SoC02 Upatu/ VICOBA/ Marejesho na Afya ya wanawake

Stories of Change - 2022 Competition

Salum Makamba

Member
Feb 26, 2018
7
6
Mwishoni mwa mwezi uliopita nilikuwa natoka maeneo ya Manzese (kufuatilia jambo) kuelekea Makumbusho. Eneo nililokuwapo lina Kituo cha Daladala kiitwacho Big Brother na ndipo nilipopandia gari.

Garini palikuwa na abiria wachache waliotawanyika mithili ya punje za mtama zilizotoswa ardhini. Nami nilijichagulia siti ya pili nyuma ya dereva na kuketi kichovu.

Baada ya muda gari lilianza kuondoka huku Kondakta akiendelea kuita abiria kwa kupayuka. Alikuwa akitaja vituo vingi kisha mwisho akimalizia kwa kusema, "...kanisani, Kinondoni Studio, kwa Mama Zakaria, Makombosho (ndivyo anavyoitamka) hiyo."

Tangu gari imeanza kuondoka mimi nilikuwa nimekodoa macho nje nikitazama hekaheka za Wana-Mzizima. Kichwa changu nilikuwa nimekilaza kwa utulivu kwenye egemeo la kiti nilichoketi.

Tulipofika maeneo ya Manzese-Darajani gari lilisimama eneo lisilo na kituo na nilimsikia kondakta akimpayukia abiria awahi kupanda kwani gari i tuli katika eneo lisilo sahihi.

Ghafla gari lilianza kuondoka, na muda huohuo nilihisi kitu mithili ya kwenzi kikitua kichwani kwangu (ashukuriwe Mola nilikuwa nimevaa Kapelo). Niliondosha macho yangu kule nilipokuwa nikitazama, nikaitoa kofia kichwani na kupeleka kiganja pale palipoambukizwa maumivu halafu niligeuza shingo kumtazama kiumbe aliyeniadhibu bila kosa.

Nilikutana na kipisi cha mwanamke. Kavimbisha uso kama mzunguko wa Kloku-Tawa. Wigi limemkaa vururu-vururu, mashavuni wekundu wa kujichubua umemshupaa halafu kanuna kwelikweli. Uzoefu wangu mfupi kwenye dunia uliniambia namtazama mtu aliyevurugwa. Ambaye kama akili zake haziko sawa basi ana mengi yaendeleayo kichwani.

Niling'amua yeye ndo aliyenitia kwenzi (kwa kukusudia au ilitokea tu. Sijui!). Tulikutanisha macho. Hakuonyesha kunijali hata kidogo kama vile hakuna alichoufanyia mwili wangu. Nikaona kwa kuwa sijafa basi wacha nikae kimya maana naelewa ndimi za baadhi ya wanawake wa Dar es salaam. Unaweza kuuliza kisha ukaamsha vita usiyoweza kuizima. Niligeuka na kutazama mbele huku nikiusikia wimbo wa "nipo nyonyo" ukichezwa kwenye redio ya daladala.

Safari iliendelea ingawa nilikuwa nimekaa kimachale nisije kutiwa konzi lingine. Tulipofika maeneo ya Usalama, simu ya mwanamke huyo iliita. Wakati huo gari lilikuwa limependeza.

"Mwantumu niambie?" Yalikuwa ni maneno ya kwanza yaliyomtoka mwanamke aliyenitia kwenzi.

Alikaa kimya kwa muda (bila shaka alikuwa akimsikiliza Mwantumu), kwani punde alianza kulalama kwa sauti ya juu. Alianza kumweleza Mwantumu kuwa ana marejesho manne (likiwemo la mkopo wa benki) siku inayofuata halafu haelewi ni wapi atapata pesa.

Alikuwa anazungumza bila kujali yu kwenye daladala. Sauti ilikuwa juu halafu inaeleza matatizo. Wala hakuonyesha kujali. Mimi na abiria wenzangu hatukuwa na namna ila kuruhusu masikio yetu yasikilize kile kisemwacho. Kama ingelitokea umepanda daladala letu kwa ghafla ungesema ni waumini wanaomsikiliza Imamu kwa utulivu uliokuwapo. Binadamu kwa umbea. Hatujambo! Ila ndo hivyo umbea hajaumbiwa pweza.

Hadi mwanamke yule anahitimisha mazungumzo na Mwantumu tulishagundua kuwa hiyo simu aliyopigiwa ilikuwa ya kumtaka atume hela ya mchezo wa siku hiyo na ndo alikuwa anajaribu kujitetea ili shoga yake atazame namna ya kumstiri.

Baada ya kukata simu, safari nzima iliyobaki alikuwa akisonya kila wakati na kuonyesha amekaa kisharishari akimsubiri mtu ajichanganye apunguziwe hasira (nashukuru sikuuingia mtego huo). Aliteremka eneo liitwalo Komakoma.

Wakati akishuka ilibidi nimtazame ili kumwona vizuri kiumbe aliyeniadhibu. Alikuwa amevaa dela la mauamaua lililoonekana kubwa kuliko mwili wake. Na mwendo wake ulionyesha kama anapepesuka ingawa sikusikia harufu ya kilevi wakati akiwa garini.

Mwili wake ulikuwa umekondeana na sina shaka hata kichwani isingalikuwa wigi alilojipachika basi mifupa ya kichwa ingekuwa inaonekana. Alinikumbusha mhusika wa simulizi moja ambaye Mwandishi alipomaliza kumwelezea alihitimisha kwa kusema, "...kwa namna alivyokondeana hata ukimtupia mbwa hamtaki."
_____________________

Anyways; nina hakika mwanamke yule hakuwa na ugonjwa wa kimwili wala kuathiriwa na kilevi. Ila kilichokuwa kikimsumbua ni msongo mkali wa mawazo juu ya marejesho anayotakiwa kuyawasilisha. Na ilionyesha dhahiri hali hiyo anakabiliana nayo kwa muda mrefu sasa.

Yeye ni mmoja, ila nina hakika ni kiwakilishi cha wanawake wengi nchini hususani kutoka katika jamii za hali ya chini na kati nchini Tanzania, ambao mikopo na matawi yake vinawataabisha kila uchao.

Wakati nikiwa mdogo mtaani kwetu kuna mama aliwahi kuitoroka familia yake kwa sababu ya marejesho ya mkopo waliyokopa kwenye "microfinance" moja kama kikundi. Mzigo wake walitwishwa wenzake.

Hivi karibuni wataalamu wameeleza kuwa, "Vikoba, mikopo, upatu na kila chenye majina hayo. Ni vyanzo vikubwa vya kutetereka kwa afya ya akili ya wanawake wengi kwenye jamii zetu."

Jambo hilo naliunga mkono mia chini ya mia. Mbali na kuivuruga Afya ya Akili, huharibu mahusiano ya familia na jamii na huwa chanzo cha chuki, kudhalilishana na kadhia nyingine kedekede.

Je! Kama jamii tunafanya nini kuwasaidia wanawake katika hili? Kwa maana, kumbukumbu zangu zinanieleza kuwa; lengo la uanzishwaji wa masuala hayo lilikuwa ni kuwaibua wanawake kiuchumi lakini naona wanazidi kuzama badala ya kuibuka.

Ushauri wangu kwa wanawake ni huu:-

1. Wajitahidi kutafuta elimu ya kifedha. Uelewa mdogo unachangia pakubwa kuvurugwa kupitia mambo haya. Kuna wanawake wengi wamepiga hatua kupitia taasisi hizi kutokana na kuwa na uelewa sahihi.

2. Waache tamaa ya muda mfupi. Wasiwe na vikundi vingi wala wasikope katika taasisi mbalimbali kwa mkupuo. Wasishindane na shoga zao maana apataye janga atakula mwenyewe.

3. Wasifanye kwa siri. Kwa aliyeolewa amshirikishe mumewe. Ikiwa yupo nyumbani basi awashirikishe wazazi. Hii itampatia pa kuegemea na kukimbilia pale litakapotokea la kutokea.

4. Wawe na malengo. Waingie katika michezo ya pesa kwa ajili ya mipango ya maendeleo. Wasichukue mkopo bila kujua wataurudishaje ili tu kwenda kununua simu ya kuwarusha watu roho.

5. Wasitumie pesa yenye matumizi mengine katika ‘upatu’ wakiamini itazalisha. Baadhi ya wanafunzi wa kike wanatumia pesa wapatiwazo kwa ajili ya chakula na masuala mbalimbali ya kimasomo kucheza michezo hii. Matokeo yake wanaishia kupata lishe duni na kukosa vifaa muhimu vya kujifunzia jambo linaloathiri uelewa na ufaulu wao.

Halafu wanaume tusijione hatumo. Imeonekana baadhi ya wanawake wanaingia katika matatizo ya mikopo kutokana na sisi kukimbia majukumu ya ulezi wa familia. Embu tuone aibu! Uanamume wetu haukamiliki kwa kutelekeza familia. Hata kama hali imekuwa ngumu tusizikwepe familia zetu. Majukumu ndiyo uanamume!

Vilevile, kuna wenzetu wamepoteza wenza wao (kwa kuwapa talaka au kukimbiwa) sababu ya mambo haya. Kama wewe hayajakukuta basi wakati wako waja. Chambilecho, "Mwenzako akinyolewa zako tia maji."

Tutafakari!

Mwanagenzi.
 
Binti anayefahamika kwa jina la Johari Tarimo (32) mkazi wa kijiji cha Ndatu kata ya Poli Wilayani Arumeru, amejiua kwa kunywa sumu na kuacha ujumbe kuwa amechukua uamuzi huo kutokana madeni ya vikoba ya jumla Tsh. milioni moja laki moja.

Mume wa marehemu Paulo Bayo amesema mke wake alikuwa amekopa katika vikoba viwili ambavyo alikuwa akirejesha jumla ya Tsh. 40,000 kwa wiki, lakini baadae alikopa kwa siri katika kikoba kingine cha tatu.

Chanzo: GADI TV
 
IRINGA: Enea Mkimbo (55) Mkazi wa Kihesa Kilolo amejinyonga leo Septemba 14, 2022 chanzo kikidaiwa ni kuzidiwa na madeni ya VICOBA na usumbufu kutoka kwa Wanakikundi wenzie

Septemba 13, 2022 alifuatwa na Wanakikundi wakimshinikiza kutoa pesa

Soma - Iringa: Ajinyonga baada ya kuzidiwa na Madeni ya VICOBA

Back
Top Bottom