SoC04 Wageni ni Tunu kwa Taifa

Tanzania Tuitakayo competition threads
Jun 25, 2023
45
31
Utangulizi
Kila mwananchi wa taifa fulani, hupenda kuona taifa lake likiwa kinara kwenye uchumi. Hii ni kwasababu, mafanikio ya taifa lolote duniani huanzia kwenye uimara wa uchumi kwanza, kwani hakuna chochote katika dunia hii unaweza kufanya bila uchumi imara, bila fedha, bila mtaji wa kuwekeza kama ni kwenye teknolojia, miundo mbinu, elimu, afya, habari na mawasiliano, na kadhalika.

Unaweza kujiuliza, kama uchumi imara yaani fedha ndiyo msingi wa shughuli zote za maendeleo, je! Tupate wapi fedha za kianzio na mtaji ili tuwekeze kwenye teknolojia, elimu, afya, habari na mawasiliano na shughuli nyinginezo za kukuza uchumi wa taifa na mtu mmoja mmoja?

Jibu ni; taifa lolote hupata fedha na kukuza uchumi wake kupitia fedha za kigeni. Hii inamaanisha kuwa, mzunguko wa fedha za ndani pekee hautoshi kwa maendeleo ya taifa lolote lile, bali fedha za kigeni ndizo zinazokuza uchumi wa kila taifa lililoendelea.

Kumbe! Kama taifa tunapaswa kujikita kwenye shughuli ambazo zinahusika na kuwavuta wageni kwa wingi kuja nchini Tanzania kwa ajili ya shughuli za papo kwa hapo, za kati na za muda mrefu. Shughuli zinazowavutia zaidi wageni kuja nchini Tanzania ni shughuli za utalii, shughuli za kidiplomasia, shughuli za kibiashara, shughuli za uwekezaji, shughuli za kiserikali, shughuli za kimasomo na kiutafiti, mapumziko, n.k.

Ni kweli kwamba nchini Tanzania tunazo shughuli nyingi sana na vivutio vingi sana vya kuwavutia wageni kuja kufanya shughuli mbalimbali. Vivutio hivi ni vya asili, vya utamaduni na vilivyotengenezwa na wanadamu, lakini changamoto zifuatazo ni vizuizi na vikwazo kwa wageni wengi kuja nchini Tanzania kwa shughuli mbalimbali zenye kuleta fedha za kigeni.

Mazingira
Ukweli ni kwamba nchini Tanzania, mazingira au mandhari pekee inayowavutia wageni ni ile ya asili tuliyobarikiwa na MUNGU, lakini tumeuharibu uhalisia wa mazingira haya kwa kukata miti, kuchoma miti, uchafuzi wa mazingira yaani hewa, vyanzo vya maji na ardhi, makelele pamoja na shughuli nyingi za kibinadamu zinazoathiri mazingira yetu.

Uharibifu huu umewafanya wageni kutofurahia mazingira ya Taifa la Tanzania, kwani yapo maeneo ambayo mgeni anapokatiza na kukutana na chemba za maji machafu, chemba za vyoo, dampo za takataka, takataka za vifungashio vya vyakula, makelele, jua kali, n.k. vimezagaa kila mahali na kusababisha harufu zisizoeleweka na joto huku kunguru wachakarikao kutafuta chochote kitu wakimfokea mgeni huyo, huweza kumfanya mgeni aidha akiondoka asirudi tena au asiwe balozi mzuri wa kuitangaza Tanzania kwa ndugu, jamaa na marafiki kwenye taifa lake ili na wao waweze kuja nchini Tanzania kwa shughuli mbalimbali zenye kuleta fedha za kigeni. Jambo kubwa linalotiliwa maanani duniani kote ni usafi na utunzaji wa mazingira, ndiyo maana mikutano na kampeni za kimataifa kuhusu mazingira zimechukua nafasi kubwa katika miaka ya hivi karibuni.

Vivyo hivyo, taifa la Tanzania linapaswa kuboresha mazingira na miundombinu; kuanzia usafi, usalama, ubora, kiwango, uimara na uzuri wa mazingira yenyewe, barabara, nyumba za kulala wageni, usafiri, vyakula vya wageni, bidhaa na huduma zote wazipatazo wageni wakiwa nchini, kupitia Mapinduzi ya Teknolojia ya Mazingira.


Haki na Usawa
Haki na Usawa kati ya wageni na wenyeji ni jambo la muhimu ambalo tumelisahau sana kama taifa. Haijalishi ni utaratibu wa duniani kote au Afrika au Tanzania pekee, lakini kwasababu Tanzania ni nchi ya amani, na mgeni hupenda kukarimiwa vizuri; tunapaswa kuwakarimia wageni katika kila eneo iwapo hawavunji kanuni, taratibu na sheria za nchi. Mgeni anapokuja nchini Tanzania, ile bidhaa au huduma anayoipata mtanzania kama ni shilingi mia tano, mgeni pia anapaswa kuipata kwa kiasi hichohicho cha fedha yaani shilingi mia tano na si kumzidishia hata senti kwasababu ni mgeni. Kama taifa tunapaswa pia kuweka sheria za kuilinda haki hii kwa wageni.

Upo mfano mmoja ambao naukumbuka, kondakta wa daladala asiyejua Lugha ya Kiingereza, alipowaona wazungu wanataka kuingia kwenye daladala yake; ghafla alijua Kiingereza na ghafla akapanga bei mpya ya usafiri wake, ambapo nauli ya kila mzungu mmoja ilikuwa ni mara zaidi ya nne au tano ya nauli ya mwenyeji mmoja iliyowekwa kwa wakati huo.

Changamoto hii pia ipo kwenye baadhi ya ofisi za serikali yetu pendwa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwenye ofisi hizi, wageni huenda kwa ajili ya huduma mbalimbali ikiwemo kujisajili kwa ajili ya kutekeleza shughuli za uwekezaji, biashara, matamasha, n.k, lakini wanapofika eneo la kujisajili hukuta gharama tofauti kati ya mwenyeji na mgeni japo huduma ni ileile moja; kwa mgeni na kwa mwenyeji.

Wageni hukumbana na changamoto hii katika nyanja mbalimbali za huduma na bidhaa; kuanzia kula, kulala, usafiri, mavazi, na mengineyo ambayo bei ya bidhaa au huduma hiyohiyo moja; hupangwa tofauti kati ya mwenyeji na mgeni lakini bidhaa au huduma hubaki kuwa ileile. Hiki ni kipimo kizuri cha uaminifu wetu kwa wageni, ambapo kwa njia hii hutuona ni watu tusio na utu, ukarimu wala uaminifu.

Nidhamu ya Muda
Changamoto nyingine ni sisi wenyeji watanzania kutokwenda na muda. Iwe ni kwenye ofisi za serikali, ofisi binafsi, mtu binafsi, usafiri, chakula, huduma au bidhaa yoyote ile, wageni hupenda kwenda na muda; hawapendi kucheleweshwa hata kwa dakika moja.

Yupo Mwingereza mmoja ambaye nilifahamiana naye kupitia mwenyeji wake. Mgeni huyu alikuja nchini Tanzania kwa shughuli za kijamii, kujitolea na kutalii. Wakati tukiwa kwenye mazungumzo, mgeni huyo na mwenyeji wake walikuwa wakipanga kuhusu kesho yake; maeneo watakayotembelea na muda watakaoanza matembezi hayo.

Mwenyeji alimwambia mgeni wake, tuanze saa tatu asubuhi.

Mgeni alimwuliza: "Saa tatu Bongo Time or Mzungu Time?"

Ilinipasa niingilie mada na kumuuliza mwenyeji, kwanini amekuuliza hivyo? Mwenyeji akanieleza kuwa; hata wao wageni wanafahamu namna ambavyo saa tatu asubuhi ya Tanzania (Bongo) inaweza kuwa saa saba au saa nane mchana.

Hitimisho
Ili kuwa na Tanzania Tuitakayo, ni jukumula kila Mtanzania kuwa mkarimu na mwaminifu kwetu na kwa wageni, kuhakikisha mazingira yanayotuzunguka ni bora, safi na salama kwa ajili yetu na wageni, kuwa na nidhamu ya muda kwetu sisi wenyewe na kwa wageni, na pia kujua kuwa wingi wa fedha za kigeni tunaouhitaji hautokani na kuwatoza wageni tozo kubwa za bidhaa na huduma zinazotolewa nchini kuliko wenyeji, bali wingi wa fedha za kigeni tunaouhitaji, huja kwa kuyaboresha mazingira yetu na tabia zetu sisi wenyewe ili tuweze kuwavutia wageni wengi zaidi kutoka duniani kote na kuja nchini Tanzania kwa shughuli nyingi mbalimbali ukiwemo utalii, biashara, uwekezaji, kazi, makazi, n.k.​
 
Back
Top Bottom