Stories of Change - 2023 Competition

prima facie

New Member
Jun 8, 2023
1
1
1.1 Utangulizi

Katika kuhakikisha suala la utawala bora linatekelezwa hapa nchini, serikali imekuwa ikifanya juhudi za mageuzi ya kutumia teknolojia na kuanzisha mifumo ya Tehama, hii ikiwa ni katika jitihada za kuimarisha uwazi na uwajibikaji kiutendaji katika ngazi mbalimbali zinazotoa huduma kwa umma. Jitihada hizo zimefanyika katika sekta mbalimbali zikiwemo za mahakama ili kuimarisha utawala bora. Hata hivyo, bado juhudi hizi zinasuasua katika kusimamia utendaji kazi hususani kwenye ngazi ya Baraza la Kata ambalo limepewa mamlaka kisheria katika kusuluhisha migogoro mbalimbali ikiwemo ya ardhi. Hivyo, andiko hili linalenga kuonyesha changamoto zinazokwamisha utawala bora katika ngazi ya Baraza la Kata hasa katika usuluhishi wa migogoro ya ardhi.

1.2 Dhana ya utawala bora na baraza la kata

1.2.1 Utawala bora


Ili kuelewa vyema dhana hii, kwanza, tuelewe nini maana ya utawala bora.

Kwa mujibu wa mwanazuoni Issa Shivji katika chapisho lake “Good Governance, Bad Governance and the Quest for Democracy in Africa: An alternative Perspective”, la mwaka 2004 anabainisha wazi kuwa utawala bora ni namna ambavyo taasisi ya mahusiano yanayohusiana na mamalaka ya kisiasa yanatekelezwa na kuhalalishwa. Kwa maana nyingine, utawala bora ni utumiaji wa mamlaka ya kisiasa kusimamia mambo ya kitaifa. Utumiaji wa mamlaka hayo, huweza kuhusisha taratibu mbalimbali ikiwemo uundaji wa sera za nchi. Mwanazuoni Shivji anazidi kubainisha kuwa utawala bora ni zana bora zaidi ya propaganda inayoweza kubadilishwa na yeyote ambaye anatumia mamlaka. Mamlaka hayo yanaweza kuwa ya kidemokrasia, kimabavu au hata kidikteta ikitegemeana na mtumiaji husika.

Kwa upande mwingine, Khan na Gray katika chapisho lao la mwaka 2010 lenye kichwa cha habari “Good Governance and Growth in Africa: What can we learn from Tanzania”, wanafafanua kuwa utawala bora ni njia kuu ya kukuza maendeleo endelevu, kupunguza umaskini, kudumisha amani na kuchochea uwazi na uwajibikaji hasa katika maslahi ya taifa.

Vilevile, Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa lijulikanalo kama “UNDP” linafafanua kuwa, utawala bora ni mifumo ya uongozi, yenye uwezo, sikivu, jumuishi na uwazi. Mifumo hii, hujumusha michakato na mikataba ya kijamii ambayo kwa pamoja huamua jinsi mamlaka yanavyotumika, jinsi maamuzi muhimu yanavyoathiri jamii na jinsi maslahi mbalimbali yanavyotolewa kwa maaumuzi husika.

Kwa maana hiyo, ni wazi kuwa utawala bora ni mchakato ambao maamuzi hufanywa na kutekelezwa kwa njia iliyowazi na halali ili kufikia sera thabiti na zenye ufanisi. Utawala bora unatazamwa kama njia ya kujenga na kudumisha mazingira jumusihi na yenye uwajibikaji. Utawala bora huweza kutumika ngazi ya kimataifa, kitaifa na ndani ya asasi mbalimbali ili kukuza maendeleo endelevu.

1.2.2 Baraza la kata
Hiki ni chombo kisheria chenye madaraka ya kusikiliza masuala ya migogoro mbalimbali ikiwemo ya ardhi katika eneo la utawala wake. Kwa mujibu wa fungu la 13 la Sheria ya Mahakama za Migogoro ya Ardhi (Sura ya 216 R.E 2019), kinabainisha kuwa Baraza hili lina uwezo wa kufanya usuluhishi na kutoa ushauri. Kwa maana nyingine, Baraza la kata haliusiki na utoaji hukumu kama inavyofanywa na mahakama nyingine ikiwemo Baraza la Ardhi la Wilaya.

1.3 Changamoto zinazokwamisha utawala bora kwenye Baraza la Kata

1.3.1 Rushwa

Rushwa ni adui wa haki na kipingamizi cha maendeleo endelevu kwa Baraza la Kata. Mfano mzuri licha ya taratibu za Baraza kueleza wazi kuwa mjumbe yoyote wa Baraza la kata ambaye katika shauri lolote atakuwa na maslahi na shauri husika, basi hapaswi kushiriki katika shauri hilo. Baadhi ya Mabaraza ya kata hapa nchini yameendelea kusikiliza mashauri wakati miongoni mwa wajumbe wa Baraza husika wana undugu, au urafiki na mdai au mdaiwa wa shauri husika. Kutokana na hali hiyo, wanasababisha kuzolotesha upatikanaji wa suluhu katika shauri husika kwa wakati. Kwa mantiki hiyo, dalili za rushwa zimekuwa zikichochewa na upendeleo ambao huaribu misingi ya utawala bora.

1.3.2 Kutokuwa na maadili ya utendaji kazi kwa baadhi ya wajumbe wanaoteuliwa kwenye Baraza la Kata

Sheria ya Baraza pamoja na marejeo yake inaelekeza kwamba, kamati ya maendeleo ya kata (ward committe) ndiyo yenye mamlaka ya kujishughulisha na upatikanaji wa wajumbe wa Baraza la kata na si vinginevyo. Kwa maana hiyo, wajumbe wanaoteuliwa wanatakiwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa mashauri ya Baraza badala ya kuteua kwa upendeleo yaani urafiki, misingi ya siasa n.k.

1.3.3 Matumizi mabaya ya mamlaka kwa waliopewa dhamana
Utumiaji wa mamlaka au matumizi holela ya madaraka, mambo haya mawili huweza kupelekea kukosekana kwa haki au usuluhishi wa migogoro wa ardhi. Mfano Baraza linaweza kutoa wito kwa mdai na mdaiwa wafike kwenye shauri saa 4 kamili asubuhi. Lakini viongozi walioitisha shauri hilo wanakuja saa 6 mchana kwa kuchelewa na bado wataanza shauri kwa muda wanaojisikia bila kuwapa taarifa waliowaita kwenye shauri. Hali hiyo huweza kuleta sitofahamu kwa mdai au mdaiwa au wajumbe wa Baraza wanachelewesha shauri kwa makusudi ili mleta shauri achoke na kukata tamaa kwa jinsi ambavyo anazungushwa na kupoteza muda.

1.3.4 Kutowajibika na kukosekana kwa uwazi
Wajumbe wa Baraza la Kata baadhi yao wanashindwa kuwajibika katika kufanya maamuzi. Mfano Baraza halina meno ya kumuajibisha mtu ambaye amepuuza wito wa Baraza. Na hivyo kufanya upatikanaji wa suluhu katika mashauri ya ardhi kuchukua muda mrefu.

Hali kadhalika, uwazi wa uamuzi unaonekana kuwa changamoto kwani kumbukumbu au mazungumzo ya mwenendo wa shauri yanayoandikwa na Katibu wa Baraza kwenye kikao cha Baraza huwa hayawekwi wazi kwa mdai au mdaiwa anapohitaji kuyapitia.

2.0 Hitimisho
Wakati umefika sasa, kuhakikisha watendaji wa Baraza la Kata wanafahamu misingi ya utawala bora na wazingatie misingi hiyo katika shughuli zao za kila siku. Vilevile, Baraza la Kata linapaswa kuhakikisha linatoa elimu kwa umma juu ya sheria, kanuni na taratibu zao jinsi wanavyofanya kazi. Hii itawajengea waleta mashauri kufahamu haki na wajibu wao katika upatikanaji wa suluhu kwenye migogoro hasa migogoro ya ardhi. Pia, sheria zinazohusika na Baraza la kata zinatakiwa kufanyiwa marekebisho ili kuwawezesha wajumbe wa Baraza hilo kufanya kazi zao kwa weledi zaidi.
 
Back
Top Bottom