Ufisadi ushuru wa forodha siri nzito

Questt

JF-Expert Member
Oct 8, 2009
3,010
422
Wahusika watajwa, ni Waarabu
Waporomosha maghorofa Kariakoo
Washirikiana na vigogo, maofisa wa TRA
TAARIFA zimekuwa zikimiminika chumba cha habari cha Raia Mwema kuelezea zaidi mtandao wa wizi wa mapato yatokanayo na ushuru katika bandari ya Dar es Salaam ya kuwa ni mpana zaidi na unawahusisha wafanyabiashara wakubwa na wanasiasa vigogo.

Taarifa hizo ni za maelezo ya ziada juu ya habari kuu ya gazeti hili ya wiki iliyopita iliyoandikwa chini ya kichwa: Ripoti Maalumu; Ufisadi wa kutisha Ushuru wa Forodha.

Familia ya wafanyabiashara vijana wenye asili ya Kiarabu, imeelezwa kujilimbikizia mali kwa ufisadi huo katika ukwepaji kodi na sasa wamekuwa wakijenga majumba makubwa katika maeneo ya Kariakoo na pembezoni mwa Dar es Salaam.

Wakiongozwa na kaka yao, vijana hao wa Kiarabu wapatao watatu kwa sasa wanaelezwa kuingiza faida ya zaidi ya Shilingi bilioni tatu kwa wiki.

Katika baadhi ya taarifa hizo, Raia Mwema limetajiwa wafanyabiashara na wanasiasa wakubwa, wa zamani na wa sasa, ambao ni washiriki katika mtandao huo lakini kwa sababu za wazi, na hasa kwa kuwa hawakuweza kupatikana, majina yao hayatatajwa kwa sasa.

“ Tunasubiri kuona kama mtaandika tena. Msije nanyi mkapewa (Sh.) milioni 50 au 100 mkaacha. Wizi huu una mtandao mpana na unahusisha wafanyabiashara wakubwa na vigogo. Mnaweza nanyi mkapewa fedha mkanyamaza, au wakakunyamazisheni kwa mbinu nyingine, ” alisema msomaji mmoja katika ujumbe wake kwa Raia Mwema wiki iliyopita akijitaja kuwa ni mfanyabiashara wa Dar es Salaam aliyekerwa na kuathiriwa na mtandao huo.

Alisema mwingine: “ Kama ni kuchangia Chama cha Mapinduzi (CCM) sisi tumekuwa tukichanga hata katika wakati ambao hawa (anataja jina la kampuni) hawakuwapo na chama hakikuwa na wachangiaji wengi.

“Nakuambieni mlichoandika ni jambo linalofahamika wazi pale TRA (Mamlaka ya Mapato). Ni kilio cha wateja na wafanyabiashara wote wanaohusika na uingizaji na utoaji mizigo bandarini. Hata huyo Kamishina Kitilya (Harry Kitilya, Kamishina Mkuu wa TRA) anajua kinachoendelea, katika majibu kwenu amejibaraguza tu.

“Nina ndugu yangu amekuwa akisumbuliwa kwa miezi sasa ili kutoa mizigo yake, mara barua, mara bima, mara sijui nukta gani kwenye barua, basi ili mradi asumbuke mpaka apitie kampuni yao.”

Kwa mujibu wa mfanyabiashara huyo, baadhi ya wafanyabiashara waliokwisha kukerwa na usumbufu huo bandarini Dar es Salaam na katika ofisi za TRA na Tiscan, wamekuwa wakipitisha mizigo yao katika bandari za Beira, Msumbiji na Mombasa, Kenya.

“Sasa tazama, Serikali kila mara inalia kwamba mapato hayatoshi, lakini hayatoshi vipi wakati inaruhusu wizi katika moja ya vyanzo vikubwa na muhimu vya mapato? Fikiria hawa wanaokwenda kupitisha mizigo Beira na Mombasa ni Watanzania, tena wengi wao wakazi wa Dar es Salaam. Wanakubali kuingia shida ya kwenda mbali lakini wafanye kazi nzuri ambayo sasa inaingiza mapato Kenya na Msumbiji,” anasema mfanyabishara huyo kwa masharti kwamba jina lake lisitajwe.

“Kwenu waandishi wa Raia Mwema, kwanza sina budi kuwapongeza kwa kazi nzuri mnayofanya kwa kutupatia habari za uhakika na bila kuonea mtu. Leo (wiki iliyopita) najitokeza kuliunga mkono gazeti lenu katika jitihada za kufichua ufisadi ambao kila kukicha Serikali imekuwa inaupigia kelele,” ndivyo alivyoanza msomaji mwingine ambaye kwa sababu za wazi naye hatutamtaja jina.

Aliongeza: “Habari yenu ya ukurasa wa mbele toleo namba 136 ni ya kweli. Vijana hawa wako watatu (anataja majina) wana asili ya Saudia japo ni Watanzania.

“Ni kweli walianzia uwakala Tanga na Holili. Walihama baada ya ofisa mmoja wa forodha, namkumbuka kwa jina la Banny, aliyehamishiwa huko, kuwabana sana.

“Wanashirikiana na viongozi wa juu wa TRA na wamejenga mtandao kuanzia bandarini, na ICD zote. Wanafanya wanavyotaka saa yoyote na wakati wowote kama vile hakuna Serikali. Ofisa yeyote atakayebisha kufanya wanavyotaka huhamishwa kituo mara moja.

“Wamesababisha maofisa kadhaa kufukuzwa kazi. Nawakumbuka baadhi ya maofisa waliofukuzwa kazi pale Longroom; DICD na Container Terminal na wengine wamehamishwa vituo.

“Kwa kawaida kampuni zote hufuata taratibu za kiforodha lakini kampuni zao hupita njia za mkato kwa kuandika barua ya kuomba provisional clearance na nyingi za barua hizo zinalenga kukwepa kodi.

“Hizo barua za provisional clearance mara nyingi huandikwa Longroom kwa maelekezo ya vigogo wa TRA na zinakuwa zinaruhusiwa kutoa mizigo bila ukomo wa idadi na muda kwa bidhaa ambazo hazina sifa za kupewa provision.

“Bidhaa zenye sifa ni kama malighafi za viwandani,vyakula na bidhaa za Serikali na za balozi. Si nguo, vitenge, kanga, saruji na nondo kama inavyofanywa sasa. Tafadhali pokeeni nakala za baadhi ya barua za aina hii za karibuni zaidi kwa uthibitisho wa mambo yanavyofanywa na wakubwa TRA kwa kushirikiana na mtandao huu.”

Taarifa zilizotufikia wakati tukienda mitamboni jana Jumanne, zilisema kwamba ukaguzi mkali wa ndani umekuwa ukifanyika TRA kutaka kubaini nini ambacho kimekuwa kikendelea kuhusiana na ukwepaji ushuru.

Wiki iliyopita, gazeti hili likikariri malalamiko miongoni mwa wafanyabiashara na wateja wapitishao mizigo yao katika bandari ya Dar es Salaam lileleza ya kuwa wakati Bajeti ya Serikali inasuasua kutokana na uhaba wa fedha za ndani, familia moja ya Dar es Salaam inayomiliki kampuni inayojihusisha na bishara ya bidhaa za nyumbani imejiingiza katika uwakala wa forodha kwa staili ya aina yake ikiwa ni pamoja na kujikita katika kuwasaidia wengine kukwepa kodi katika mtandao unaohusisha wanasiasa.

Biashara hiyo ya aina yake ya uwakala wa ukwepaji kodi, imedaiwa imekuwa inaipotezea Serikali mabilioni ya shilingi ambazo zilistahili kukusanywa kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali wanaoingiza bidhaa mbalimbali kutoka China na Dubai.

“Sasa ni vigumu sana, na kwa kweli hakuna wakala mwigine anayethubutu kutoa bandarini bidhaa za nguo kwa kuwa nyaraka za kampuni nyingine zifikapo Tiscan au Longroom huwekewa bei za juu ambazo hazilipiki ili kuwakatisha tamaa waagizaji ambao kwa sasa wamechoshwa na huduma za vijana hawa zilizojaa kiburi na dharau.

“Hali hiyo imewafanya waagizaji kukosa pa kwenda bali kwa vijana hao na wakabaki wakisikitika jinsi vyombo vya dola vinavyowekwa mfukoni kwa hasara ya jumla ya Taifa. Waagizaji wanalalamika kwamba hawana tena uhuru kwa kuwa wanalazimika kutumia kampuni moja tu ambayo bei zake hazina majadiliano. Ukienda kubembeleza unaambiwa katafute wakala mwingine ambaye hata hivyo huwezi kumpata kwa kuwa hawa wamehodhi kila kitu,” alieeleza mtoa habari Raia Mwema aliyeko ndani ya sekta ya kodi.

Mfanyabiashara mwingine alisema kwa hali halisi iliyopo kwenye mfumo wa ukusanyaji kodi, ni vugumu kukwepa ushuru kwa kudanganya kiasi (idadi) cha mali kilichomo kwenye kontena (false declaration) au kuweka bei ndogo au ya chini ya ile bei halisi (under invoicing), lakini kwa kampuni hii hilo linawezekana kwa kuwa mfumo mzima tangu serikalini, Tiscan na TRA umekuwa nyuma yao kutokana na nguvu kubwa ya kifedha waliyonayo.

Imeelezwa kwmaba kwenye kampeni za mwaka 2005 kampuni hiyo ilichangia chama tawala Sh. Milioni 200 na kwamba katika mwaka huu wameahidi kuchangia milioni 500.

Ili kufahamu kiasi cha mapato ya Serikali yanayopotea angalia hesabu hizi:

Kontena la nguo za kawaida lenye urefu wa futi 20 laweza kuwa na thamani ya Dola za Marekani 60,000.00 hadi Dola za Marekani 80,000.00 kutegemeana na aina, ubora na idadi ya nguo zenyewe. Ushuru wa jumla ni 48% ya thamani halisi (cif value). Kwa hiyo kama thamani ni Dola za Marekani 60,000.00 x 48% = Dola za Marekani 28,000. Kwa thamani ya Dola 1 ya Marekani = Sh.1400, ushuru kwa kontena hili katika shilingi ni 40,320,000.

Kama kontena ni la thamani ya Dola za Marekani 80,000, ushuru ni 80,000.00 x 48% ambazo ni sawa na Dola za Marekani 38,000.00 na kwa Sh ni 53,760,000.

Kwa mujibu wa habari za ndani ya TRA, kampuni hii hukadiria gharama zote kwa meta za ujazo kutoka China hadi Dar es Salaam, na hivyo kontena la futi 20 ambalo lina meta za ujazo 36, ina maana gharama zote zitakuwa ni Dola za Marekani 450 x 36 = Dola za Marekani 16,200 ambazo ni sawa na Sh. milioni 22.68.

Ikiwa utaondoa gharama halisi za kusafirisha kontena hadi Dar es Salaam ambazo ni Dola za Marekani 2,500, basi kinachobaki ni Dola za Marekani 16,200 – 2500 = Dola za Marekani 13,700.00 au Sh. 19,180,000.

Uchunguzi wa Raia Mwema umeonyesha kwamba sehemu kubwa ya fedha hutumika katika kulipia ushuru kidogo, rushwa kwa maofisa sehemu mbalimbali husika, gharama za bandari na usafiri wa bandarini kwenda kwenye maghala yao.

“Kwa uzoefu wangu kampuni hii kwa kontena la nguo la futi 20 hawalipi zaidi ya Sh. milioni 10. Hii ina maana ya kuwa badala ya kulipia gharama halisi ya zaidi ya Sh. milioni 40 wao wanalipa milioni 10 tu. Kwa hiyo, kwa mfano mmoja tu, Serikali hupoteza Sh. milioni 30 kwa kila kontena la nguo la futi 20 linalotoka bandarini. Ikiwa makontena 100 yanaweza kutoka bandarini kwa wiki moja, ina maana Serikali hupoteza milioni 30 x 100 = bilioni 3 kwa wiki. Kwa mwaka mmoja hii ni sawa na shilingi bilioni 156,” alieleza mtaalamu wa kodi ambaye kwa sasa ni mstaafu.
 
Back
Top Bottom