Ukweli na uwazi utauweka huru muungano wa Tanganyika na Zanzibar

abdulahsaf

JF-Expert Member
Aug 31, 2010
858
130
images

Mbunge wa Singida Mashariki na Mnadhimu wa kambi ya upinzani Bungeni Tundu Lissu
Wednesday, 06 June 2012 10:23

KUTOKANA na vurugu zilizotokea Zanzibar Mei 26 mwaka huu zikilihusisha kundi la Jumuiya ya Uamsho wa Mihadhara ya Kiislamu (Jumiki) inayopinga muungano, suala la muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar limeingia katika mjadala mpana huku Sheria ya mabadiliko ya Katiba ikiliweka suala hilo katika mambo matakatifu yasiyotakiwa kuondolewa kitaifa.

Wakijadili chanzo cha fujo hizo na mustakabali wa muungano katika kipindi cha Kipima Joto kinachorushwa na kituo cha Televisheni cha ITV hivi karibuni, wanasiasa na wanaharakati wa masuala ya siasa wamesisitiza haja ya wananchi kupewa nafasi ya kutosha kuujadili muungano huo.

Akifungua mjadala huo, Mbunge wa Singida Mashariki na Mnadhimu wa kambi ya upinzani Bungeni Tundu Lissu anasema vurugu hizo zimesababishwa na serikali kuwazuia watu kujadili muungano.

"Mwalimu Nyerere aliandika kitabu mwaka 1995 kinachoitwa ‘Uongozi wetu na hatima ya Tanzania', ambacho kilizungumzia sana tofauti zilizokuwa zinatokea katika muungano.
Akatahadharisha kwamba, haya matatizo yasipotafutiwa suluhisho mapema huko mbele tunakokwenda ni giza tupu, ikiwa hizi tofauti za kidini na kikabila zikiachwa ziwe kama zilivyo na akasema kwamba tutakuja kujuta, majuto ni mjukuu."anasema Lissu.

Anaongeza kuwa vurugu hizo siyo za kidini kama wanavyodhani watu wengi bali ni njia iliyotumika kufikisha ujumbe wa walalamikaji.
"Ukristo wa bara ulitokea Zanzibar. Makanisa ya kwanza Afrika Mashariki na kati yalijengwa Zanzibar karibu na soko la watumwa. Baada ya Zanzibar ndiyo yakaja, Bagamoyo na Rabai na sehemu nyingine. Si suala la kidini, ni hoja za kujishikiza tu, kuna masuala ya msingi yanayovishwa hoja za kidini."anasema Lissu.

Lissu pia anakumbushia chochoko kama hizo akisema kuwa ndiyo zilizomwondoa madarakani aliyekuwa Rais wa Zanzibar Aboud Jumbe mwaka 1984 na kushauri kuwwepo kwa mjadala kwa masuala ya msingi kama muungano.
Lissu anasema hoja ya muungano imeibuka sasa kutokana na mjadala wa Katiba uliopo jambo linaloendelea kuzua hofu kwa pande zote mbili.

"Katiba hii ya sasa hivi inasema unaweza kuvunja muungano ukipata theluthi mbili ya wabunge wa Zanzibar na theluthi mbili ya wabunge wa bara kama watakubaliana kwamba hawataki muungano. Lakini watawala wetu wanasema kuwa uwepo wa muungano siyo suala la mjadala.
Kwa nini siyo suala la mjadala, kuna kitu gani kinafichwa? Itakuwaje kama sisi wananchi wa Tanzania Bara na wananchi wa visiwani tunaomba kwamba huu muungano hauturidhishi?" anahoji na kuongeza,

"Ukishaanza kuziba watu wasijadili unafungua mlango wa watu kutumia njia nyingine. Mlango wa amani ukifungwa, mlango wa vurugu unafunguliwa."

Naye mkazi wa Zanzibar Hamad Yusuf anasema chanzo cha vurugu hizo ni baada ya wananchi kuona wanazuiwa kujadili muungano wakati wenyewe wanadhani umefika wakati wa kuvunja muungano.

"Kilichojitokeza ni suala la Rais alipotoa hadidu za rejea kwa tume ya Katiba kwamba suala kuwepo kuwepo au kutokuwepo kwa muungano, si suala litakalohojiwa kule.
Ni ukweli usiopingika kwamba suala muungano limekuwa tete kwa Zanzibar na kwa muda mrefu kumekuwa na matatizo ya muungano."anasema Yusuf.

Yusuf anasema pamoja na kuwepo kwa kamati inayojadili kero za muungano bado Wazanzibari wamegundua kwamba hakuna kitu kinachoitwa kero bali muungano wenyewe ndiyo umekuwa kero.

"Kupitia fursa hii ya Katiba tulidhani kwamba Wazanzibari wataamua muungano wanaoutaka, badala ya zamani ambapo muungano ulikuwa ni wa viongozi. Sasa huu mlango umefungwa. Paka ukishamfungia chumbani na wewe uko ndani, kupitia wewe atatafuta namna ya kutoka. Hoja za mihadhara ya Uamsho zimejikita hapo." Anasema.

Yusuf anasema kuwa mchakato wa Katiba hautaleta suluhisho la kudumu, bali matatizo zaidi na hoja ya Jumuiya ya Uamsho.
Kwa upande wake mwanasheria kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Jeremy Ntobesya anasema kundi hilo lilifanya makosa ya kisheria kwa kufanya maandamano bila kupata kibali kutoka kwa Mufti wa Zanzibar.
Anataja pia Kanuni za makosa ya jinai za Zanzibar kifungu cha 25, kinachozuia mkusanyiko bila kibali na vifungu vingine vinavyozuia uharibifu wa mali kwa kuchoma moto na kukebehi dini za watu.

Naye mwanaharakati wa siasa kutoka Zanzibar Rashid Salum Adiy anasema kwakuwa tatizo limeshatokea, kinachotakiwa ni kuangalia suluhisho.
Anaongeza kuwa vurugu hizo siyo za kukurupuka bali ni za kihistoria.

"Wazanzibari hata ukiwaona wanasema, huwa hawasemi kwa kukurupuka tu. Wazanzibari wana historia ya kupinga watawala, hasa pale tunapoona haki yetu inaporwa. Kwa hiyi tuangalie suluhisho lake." Anasema Adiy.

Kwa upande wake Suleima Juma mkazi wa Zanzibar anayeishi Dar es Salaam anatofautiana na wanaounga mkono kuvunjika kwa muungano akisema kuwa nafasi imeshatolewa kwenye Sheria ya Katiba ya kuboresha muungano.

"Suala la kudai kura ya maoni katika muungano nadhani hili ndiyo suala lililotufikisha hapa. Kama ni suala la muungano mchakato wa Katiba utatoa fursa ujadiliwe." Anasema Juma.
Hata hivyo Lissu anamkosoa akisema kuwa sheria hiyo imetoa mwanya wa kuboresha tu na siyo kuamua vinginevyo.

"Nilisema mwanzoni kwamba, vitu vinavyotakiwa kujadiliwa vikizimwa, unakaribisha majanga kama haya tunayoyaona. Wala siyo Tanzania tu, wala Zanzibar, ukienda Misri, Ukristo umekuwepo zaidi ya miaka 4000 baada ya Yesu Kristo, uislamu umekuja baadaye kabisa. Leo asilimia 90 ni waislamu na asilimia 10 tu ni wakristo. Lakini leo makanisa yanachomwa moto." anasema Lissu.

Nini kifanyike?
Akitoa suluhisho la kumaliza mivutano hiyo, Hamad Yusuf anashauri kuwepo kwa mijadala ya muungano na mustakabali wake,
"Tuyaache mambo haya wazi, Wazanzibari , Watanganyika wajadili kwa upana kwa sababu hili si suala la viongozi wachache. Rais kama hataki suala la muungano hayo ni maoni yake lakini isiwe kauli yake, iwe ni kauli yake kama Jakaya Kikwete. Watanzania wana akili na mawazo waachwe waamue."anasema Yusuf.

Lakini Ntobesya anasema kwa sababu milango ya Tume ya Katiba iko wazi kwa watu wanaotoa elimu ya Katiba, Watu waelimishwe, sababu za kuingia kwenye muungano, faida za muungano nini au Wazanzibari wanaotaka muungano uvunjike wana sababu zipi.
Anaongeza kwamba, kuuvunja muungano siyo suluhisho la matatizo, bali kinachotakiwa ni kuuboresha tu.

"Huu muungano ni wetu sote, siyo mali ya viongozi, tuangalie huyu anasema vipi halafu tupime pande zote. Kama tumeambiwa tusiuvunje tuuboreshe, mimi naamini kabisa tunaweza kuuboresha. Tukiuvunja tutapata hasara kubwa."

Naye Suleiman Juma anamuunga mkono Ntobesya akipinga wanaosema kuwa fursa ya kujadili muungano imefungwa.

"Unaposema milango imefungwa katika kuzungumzia suala la muungano, mimi nashindwa kuelewa. Fursa za watu kujadili muungano zimetolewa kwa kadiri watu wanavyotaka uwe. Imezuiwa kujadili kuvunja muungano, haijazuiliwa kujadili namna ya kuboresha muungano."

Juma anawatupia lawama wanasiasa akisema wanatumia mwanya huo kujitafutia madaraka.

"La ajabu wanasema muungano una kasoro, badala watumie fursa hii kujadili wanapinga. Fursa iliyotolewa watu waitumie. Kama hawataki basi watumie majukwaa yao kukataa, kwa sababu kuna nafasi imetolewa kwa wanaotaka serikali tatu. Vyama vyote vya siasa vinakubali kuwepo kwa muungano, lakini wanatumia majukwaa kusema kuwa kuna watu hawataki muungano kwa nia wanazozijua wao" anasema Juma.

Kwa upande wake Lissu anahoji akisema kama sheria ya Katiba inasema mjadala wa muungano uwe ni namna ya kuuboresha zaidi. Je, wale ambao hawautaki wao wakazungumzie wapi?

"Mtu akisema anataka Jamhuri ya Zanzibar irudi kama ilivyokuwa April 25, huyo haruhusiwi. Anasema anataka Jamhuri ya Tanganyika huyo haruhusiwi kwa sababu atakuwa anavunja muungano. Sasa watu wenye mawazo kama hayo wao wakasemee wapi? Na mtu anayesema mambo ya namna hii msiyazungumze hiyo haki anaipata wapi?"

Kwa upande wake Rashid Salum Adiy anasema kinachosababisha yote hayo ni viongozi kuficha ukweli wa mambo, hivyo anashauri viongozi kuwa wazi ili kuwaondoa watu kwenye hasira.

"Jambo lolote unapotaka kulitatua, kwanza unatumia akili, kwa sababu Mungu ametupa mambo matano, kwanza ukweli, pili subira, tatu tafakari nne akili na tano ni elimu."anasema na kuongeza,

"Jambo lolote mnapotaka kuliondoa lazima mseme ukweli tu. Hawa wenzetu siyo wakweli. Ukweli ni kwamba hakuna muungano kuna fikra ya muungano na viongozi wote walishindwa kuisimamia ikasimama, kwa sababu kinachofanya muungano ni sheria siyo siasa.
Ukiangalia kwenye mfumo wa sheria, hakuna muungano. Wanata kuleta Katiba wakati hata huo muungano haupo," anasema Rashid Salum Adiy.

Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom