Vigogo kustakiwa meli iliyoua Z`bar

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,322
33,126


Shein1(26).jpg

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.


Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, ametangaza ripoti ya uchunguzi wa kuzama kwa meli ya MV Spice Islanders, inayopendekeza vigogo wa serikali katika sekta ya usafirishaji Zanzibar na wamiliki wake kukamatwa na kufunguliwa mashtaka.


Ripoti hiyo ilitangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, ambaye alisema tume imegundua chanzo cha kuzama kwa meli hiyo ni kupakia abiria kupita kiwango, mizigo kupakiwa bila ya kuzingatia utaratibu na kusababisha meli hiyo kutitia sehemu ya nyuma kutokana na mzigo kuelemea upande mmoja.


Sababu nyingine ni kuruhusiwa kuendelea kutoa huduma wakati ilikuwa inakabiliwa na matatizo ya kiufundi.
Alisema meli hiyo ilikuwa imepakia abiria 2,470, lakini tume hiyo imeshindwa kufahamu kiwango cha mzigo kilichokuwa kimepakiwa kabla ya kuzama usiku wa Septemba 10, 2011, katika eneo la Nungwi, ilipokuwa ikitoka katika bandari ya Malindi kuelekea Pemba.


Alisema abiria 203 walifariki dunia, 941 waliokolewa na 1,370 hawaonekani licha ya kuwepo taarifa ya kuthibitika kuwa walisafiri na chombo hicho.


Watu 216 zikiwemo taasisi mbalimbali kama Shirika la Bandari Zanzibar(ZPC), Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar(ZMA), Mamlaka ya Usafiri wa Baharini na Nchi Kavu (SUMATRA), walihojiwa na tume hiyo, ambayo iliundwa Septemba 27 mwaka jana na kukamilisha kazi hiyo Novemba 31.


“Kabla ya meli kupinduka na kuzama ilikaguliwa na Sumatra mkoani Tanga, na kubainika ina matatizo ya kiufundi, Mamlaka ya usafiri baharini Zanzibar waliruhusu meli hiyo kuendelea kutoa huduma za usafiri bila ya kuzingatia sheria za usalama wa vyombo vya usafiri baharini,” alisema Dk. Abdulhamid.


Alisema tume hiyo imependekeza watendaji wakuu wenye dhamana kukamatwa na kushitakiwa kutokana na kushindwa kusimamia sheria na kanuni za usafirishaji na kusababisha watu kupoteza maisha na wengine kupoteza mali zao.


Wanaotakiwa kushitakiwa ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafirishaji Zanzibar, Vuai Haji Ussi, kutokana na kosa la kutoa cheti cha usajili wa meli hiyo licha ya kuwa inakabiliwa na matatizo ya kiufundi na kushindwa kusimamia ipasavyo usalama wa abiria na mali zao.


Aidha alisema Mkurugenzi huyo alishindwa kusimamia suala la ajira kwa mabaharia wenye sifa, na kushindwa kusimamia wasaidizi wake, hasa katika suala zima la kusimamia sheria na kanuni za usafirishaji baharini.


Mwingine ni Mrajis wa Meli Zanzibar, Mohamed Abdallah, ambaye alishindwa kuheshimu ripoti ya ukaguzi ya SUMATRA kuhusu matatizo ya kiufundi ya meli hiyo, badala yake aliruhusu meli hiyo kuendelea kutoa huduma kabla ya kupinduka na kuzama.


Mwingine ni Ofisa Mkaguzi wa Meli, Juma Seif Juma, ambaye alishindwa kusimamia majukumu yake ikiwemo kukagua sifa za mabaharia na kuruhusu meli kuendelea na safari licha ya kujitokeza kwa matatizo kabla ya kuondoka ikiwemo uzidishaji wa abiria kupita kiwango.


Mwingine ni Ofisa Usalama wa Bandari, Simai Nyange Simai, ambaye alishindwa kusimamia majukumu yake ikiwemo meli kupakia abiria kulingana na uwezo wake na kitendo cha kuwazuia abiria waliokuwa wakitaka kuteremka kabla ya meli kuondoka baada ya kuona meli hiyo imepakia abiria kupita kiwango.


Mwingine ni Ofisa Usafirishaji Bandari, Hassan Mussa Mwinyi, ambaye amebainika kutoa kibali cha kuruhusu meli kuondoka bila kuzingatia usalama wa meli na abiria.


“Hawa wamependekezwa washitakiwe na kwa upande wa Serikali tayari ripoti tumeifanyia kazi, na jukumu lililobakia ni la Jeshi la Polisi na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, lakini haya ni mapendekezo ya tume, bado haijawa hukumu na kazi hiyo ni ya Mahakama,” alisema.


Alisema kwa mujibu wa sheria za utumishi serikalini, watakaoshitakiwa watasimamishwa kazi, hadi kesi zao zitakapoamuliwa na mahakama.


Aliwataja wengine watakaoshitakiwa ni wamiliki wa meli, Salum Said Mohamed ‘Batashi’, Hasnuu Makame Hasnuu na Yusuph Suleiman Issa, ambao alisema tume imegundua wametenda makosa ya kuruhusu meli kufanya kazi wakijua inakabiliwa na matatizo ya kiufundi na usalama wake mdogo.


Aidha, Katibu Mkuu Kiongozi alisema wamiliki hao ndio wenye hisa katika kampuni ya Visiwani Shiping, lakini alisema kampuni hiyo inaonekana ikifanya kazi kwa karibu na kampuni nyingine ya meli ya Al Qubri inayomilikiwa na Jaku Hashim Ayoub, Salim Said Mohamed na Hasnuu Makame Hasnuu.


Aidha, tume hiyo imegundua wamiliki wa meli walikuwa wakifanya vitendo vya kuikosesha mapato serikali ikiwemo vya udanganyifu katika matumizi ya orodha ya abiria.

Pia, alisema mabaharia wote wa meli hiyo watashitakiwa kutokana na kushindwa kusaidia abiria wakati meli ilipoanza kupata dalili za kuzama pamoja na nahodha wa meli hiyo, Saidi Kinyenyete.

Serikali haifahamu kama nahodha wa meli hiyo yupo hai ama amekufa, hata tume imeshindwa kubainisha, lakini imesema atafutwe popote alipo na kufunguliwa mashitaka, alisema Dk.Abdulhamid.
Aliwataja maofisa wengine watakaoshitakiwa ni Abdallah Juma Hussein na Shaibu Said ambaye anatuhumiwa kutoa kauli za vitisho kwa abiria na kuwazuia kuteremka kabla ya meli kuondoka.


Vigogo wengine watakaochukuliwa hatua ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar, Mustapha Aboud Jumbe, ambaye amehusishwa na makosa manne, ikiwemo kushindwa kusimamia vyema wafanyakazi wake kwa kutowapa miongozo ya kazi na kushindwa kudhibiti usalama wa bandari kwa kuruhusu abiria kuingia kwenye meli na tiketi kukatwa chini ya ngazi ya kuingilia melini na wengine kuingizwa bila ya kuwa na tiketi.


Makosa mengine ni kushindwa kudhibiti usalama wa vyombo kwa kuruhusu meli za abiria kupakia abiria pamoja na mizigo kwa wakati mmoja, kuruhusu wachukuzi kuingia bandarini na kufanya kazi bila ya kuwa na sare na kushindwa kudhibiti usalama wa bandari.


Wengine waliopendekezwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu ni Kaimu Mdhibiti Bandari, Sarboko Makarani Sarboko; Mkuu wa Kituo cha Usalama wa Bandari, Usawa Khamis; askari wa Jeshi la Polisi Sajenti Jumbe na Koplo Juma na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).


Wengine ni Fundi Mkuu wa Meli hiyo, Abdallah Ali, ambaye alibainika kutopanga vizuri mizigo na mhandisi wa meli, Hamis Ahmada Hilika, ambaye pia amebainika kutosimamia vyema majukumu yake.


Tume hiyo pia imependekeza kampuni ya Visiwani Shipping na Al Qubra kusimamisha mara moja kutoa huduma za usafiri kutokana na vitendo vya ukwepaji wa kodi na kutozingatia usalama wa abiria na mizigo.


Kadhalika, tume imependekeza Zanzibar kuanzishwa chuo cha ubaharia ili waajiriwe watu wenye sifa na Serikali izuie uuzaji holela wa tiketi katika maeneo yasiyokuwa rasmi na Bandari kujenga eneo maalum la abiria na vikosi vya SMZ kupatiwa nyenzo na vifaa vya kisasa vya uokozi ikiwemo boti ziendazo kwa kasi pamoja na helikopta kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Pia tume hiyo imependekeza kuanzishwa kwa kituo maalum cha mawasiliano kitakachokuwa kikipokea kesi za ajali baharini na kiwe na ofisi zake kuanzia ngazi za wilaya hadi mikoa.


Kuhusu fidia, Dk.Abdulhamid alisema waathirika wote, watalipwa kwa kuzingatia sheria za bima, ambapo tume hiyo imependekeza waliopoteza maisha walipwe fidia ya kima cha chini cha mshahara wa SMZ (125,000) kwa kipindi cha miezi 80, sawa na Sh. milioni 10 kwa kila mtu, wakati walionusurika ama kwa kupatwa na ulemavu wa mwili au akili walipwe asilimia 75 ya kiwango hicho.


Vile vile, tume hiyo, imegundua kuwa meli iliyozama ilikuwa imekatiwa bima ya aina tofauti ikiwemo Dola 300,000 kwa abiria bila ya kukatiwa bima ya mizigo, ambapo kiwango hicho ni sawa na Dola 500 kwa kila abiria. Uwezo wake ulikuwa ni kuapkia abiria 600 na tani 500 za mizigo.


Tume hiyo pia imependekeza kuwekwa mwa mizani katika bandari zote kwa ajili ya kupima kiwango cha mizigo kinachopakiwa na vyombo vya usafiri.


Kuhusu hatma ya Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masoud, tume hiyo imependekeza kutumika kwa utaratibu wa Jumuiya ya Madola ya kuwajibika pindi yanapotokea maafa kama hayo kwa viongozi wenye dhamana ili kujenga misingi ya utawala bora.


Tume hiyo ya wajumbe 10 iliongozwa na Jaji Abdulhakim Ameir Issa.

KAMATA KAMATA YAANZA
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Zanzibar limeanza kuwakama viongozi na watendaji katika sekta ya usafirishaji baharini.


Uchunguzi wa NIPASHE umebaini kuwa vigogo hao walianza kukamatwa juzi na maafisa wa upelelezi kutoka Makao Makuu ya Jeshi hilo huko Ziwani Mkoa wa mjini Magharibi Zanzibar.


Kamishina wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alithibitisha jana kuwa tayari viongozi wawili na maafisa watatu katika sekta hiyo wamekamatwa na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kuanzia leo.


Aliwataja waliokamatwa na kuhojiwa kuwa ni Mkurugenzi wa Mamalaka ya Usafarishaji Zanzibar (ZMA) Haji Vuai Ussi (53) na Msajili wa Meli Zanzibar, Abdalla Mohammed Abdalla (53) ambao baadaye waliachiwa kwa dhamana kabla ya kufikishwa mahakamani.


Wengine ni Mkaguzi wa Meli wa Mamlaka ya Usafirishaji Baharini Zanzibar, Juma Seif Juma; Ofisa Usafirishaji wa Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC), Hassan Mussa Mwinyi (50), Msimamizi wa tiketi wa Kamapuni ya Visiwani, Shaib Said Mohammed (39) na msimamizi wa abiria, Juma Abdalla Hussen.


Kamishina Mussa alisema kwamba baada ya watu hao kuhojiwa majalada yao yamepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar ili kukamilisha taratibu za kuwafikisha mahakamani.


CHANZO: NIPASHE


 
Back
Top Bottom