Utaratibu wa Kuomba Dhamana Nchini Tanzania (Bail Procedures)

Apr 26, 2022
64
100
Habari, leo nakuletea makala fupi kuhusu dhamana kwa mujibu wa Sheria za Tanzania.

Kwa kusoma makala hii utajifunza mambo yafuatayo:

(i) Utajua maana ya dhamana
(ii) Msingi wa dhamana kisheria
(iii) Aina za dhamana
(iv) Jinsi ya kuomba dhamana kwenye makosa ya uhujumu uchumi (economic offences)
(v) Jinsi ya kuomba dhamana kwenye makosa ya kawaida (non economic offences)
(vi) Nyaraka (documents) zinazotumika
(vii) Ufanyeje ukinyimwa au kufutiwa dhamana na
(viii) Nini kitatokea kwa wadhamini ikiwa mshtakiwa atakimbia

Makala hii imeandaliwa na kuletwa kwako nami Zakaria Maseke, Advocate Candidate - Law School of Tanzania. (zakariamaseke@gmail.com)

MAANA YA DHAMANA:

Dhamana ni kumwachia huru mtuhumiwa kwa masharti na kwa ahadi kwamba atapatikana baadae kama akihitajika.

Dhamana sio bure, lazima upeleke wadhamini au usalimishe vitambulisho vyako, utoe pesa n.k.

UHALALI WA DHAMANA KISHERIA (LEGAL BASIS YA BAIL)

Msingi au uhalali wa dhamana kisheria ni Katiba. Dhamana ni HAKI na ipo kwenye Katiba. Katiba inasema mtuhumiwa anachukuliwa kuwa hana hatia hadi pale itakapothibitishwa vinginevyo na Mahakama. Kanuni hii kwa kiingereza inaitwa “presumption of innocence.”

Kwa hiyo, kama ukimnyang'anya mtu uhuru wake na kumuweka gerezani kabla Mahakama haijamkuta na hatia, ni kana kwamba umeshamhukumu kuwa mkosaji tayari. Ndio maana dhamana inatolewa ili mtu asiteseke gerezani wakati bado haijathibitika kama kweli alifanya kosa au la! Soma Ibara ya 13(6)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ila kuna aina moja ya dhamana sio haki. Inaitwa bail pending appeal ( DHAMANA ANAYOOMBA MTU HUKU ANASUBIRIA MAOMBI YAKE YA RUFAA KUAMULIWA). Kwa nini dhamana hii (bail pending appeal) sio haki?

Kwa sababu dhamana ni haki ya mtu ambaye bado hajatiwa hatiani tukiamini hana hatia mpaka Mahakama ithibitishe. Lakini ukikutwa na hatia “presumption of innocence” inaisha unakuwa hauna haki ya kupewa dhamana. Hadi unakata rufaa maana yake unakuwa tayari umekutwa na hatia na umefungwa. Sasa kama umefungwa kwa nini tukupe dhamana wakati wewe sio innocent person?

Hivyo ukifungwa, dhamana inakuwa sio haki tena, ILA INAWEZA KUTOLEWA KATIKA MAZINGIRA MAALUM TU, kama vile ikionekana kuna uwezekano mkubwa wa kushinda rufaa n.k. (Tutaona baadaye lengo la kutoa dhamana wakati wa rufaa).

AINA ZA DHAMANA:

Kuna aina kuu mbili (2) za dhamana:
1: Dhamana inayotolewa polisi (police bail)
2: Dhamana inayotolewa Mahakamani (Court bail).

1: DHAMANA YA POLISI (POLICE BAIL)

Ni aina ya dhamana anayopewa mshukiwa wa uhalifu (suspect) akiwa kituo cha polisi wakati bado uchunguzi unaendelea.

Rejea kifungu cha 64 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (the Criminal Procedure Act [CAP. 20 R.E. 2022] (kwa kifupi tunaita CPA) na kifungu cha 16 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai katika Mahakama ya Mwanzo (the Primary Court Criminal Procedure Code) kwa kifupi inaitwa the PCCPC.

JINSI YA KUOMBA DHAMANA POLISI:

Kama ukikamatwa na polisi, unaomba dhamana kwa njia ya mdomo (you apply orally) kwa mkuu wa kituo cha polisi. Unaweza kuomba wewe mwenyewe au kupitia Wakili wako kama una Wakili.

Swali la msingi ni je, kuna wakati polisi hawataki kutoa dhamana hata kama kosa linadhaminika. Je, ukikutana na hiyo changamoto utafanyaje?

Kama polisi hawataki kutoa dhamana na hawataki kumpeleka mtuhumiwa Mahakamani ndani ya muda uliowekwa kisheria, unaweza kufungua kesi Mahakamani kuomba “habeas corpus,” ili Mahakama iwalazimishe, (ama watoe dhamana au waandike mashtaka haraka) wampeleke mtuhumiwa Mahakamani, kisha utamuombea dhamana Mahakamani (Court bail).

Kama ukifungua hiyo kesi wahusika (parties) wanakuwa ni mtuhumiwa mwenyewe kama muombaji (applicant), unawashtaki mkuu wa kituo, mkuu wa polisi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Mara nyingi kesi ya hivi haifiki hata kusikilizwa, simu zitapigwa kutoka juu, mwisho polisi huwa wanatoa dhamana au watampeleka mshtakiwa Mahakamani.

Nyaraka (document) ya kufanyia maombi (application) ya habeas corpus ni chamber summons. Alafu unawapelekea nakala (copy) hao uliowaunganisha kwenye kesi. (Hiyo ndo njia mbadala kama polisi wanakatalia dhamana).

2: DHAMANA YA MAHAKAMA (COURT BAIL):

Ni dhamana inayotolewa na Mahakama baada ya kuwa mtuhumiwa ameshapelekwa Mahakamani. Kwa sababu dhamana ya polisi inaisha automatic punde tu ukifikishwa Mahakamani. Kuanzia hapo Mahakama inakuwa ndio sasa ina mamlaka ya kutoa dhamana.

AINA ZA DHAMANA YA MAHAKAMANI:

1: DHAMANA KABLA KESI HAIJAISHA (BAIL PENDING TRIAL).

2: DHAMANA INAYOSUBIRI RUFAA AU MAPITIO YA HUKUMU (BAIL PENDING APPEAL OR REVISION).

3: DHAMANA KWA MAKOSA YANAYOPITIA MAHAKAMA ZA CHINI YAKISUBIRI KUPELEKWA MAHAKAMA KUU (BAIL DURING COMMITTAL PROCEEDINGS).

1: Tuanze na DHAMANA KABLA KESI HAIJAISHA (BAIL PENDING TRIAL).

Dhamana hii inaombwa baada ya kesi kuanza na kabla kesi haijaisha. Na kesi inaanza pale tu mtuhumiwa anapopelekwa Mahakamani, akasomewa mashtaka na akakiri au kukana kosa.

Haki hii ya dhamana ipo Kifungu namba 148 cha CPA na kifungu cha 36 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi. (the Economic and Organised Crimes Control Act [Cap. 200 R.E. 2022] kwa kifupi inaitwa EOCCA).

JINSI YA KUOMBA DHAMANA HUKU UNASUBIRIA KESI KUISHA (BAIL PENDING TRIAL):

Unaomba kwa njia ya mdomo (orally). Unamuomba Mheshimiwa Hakimu au Jaji kwa mdomo. Baada tu ya kusomewa mashtaka na kukataa kosa, wakati upande wa mashtaka wanaomba kesi iahirishwe kwa sababu upelelezi haujakamilika, hapo hapo omba dhamana kabla Mahakama haijaahirisha kesi kama kosa linadhaminika. (Ukikaa kimya unarudishwa selo).

Na mtuhumiwa au Wakili wako akishakuombea dhamana, Mahakama haitatoa dhamana kwanza hadi wawaulize upande wa mashtaka (Jamhuri) kama wanakubali au wanapinga. Kama Jamhuri ikikubali utapewa dhamana, lakini kama wakipinga na wakatoa sababu za msingi, hautapewa dhamana. (Kuna mambo ya kuzingatia pia kabla ya Mahakama kutoa dhamana).

JE UKIKOSA NAFASI YA KUOMBA DHAMANA MAHAKAMANI UTAFANYAJE:

Ikiwa ule wakati unasomewa mashtaka ili ukiri au ukane kosa (plea taking), hukupata nafasi ya kuomba dhamana kwa mdomo, utafanyaje upate dhamana?

Mfano mtuhumiwa wakati amepelekwa Mahakamani hakuwa na Wakili, labda hakuwa na hela muda huo ya kumlipa Wakili, linapokuja suala la dhamana anashindwa kujitetea kwa sababu hajui sheria na hana Wakili, anakosa dhamana. Hakimu anasema nenda rumande, alafu baadae ndo mtuhumiwa akatafuta Wakili, labda ndugu zake wanachanga hela wanatafuta wakili, wakati tayari yule mtuhumiwa ameshakosa dhamana na yupo rumande.

Kama Wakili ambaye umepewa kusimamia hiyo kesi leo, ukiwa umeshachelewa ile nafasi ya kuomba dhamana kwa mdomo mbele ya Mheshimiwa Hakimu, na kesi itakuja tena Mahakamani baada ya siku kumi na nne (14) utafanyaje? Je utasubiri siku 14 mteja wako aendelee kukaa ndani au uende Mahakamani kuomba dhamana? Na utaendaje Mahakamani kuomba dhamana na kesi ilishapangwa ije baada ya wiki mbili?

Ikitokea hivyo, kama unatamani kumuombea dhamana mteja wako aliyeko gerezani, Wakili unatakiwa kuiomba Mahakama itoe Amri ya Kutolewa (REMOVAL ORDER). Hii ni Amri inayotolewa na Mahakama ikimuagiza Mkuu wa Gereza kumleta mtuhumiwa Mahakamani tarehe iliyotajwa ili kwamba kesi inayomhusu ifanyike.

UNAOMBAJE REMOVAL ORDER?

Removal order inaombwa kwa njia ya MDOMO au kupitia BARUA rasmi. Wakili anaweza kwenda mbele ya Mheshimiwa Hakimu kumuomba atoe removal order au anaweza kuiandikia Mahakama barua rasmi kuiomba Mahakama itoe removal order ili mtuhumiwa aletwe Mahakamani ili Wakili amuombee dhamana.

Mheshimiwa Hakimu akikubali, atatoa form anaandika removal order, ambayo ni CR FORM NO. 13, inapatikana kwenye Criminal Procedure (Approved Forms) Notice, G.N. No. 429, 2017. Hakimu akishaandika removal order atampelekea afisa magereza ili amlete yule mtuhumiwa.

Zingatia, sijasema dhamana inaombwa kwa removal order! REMOVAL ORDER HAITOI DHAMANA, ila kazi ya removal order ni kumleta mtuhumiwa kutoka gerezani na kuja Mahakamani alafu akishaletwa Mahakamani unaomba dhamana kwa mdomo.

Pia, SIJASEMA DHAMANA INAOMBWA KWA BARUA. Dhamana wakati kesi haijaisha (bail pending trial) inaombwa kwa MDOMO (ORALLY), lakini ukikosa hiyo nafasi ya kuomba dhamana kwa mdomo, utafanyaje ili mshtakiwa eletwe Mahakamani ili umuombee dhamana kwa mdomo? Omba removal order. Na unaombaje removal order? Unaomba kwa mdomo au kupitia barua rasmi (official letter).

Ukiandika barua usiseme Mheshimiwa Hakimu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma, “MAOMBI YA DHAMANA” au maombi ili kumruhusu mtuhumiwa apate dhamana, utakuwa umekosea, hatuombi dhamana kupitia removal order.

Badala yake sema hivi, Mheshimiwa Hakimu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma, Maombi ya wewe kutoa removal order, ili mtuhumiwa fulani aletwe mbele yako ili nimuombee dhamana.

Twende aina ya pili.
2: DHAMANA INAYOSUBIRI RUFAA AU MAPITIO (BAIL PENDING APPEAL OR REVISION).

Aina hii ya dhamana inaombwa na mtu ambaye amekata rufaa (appeal) au ameomba mapitio (revision) kwenye Mahakama ya juu, akiiomba Mahakama kwamba akae nje ya gereza wakati rufaa au revision yake inaendelea.

Kama jina lake lilivyo, ina maana hapa kesi inakuwa imeisha, umekutwa na hatia, na umefungwa alafu umekata rufaa au umeomba mapitio upya ya hukumu (revision) kwenye Mahakama ya juu, kwa hiyo unataka ukae kwanza nje ya gereza wakati unasubiria rufaa yako au revision iishe.

Lengo ni kuzuia kuteseka gerezani ikitokea rufaa au revision yako imefanikiwa. Kwa sababu haitakuwa haki kukaa gerezani alafu baadae unakuja kushinda rufaa, unaambiwa huna hatia inabidi uachiwe huru wakati huo umeshasota gerezani muda wa kutosha. Itakuwa ni uonevu.

Sasa ili huo uonevu usitokee, sheria inaruhusu bail pending appeal or revision, ili badala ya kusota gerezani miaka mingi, uwe unatokea nyumbani kwako ili ukishindwa rufaa ndo uende jela. Kwa sababu, wakati mwingine rufaa zinachelewa kuisha, unaweza kuja kushinda rufaa na hapo hapo unakuta umetumikia muda wako wa kukaa gerezani umemaliza. Sasa kuna faida gani ya kushinda rufaa wakati ulishatumikia kifungo? Umekaa mwaka mzima gerezani au zaidi, kumbe hauna hatia.

Hiyo ndiyo sababu ya kutoa dhamana huku tunasubiria uamuzi wa rufaa. Rejea Kifungu cha 368 “CPA” na kifungu cha 24 cha Sheria ya Mahakama za Mahakimu (The Magistrates’ Courts Act [CAP. 11 R.E. 2019] kwa kifupi tunaiita “MCA”).

NB: Tunatumia “MCA” kwa kesi zilizoanzia Mahakama ya Mwanzo (Primary Court) na sio “CPA.” Kwa sababu “CPA” haitumiki kabisa Mahakama ya Mwanzo.

Mfano mtu amefungwa na Mahakama ya Mwanzo, kisha akakata rufaa Mahakama ya Wilaya (District Court), tukienda kwenye rufaa kule Mahakama ya Wilaya tunatumia MCA (kifungu cha 24) ambayo inatoa Mamlaka ya Mahakama ya Wilaya kwenye rufaa kwa kesi zinazotoka Mahakama ya Mwanzo. Sheria nyingine inayotumika ni the Judicature and Application of Laws (Criminal Appeals and Revisions in Proceedings Originating from Primary Courts) Rules, 2021, GN NO. 390.

Hata nyaraka (documents) unazoandaa chini ya sheria zinazotumika kwenye rufaa iliyotoka Mahakama ya Mwanzo ni tofauti na nyaraka utakazoandaa kwa rufaa zinazotumia sheria ya CPA.

Kwa hiyo mtu anayeomba dhamana huku anasubiria rufaa yake kuamuliwa (bail pending appeal), kwa kesi ambayo imeanzia Mahakama ya Mwanzo utatumia MCA na sio CPA.

JINSI YA KUOMBA DHAMANA WAKATI WA RUFAA:

Tuangalie sasa jinsi ya kuomba dhamana huku unasubiri rufaa yako itolewe uamuzi (bail pending appeal).

Maombi ya dhamana kipindi rufaa inaendelea yanafanyika kupitia maombi rasmi (formal application) kupitia documents - CHAMBER SUMMONS na AFFIDAVIT (hati ya kiapo). Na unaomba kwenye Mahakama ambayo umekata rufaa (it is done in the court where appeal or revision has been lodged).

Kuna mazingira mawili (scenarios mbili):

i): Kama kesi yako ilianzia Mahakama ya Mwanzo na umekata rufaa Mahakama ya Wilaya, basi utaomba dhamana (bail pending appeal) Mahakama ya Wilaya. Cha Kwanza unakata rufaa Mahakama ya Wilaya, alafu unaomba dhamana hapo hapo Mahakama ya Wilaya. Kwenye chamber summons unaweka kifungu / enabling provision ya MCA section 24. (Kwa sababu CPA haitumiki Mahakama ya Mwanzo).

ii): Kama Kesi ilianzia Mahakama ya Wilaya au Mahakama ya Hakimu Mkazi na rufaa iko Mahakama Kuu, basi omba dhamana (bail pending appeal) Mahakama Kuu. Kwamba, kama mtu amefungwa na Mahakama ya Wilaya au Mahakama ya Hakimu Mkazi, unakata rufaa Mahakama Kuu. Sheria ni CPA section 368.

Kama nilivyotangulia kusema juu, kesi zinazoanzia Mahakama ya Mwanzo zina sheria zake (na nikazitaja), hata kama kesi kutoka Mahakama ya Mwanzo itaendelea mpaka Mahakama Kuu, Sheria inayotumika sio CPA, lakini kesi ikianzia Mahakama ya Wilaya au Hakimu Mkazi - tumia CPA.

MAMBO YA KUZINGATIA ILI KUTOA DHAMANA WAKATI WA RUFAA (FACTORS FOR THE GRANT OF BAIL PENDING APPEAL).

Nilieleza mwanzo kabisa kwamba dhamana wakati wa rufaa sio haki yako ni upendeleo tu (privilege), na inatolewa katika mazingira maalum tu kama vile:

(i) Kama kuna mazingira yasiyo ya kawaida (existence of exceptional and unusual circumstances) mfano ikionekana kuna uwezekano mkubwa wa kushinda rufaa, kama adhabu ni fupi sana n.k.
(ii) Kama kuna hoja ya kisheria inayotosha kufungua kesi (where there is an arguable point of law).
(iii) Kama kuna ugonjwa wa kuambukiza unaoua haraka (where there is evidence of contagious disease resulting to immediate death) n.k.

NYARAKA (DOCUMENTS) ZINAZOTUMIKA KUOMBA DHAMANA WAKATI WA RUFAA (BAIL PENDING APPEAL):

Documents ni mbili, wakati wa rufaa unaomba dhamana kwa kutumia: Chamber summons na Affidavit.

Kwenye affidavit (hati ya kiapo) utatakiwa kutoa maelezo ambayo yanaonesha hayo mazingira maalum, sio uandike tu “hii kesi ina mazingira maalum”, lakini toa hoja au maelezo yanayoonesha kwamba hiyo kesi ina mazingira maalum au yasiyo ya kawaida. Mfano tengeneza mazingira kuonesha kwamba rufaa yako ina uwezekano mkubwa wa kufanikiwa (kushinda), usiandike tu “rufaa ina uwezekano mkubwa wa kufanikiwa” toa maelezo kuonesha huo uwezekano mkubwa.

Kwenye chamber summons unaandika kifungu husika na maombi unayoomba Mahakama. Hivyo ndivyo tunavyoomba dhamana wakati wa rufaa.

DHAMANA KWA MAKOSA YANAYOPITIA MAHAKAMA ZA CHINI KABLA YA KWENDA MAHAKAMA KUU (LAKINI YASIYO YA UHUJUMU UCHUMI) BAIL PENDING COMMITTAL PROCEEDINGS (IN NON ECONOMIC OFFENCES):

Kwanza tufahamu, committal proceedings ni nini? Committal proceedings inafanyika kwa makosa ambayo yanasikilizwa na Mahakama Kuu. Utayajuaje? Soma Jedwali (schedule) nyuma ya “CPA” utaona hayo makosa, kosa maarufu sana ni la mauaji (murder).

Sasa utaratibu uko hivi, kwa makosa ambayo yanapaswa kusikilizwa na Mahakama Kuu, lazima mtuhumiwa apelekwe kwanza Mahakama ya chini (Mahakama ya Wilaya au Mahakama ya Hakimu Mkazi) ili kufanyiwa committal proceedings.

Mfano kesi ya mauaji inatakiwa kusikilizwa Mahakama Kuu, lakini haitafunguliwa Mahakama Kuu moja kwa moja mpaka kwanza ipitie Mahakama ya Wilaya au Mahakama ya Hakimu Mkazi kwa ajili ya committal proceedings kwa kutumia nyaraka inaitwa P.I Charge (P.I maana yake ni preliminary inquiry). Kesi inaandikwa hivyo hivyo, mfano “in the District Court of Musoma, At Musoma, P.I number … of 2020, Republic vs Zakaria, charge, statement of the offense …. c/s …. of the Penal Code, Particulars of the offense….

Sasa kwa sababu ni kosa linalotakiwa kusikilizwa na Mahakama Kuu, mtuhumiwa akisomewa shtaka huko Mahakama ya Wilaya au Mahakama ya Hakimu Mkazi, haruhusiwi kusema (kujibu) chochote kwa sababu Mahakama aliyopo haina Mamlaka ya kusikiliza kesi yake.

Baada ya hapo wanaanza upelelezi wa kesi. Upande wa Jamhuri watafanya upelelezi, baada ya upelelezi kukamilika wanakuja kumsomea mshtakiwa maelezo ya ushahidi. Baada ya hapo ile Mahakama ya chini inamkabidhi (kumpeleka) yule mshtakiwa Mahakama Kuu kuanza kesi. (Hiyo ndo inaitwa committal proceedings).

Saa huu mlolongo unaweza kuchukua mwaka au hata miaka mitano. Sasa huo muda wote unaosubiri upelelezi ukamilike je utakaa gerezani tu? Na hata kama upelelezi utakuwa umekamilika wakakupeleka Mahakama Kuu, haimaanishi Mahakama Kuu itaanza kusikiliza kesi yako siku hiyo hiyo.

Mahakama Kuu inasikiliza kesi za jinai kwenye awamu maalumu (special session), nne kwa mwaka. Mfano labda mwezi wa tatu hadi wa nne ndo wanasikiliza kesi za jinai, baada ya hapo mpaka session ijayo mwezi wa sita hadi wa saba. Baada ya hapo mpaka mwezi wa tisa. Baada ya hapo mpaka mwakani tena mwezi wa pili mpaka wa tatu. Je, huo muda wote mshtakiwa atakaa jela au atakaa nje kwa dhamana? Kwa hiyo katika mazingira hayo, mshtakiwa hana budi kupewa dhamana.

Kwa hiyo, unaweza kuomba dhamana wakati wa committal proceedings, maana sio makosa yote yanayoenda kwenye committal proceedings hayana dhamana mfano kuua bila kukusudia (manslaughter) ni kosa lenye dhamana. Pia baadhi ya makosa ya uhujumu uchumi yana dhamana.

Swali la msingi ni je, ni Mahakama ipi inatakiwa kutoa dhamana wakati wa committal proceedings? Au mtu anatakiwa kuomba wapi dhamana? Je, ni kwenye Mahakama ile ile inayofanya committal au atakwenda Mahakama ya kule juu (Mahakama kuu) ambapo ndo mamlaka ya kusikiliza kesi yake ilipo (na wakati huo bado hawana hata faili lako)? Hapa ndo kuna utata.

Mfano umeshtakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia, ambalo linatakiwa kusikilizwa Mahakama Kuu, lakini umepelekwa kwenye committal proceedings Mahakama ya Wilaya na kosa linadhaminika. Je, Mahakama ya Wilaya ikupe dhamana kwa kesi ambayo haina mamlaka, maana hii kesi inatakiwa kusikilizwa Mahakama Kuu tu, hapo Mahakama ya chini ipo kwa ajili ya committal tu.

Je, inawezekana mahakama ya chini inayofanya committal kutoa dhamana? Maana ingawa haya ni makosa yanayosikilizwa na Mahakama Kuu tu lakini baadhi yana dhamana mfano kujaribu kuua (attempt to murder), kuua bila kukusudia (manslaughter) n.k.

Au ukisema ukaombe dhamana kule Mahakama Kuu, je Mahakama Kuu inaweza kukupa dhamana wakati kesi haijaenda (haijaanza bado) Mahakama Kuu? Kwa sababu wakati wa committal unakuwa haujapelekwa bado Mahakama Kuu. Sasa Mahakama Kuu itakupaje dhamana wakati bado kesi yako haijafika Mahakama Kuu?

Kunakuwa na kurushiana mpira, huyu wa chini anasema hii sio kesi yangu kama unataka dhamana subiri tumalize committal uende Mahakama Kuu ndo uombe dhamana, kwa hiyo unarudishwa rumande na kosa linadhaminika. Na ukienda Mahakama Kuu wanasema tutakupaje dhamana na kesi haijaja, kesi ipo Mahakama ya Wilaya au Hakimu Mkazi, unakujaje kuomba dhamana Mahakama Kuu?

Ashukuriwe Mungu, hiyo changamoto imeshatatuliwa na sheria. Soma maelezo yafuatayo hapa chini.

DHAMANA KWA MAKOSA YANAYOPITIA MAHAKAMA ZA CHINI KABLA YA KWENDA MAHAKAMA KUU IKO HIVI:

Kwa makosa ya kawaida (ambayo sio ya uhujumu uchumi) yanayosikilizwa na Mahakama kuu tu, dhamana inatolewa na Mahakama ya chini ambayo inafanya committal proceedings (kama kosa linadhaminika).

Kwa hiyo wakati unasubiria kesi yako kupelekwa Mahakama Kuu, kuna uwezekano wa Mahakama ya chini (committal court) kutoa dhamana (bail pending trial) wakati wa P.I (committal). Soma kifungu cha 245(4) CPA na kesi ya Republic. v. Dodoli Kapufi & Patson Tusalile, Criminal Revision No. 1 of 2008, CAT (unreported).

Mahakama ya Rufani ilisema, Mahakama ya chini ina mamlaka ya kutoa dhamana wakati wa committal proceedings kwa kosa lolote ambalo linadhaminika.

HOW DO YOU APPLY THAT BAIL (UNAOMBAJE HIYO DHAMANA):

Unaomba kwa njia ya mdomo. Unatamka tu, Mheshimiwa Hakimu, wakati committal proceedings inaendelea naomba mteja wangu awe nje kwa dhamana. Hiyo ni kwa upande wa makosa yasiyo ya uhujumu uchumi (ordinary offences). Kifungu cha 148 CPA.

DHAMANA KWA MAKOSA YA UHUJUMU UCHUMI YANAYOPITIA MAHAKAMA ZA CHINI KABLA YA KWENDA MAHAKAMA KUU (BAIL PENDING COMMITTAL PROCEEDINGS IN ECONOMIC OFFENCES):

Wakati wa committal (preliminary inquiry) kwa ajili ya makosa ya uhujumu uchumi ambayo yanapitia Mahakama ya chini kabla ya kwenda Mahakama Kuu, dhamana utaomba wapi? (Kwa makosa ambayo sio ya uhujumu uchumi ila yanapitia kwanza Mahakama ya chini kufanyiwa committal, tumeona utaenda kuomba dhamana kwenye Mahakama ile ile inayofanya committal).

Sasa iko hivi, dhamana katika makosa ya uhujumu uchumi inategemea na kiwango cha hela husika (monetary value involved).

Ukisoma kifungu cha 29(4) EOCCA, sheria inasema dhamana wakati wa committal proceedings kwenye kesi za uhujumu uchumi, inaweza kutolewa na Mahakama zifuatazo:

(i) Mahakama ya chini ambayo inafanya committal proceedings au
(ii) Mahakama Kuu ya KAWAIDA au
(iii) Mahakama Kuu KITENGO CHA UHUJUMU UCHUMI.

Kiujumla, utaratibu ni ule ule ila huku shida iko kwenye matumizi ya maneno “The Court” and “High Court” kwenye kifungu namba 29(4)(a) na 29(4)(d) cha EOCCA.

Ukisoma EOCCA inataja “High Court (Mahakama Kuu)” na the “Court (Mahakama).” Ukisoma kwenye ufafanuzi, “the Court (Mahakama)” kwenye hiyo sheria wamemaanisha Mahakama Kuu kitengo cha uhujumu uchumi alafu “High Court” ni ile Mahakama Kuu ya Kawaida.

Hivyo kwa minajiri ya dhamana kwenye uhujumu uchumi, tuna Mahakama Kuu mbili;- Mahakama Kuu ya uhujumu uchumi (the Court) na Mahakama Kuu ya Kawaida (Ordinary High Court).

Kiufupi kwenye makosa ya uhujumu uchumi, dhamana utaomba kwenye mahakama zifuatazo kutegemeana na mazingira yafuatayo:

(i) Dhamana hutolewa na Mahakama ya chini (Mahakama ya Wilaya {District Court} na Mahakama ya Hakimu Mkazi {the court of a Resident Magistrate}) ambayo inafanya committal, kama thamani ya hicho kitu haizidi shillingi million 300.

Mfano, mtu amekamatwa ila bado hajapelekwa (hajawa committed kwenda) Mahakama Kuu ya uhujumu uchumi (au wakati bado mchakato wa committal / inquiry unaendelea) utaomba dhamana Mahakama ya chini inayofanya committal, ikiwa tu thamani yake haizidi million 300. Section 29(4)a ya EOCCA.

Sheria ya 2019 ilikuwa inasema million 10, lakini kufuatia marekebisho ya mwaka 2022, sheria imeongeza kiasi mpaka million 300. Soma Section 29(4)(a) pamoja na kifungu cha 35 cha marekebisho ya Sheria mbalimbali namba 1, ya mwaka 2022 (the Written Laws (Miscellaneous Amendments) Act, 2022), ambayo imerekebisha kifungu cha 29(4)(a) kwa kuongeza pesa kutoka million 10 hadi 300.

Kwa hiyo ikizidi million 300, dhamana wakati wa committal itatolewa na Mahakama Kuu ya kawaida au Mahakama Kuu kitengo cha uhujumu uchumi (kutegemeana na kesi iko hatua gani kama tutakavyoona hapa chini).

(ii) Pili, dhamana hutolewa na Mahakama Kuu ya kawaida (ambayo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi) kama Mahakama ya chini imemaliza committal na wametoa amri (committal order) ya mshtakiwa kupelekwa Mahakama ya uhujumu uchumi. Ina maana mshtakiwa hayupo tena kwenye mamlaka ya Mahakama ya chini, hapo katikati wakati bado tarehe ya kesi yake haijaanza Mahakama Kuu ya uhujumu uchumi, ukitaka dhamana utaenda Mahakama Kuu ya kawaida (Ordinary High Court).

(iii) Na unaomba dhamana Mahakama ya uhujumu uchumi kama tayari kesi imeshaanza hapo. Kwamba, kama kesi imeshaanza kwenye Mahakama Kuu ya uhujumu uchumi, basi dhamana unaombea hapo hapo Mahakama Kuu kitengo cha uhujumu uchumi (kama kosa linadhaminika). Section 29(4)(c).

Mfano kama committal proceeding imefanyika, (mshtakiwa amefanyiwa committal na Mahakama ya Wilaya au Hakimu Mkazi), baada ya kumaliza, kesi yake ikapelekwa Mahakama Kuu ya uhujumu uchumi (kesi imekuja Mahakama Kuu ya uhujumu uchumi), tayari ilishafunguliwa na imeshapangiwa tarehe ya kusikilizwa, unatakiwa kwenda kuomba dhamana Mahakama Kuu ya uhujumu uchumi.

(Lakini kama kesi bado haijaanza kusikilizwa kwenye Mahakama Kuu ya Uhujumu Uchumi (ile scenario ya pili (ii) hapo juu), mfano committal proceeding imekamilika Mahakama ya Wilaya, mshtakiwa ameamriwa kupelekwa (amekuwa committed) kwenda Mahakama Kuu ya uhujumu uchumi, lakini kesi yake haijaletwa bado hapo Mahakamani (ya uhujumu uchumi), ina maana bado tunasubiri ifunguliwe, unatakiwa ukaombe dhamana kwenye Mahakama kuu ya Kawaida (ordinary High Court) kwa sababu kesi bado haijaletwa kwenye Mahakama Kuu kitengo cha uhujumu uchumi).

(iv) Pia sheria inasema “AT ANY STAGE” {wakati wowote) ambapo kesi haijaanza Mahakama Kuu kitengo cha uhujumu uchumi na thamani ya kitu ni million 10 au inazidi million 10, unatakiwa kuomba dhamana Mahakama Kuu ya Kawaida. HAPA SASA NDIO KUNA UTATA. Kuna jambo halijakaa sawa kwenye sheria

Ukisema at any stage (katika hatua yeyote) kabla kesi haijaanza Mahakama Kuu ya uhujumu uchumi, ina maana hata wakati wa committal kesi iko Mahakama ya Wilaya/Hakimu Mkazi, kwamba kama thamani ya kitu ni million 10 au imezidi millioni 10, uende kuomba dhamana Mahakama Kuu ya Kawaida, sasa kwa nini usiombee pale pale committal Court?

Soma kifungu namba 29(4)d cha EOCCA. Sheria imerekebishwa kifungu cha 29(4)a wakaongeza kiasi kutoka million 10 hadi 300, lakini kifungu cha 29(4)d bado sheria inasoma million 10. (Paragraph (d) haijarekebishwa bado ni million 10).

Cha ajabu Mahakama za chini zimewekewa kiwango kikubwa zinaweza kutoa dhamana kama thamani haizidi million 300, lakini hapa Mahakama Kuu imewekewa million 10. Je, ikizidi hiyo million 10 uende kuomba dhamana Mahakama Kuu au uende Mahakama ya chini kwa sababu iko ndani ya million 300? Kwa sababu paragraph (a) inasema million 300 (ni kwa Mahakama za chini), lakini (d) inaishia million 10 (kwa Mahakama Kuu), sheria imekinzana.

Anyway, hivyo ndo dhamana inavyotolewa kwenye kesi za uhujumu uchumi na mazingira yake.

Kwa hiyo, sio Mahakama yoyote tu inaweza kutoa dhamana kwenye makosa ya uhujumu uchumi, inategemeana na mazingira, thamani ya hela na hatua (stage) kesi ilipo. Mfano, Je, committal imeisha, kesi imeshahamia Mahakama Kuu ya uhujumu uchumi au bado?

Utajuaje kwamba, hapa dhamana ni Mahakama Kuu kitengo cha uhujumu uchumi (the Court) na hapa ni Mahakama Kuu ya kawaida (High Court)? Kifungu cha 29(4) EOCCA kinatoa majibu. Kiufupi, ili kujua Mahakama ipi itatoa dhamana na katika mazingira yapi, soma kifungu cha 29(4)(a), (b), (c) na (d) EOCCA.

Swali lingine, Je pale ambapo thamani ya hela ya hicho kitu haijulikani, dhamana utaombea wapi? Kwa sababu kuna makosa mengine ni ya uhujumu uchumi ila hayana thamani ya pesa, mfano kukutwa na silaha bila kibali, hawawezi kusema ulikuwa unamiliki bunduki ya shillingi kadhaa: - Kama thamani ya kitu haijulikani, maamuzi ya Mahakama (case laws) imeamua kwamba utaomba dhamana kwenye Mahakama Kuu ya Kawaida.

JINSI YA KUOMBA DHAMANA WAKATI WA COMMITTAL (HOW TO APPLY BAIL PENDING COMMITTAL PROCEEDINGS)

Ukiombea Ordinary High Court (Mahakama Kuu ya kawaida) peleka maombi rasmi (formal application). Ukiombea kwenye trial court yaani Mahakama inayosikiliza kesi muda huo unaweza kuomba kwa mdomo (orally).

Lakini mfano, kama hiyo kesi imezidi million 300 inabidi uende High Court (Mahakama kuu) kuomba dhamana. Tumia formal application. Documents (nyaraka) ni CHAMBER SUMMONS na AFFIDAVIT (hati ya kiapo).

NJIA ZA KUTOA DHAMANA:

Dhamana yoyote ikitolewa (iwe ni dhamana ya polisi / police bail, dhamana wakati kesi inaendelea Mahakamani / bail pending trial, au wakati wa rufaa / bail pending appeal, au bail pending committal), dhamana inatolewa kwa njia mbili.

(i) By recognizance (bila wadhamini):
Hapa mshtakiwa anapewa dhamana bila kuwa na wadhamini. Unajidhamini mwenyewe unatoa kitambulisho chako cha kazi unaondoka. Hakuna mtu anakuja kukudhamini hasa kwenye makosa madogo madogo ambayo mtu ana utambulisho kamili.

(ii) By bail bond (kwa kuweka wadhamini):
Hapa mshtakiwa analeta wadhamini ambao wanatoa pesa au mali fulani kama dhamana (bond) kwa serikali. Huu ni mkataba wa pande tatu, upande mmoja iko Mahakama, upande wa pili mshtakiwa na upande wa tatu wadhamini ambao watasaini mkataba wa dhamana.

Huo mkataba wa dhamana ambao unasainiwa na wadhamini sample yake ipo kwenye CR FORM NO. 10 ya sheria inayoitwa “the Criminal Procedure (Approved Forms) Notice, 2017, G.N. No. 429.” Kwa hiyo kama Hakimu au polisi anatoa dhamana atachukua hiyo fomu atajaza.

NINI KITATOKEA KAMA MSHTAKIWA ATAKIMBIA:

Kama mshtakiwa amepewa dhamana alafu amekimbia na wadhamini wake wakashindwa kumleta, zile mali zao zitataifishwa. Kesi haiwi ya kwako wala hubebi kosa la huyo mtu.

Mshtakiwa aliye nje kwa dhamana akitoroka, wadhamini wanatakiwa kupewa muda wa kutosha kumleta. Wakishindwa kumtafuta na kumleta, kile kitu walichoweka dhamana kitataifishwa na Mahakama. Mfano kama uliweka gari dhamana, gari hilo litakuwa la serikali kama ni nyumba itakua ya Serikali, kama ni hela utatoa hiyo hela. Ukishindwa kulipa kabisa utafungwa miezi sita. Soma section 160 CPA na Section 17 ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kwa Mahakama ya Mwanzo (the Primary Court Criminal Procedure Code/PCCC).

KUFUTIWA DHAMANA:

Mahakama inaweza ikakufutia dhamana au ikabadilisha masharti ya dhamana kutokana na sababu mbalimbali, lakini lazima kwanza mshtakiwa apewe nafasi ya kujitetea kwa nini asifutiwe dhamana. Section 150 CPA.

HAKI YA KUKATA RUFAA

Kama hujaridhika na uamuzi wowote wa Mahakama kuhusu dhamana unaweza kukata rufaa au kuomba revision (mapitio).

-----MWISHO----

Angalizo: Position au maelezo haya ni kwa mujibu wa kesi na sheria zilizokuwa zinatumika mpaka siku ya kupost hili andiko. Hivyo unaposoma leo haya maelezo, soma kesi na sheria zilizopo sasa hivi, ili ujue utaratibu bado ni ule ule au la! Sheria zinarekebishwa na mpya zinatungwa kila siku.

Pia natoa angalizo, wale wazee wa kukopi machapisho ya watu na kuweka majina yenu. Ni kosa kisheria. Hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayejimilikisha andiko hili. Unaruhusiwa tu kusambaza lakini usibadili yaliyomo. Ni heri uanze kuandika ya kwako mpya.

Disclaimer: Lengo la hii makala ni kutoa elimu kwa jamii. Huu sio ushauri wa kisheria kwa mtu yeyote. Ikiwa utaamua kufungua kesi kwa kufata haya maelezo na ukapata hasara, mwandishi wa maelezo haya hatawajibika kwa vyovyote vile. Kama unahitaji ushauri wa kisheria wasiliana na Mawakili.

Na kwa wanafunzi, hili andiko halijamaliza kila kitu. Hizi ni hints tu kwa ajili ya kukupa mwanga msomaji, ni ngumu kuandika hapa kila kitu kwa sababu hiki sio kitabu. (Kama mtu hujaelewa sehemu au unataka ufafanuzi uliza au kama una maoni au unataka kuongezea chochote karibu).

Yours sincerely,
Zakaria Maseke,
zakariamaseke@gmail.com
(0754575246 - WhatsApp)
Advocate Candidate,
Law School of Tanzania.
 
samahani naomba kujua hivi ukienda polis kumdhamin mtu ukaweka bond gari mfano. Je sku dhamana imefikia kikomo police hufaidika na nn au kuna pesa nayy huwa anapewa ?
 
haya mambo bakini nayo kwenye makaratasi ila latika maisha halisi hakuna kitu kama hicho.

unawashtaki vp ukiwa nyuma ya nondo ?
 
Makala ndefu samahan kama itakuwa ishaulizwa.
Mtu kakamatwa anaombwa atoe ela ili awepo nje.

1. Ni lazima kutoa hiyo ela?
2 baada ya kesi kuisha unarudishiwa ela yako?
3.
 
Back
Top Bottom