Mwafrika wa Kike
JF-Expert Member
- Jul 5, 2007
- 5,185
- 56
Ufisadi ukishangaa la Richmond la IPTL je?
Joseph Mihangwa Machi 12, 2008
Raia Mwema
Katika sehemu kwanza ya makala yetu katika gazeti hili toleo namba 16 la Februari 27-5 Machi 2008, tulieleza jinsi mkataba mbovu wa miaka 20 wa kuuziana umeme kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kampuni ya kimataifa ya kuzalisha umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ulivyofikiwa kwa hasara ya taifa
Tulieleza kwamba wakati mkataba huo ukipigiwa upatu kwa nguvu zote na baadhi ya vigogo serikalini, tayari Benki ya Dunia ilikuwa imejitolea kusaidia kununua mitambo miwili ya megawati 75 kila mmoja ili kuokoa hali ya umeme nchini na kufanya mkataba wa TANESCO /IPTL usihitajike.
Lakini vigogo wa serikali waliziba masikio na kuendelea na IPTL. Wakati huo TANESCO ilikuwa ikiwadai wateja wake deni la dola 55m pamoja na serikali ya Zanzibar.
Isitoshe kabla ya mradi wa IPTL, Benki hiyo ilijitolea kufadhili kupitia serikali ya Canada mradi wa gesi wa SONGAS ambao ulikuwa nafuu zaidi na tayari Canada ilikuwa imelipa dola milioni 200 za Marekani lakini bado serikali ilifumba macho na kuendelea na IPTL.
Tuliona pia jinsi gharama za ujenzi zilizokadiriwa kufikia dola za Marekani milioni 126.39 zilivyoongezwa kinyemela kwa zaidi ya asilimia 33, na jinsi mitambo iliyokusudiwa (SSD) yenye thamani ya dola milioni 163.5 iliyobadilishwa na kusimikwa mitambo hafifu (MSD) kwa bei hiyo hiyo ambapo bei halisi ilitakiwa kuwa dola miloni 85.7 ingawa mtambo kama huo (aina ya wartsila ) uliuzwa kwa dola million 60 kwa nchi nyingine za kiafrika ikiwamo Kenya.
Haifahamiki kwa nini mradi wa IPTL ulitetewa kwa nguvu zote na vigogo katika kipindi ambacho tatizo la umeme lilikuwa la muda mfupi tu na hata baada ya kumalizika ikiwa ni pamoja ka ukweli kwamba tayari kulikuwa na mradi rahisi mbadala kama vile mradi wa SONGAS na kusimikwa kwa mitambo wa megawati 75 Ubungo, Dar es Salaam (1995) na ule wa kihansi wa megawati 180.
Inadhaniwa kuwa kama isingekuwa hila za viongozi dhidi ya mradi wa Songas na kuipendelea IPTL Tanzania ingeanza kutumia umeme wa gesi tangu mwaka 1997.
Mradi wa IPTL ambao ulionekana dhahiri kugubikwa na ufisadi kwa ngazi na kwa kiwango chote, uliendelea licha ya serikali kutahadharishwa na washauri wa TANESCO, Kampuni ya Acrea (Canada) na Kampuni ya Bunton and Williams (U.K) kwamba ulikuwa haufai ulikuwa wa kipindi kirefu (miaka 20) kwa tatizo la muda mfupi gharama kubwa (asilimia 130 zaidi ya gharama za kawaida bila sababu ulizidi mahitaji ya umeme hivyo kwa lengo la kuinufaisha IPTL.
Jumuiya ya kimataifa yenye mapenzi sana kwa Tanzania pamoja na kutahadharisha kushauri na kusikitika kuhoji uhalali na mantiki juu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Waziri wa Madini na Nishati kutia saini mkataba huo (badala ya watendaji wanaostahili) licha ya mradi huo kuelezwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFM) na Benki ya Dunia (WB) kuwa nimzigo usio wa lazima kwa uchumi wa taifa na kwa walipa kodi wa nchi hii.
Ofisi ya Mwanaheria Mkuu, ndiyo iyoupitia mkataba wa IPTL/TANESCO sambamba na ushauri wa Acrea na Bundon Williams ambapo mmoja wa wanasheria wa Serikali (Mary Mdosi) aliandika maoni yake kwa ufupi ushauri wao (Acress/Bundon) uchukuliwe tu kama sehemu ya usshauri wetu juu ya mkataba huu kwa kiwango ambacho hakipingani na kilichoandikwa humu.
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Waziri wa Nishati na Madini (William Shija na baadaye Dk Abdallah Kigoda (Feb 1977) na Edgar Maokola Majogo (2000) na Waziri wa Fedha (Daniel Yona) walisimama kidete kuhakikisha mkataba wa IPTL unapita na ilipendekezwa wakati mmoja kwamba Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Patrick Rutanzibwa ambaye aliapa kutokukubaliana na IPTL na kumjulisha Rais Benjamini Mkapa uchafundani ya mkataba huo afukuzwe kazi.
Nayo Taasisi ya Kuzuia Rushwa (PCB wakati) huo ilifuatilia kwa karibu mwenendo wa sakata hili na ilifikia mahali Mkurugenzi wa Oporesheni wa taasisi hiyo, Edward Hosea achukue hatua za kuwakamata baadhi ya wahusika lakini inasemekana alirudishwa nyuma kufanya hivyo na nguvu zilizokuwa juu yake.
Kuna wakati pia Rais Benjamini Mkapa alipoingia madarakani alitamka kuwa asingependa kuona mkataba huo wenye kuwaumiza wananchi na taifa kwa ujumla lakini haifahamiki kwa nini aliunyamazia ukaendelea.
Inasemekana baada ya kubaini kwamba serikali ilikuwa imejinyonga kwa mkataba huo, aliamua kunyamaza na nyundo ya mwisho iliyomnyamazisha ilikuwa 1998 alipolalamikiwa na Waziri Mkuu wa Malaysia, Mohamed Mahathir juu ya yeye kutaka kuingilia mkataba huo walipokutana kwenye kikao cha wakuu wa nchi na Jumuiya ya Madola mjini Edinburgh kwa misingi kwamba Malaysia na Tanzania zilikuwa nchi mbili zilizounganishwa na kushabihiana ndani ya ushirikiano wa nchi za dunia ya tatu (south-south Commission) ambapo Mahadhir alitia msukumo mkubwa kwa wawekezaji wa kimalaysia kuwekeza barani Afrika.
Kuna taarifa pia kuwa nchi hiyo ilifadhili kwa kiwango kikubwa kampeni za chama cha African National Congress (ANC) cha Afrika kusini katika uchaguzi wa 1994.
Huku ikionekana dhahiri kwamba mkataba huo ulijaa mizengwe kwa hasara ya taifa huku jumuiya ya kimataifa ikitishia kusitisha misaada kwa Tanzania, Rais Mkapa alibaki njia panda, kisha akaelekeza mgogoro huo uwasilishwe kwenye Baraza la Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) mjini London hasa baada ya Katibu Mkuu, Rutabanzibwa kushikilia kwamba mkataba huo ufutwe (the African, Novemba 27, 1998).
Ni katika baraza hilo baadhi ya mambo yenye kuashiria ufisadi ndani ya mkataba wa IPTL yalipobainika kama vile kwamba baada ya mvua za El-nino, Desemba 1997 hapakuwa na sababu tena za mkataba wa miaka 20 na IPTL. Maelezo haya ni kwa mujibu wa shahidi James Rugemelila wa VIPEN/IPTL ya Mei 8, 2000.
Ilidhihirika pia kuwa nyumba 37 zilizopangwa kujengwa zilipunguzwa kufikia 10, lakini zilizojengwa ni sita kwa gharama zilezile za mkataba ambazo nazo hata hivyo ziliongezwa kwa asilimia 130 (ICSID 2000-uk 41).
Vivyo hivyo ilielezwa kuwa mitambo iliyokusudiwa haikuwekwa badala yake ililetwa mitambo hafifu kwa bei kubwa zaidi (ICSID 200 uk 41-2).
Maelezo kwa njia ya kiapo ya mmoja wa watendaji wakuu wa wizara (Aprili 19, 2000, uk 3) yanaonyesha kuwa alipelekewa dola milioni 200,000 kuunga mkono mpango wa IPTL akazikataa lakini siku ya krismasi, 1994 alikuta nyumbani bahasha yenye 5000,000/- lakini akamrudishia mletaji.
Mwingine naye alieleza kuwa aliahidiwa kupitia mmoja wa watumishi wa ofisi ya mwanasheria mkuu kwamba kama angewasaidia kusukuma mkataba wa IPTL ukapita ungelipwa Sh milioni 100.
Mwingine aliieleza PCB kwamba aliahidiwa dola 20,000 (Tshs 20m/= akazikataa lakini alikiri kuwa baadaye alikubali na kupokea Sh 100,000/= tu kama chai ambayo gharama haiwezi kuchukuliwa kama rushwa.
Hawa walikuwa maofisa wa ngazi za chini tu. Vigogo walipata kiasi gani inahitajila uchunguzi wa kina kama ule wa Richmond.
Baraza lilikataa madai ya TANESCO kuhusu kuwapo kwa rushwa kutokana na ushahidi mdogo uliowasilishwa na ambao hata hivyo uliwasilishwa kwa kuchelewa.
Kulikuwa na taarifa kuonyesha kwamba PCB na Idara ya Upelelezi ya Makosa ya Jinai (OCD) zilikusanya ushahidi mwingi muhimu kuthibitisha vitendo vya rushwa lakini haukuwasilishwa baada ya serikali kukataa kwa hofu ya aibu ya kuitwa taifa la wala rushwa wala hapakuwa na ufuatiliaji tena.
Kwa sababu hii TANESCO ilishindwa kesi katika Baraza la Usuluhishi na Serikali ilitumia Sh milioni 7 katika kesi hiyo.
Wananchi na vyombo vya habari hazikukaa kimya juu ya ufisadi huu, lakini kwa sababu ya uhuru duni na kupuuzwa kwa vyombo hivyo hakuna lililofanyika kurekebisha hali.
Brigedia Jenerali (mstaafu), Joachim Buchard Ngonyani alinukuliwa akisema, IPTL ni kaburi la Watanzania tunataka wote walioidhinisha washughulikiwe (the African, Agosti 3,1996). Hakusikilizwa.
Mbunge wa Dodoma mjini (wakati huo), Hashim Saggaf alishangaa kutohojiwa wote wanaohusika na mkataba huo waeleze kwa nini wametufikisha hapo (the East African Aprili 26, 1999), hakuna aliyemsikiliza.
Chini ya mkataba wa IPTL TANESCO itailipa IPTL dola 3.6m kama ada ya huduma ya mtambo (capacity charge) kama imezalisha au haijazalisha umeme na TANESCO imetumia umeme au haikutumia.
Juu ya ada hiyo TANESCO imetozwa dola tano za kimarekani kwa kila yuniti ya umeme kwa kuendesha mtambo nusu ya uwezo wake (inalipa dola milioni moja) kwa mwezi na kufanya malipo ya TANESCO kwa IPTL kuwa dola billion 4.5 kwa mwezi.
Gharama hizi za TANESCO ni mbali na zile za mradi wa umeme wa gesi wa SONGAS, Richmond (inayolipwa 12m kwa siku na ule wa Kiwira ambao kuanzia mwakani, TANESCO itatakiwa kuilipa kampuni ya utunzaji umeme ya Tanpower Resourses LTD inayodhaniwa kumilikiwa na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamini Mkapa) Sh milioni 300 kwa siku na kufanya Tanzania kuwa na umeme ghali zaidi barani Afrika na kwa nchi zote za dunia ya tatu hali ambayo haiwezi kuvutia wawekezaji licha ya kuumiza wananchi.
Baada ya kufanikiwa kulindwa na kufumbiwa macho kwa ufisadi ndani ya mkataba wa IPTL mafisadi wameona mahali pa kuchuma bila jasho ni sekta ya umeme nchini.
Tumeyaona ya Richmond na mwakani yatafuatiwa na ya Tanpower Resources wakati IPTL wakiendelea kula. Ni kiasi gani hicho (kwa sana ) wanachoendelea kupora?
Hasara kutokana na mkataba wa IPTL kwa uchumi wetu ni kubwa mno. Kama tusingejiingiza katika mkataba huo wa kimagendo tungekuwa tayari tumeanza kutumia utajiri wetu wa umeme na kuokoa fedha za uagizwaji wa mafuta kwa ajili ya mitambo ya pale ubungo hasara kutokana na tatizo la umeme la 1997 lingeepukika kama mradi wa SONGAS ungetekelezwa badala ya kukimbilia IPTL.
Vivyo hivyo gharama kutokana na wawekezaji binafsi kwa kuleta jenereta za umeme wa dharura zingeepukika pamoja na shiringi billion saba zilizotumika kuhusiana na kasi ya TANESCO mjini London.
Tukishangaa la Richmond na la BOT (EPA) na hili la IPTL je? Uchumi wa nchi na maendeleo ya kijamii hawezi kupatikana kama tutaendelea kuongozwa na kikundi kidogo cha wasomi walafi, waliotekwa nyara na ubepari na mitaji ya kimataifa wenye ujasiri wa kifisadi, wasiotaka kukosolewa na kujirudi na kuwajibika kwa umma.
Ni kitu kimoja kwa wanasiasa na watendaji kunufaika kidogo kutokana na miradi ya uwekezaji inayorudisha ajira, bidhaa muhimu na kuchangia katika pato la serikali lakini ni kitu kingine tena kibaya na cha kiuaji kwa kikundi hicho kujishibisha kwa rushwa kutokana na miradi inayovunja sera kuu za kitaifa na kuwabebesha mzigo mkubwa wa ziada walaji walipa kodi wa nchi hii. Hawa ni wasaliti wa taifa.
Kwa kuendeleza uswahiba wa kuikumbatia IPTL na sasa Richmond, Tanzania imerudi nyuma miaka 30 ya Maendeleo wakati nchi nyingine zikikimbia na sisi tukitembea. Viongozi hawa wasio na soni wanataka kuacha majina gani? Wanataka makaburi yao kupondwa mawe na vizazi vijavyo?
Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela alitahadharisha Bunge hivi karibuni kwamba kiongozi bora na mwema ni yule anayesaka kutafuta jina zuri akiondoka.
Na vivyo hivyo mshairi Shaaban Robert ndivyo anavyosema katika shairi lake huru jina anaposema:
Mtu wa fikra njema, kwa watu huacha jina,
Na watu wajao nyuma, wakapenda kuliona,
Katika dunia nzima, likawa kubwa heshima
Na akili si kusema, lakini ni kufikiri,
Kwa kujua jambo jema, lisilokuwa na shari
Mvuka nguo chutama, endapo wajiadhari,
Na busara kutenda tendo, ambalo ni jema
Viumbe wakalipenda, ukapata na heshima
Maisha daima yenda, utaacha nini nyuma?
Basi tunasema ole kwa wasaliti hawa hali ni jambo la hatari, mwenye kiburi bila utulivu wa moyo; ndiye mchoyo kama kuzimu anayeshibishwa kama kifo. Ndiye hukusanya (vya watu) mataifa kwa maslahi yake mwenyewe.
Je hawatamdhihaki kwa nyimbo na kumsimanga wakisema; ole wake huyo anayejilimbikizia mali isiyo yake (ataachwa kupora vya masikini ) mpaka lini?
Nakuambia hili ndilo Kikwete hawezi kugusa kabisa maana yeye kwake kila kitu amekikuta!