatua yake ya kutaka Waziri Mkuu ang'olewe inampa nguvu zaidi CAG tofauti na wengi wanavyotafsiri.


Zitto mwenyewe amelieleza gazeti hili akisema: "Vyovyote itakavyokuwa, kufanikiwa au kutofanikiwa kumng'oa Waziri Mkuu, ripoti za CAG zitaheshimiwa kwa kufanyiwa kazi ili makosa ya ufisadi yasiwe yanajirudia na yakijirudia basi, siku nyingine Waziri Mkuu atang'oka, rekodi zimeshajiandika."


Zitto alifanikiwa kukusanya saini za wabunge 73, ambao ni kutoka vyama karibu vyote vyenye wabunge bungeni, isipokuwa UDP tu.


Hatua ya wabunge wa CCM

Ingawa kuna hali ya kusononeka miongoni mwa viongozi wa Serikali kutokana na hatua ya wabunge wa CCM kutaka mawaziri wawajibishwe na wengine kusaini ‘tishio' la kumng'oa Waziri Mkuu, kwa namna fulani hatua ya wabunge hao inakisaidia chama chao cha CCM.

CCM inasaidiwa na hatua ya wabunge hao kwa sababu shinikizo lao linaelekea kusababisha kuundwa upya kwa Serikali yenye mawaziri watakaokuwa wakichapa kazi, tofauti na hali ilivyobainika ambapo baadhi ya mawaziri na naibu mawaziri katika wizara zao wamekuwa hawaelewani.


"Hatua tuliyochukua haina maana tunaing'oa madarakani Serikali yetu. Hapana, haiwezi kung'oka kwa mujibu wa Katiba, kinyume chake tunajiandaa kuzuia chama chetu kising'olewe madarakani katika Uchaguzi Mkuu ujao. Tunaamini, shinikizo hili litatuimarisha na tunayo miaka mitatu ya kuthibitisha kuwa sisi kama chama ni imara, tunaweza kujikosoa na kuwajibishana kwa maslahi ya nchi," anaeleza mbunge mmoja wa CCM ambaye licha ya kusaini kutishia kumng'oa Pinda, lakini ametaka jina lake lisiwekwe wazi.


Bunge lajisafisha tope la posho

Mjadala mzito ndani ya Bunge ambao msingi wake ni ripoti za CAG, kwa kiasi kikubwa umerejesha imani ya wananchi kwa Bunge ambayo ilitikisika baada ya wabunge kung'ang'ania nyongeza ya posho za kukaa kitako za kufikia Sh 200,000 kwa siku.

Ingawa hoja ya kupinga nyongeza ya posho kwa wabunge ililenga kuhimiza matumizi mazuri ya fedha za walipa kodi, wabunge safari hii wamekuwa mstari wa mbele kupinga ufisadi uliofichuliwa katika ripoti za CAG, kiasi cha kutaka baadhi ya mawaziri wajiuzulu na ikibidi hata Waziri Mkuu.











 
Tuone matokeo kuliko maneno... Tuona kama atafanya uamuzi mgumu kama wa Mwaka 1978
 
weka na ukurasa wa makala ya jenerali ulimwengu, raia mwema ya leo ndio majibu ya hili.
 
Back
Top Bottom