Wahitimu wa elimu ya juu Tanzania na kitendawili cha kujiajiri

Jun 7, 2017
9
1
Na; Joseph Malekela, Dar es Salaam, Tanzania - Mei, 2022.

Miaka ya hivi karibuni, kumeibuka tabia ya kulalamika katika jamii ambapo kundi moja hunyoosha vidole na kutupa lawama kwa kundi jingine juu ya utekelezwaji ama ufanisi wa wajibu wake. Kimsingi, Kulalamika ni haki ya raia, na kulalamikiwa ni haki ya kiongozi yeyote yule. Kati ya mambo mengi yanayolalamikiwa katika jamii yetu hivi sasa, nimechagua kuzungumzia jambo moja muhimu, ambalo ni juu ya wahitimu wa elimu ya juu kuilamikia serikali kwa kukosa ajira mara baada ya kuhitimu elimu ya juu. Aidha, viongozi kadhaa wa Serikali nao wamekuwa wakiwalalamikia wahitimu wa elimu ya juu kwa kile kinachoitwa “kutokujiongeza” na kujiajiri huku wakiendelea kusubiria ajira za Serikali ambazo kwa vyevyote vile haziwezi kutosheleza kuajiri wahitimu wote wanaohitimu kila mwaka.

Pamoja na mambo mengine, andiko hili linalenga kujadili kwa kina juu ya uhalali wa malalamiko ya wahitimu dhidi ya Serikali kuhusu kutokuajiriwa kwa hoja kwamba Serikali inakosa mbinu mbadala za kutengeneza sera na mikakati inayoweza kuzalisha ajira nyingi zaidi ilihali inauwezo wa kujua mapema juu ya ongezeko la wahitimu kwa miaka mingi ijayo. Pamoja na malalamiko ya upande wa Serikali dhidi ya wahitimu wa vyuo na vyuo vikuu kwa hoja kwamba, jitihada nyingi zinafanyika kuwapa elimu na kuwatengenezea mipango wezeshi, lakini wahitimu bado hawaoni fursa ya kujiajiri hata kwa kuchangamkia fursa zilizowekwa na serikali ili kuwakwamua kiuchumi kwa kutumia ujuzi na maarifa waliyoyapata vyuoni.

Ifahamike kwamba, Andiko hili halilengi kutetea au kufungamana na upande wowote, isipokuwa ni kuleta mjadala wa kina juu ya jambo hili na ikiwezekana kutoa maoni ya kipi kinaweza kuwa suluhisho la kudumu la changamoto hii, ambapo yaweza kuwa ni kuhalalisha lawama za upande mmoja kwenda upande mwingine au kumaliza kabisa lawama katika eneo hili kwa kushughulikia kiini cha tatizo. Hata hivyo, kwa asili ya binadamu, natambua kwa uhakika kabisa, hata lipatikane suluhisho bora kiasi gani, huenda malalamiko yasiishe kabisa, japo yanaweza kupungua na kutoa mwanga zaidi wa kukabiliana na changamoto ya ajira kwa wahitimu na kuboresha uchumi wao na wa taifa kwa ujumla.

Maswali muhimu yaliyojadiliwa katika andiko hili ni pamoja na; Kwa nini wahitimu wanailalamikia Serikali juu ya suala la ajira? Nini kinawazuia wahitimu wa vyuo na vyuo vikuu nchini kujiajiri? Je, kuna mikakati gani ambayo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye lengo la kuwainua vijana kujitegemea kiuchumi ambayo inaipa uhalali Serikali kulalamikia vijana juu ya kutokujiajiri? Je, ni wahitimu ndio wanaopaswa kubadili mtazamo wao juu ya suala la ajira na ni kivipi? au ni Serikali ndio inayopaswa kubadili mbinu za kuwawezesha vijana kiuchumi ili kupunguza malalamiko ya vijana wanaohitimu elimu ya juu kuhusu suala la ajira? Je, kuna mbinu gani nyingine bora zaidi, isiyoathiri jitihada zilizopo na inayoweza kutumika ili kukabiliana na tatizo la ajira nchini kwa vijana hasa wahitimu wa vyuo vikuu? Tunatokaje kwenye mkwamo huu wa kulalamikiana juu ya kutokujiajiri na kukosa ajira rasmi?

Kutafuta majibu ya maswali magumu katika jamii ni kazi ya wanataaluma wa nchi yetu ambao wameigharimu nchi rasilimali nyingi sana ili kuwaelimisha. Binafsi kama mwanafunzi na mhitimu wa siku zijazo, wajibu huu siwezi kujitenga nao, kwa maana nimeshatumia vipande kadhaa vya walipakodi wa nchi hii (mimi nikiwemo) kupata hata elimu hii ndogo niliyonayo. Hivyo basi, japo kwa uchache, nitajitahidi kutimiza jukumu hilo muhimu kwa ustawi wa vijana wa nchi yetu ya Tanzania.

KWANINI WAHITIMU WANASHINDWA KUJIAJIRI?
Nimejaribu kujielimisha kidogo kuhusu malalamiko ya kundi la wahitimu juu ya kukosa ajira baada ya kuhitimu na kama kuna ugumu wowote katika kujiajiri. Msingi wa hoja ya walalamikaji, iko katika kanuni ya mkataba wa kijamii (social contract) ambapo inatazamiwa kwamba, wananchi wanategemea kupata majibu ya maswali au ufumbuzi wa kila changamoto kutoka kwa wenye mamlaka.

Huu ndio mtazamo wa vijana wengi na msingi wake ni uvivu tu ambao ninadhani umejengeka kama tabia kutokana na mfumo wa elimu unavyowaandaa. Wahitimu wanacholalamikia ni kwanini hakuna sera bora na wezeshi zinazoweza kutengeneza ajira rasmi zaidi katika serikali ili kuwaajiri wahitimu mara baada ya kumaliza masomo yao ilhali ikizingatiwa kwamba suala la wao kihitimu sio suala la dharura, lingeweza kuandaliwa mazingira mapema.

Hapa kuna hoja kubwa mbili, hoja ya kwanza, ni juu ya uhaba wa ajira rasmi ambalo ni jukumu la Serikali kuziandaa. Hoja ya pili, ni juu ya wahitimu kuandaliwa kuajiriwa kwa ajira rasmi pekee kupitia mfumo wa elimu tulionao. Pia, najiuliza nini kinawazuia vijana kujiajiri ilihali wanajua kabisa ajira rasmi ni chache na haziwezi kumudu uhitaji mkubwa wa wahitimu wasio na ajira?

Kimsingi, changamoto ya ajira sio changamoto ya Tanzania peke yake, kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2022 ya Shirika la Kazi Duniani – ILO, kiwango cha ukosefu wa ajira duniani kote kinazidi kuongezeka ambapo kinategemewa kifikia milioni 207 (sawa na asilimia 5.9), huku mambo kama mlipuko wa ugonjwa wa Uviko-19 yakitajwa kuchangia bila kusahau mabadiliko ya sayansi na teknolojia ambayo yanapunguza kwa kiasi kikubwa uhitaji wa wafanyakazi wengi kwa kuwa kazi nyingi hivi sasa zinafanywa na teknolojia. Aidha, kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2014 wa mamlaka ya Takwimu Tanzania – NBS juu ya nguvu kazi ya pamoja nchini, ulibaini kuwa ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana wenye umri wa miaka 15-24 kuwa ni asilimia 13.7 na wale wenye umri kati ya 25 - 35 ikiwa ni asilimia 9.8. Hata hivyo, utafiti uliofanywa na Shirika la Vijana la Restless Development mwaka 2012/2013 katika mikoa 7 ya Tanzania bara inaonyesha ukosefu wa ajira miongoni mwa washiriki 1,000 walikuwa zaidi ya asilimia 50%, kupita kiwango cha kitaifa.

Kuhusu suala la mfumo wa Elimu kuwaandaa wahitimu kuajiriwa, hoja ni kwamba, mfumo wa elimu unaowaweka wahitimu wa elimu ya juu (ngazi ya shahada) darasani kwa walau miaka 16, haumuandai mwanafunzi kuja kujiajiri kutokana na kukosekana program mahususi za kujiajiri. Kwa mfano, vyuo vingi vikubwa nchini ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – CKD na Chuo Kikuu cha Dodoma vina kozi ambazo wanafunzi wote lazima wazisome, ikiwemo Maarifa ya Mawasiliano, Fikra Yakinifu na Somo la Maendeleo. Pamoja na uhalisia kwamba, kujiajiri ni suluhisho la changamoto ya ajira nchini na duniani kote, kozi ya kujiajiri inafundishwa kwa wanafunzi wachache tu ama wanaosomea masomo ya biashara au kupitia semina za kujiajiri ambazo mara nyingi haziwafikii wanafunzi wote. Linapokuja suala la kulaumu wahitimu kutokujiajiri, jamii haiangalii hawa wahitimu walipata fursa ya kupata walau elimu kidogo ya ujasiriamali au kujiajiri au la, isipokuwa kwakuwa tu ni wahitimu basi wangepaswa kuja na masuluhisho ya changamoto za jamii wakianza na changamoto za kwao wenyewe za kukosa ajira.

Kukosekana kwa elimu ya kujiajiri kunapunguza uwezo wa wahitimu kujiajiri kwakuwa wanakosa maarifa ya msingi ya nini cha kufanya katika suala zima la kujiajiri. Hata hivyo, program mbalimbali zinazotolewa za kujiajiri na mafunzo kwa vitendo kupitia taasisi zinazosimamiwa na Mamlaka ya Elimu ya Mafunzo ya Ufundi – VETA na wadau binafsi, jitihada ambazo haziwafikii wanafunzi wote.

Hapa ndio msingi wa hoja ya wahitimu kushindwa kujiajiri, ikiwa ni pamoja na kukosa maarifa muhimu ya kujiajiri licha ya kutumia zaidi ya muongo mmoja na nusu katika kujielimisha katika mlengo wa kuajiriwa. Swali ni je, kama ajira ni tatizo la ulimwengu mzima na suluhisho lake ni watu kujiajiri, kwanini wanafunzi hawafundishwi kujiajiri? Je, si kazi ya taasisi za elimu kutengeneza masuluhisho ya changamoto za jamii kwa kuwaelimisha wanafunzi?

Hoja nyingine ya kwanini vijana wanashindwa kujiajiri mara wanapomaliza masomo yao ni suala la upatikanaji wa mitaji. Inajulikana kwamba, pamoja na kuwa na uelewa wa biashara/kujiajiri kwa baadhi ya wahitimu, bado watahitaji kuwa na mtaji ili waweze kuanzisha biashara zao. Swali ni angalau kiasi gani kinaweza kumsaidia mhitimu wa chuo kikuu kuanzisha biashara yake hata kwa udogo tu? Swali ni je, kuna mazingira wezeshi kiasi gani ya kumsaidia mhitimu apate mtaji wa kumuwezesha kuanza kujiajiri? Swali linguine, ni je, vijana wanajua wanahitaji mtaji kiasi gani na wapi wanaweza kupata mitaji?

Kuhusu suala la upatikanaji wa mitaji, msingi wa hoja ya ugumu wa kujiajiri ni mazingira yasiyo rafiki ya kupata mitaji nchini. Utaratibu uliopo, mhitimu anaweza kupata mtaji ama kutoka katika Benki/ Taasisi za fedha au katika mifuko ya uwezeshaji wa vijana inayoanzishwa na serikali kupitia makusanyo ya Halmashauri. Fursa ya kupata mikopo ya mitaji kutoka benki ina changamoto nyingi sana ikiwemo masharti magumu ya kuwa na dhamana ya hati ya mali isiyohamishika kama vile nyumba, kiwanja au gari, vitu ambavyo mhitimu huenda asiwe navyo. Changamoto ya fursa ya pili ya kupata mikopo ya serikali kupitia Halmashauri inatokana na masharti magumu ambayo hayamruhusu mtu mmoja mmoja kupata mkopo na pia, hata akitimiza matakwa ya kuwa na kikundi cha watu watano, wanatakiwa kuwa na biashara ambayo tayari wamekwisha kuanza pamoja na mpango wa biashara. Fursa ya pili ndio pengine chaguo lisilo na vizingiti vingi, lakini bado changamoto ipo katika kuifikia hiyo mikopo ya Halmashauri na huenda wahitimu wengi wa elimu ya juu hawaoni nafasi yao katika fedha hizo ama wahitimu wachache tu ndio wananufaika nayo.

Kwa misingi ya hoja ya kukosa elimu ya kujiajiri na ugumu wa kupata mitaji ya kuwawezesha kujiajiri, vijana wamekuwa wakihalalisha malalamiko yao kwa serikali na kwamba serikali ina kila sababu ya kutengeneza masuluhisho ya changamoto hizo kwa kuweka mazingira rafiki ya kupata ujuzi na kupata mitaji.

KUNA JITIHADA GANI ZA SERIKALI KUWAWEZESHA VIJANA HASA WAHITIMU KUJIAJIRI NCHINI?
Jitihada mbalimbali zinafanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwawezesha vijana. Kwanza, katika kuwapa elimu. Pili, katika kutengeneza ajira rasmi serikalini, huku uwezeshaji ukiendelea katika nyanja za kiuchumi ili kuwawezesha wajiajiri.

Tukianza na suala la elimu, serikali inawawezesha vijana kupata elimu ambapo, tangu mwaka 2016, elimu msingi (Shule za Msingi na Sekondari) katika shule za umma inatolewa bure (bila malipo), huku kukiwa na nia ya kuondoa ada ya kidato cha tano na sita katika shule za umma, kuweka ada elekezi kwa shule binafsi hii yote ikiwa ni kuhakikisha vikwazo vya kupata elimu kwa kijana wa kitanzania vinaondolewa. Kubwa zaidi, zaidi, uwekezaji mkubwa unafanywa katika kuongeza bajeti ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu - HESLB ambayo imeongezeka kutoka Bilioni 341 mwaka wa masomo 2014/2015 (zilizokuwa zikiwasaidia wanufaika wapya wa mwaka wa kwanza 34,128 tu) hadi kufikia Bilioni 570 mwaka wa masomo 2021/2022 (ambazo sasa wanufaika wapya hadi 65,000 sawa na asilimia zaidi ya 83% ya waombaji wapya 78,000 waliojitokeza kuomba mikopo wamepata mikopo hiyo) ili kuwawezesha wanafunzi wengi wa elimu ya juu kupata elimu bila vikwazo. Nadhani (na ni imani yangu wakati wote), kwa jinsi ya ongezeko la kila mwaka la uwekezaji katika sekta ya elimu, ninaamini serikali ina dhamira ya dhati kabisa ya kuhakikisha siku moja wanafunzi wote wa elimu ya juu wanaojitokeza kuomba mikopo nchini wanapata mikopo hiyo ili kupata elimu ya juu bila vikwazo wala ubaguzi.

Jitihada zaidi katika suala la kuwapa elimu, maarifa na ujuzi zinafanywa na serikali kupitia taasisi za mafunzo ya ufundi zilizo chini ya Mamlaka ya Elimu ya Mafunzo ya Ufundi – VETA ambapo vijana ambao hawakupata fursa ya kuendelea na mfumo rasmi wa elimu wanaweza kujiendeleza na kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri kwa kuwapatia maarifa na stadi mbalimbali ambazo zinahitajika na jamii kwa wakati huu na siku zijazo. Vilevile, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – OWM programu mbalimbali zinafanyika kwaajili ya kuwawezesha vijana kuongeza maarifa na ujuzi ambazo ni pamoja na; (1) Mafunzo ya Ujasiriamali na Usimamizi wa Biashara chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (KVAU). Mafunzo haya ni kwaajili ya kutoa elimu ya Ujasiriamali na Usimamizi wa biashara kwa vijana ambao wamejiajiri katika sekta isiyo rasmi ili waweze kukuza na kuendeleza shughuli zao kwa weledi zaidi, walengwa wakiwa ni vijana wenye umri wa miaka 15 – 35; (2)Mafunzo ya Stadi za Ujuzi Ofisi ya Waziri Mkuu (KVAU), lengo ni Kuwapatia vijana walioko nje ya shule stadi za ujuzi mbalimbali zitakazowawezesha kujiajiri na kujipatia kipato (Mfano Ufundi Uashe, Ufundi Magari, Ufundi Umeme, Mapishi n.k) huku walengwa wakiwa ni vijana wenye umri wa miaka 15 – 35; (3) Mpango wa Kuhamasisha na kukuza Moyo wa Kujitolea miongoni mwa Vijana chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (KVAU) ili kujenga ari ya kujitolea miongoni mwa vijana pamoja na kuwa na makambi kazi (Work Camp) ya vijana ya kutekeleza shughuli mbalimbali za kujitolea na ushiriki wa shughuli za kijamii.

Tukija katika sula la uwezeshaji kiuchumi, moja ya mikakati ya wazi ya serikali katika kuwawezesha vijana kiuchumi ni pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu (PMO-YDF), ambapo lengo la mfuko huu ni kuwawezesha vijana kupata mitaji kwa njia ya mikopo ili kuanzisha au kuendeleza miradi yao ya uzalishaji mali kwa Vijana wote wa kike na kiume walio katika vikundi vya uzalishaji mali, wenye umri kati ya Miaka 15 hadi 35. Utaratibu wa kuzipata fedha hizi ni kupitia kuandika barua za maombi ambazo lazima zithibitishwe na Halmashauri husika.

Aidha, serikali kupitia Halmashauri zote nchini, hutenga asilimia 4% ya mapato ya Halmashauri kwa ajili ya kukopesha vikundi vya vijana wajasiliamali, huku asilimia 4% ikitengwa kwaajili ya wanawake na asilimia 2% kwaajili ya watu wenye ulemavu. Kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa, vijana wanapaswa kuwa katika kundi la watu angalau watano, kuwa na malengo ya ujasiliamari yanayofanana, kuanza kutekeleza biashara yao, kuandika mpango wa biashara unaoainisha namna gani watazitumia fedha wanaziomba kuboresha biashara yao na ndipo waweze kuomba mkopo wa halmashauri. Kupitia mipango hii miwili, wapo vijana wengi ambao wamenufaika, na kwa mujibu wa ripoti za Halmashauri mbalimbali nchini, fedha hizi kuna muda hubakia kutokana na idadi ndogo ya vikundi vya vijana vinavyojitokeza kuziomba.

Kupitia Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi - NEEC ambalo ni Taasisi ya Serikali iliyoanzishwa na sheria namba 16 ya mwaka 2004 kama njia ya kuharakisha mchakato wa kuwawezesha Watanzania kiuchumi. Baraza lina majukumu ya kuwezesha kubuni, kupanga, kusimamia, kufuatilia na kutathmini na pia kuratibu shughuli zote za uwezeshaji wa kiuchumi nchini. Pia, inajukumu la kuhamasisha rasilimali na kusimamia fedha maalum kwa ajili ya shughuli za uwezeshaji wa kiuchumi. Kwa vijana, Baraza hili linatoa fursa nyingi katika kuwajengea na kuendeleza uwezo katika eneo la ujasiriamali kwa vijana wote walio ndani ya mifumo rasmi ya elimu na wasio katika mifumo ya elimu. Baraza hili linatoa Fursa la kutafutiwa na kuunganishwa na masoko ya ndani na nje ya nchi ikiwa na lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi. Sambasamba na hilo Baraza hutoa pia mikopo kwa masharti nafuu pamoja na kuwaunganisha wadau wa maendeleo na wajasiriamali. Baraza hili husimamia uanzishwaji na uimarishaji wa vikundi vya kiuchumi, hasa vikundi vya kifedha vya kiuchumi (Community Financial Group-CFG). Vikundi hivi vinavyoanzishwa, humilikiwa na kuongozwa na wanavikundi wenyewe kwa lengo la kujiwekea akiba na kukopeshana wenyewe kwa ajili ya kupata mitaji ya kufanya shughuli za kiuchumi. Vikundi hivi vinajumuisha vile vinavyoweka akiba na kukopeshana kwa njia ya mzunguko (ROSCAs), ASCAs, Vikundi vya VICOBA, n.k.

Mahususi kwaajili ya wahitimu wa elimu ya juu, serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (OWM-KVAU) imetengeneza muongozo wa mafunzo kazini na uanagenzi (Internship and Apprenticeship Guidline) za mwaka 2017 ambazo zinawawezesha wahitimu kuomba na kupata fursa ya kujitolea katika taasisi mbalimbali za umma, taasisi binafsi na makampuni ili kuwajengea uwezo wa kupata uzoefu wa kazi wakati wakisubira ajira rasmi (kama zitajitokeza) huku wakipata walau kiasi kidogo cha fedha kuweza kujikimu kwa mujibu wa taratibu za taasisi husika zinazowekwa kwa kuzingatia masharti na kanuni za muongozo huo. Kwa mfano, mhitimu mwenye shahada ya utabibu ni sharti apitie walau kwa mwaka mmoja katika programu ya mafunzo kazini (internship) au uanagenzi (apprenticeship) ndio awe na sifa za kwenda katika ajira rasmi. Wahitimu wa proramu nyingine wanayo fursa pia ya kuomba nafasi za kujitolea ama za mafunzo kazini katika taasisi mbalimbali ili kukuza ujuzi wa kazi na kufanyia kazi maarifa waliyosomea.

Changamoto iliyopo katika fursa hii, ni kwamba Muongozo wa Kitaifa wa Mafunzo Kazini kwa wahitimu wa Elimu ya Juu, toleo la 2017, unakosa mfumo wa kisheria unaowabana walengwa wa utekelezaji, kiasi kwamba wadau wengine wadhani ama hawana wajibu wa kuufuata au hauwahusu kabisa, jambo ambalo limesababisha baadhi ya wahitimu ama kukosa nafasi za kujitolea/mafunzo kazini wanazoziomba katika makampuni au taasisi mbalimbali, au kutokupewa stahiki na hadhi inayostahili kama watu wanaojitolea kwa mujibu wa sera tajwa.

Pamoja na jitihada zilizoainishwa hapo juu na nyingine nyingi zinazofanywa na Serikali, ni kwa msingi huo baadhi ya viongozi wa serikali na raia wengine wanaoegemea upande wa Serikali wanadhani kwamba Serikali inatimiza vyema wajibu wake kwa vijana wa nchi hii na kwamba sasa vijana nao wanapaswa wajiongeze kwa kuchangamkia fursa zilizopo pamoja na kuutumia vizuri ujuzi walioupata kutoka kwenye elimu waliyohitimu ambayo imegharamiwa mabilioni ya fedha za umma.

Suala la msingi hapa ni kwamba, Serikali inatambua dhahiri kuwa ajira ni changamoto kubwa kwa vijana nchini na tayari inafanya jitihada nyingi kuweka mazingira wezeshi ya changamoto hiyo. Suala lingine katika eneo hili ni kwamba, serikali inaamini kwamba vijana hawatumii kikamilifu fursa zilizopo na zinazoendelea kutengenezwa kwaajili yao huku wakibakia kulalamika, jambo ambalo si zuri na sio afya kwa wasomi na ustawi wa nchi.

NINI KIFANYIKE ILI KUWAWEZESHA WAHITIMU KUJIAJIRI?
Kwa mujibu wa Sera ya Maendele ya Vijana ya mwaka 2007 – 2017 (iliyoisha muda wa wake wa matumizi miaka 5 iliyopita) iliwatambua vijana kama watu wenye umri kuanzia miaka 15 – 35, ambao kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, vijana walichukua angalau asilimia 34 ya idadi ya watu nchini huku wakichangia jumla ya 65% ya nguvu kazi ya Taifa kwa mujibu wa utafiti wa NBS wa nguvu kazi jumuishi (2001). Kiuhalisia, wahitimu wa elimu ya juu sio tu ndio vijana pekee katika nchi, na huenda idadi yao ikawa ni ndogo Zaidi kuliko kundi kubwa la vijana ambao hawafikii viwango vya kupata elimu ya juu. Hata hivyo, mimi ninawatazama wahitimu wa elimu ya juu kama kuku wa kisasa, ambao pamoja na uhalisia kwamba kuku wa kisasa nao ni kuku, bado wanahitaji kuwekewa mazingira wezeshi ya aina yake na kwa upekee mkubwa sana pengine kuliko kuku wa kienyeji kutokana na ukweli kwamba kuku wa kienyeji tayari wanakuwa na uzoefu mkubwa wa changamoto za mtaani. Kwa vijana ambao hawakupata fursa ya kuendelea hadi elimu ya juu, suala la kujiajiri kwao sio suala la kulijadili ila ni jambo la lazima, lakini kwa wahitimu wa elimu ya juu, ambao muda mwingi wameupoteza darasani, kujiajiri linaweza kuwa jambo lenye changamoto kidogo kama hawakuandaliwa vizuri hasa kisaikolojia.

Tumeshaona kwamba, changamoto ya wahitimu wa Elimu ya Juu nchini ni ajira, na kutokana na uhalisia kwamba ajira rasmi ni chache ikilinganishwa na uhitaji wake, suluhisho la kudumu na la uhakika ni kujiajiri. Tumeshaona vilevile kuwa, vijana wanaohitimu elimu ya juu hawana tatizo kabisa na kujiajiri ila huenda wengi wao hawajui kujiajiri ni kufanya nini hasa na pia namna gani ya kupata uwezeshaji wa kujiajiri.

Pamoja na jitihada nyingi zilizoainishwa juu ya mikakati ya Serikali inayofanyika kuwajengea mazingira mazuri vijana wa nchi hii katika kuwakomboa kifikra na kiuchumi, na kwakuwa bado tunaona kuna ombwe la kukitumia kile ambacho vijana wamejifunza vyuoni kukibadili ili kukabiliana na changamoto zinazoikabili jamii ikiwemo suala la ukosefu wa ajira. Nadhani, bado jitihada zaidi zinapaswa kufanywa na Serikali ili kuhakikisha kwamba uwekezaji wa mabilioni ya fedha kwa wahitimu wa vyuo vikuu hauendelei kuwa hasara na mzigo kwa kudai vitu vingi kutoka serikalini, bali ulete faida kwa kusaidia katika kutatua changamoto za jamii.

Laiti ningepewa nafasi ya kushauri nini kifanyike, basi ningependekeza mambo mawili makubwa. Kwanza, Elimu ya Ujasiliamali itolewe kwa wanafunzi wote nchini kwa ngazi zote za elimu. Pili, kuundwe mfuko wa uwezeshaji wahitimu kiuchumi (Graduates’ Economic Empowerment Fund – GEEF). Nitafafanua kama ifuatavyo:

1. Elimu ya ujasiriamali Itolewe kwa Wanafunzi wa Ngazi zote Nchini
Kujiajiri/Ujasiriamali kamwe hakuwezi kuwa mbadala wa ajira rasmi. Na hapa ndio tunafanya makosa, kwa kuwaambia wahitimu kwamba, kama hakuna ajira rasmi basi mjiajiri. Kimsingi, kwa mujibu wa ripoti za tafiti mbalimbali ikiwemo ya McAdam, M., Cunningham, J.A. (2019), kujiajiri kunajengwa na tabia ya ujasiriamali, ambayo mtu anapaswa kuwa nayo, na tunajua kwa hakika, tabia ni kitu kinachojengwa kwa muda mrefu sana na sio usiku mmoja. Hii inamaanisha kwamba, hata kama mtu atapata fursa ya kujifunza kozi ya ujasiriamali kwa muhula mmoja au hata mwaka mzima wa masomo, na akapata mtaji wa kujiajiri, bado inaweza kuwa ni vigumu kwenda kujiajiri atakapomaliza mafunzo yake endapo hiyo sio tabia yake. Ujasiliamali ni tabia, na tabia inatawala mawazo na vitendo vya mtu. Kwakuwa tunajua kuwa suala la ajira ni tatizo la dunia na kwamba kujiajiri ni suluhisho, na kwamba kujiajiri au ujasiliamali ni tabia, basi ushughulikiwaji wa tatizo hili unapaswa uanzie katika kujenga tabia ya wanafunzi kuwa wajasiliamali kwa kuwabarisha mitizamo wakiwa wadogo.

Ipo methali ya Kiswahili inasema, “Samaki mkunje angali mbichi”, ikimaanisha kwamba, mtoto mfunde tabia njema angali mdogo. Katika suala la kujenga tabia ya ujasiliamali, tunaweza kuanzia na elimu msingi, kwa kurejelea mitaala na kurudisha au kuweka somo au vitu fulani ndani ya masomo yaliyopo ambavyo vitajenga tabia ya ujasiliamali au kujiajiri. Nadhani, tunaweza pia kuweka somo la ujasiliamali kama lilivyo, badala ya kupachika vitu vichache katika somo jingine. Katika somo hili, mwanafunzi aanze kujifunza kutokana na daraja lake la elimu nini maana ya kujiajiri au ujasiliamali. Endapo mtaala utatengenezwa vizuri, somo hili lizidi kupanua wigo wa ufahamu wa suala la ujasiliamali kutoka darasa moja kwenda darasa la hatua nyingine hadi kufikia elimu ya juu. Ninaamini kwa kufanya hivi, mwanafunzi atakuwa amepata vitu vingi sana, pengine amejifunza suala la kujiajiri kwenye kila sekta hadi kufikia kumaliza elimu ya juu. Na hata kwa wale ambao hawapati fursa ya kuendelea na elimu ya juu kutokana na ufaulu, basi na wao watakuwa wameambulia kitu cha kwenda kuanzia nacho kujiajiri kulingana na elimu ya kujiajiri waliyoipata kuanzia darasa la kwanza hadi kufikia kiwango cha elimu wanachoishia.

Mwingine atahoji kwanini kila mtu ajifunze kujiajiri ilhali wengine hawana maono ya kijiajiri au hawana nia na suala la ujasiliamali. Jibu ni rahisi tu, katika ulimwengu wa sasa wa kibepari, maisha ni mchezo wa kutengeneza faida, na kwakuwa dunia inakabiliwa na changamoto ya ajira, kujiajiri ni suala la lazima, na kufanya hivyo kutaisaidia Serikali kwakuwa watu wengi zaidi wakijiajiri, wataweza kuwaajiri na watu wengine hivyo kutengeneza fursa nyingi za ajira zisizo rasmi na kuongeza wigo mkubwa wa kulipa kodi.

2. Uanzishwe Mfuko wa Uwezeshaji Wahitimu Kiuchumi (Graduates Economic Empowerment Fund - GEEF)
Katika kujibu hoja ya pili juu ya ugumu wa kupata mikopo ya mitaji kwa ajili ya kujiajiri kutoka kwenye taasisi za fedha sio rafiki kabisa kwa wahitimu wa elimu ya juu kwakuwa taasisi hizo huwa zina masharti magumu ikiwemo kuwa na rasilimali isiyohamishika na yenye thamani kubwa zaidi ya mkopo ambao mtu anauomba, jambo ambalo ni kikwazo kwa wahitimu; na kwakuwa tumeshaona ugumu uliopo kwa wahitimu wa elimu ya juu kupata fursa ya fedha za Serikali zinazotolewa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (OWM-KVAU) na Fedha za maendeleo ya vijana zinazotolewa kupitia Halmashauri kutokana na masharti magumu yanayowekwa ikiwemo kuwa kwenye vikundi vya watu angalau watano wenye mawazo yanayofanana, kuwa na biashara ambayo tayari imeshaanza na yenye thamani kubwa inayoendana na mikopo hiyo, n.k); na kwa kuzingatia ukweli kwamba wahitimu ni kundi maalum linalopaswa kupewa ungalizi wa kipekee tofauti na vijana wengine katika jamii, ninapendekeza kwamba, uanzishwe mfuko maalum wa kuwawezesha wahitimu wa elimu ya juu kiuchumi (Graduates Economic Empowerment Fund – GEEF) ambao utatatua kitendawili cha upatikanaji wa mitaji kwa wahitimu bila masharti magumu. Jukumu kubwa la mfuko huu liwe ni kuwawezesha vijana kupata mitaji, si kwa ufadhili, bali kwa mkopo, ila kwa masharti nafuu zaidi kuliko jitihada zozote zilizopo hivi sasa.

Pendekezo la kuanzisha Mfuko Maalum wa kuwawezesha Wahitimu wa Elimu ya Juu Kiuchumi – GEEF lina lenga kuhakikisha kwamba, wahitimu wote wa ngazi ya Shahada wanapata mikopo ya mitaji mara tu baada ya kumaliza masomo yao, ili kwa kutumia elimu waliyoipata ya kujiajiri/ujasiliamali tangu waanze masomo yao na kwa kutumia kiasi kidogo cha fedha ambacho mfuko huo utawawezesha, basi wakawe na sehemu ya kuanzia katika kujitegemea na kujiajiri huko mtaani. Kwa kuzingatia jitihada nyingi ambazo tayari zinafanyika na Serikali katika kuwawezesha vijana nchini, nadhani haitakuwa sahihi kuongeza mzigo mwingine kwa Serikali katika kushulikia changamoto hii ilhali fursa zilizopo zinaweza kutatua changamoto. Kwa maana hiyo, sina lengo la kupendekeza kitu kipya sana, isipokuwa nitaonesha njia kadhaa zinazoweza kuuwezesha mfuko huu kutoka kwenye jitihada zilizopo, ili mwisho wa siku kila mhitimu apate fedha ya mtaji ya kuanzia kujiajiri.

Kwanza, kabla sijazungumzia namna ya kuuwezesha huo mfuko wa uwezeshaji wahitimu kiuchumi, ni vyema tukajiuliza swali, ni kiasi gani hasa (kima cha chini kabisa) ambacho kinaweza kumsaidia mhitimu wa elimu ya juu angalau kuanza kujiajiri. Hapa, maoni yangu yanaweza yasijitosheleze, nilihitaji walau kuuliza wanafunzi wanaotazamia kuhitimu hivi karibuni na wale ambao tayari wameshaahitimu, wanadhani wangepata kiasi gani cha chini zaidi wangeweza kujiajiri. Kati ya wanafunzi wanaotarajia kumaliza, pamoja na wahitimu wachache walionipa maoni yao, wengi walisema, mhitimu angalau anahitaji kiasi kisichopungua Shilingi za Kitanzania 1,000,000/= hadi 2,000,000 ili walau kuweza kuanza jitihada za kujiajiri. Kwa maana hiyo basi, suluhisho ninaloenda kulipendekeza ni kuwezesha mhitimu kupata mtaji wa walau kiasi kisichopungua shilingi milioni moja hadi milioni mbili bila masharti magumu ili aweze kujiajiri. Katika majadiliano yetu, ilionekana kwamba, ugumu wa kupata mikopo kwenye taasisi za fedha ni masharti ya dhamana ambayo ni magumu sana, hivyo ni muhimu kuwa na njia mbadala itakayomfanya mhitimu aaminike na kupewa mkopo wa mtaji ili aweze kujiajiri, na bila shaka, mtu/taasisi pekee inayoweza kumuamini mhitimu na kumpatia mtaji bila dhamana wala masharti magumu ni Serikali tu kwakuwa itakuwa inafahamu thamani ya mhitimu na uwezo mkubwa alionao katika kujiajiri kutokana na elimu ya kujiajiri ambayo imempatia.

Pili, ni vyema kuwa na akisi ya ni watu wangapi wangepaswa kuwezeshwa ili kutokana na ukubwa wa kundi lao lilivyo kwa sasa na linavyotarajiwa kuwa siku zijazo, tuone ni njia zipi zinaweza kuleta masuluhisho rahisi na yasiyoumiza, yanayoweza kuupa fedha mfuko huu wa wahitimu. Kwa mujibu wa ripoti ya takwimu za vyuo vikuu iliyotolewa mwezi Mei 2022 na Tume ya Vyuo Vikuu - TCU, jumla ya wanafunzi 54,810 wa vyuo na vyuo vikuu walihitimu mwaka 2021 huku kati yao, wanafunzi wa ngazi ya shahada (ambao ndio walengwa zaidi katika makala hii) walikuwa 38,111 sawa na 69.5% ya wahitimu wote. Hata hivyo, ripoti hiyo inaonesha idadi ya wahitimu imeongezeka kutoka 46,294 mwaka 2017 hadi 54,810 mwaka 2021 ikiwa ni ongezeko la 18.3. Kwa kutumia makadirio ya ongezeko tajwa, na kwa kuzingatia kuwa kuna udahili mkubwa umefanyika wa wanafunzi katika elimu msingi, sekondari na kidato cha tano na sita kufuatia mpango wa elimu bila malipo ulioanza 2016 na 2022, tutegemee pengine wahitimu wa elimu ya juu watakuwa zaidi ya 64,000 hadi kufikia mwaka 2024 huku endapo uwiano ukiwa ni ule ule, basi wahitimu wa ngazi ya shahada watakuwa zaidi ya 44,500.

Kitaka andiko hili, nitapendekeza namna 3 ambazo zinaweza kuuwezesha mfuko wa uwezeshaji wahitimu kiuchumi – GEEF kupata fedha za kuwakopesha mitaji ya kujiajiri wahitimu wa elimu ya juu tukianza na makadirio ya idadi hapo juu. Njia hizi ni kama zifuatavyo;

i. Kupitia fedha za wanufaika wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu - HESLB
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu – HESLB inawapa mikopo wanafunzi wapya hadi elfu 65,000 kwa mujibu wa ripoti yake ya upangaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2021/2022. Hii inamaanisha kuwa, wanafunzi watakaomaliza masomo kuanzia mwaka 2024 watakuwa ni pamoja na wale walionufaika na mikopo ya HESLB kwa mwaka 2021/2022. Nje ya ada na mahitaji mengine ambayo wanafunzi wanakopeshwa, wanufaika wote wa mikopo ya HESLB wanapata shilingi 8,500/= kwaajili ya chakula na malazi, fedha ambazo wanakabidhiwa mikononi na wanaouhuru wa kupanga matumizi yake. Sasa, tunajua kwamba, kinachotoka HESLB ni Mkopo, lakini tunajua vilevile kwamba, kwa mwanafunzi Bodi ya Mikopo ni moja ya chanzo chake cha mapato, na kwa kawaida, mapato yanapaswa kupangiwa matumizi.

Kwa maisha ya chuo, kwa uzoefu nilionao, kwa namna yeyote ile, ni vigumu kwa mwanafunzi kutumia shilingi 8,500/= yote kwa siku moja kwa ajili tu ya kula na kulala. Hosteli nyingi za chuo, zinakodishwa kwa kati ya shilingi 500 hadi 1,000 kwa siku. Kantini katika vyuo vingi nchini, chakula kinaweza kupatikana kwa mlo mmoja kwa kati ya shilingi elfu 1,000 – 2500. Hii inamaanisha, matumizi ya chini kwa mwanafunzi kwaajili ya kula na kulala yanaweza kufikia shilingi 3,500 na matumizi ya juu yanaweza kufikia 7,000, na kumfanya mwanafunzi kuwa na walau fedha ya ziada kwa matumizi mengine. Fedha hii ya ziada, wapo wanaoweza kuitumia kwa kuweka akiba ili mwisho wa siku wapate kitu cha kuwawezesha kujikwamua kiuchumi. Lakini tabia za wanafunzi wengi hawaweki akiba, kiasi kwamba mwisho wa miaka ya masomo anajikuta aliwahi kupewa zaidi ya shilingi 6,000,000 za HESLB kwa kipindi cha miaka mitatu na hadi muda anamaliza chuo hana hata shilingi moja ambayo aliweka akiba.

Pendekezo langu la kwanza ni kwamba, serikali ikijiridhisha kuwa shilingi 7,000/= inaweza kumtosheleza mwanafunzi kutumia akiwa chuoni kwa siku moja, basi ikate kiasi kinachozidi yaani shilingi 1,500/= ambayo ni sawa na 17% kutoka kwenye fedha anayopewa hivi sasa mwanafunzi (8,500/=), ambapo fedha hiyo iliyokatwa ifanyike kuwa akiba ambayo itatunzwa kwenye mfuko wa uwezeshaji wahitimu kiuchumi – GEEF na itamuwezesha mhitimu kupata mtaji wa kujiajiri mara baada ya kuhitimu. Hii inamaanisha kwamba, hadi kufikia mwaka wa tatu, mwanafunzi atakuwa amekusanyiwa kiasi cha shilingi 1,080,000/=, kiasi ambacho kwa mujibu wa maoni niliyoyapokea kwa vijana kadhaa, japo hakiwezi kutosha kwa 100% kutokana na kutofautiana kwa mawazo ya biashara, ila kitasaidia sana mhitimu kuweza kupata pa kuanzia kujitegemea.

Kimsingi, pendekezo hili sio kitu kigeni, tayari Tanzania inatekeleza Sera ya Hifadhi ya Jamii (The National Social Security Policy) ya mwaka 2003 pamoja na sheria zilizotungwa chini ya sera hiyo, ambapo wafanyakazi wote, iwe wa sekta binafsi au sekta ya umma, hukatwa asilimia kadhaa katika mapato ya mishahara yao, na fedha hiyo iliyokatwa huwekwa katika mfuko wa hifadhi ya jamii kama vile NSSSF na PSSSF. Fedha hizi ni mali ya mfanyakazi na mara tu baada ya kufikia muda wake wa kustaafu, mfanyakazi hupewa fedha zake kwaajili ya kuzitumia kwa mujibu wa miongozo iliyowekwa na Sheria. Kwahiyo, pendekezo la GEEF halitofautiani sana na kinachofanyika katika mifuko ya hifadhi ya jamii, na ninapendekeza hivi kwakuwa ninaamini, kwa mwanafunzi, fedha inayotoka Bodi ya Mikopo ni chanzo cha mapato na ni jambo la kawaida kuigawanyisha katika matumizi mbalimbali kwa faida yake mwenyewe. Jambo hili linawezekana endapo tu, Sheria ya Bodi ya Mikopo namba 9 ya mwaka 2004 (iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2007, 2014 na 2016) na kanuni zake zitafanyiwa marekebisho ili kuweka wazi kuwa, bodi itamkopesha kiasi gani mwanafunzi, kiasi gani atapewa mkononi na kiasi gani kitawekwa kwenye Mfuko wa Uwezeshaji Wahitimu Kiuchumi – GEEF. Jambo hili linawezekana tu endapo litaanzia kwa wanafunzi wapya wanaojiunga na vyuo ambao watakuta utaratibu huo mpya, na kwakuwa hawakuzoeshwa kupata fedha nyingi mkononi, watalazimika kuendana na utaratibu huo mpya.

Ninafahamu, kutokana na kupanda kwa gharama za maisha, pengine Serikali inaweza kuhofia kupunguza fedha ya mwanafunzi na kuiweka kuwa akiba kwa wasiwasi wa kumuumiza mwanafunzi kimaisha chuoni. Nadhani wasiwasi huo sio mbaya sana, ila kama kweli dhamira ya dhati itakuwepo ya kuwawezesha wahitimu kupata mitaji isiyo na masharti magumu ili wajiajiri, namna ya pili ninayopendekeza ambayo ni bora zaidi ya kutekeleza adhma hii hii bila kumuumiza mwanafunzi, ni kuongeza fedha ya mkopo wa wanafunzi anayopewa kwaajili ya kula na kulala M & A) kwa kiasi cha Shilingi 1,500/= (yaani iongezeke kutoka shilingi 8,500/= za sasa iwe Shilingi 10,000/=) ambapo mwanafunzi ataendelea kupata mkononi fedha ile ile ya sasa (8,500/= kwa siku), na kiasi kilichoongezeka kitaingia katika mfuko wa uwezeshaji wa wahitimu kiuchumi – GEEF na atapatiwa mara baada ya kuhitimu kama mtaji wa kuanzia.

Vyovyote itakavyokuwa, iwe ni kwa kupunguza kiasi cha fedha anachopokea sasa au kwa kuongeza kiasi kilichopendekezwa, namna hii ni namna rahisi zaidi na yenye uhakika wa kusaidia wanafunzi wengi (mfano, mfumo huu ungeanza kutumika mwaka 2021/2022, basi kati ya wahitimu wengi wa mwaka 2024, angalau wahitimu waliokuwa sehemu ya wanufaika 65,000 wa mikopo ya HESLB wangekuwa na uhakika wa kupata mtaji wa kuanzia usiopungua Shilingi 1,080,000/=).

Kwa kuwa tayari fedha hizi zinatolewa kwa wanafunzi, na hata kama pendekezo langu lisipofanyiwa kazi, bado mwanafunzi ataendelea kupokea fedha ya bodi na kuzitumia zote (kama hana tabia ya ujasiliamali) atazitumia, na akifikia wakati wa kuhitimu anabaki hana chochote mkononi na bado atailaumu Serikali kwa kutokumuwekea mazingira mazuri ya kupata mtaji.

Kwa ufupi, kutoka kwenye fedha za mkopo anazopata mwanafunzi za HESLB, tunaweza kuwawezesha kuwajengea mazingira wanafunzi ama ya wao kupunguza matumizi au kwa serikali kuongeza bajeti ili baada tu ya kuhitimu, kama ambavyo huwa wazipokea fedha za HESLB, baada ya kukamilisha taratibu zitakazowekwa, kila mwanafunzi angeweza kusaini na kupokea kiasi kisichopungua Shilingi 1,080,000/= kama changamoto ya kwenda kutumia elimu aliyoipata, kuweza kujiajiri au kuanzisha fursa za ujasiliamali wakati wakisubiri bahati ya kuajiriwa. Hata hivyo, ninafahamu kwamba, njia hii haijitoshelezi kwakuwa sio wanafunzi wote wa elimu ya juu wananufaika na mikopo ya Bodi, kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutokukidhi vigezo vilivyowekwa. Kwahiyo, lipo kundi ambalo, njia hii pekee haitowasaidia, ndio maana, ninapendekeza njia ya pili ya kuupatia fedha mfuko wa uwezeshaji vijana kiuchumi kwa kwa kutumia mfuko wa Halmashauri wa uwezeshaji vijana kiuchumi.

ii. Kupitia Mfuko wa Mapato ya Halmashauri wa Uwezeshaji wa Vijana Kiuchumi
Kama ilivyoelezwa awali, kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa ya Mwaka 1983 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019, kila Halmashauri nchini zinapaswa kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwaajili ya kutoa mikopo kwa vijana (4%), wanawake (4%) na watu wenye ulemavu (2%). Tumeona hapo awali kwamba, wahitimu wengi wa elimu ya juu kutokana na tabia zao (ambazo huenda zinatokana na jinsi walivyoandaliwa na mfumo wetu wa elimu), japo kuna fursa hizi za mikopo kwa vijana ambazo ni 4% ya mapato halmashauri bado hawaendi kuzifuata. Kwahiyo, ninachopendekeza, kwa lengo la kuwawezesha vijana kujikwamua na tatizo la pili la kujiajiri ambalo ni mitaji, basi ikiwezekana, asilimia 1% tu kati ya 4% za mapato ya halmashauri ambazo hutengwa kwaajili ya vijana, zipelekwe kwenye mfuko wa Taifa wa Uwezeshaji wahitimu kiuchumi GEEF. Hii itasaidia kuongeza uwezo wa mfuko huo kuwawezesha wahitimu wengi zaidi kiuchumi mara tu baada ya kuhitimu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI ya ya Robo mwaka ya makusanyo ya halmashauri nchini kwa mwaka 2021, jumla ya makadirio ya mapato ambayo halmashauri zote nchini zilijiwekea ni Shilingi Bilioni 863.9. Hii inamaanisha kuwa, kwa pendekezo langu katika eneo hili, asilimia 1% ya mapato yote ya halmashauri (ambazo awali zilikuwa zinatumika kukopesha vikundi ndani ya hamshauri) iende kwenye mfuko wa kuwezesha wahitimu kiuchumi. Hii ni sawa na Shilingi Bilioni 8.6 (kwa kutumia akisi ya makusanyo tajwa). Fedha hiyo pekeyake, inaweza kuwawezesha wahitimu 8,600 kwa mgawanyo wa shilingi 1,000,000/= kwa kila mhitimu. Ikumbukwe kuwa, hapa anawezeshwa mhitimu mmoja, na sio kwa kikundi, hivyo kama masharti yatawataka wahitimu kwenda kwa kikundi, bado wastani wa mkopo watakaopata si chini ya kiwango hicho.

Pendekezo hili litachangia kwa kiasi kikubwa pale ambapo fedha ya bodi ya mikopo iliishia. Na ninapendekeza kwamba, ufikiwaji wa fedha hizi kwa walengwa uwe sawa na wanufaika wa bodi ya mikopo, yaani wahitimu wasaini na kupewa fedha mara tu wanapomaliza elimu ya juu, ikiwa ni pamoja na kukidhi vigezo na masharti mahususi yatakayowekwa labda pengine ikiwemo kuwasilisha mpango wa biashara kama itahitajika.

Nafahamu kunaweza kuwa na hoja ya kwanini wahitimu pekee watengewe robo ya fedha za mikopo ya vijana katika Halmashauri ilihali vijana ambao hawakufikia viwango vya kuhitimu ni wengi zaidi kwenye kila Halmashauri ikilinganishwa na wahitimu wa elimu ya juu. Jawabu langu ni rahisi sana, njia hii inafaa endapo tu wahitimu hawa watakuwa na elimu ya kina ya kujiajiri na ujasiliamali, elimu ambayo inaweza kuwawezesha kwenda kujiajiri endapo watapata msingi wa mtaji. Kwahiyo, kukiwa na mafanikio mazuri, vijana wanaojiajiri wanaweza kuwaajiri vijana wengine na hivyo kutanua wigo zaidi.

iii. Kupitia Uwekezaji wa Sekta Binafsi
Duniani kote, sekta binafsi imekuwa na mchango mkubwa sana katika kutatua changamoto za jamii. Ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi (Private-Public-Partnership) ni moja ya mambo yanayoungwa mkono na wadau wengi wa maendeleo kwa umuhimu wa sekta hii. Serikali kama ikiridhia, chini ya masharti fulani, inaweza kuikaribisha sekta binafsi (kama vile mifuko binafsi ya hifadhi ya jamii au mifuko binafsi ya bima) kuwekeza katika mfuko huu ili kuwawezesha vijana kupata mikopo ya mitaji chini ya masharti nafuu. Hii itasaidia sana kumalizia sehemu ndogo inayobakia baada ya jitihada kubwa sana za Serikali katika kukabiliana na changamoto hii.

Kwa mfano, kama wanufaika wapya wa mikopo ya elimu ya juu 65,000 kwa mwaka wa masomo 2021/2022 wangekuwa ndani ya pendekezo la kwanza, na endapo 60% tu ya wanafunzi hao ndio wangehitimu elimu ya juu mwaka 2024 (kwa sababu yeyote ile inayoweza kuzuia baadhi ya wanafunzi walioanza kupewa mikopo wasihitimu mwaka huo), basi zaidi ya wahitimu wa shahada 39,000 (kati ya 44,500 wanaotazamiwa kuhitimu mwaka huo) wangenufaika na fedha za GEEF. Pia, endapo pendekezo la pili litafanyiwa kazi na kwa kutumia makadirio hapo juu, basi kwa mwaka huohuo 2024, zaidi ya wahitimu 8,600 wangekuwa na fungu kwa ajili ya kuwawezesha kujiajiri. Kwa kutumia makadirio ya wahitimu 44,500 wa shahada mwaka 2024, njia ya kwanza na ya pili pekee zingetosha kuwapa mitaji ya kuanzia kujiajiri wahitimu wote wa ngazi ya shahada.

Hata hivyo, kutokana na hoja za ujumuishi kwa wahitimu wengine wasio wa shahada, Serikali inaweza kukaribisha sekta binafsi kuchangia katika mfuko wa GEEF ili uwanufaishe wahitimu wa ngazi zote kama ikiwezekana. Sekta binafsi ingeweza pia kuchangia pale ambapo njia mbili za mwanzo zingeishia katika kuuwezesha mfuko wa GEEF.

HITIMISHO:
Endapo nikiulizwa kwa nini ninapendekeza mambo hapo juu, majibu yangu ni kwamba: moja, kabla ya kumlaumu kijana anaehitimu elimu ya juu kwanini hajiajiri, nadhani itakuwa ni hekima zaidi kuhakikisha kwamba anafahamu kujiajiri ni kufanyaje. Kwa bahati mbaya sana, vijana wanalaumiwa kwanini hawajiajiri licha ya ukweli kwamba, huenda hadi wanahitimu elimu ya chuo kikuu hawajapata fursa ya kufundishwa kwa kina kitu kinachoitwa ujasiriamali au kujiajiri na misingi yake. Nadhani hapa panaweza kuwa ni sehemu sahihi kabisa ya kuanzia, kuhakikisha wanafunzi wote nchini wanajifunza kuhusu kujiajiri kupitia mfumo rasmi wa elimu, ikiwezekana kwenye ngazi zote za elimu, kuanzia shule za msingi hadi chuo kikuu.

Pili, gharama inayotumika kujenga uwezo wa kielimu kwa vijana nchini ni kubwa sana, kuanzia kutoa elimu bila malipo kwa elimu msingi hadi kutoa mikopo ya elimu ya juu. Kuhakikisha wahitimu wanawezeshwa kupata mitaji kwa uhakika kutasaidia kulinda thamani ya gharama zilizotumika kuwapatia elimu kwa kuwawezesha kuanza kutumia ujuzi wao kwaajili yao na familia zao. Kwa mfano, kwa mujibu wa Sheria ya HESLB namba 9 ya mwaka 2004 (kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2016 pamoja na kanuni zake), mnufaika wa bodi ya mikopo anapaswa kuanza kurejesha mkopo wa elimu ya juu miaka miwili baada ya kumaliza chuo. Sheria hiyo inaamini kwamba, kwa kipindi cha miaka miwili baada ya mwanafunzi kumaliza elimu ya juu basi ama atakuwa amepata ajira au amejiajiri hivyo atakuwa na uwezo wa kuanza kurejesha deni la elimu ya juu. Kwa bahati mbaya, hiki ni kitu ambacho ama hakitekelezeki au utekelezekaji wake ni wa mashaka, ndio maana HESLB imekuwa na idadi kubwa sana ya wadaiwa sugu, wale ambao muda wa kurejesha mikopo yao umefika lakini hawarejeshi. Hapa tatizo ni kwamba, wanafunzi wanakopeshwa hela kwaajili ya kula na wanatazamiwa kutengeneza faida baada ya miaka miwili ya kuhitimu bila kujua watakuwa wamejiajirije; hivyo, chini ya pendekezo hili, bodi itakuwa inatengeneza mazingira mazuri zaidi na ya uhakika ya kupata marejesho ya mikopo ya wahitimu kwakuwa watakuwa na kiasi cha kuanzia kujiajiri, kiasi kwamba hata wasipopata ajira rasmi, baada ya miaka miwili wanawezaa kuwa wamepata uwezo wa kurejesha hata kwa sehemu. Hii itasaidia sana kuiimarisha bodi ya mikopo yenyewe kuliko ilivyo hivi sasa.

Tatu, namna ninayoipendekeza inaweza isiwe na matokeo kwa asilimia 100, lakini hata kama itakuwa na ufanisi kwa asilimia 2, bado ni bora kuliko ilivyo hivi sasa. Pia, suala la ukosefu wa ajira ni changamoto kubwa sana ambayo isiposhughulikiwa madhara yake ni makubwa katika jamii ikiwemo kuhatarisha amani na usalama. Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa – UNDP ya mwaka 2019 juu ya vichocheo vya kuibuka kwa vikundi vya vurugu katika jamii ni kukosekana kwa ajira kwa vijana kunakopelekea umasikini kiasi cha kuwavuta vijana kutumia njia mbadala zisizofaa kujitafutia kipato, ikiwemo uhalifu. Kuweka suluhisho katika changamoto hii ni muhimu si tu kwa kukuza uchumi wa vijana bali pia kwaajili ya kudumisha amani na usalama wa jamii na nchi kwa ujumla.

Zaidi ya yote, dunia ya sasa ni dunia ya kibiashara. Akili na tabia ya ujasiliamali haiepukiki katika nyanja zote iwe ni biashara au sekta za teknolojia. Nchi inapaswa kuwajengea uwezo wahitimu kuwa wabunifu ili kukamata fursa za kujiajiri kwakuwa kadiri siku zinavyozidi kusogea, fursa za ajira zinapungua ikilinganishwa na uhitaji wa fursa hizo kutokana na ongezeko la wahitimu. Vijana wakipata elimu ya kujiajiri, itasaidia kujenga tabia kuanzia ngazi za chini za jamii ili kupunguza idadi ya vijana wavivu na walalamikaji. Muhimu zaidi, pendekezo hili ni moja tu ya masuluhisho mengi yanayoweza kutumika kutatua changamoto ya wahitimu kutokujiajiri. Asante.

KWAAJILI YA REJEA:
- Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Na. 9 ya Mwaka 2004 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2016

- Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2003

- Sheria ya Hifadhi ya Jamii ya Mwaka 2018 pamoja na marekebisho ya mwaka 2022

- Ripoti ya Ofisi ya Rais - TAMISEMI juu ya makusanyo ya Halmashauri kwa robo mwaka 2020.

- Taarifa ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu – HESLB juu ya upangaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu mwaka wa masomo 2021/2022.

- Sheria ya makusanyo ya fedha za serikali za mitaa ya mwaka 1983 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

- Ripoti ya Takwimu za Vyuo Vikuu nchini (VitalStats 2021) iliyotolewa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania – TCU, Mei 2022.

- Muongozo wa Taifa wa Mafunzo Kazini wa mwaka 2017 kwa wahitimu wa elimu ya juu.

- Ripoti ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa juu ya viashiria vya uvunjifu wa amani ya mwaka 2019.

- Ripoti ya ILO juu ya hali ya ukosefu wa ajira kwa mwaka 2022.

- Ripoti ya utafiti wa Mamlaka ya Takwimu Tanzania - NBS juu ya nguvu kazi jumuishi ya Taifa mwaka 2014.

- McAdam, M., Cunningham, J.A. (2019). Entrepreneurial Behaviour: A Research Outlook. In: McAdam, M., Cunningham, J. (eds) Entrepreneurial Behaviour. Palgrave Macmillan, Cham. https://doi.org/10.1007/978-3-030-04402-2_1

- Arif Fazael N. (2021). Fursa za Kiuchumi kwa Vijana Nchini Tanzania.

- Swahibu Kanju (2022). Makala; Wahitimu wa Vyuo Vikuu Tanzania na mtazamo hasi dhidi ya ajira na kujiajiri.

- Oscar Kimaro (2016), Vijana wa Tanzania: Vipaumbele vyao, Changamoto na Fursa.
 
Attachments

  • Makala - Wahitimu wa Elimu ya Juu Nchini na Kitendawili cha Kujiajiri..pdf
    1.1 MB · Views: 23

Kupitia Uwekezaji wa Sekta Binafsi

    1.1 MB · Views: 8
Nimelisoma andiko lako ni zuri Sana,limetoa ufahamu Mpana juu ya changamoto ambazo zinawakuta vijana wengi hasa linapokuja swala la Ajira.

Naamini likifanyiwa kazi linaweza leta mabadiliko makubwa hapa inchini kwetu.

Hongera Sana.
 
Barua ndefu kama hii

Kwann ucweke summary tu kisha ukaacha attachment ya hyo makala yako kwa mwenda deep aiddownload na kuisoma.
Sasa umecopy na kuipaate wavivu wa kusoma kama mimi tumeiruka hii makala tukaja kucomment bila kuelewa yote uliyoyaandika kwa ufupi wa muda wa kusoma na maneno mengi
 
Nimependa Sana ndugu malekela unavyojenga hoja kisayansi jamii zaidi. Hata hivyo umetumia nadharia hii pendwa inayocheza na maono ya kikundi tengwa "marginalization". Nikiri tu kwamba hili tatizo la ajira ni tatizo kubwa, na kubwa zaidi. Ninavyosema kubwa namaanisha idadi ya wanao kosa ni wengi. Pia ninaposema kubwa zaidi namaanisha Kuna watu Wanaliishi Kwa ukali tofauti. Wenye koneksheni wanasubiri muda huku wakilia ajira. Wasio nayo wanalia na tatizo hili Kwa miaka yote. Hii ni Sawa na kusema kwamba suala la kutoa jibu la KUJIAJIRI kunajenga picha ya kuwa tusi Kwa hawa wasomi ilhali hawa wenye koneksheni (kipato cha Kati) wengi wao Kwa namna moja au nyingine WANALIWEZA. sisemi kwamba hawa watu wajiajiri. Pia naomba nikutambulishe Kwa huu mtazamo wa sayansi jamii kwamba, hawa wanatoa Suluhu kuwa "Vijana Wajiajiri" ni wanufaika wa huu mfumo wa uzalishaji faida. Hakuna yoyote Kati yao ambae yeye na mwanae wanaichukulia hii kauli Kwa maumivu Yale ambayo wanaolengwa wanapata. Itoshe tu kusema tunahitaji kulijenga jamii kivingine kabisa, elimu ya DARASANI ikiendelea kutoa sauti ya mkombozi wa maisha. Hakuna kitakachokuwa cha kweli Katika mapendkezo yako
Pili, ukisema 8500 inatosha si kweli. Hawa vijana Kuna ambao wanasaidia Familia zao majumbani bila kupenda. Hii ni msukumo wa maisha halisi ya wanapotoka ulivyo. Nikitoa uzoef wangu mimi, hawa watu wanaishi maisha magumu mnoo.. Jiulize kama mtu akikosa mkopo hawez kusoma chuo je akipata atanufaika mwenyewe!?. Nafkir Kwa nadharia hii ulitakiwa umguse yule masikini kuliko masikini wenzake ili upime ukweli wa hoja zako
 
Nimerudi kugusa mambo mawili matatu:

Mosi,nakubaliana na wewe elimu ya ujasiliamali ni muhimu Sana kutoelewa katika ngazi zote za elimu kutokana na level ya mhusika,ni kweli kbs mtu ambaye Hana idea ya ujasiliamali hata sasa HV umpe mtaji inaweza kumuwia vigumu kushiriki kikamilifu ktk biashara.

Pili, ktk 8,500 ya wanafunzi ni Bora ikaongezwa ikawa 10,000 ili Ile 1,500 iwe ndo kibubu chake ambapo mara baada ya mafunzo yake awe na kianzio cha biashara,inaweza kuwekwa ktk mfuko wq wahitimu kama ulivyosema au ikawekwa kama sehemu ya mfuko wa hifadhi ya jamii na mara baada ya kuhitimu akapata kianzio.

Kwakumalizia maandiko kama haya ni mazuri Sana na yanatoa suluhisho zuri katika kutatua changamoto mbali mbali ambazo zinaikumbuka jamii yetu kwasasa,tatizo huwekwa katika mashelfu na matokeo yake hatupati matunda ya kile ambacho wenzetu wamekifanyia utafiti.

Mwisho ingawa sio Kwa umuhimu,watanzania tujitahidi kusoma makala ndefu,huwezi pata maarifa Kwa viujumbe vidogo vidogo kama SMS,no tunafeli big time,ila mambo ya umbea tunaweza soma gazeti zima,kusoma kunahitaji jitihada kama jitihada nyingine Tu,Ila ukijiendekeza aah mi siwezi soma makala ndefu ujue unakosa maarifa mengi Sana,ndio maana kuna ule msemo UKITAKA KUMFICHA KITU MWAFRIKA BASI WEKA KWENYE KITABU!

Unaweza kutengemeza hobby ya kusoma Kwa kujitahidi kidogo kidogo kusoma maandiko marefu baada ya Mda utajikuta interest ya kusoma inaongezeka.
 
Hamna kitu hapa , anaandika bla blaa Tu za nadharia zisizo na mashiko katika uhalisia WA sasa na Hali ilivyo on ground .
 
Kwa jinsi ulivyoandika mambo mengi iko wazi hayo uliyoandika hayafanyi kazi kwenye ground. Uzi wako ni wa kuzidi kuwapotezea muda vijana.
 
Tunahitaji incubators na wawekezaji au urahisi wa kupata mikopo ya masharti nafuu.

Chukua madaktari, manesi, wafamasia, wateknolojia maabara nk takribani 20 wasio na kazi waingize kwenye incubator miezi 6 hadi mwaka mmoja kisha wajengee hospitali ya millioni 600 waiendeshe huku ukirejesha millioni 80 kila mwaka kule ulikotoa mtaji. Baada ya miaka 10 waachie hospitali yao na wewe utakuwa umetengeneza millioni 80 x 10 = 800,000,000 ambayo ni sawa na faida Tsh millioni 200 na wao watakuwa wamepata hospitali!
 
Kuna mtu ameandika hivyo Twitter

Screenshot_20220720-221559_1.jpg
 
Hili gazeti lote umemuandikia nani?

Weka summary kazi zenyewe hatuna halafu unakuja na bandiko refu ili utuchoshe.

#MaendeleoHayanaChama
 
Nimerudi kugusa mambo mawili matatu:

Mosi,nakubaliana na wewe elimu ya ujasiliamali ni muhimu Sana kutoelewa katika ngazi zote za elimu kutokana na level ya mhusika,ni kweli kbs mtu ambaye Hana idea ya ujasiliamali hata sasa HV umpe mtaji inaweza kumuwia vigumu kushiriki kikamilifu ktk biashara.

Pili, ktk 8,500 ya wanafunzi ni Bora ikaongezwa ikawa 10,000 ili Ile 1,500 iwe ndo kibubu chake ambapo mara baada ya mafunzo yake awe na kianzio cha biashara,inaweza kuwekwa ktk mfuko wq wahitimu kama ulivyosema au ikawekwa kama sehemu ya mfuko wa hifadhi ya jamii na mara baada ya kuhitimu akapata kianzio.

Kwakumalizia maandiko kama haya ni mazuri Sana na yanatoa suluhisho zuri katika kutatua changamoto mbali mbali ambazo zinaikumbuka jamii yetu kwasasa,tatizo huwekwa katika mashelfu na matokeo yake hatupati matunda ya kile ambacho wenzetu wamekifanyia utafiti.

Mwisho ingawa sio Kwa umuhimu,watanzania tujitahidi kusoma makala ndefu,huwezi pata maarifa Kwa viujumbe vidogo vidogo kama SMS,no tunafeli big time,ila mambo ya umbea tunaweza soma gazeti zima,kusoma kunahitaji jitihada kama jitihada nyingine Tu,Ila ukijiendekeza aah mi siwezi soma makala ndefu ujue unakosa maarifa mengi Sana,ndio maana kuna ule msemo UKITAKA KUMFICHA KITU MWAFRIKA BASI WEKA KWENYE KITABU!

Unaweza kutengemeza hobby ya kusoma Kwa kujitahidi kidogo kidogo kusoma maandiko marefu baada ya Mda utajikuta interest ya kusoma inaongezeka.
Huko ni kupangiana maisha..fupi tambu ndefu zina kera na kuboa.

#MaendeleoHayanaChama
 
Hamna kitu hapa , anaandika bla blaa Tu za nadharia zisizo na mashiko katika uhalisia WA sasa na Hali ilivyo on ground .
Hawa chawa wa kijani..huwa wakianza kuvaa vikauanda suti na kuweka baji ya bendera ya taifa wanajionaga smart sana kumbe hamnazo..wanatafuta atentio ya teuzi..wakipewa teuzi utawaona walivyo wanafiki..absurd.

Uzuri tunawafahamu sana..na vijitabia vyao vya kujipendekeza ka kujifanya smart kumbe njaa na unafiki mtupu.

Kiufupi andiko lake hata hao waliopo sasa hawaezi lifanyia kazi hata yeye akipewa uteuzi hawezi fanyia kazi anayoyasema.

#MaendeleoHayanaChama
 
Bandiko zuri unafaa kuwa mshauri wa serikali ila naona kwa ukanda tulionao tuna ardhi hatuitumii huko ujasirimali wasomi walime wakae camps kijijini tukiwa na chakula pamoja tunakula na kuuziana maisha yanaendelea madeal mengine yanakuja ya miradi mikubwa naamini.
 
Asante sana ndugu yangu.
 
Back
Top Bottom