Uenyekiti wa Sitta kituko kingine Bunge la Katiba

Kakke

JF-Expert Member
Dec 4, 2010
1,883
1,482
mbwambo.jpg
Johnson Mbwambo


Muhariri wetu Johnson Mbwambo raia mwema


Ilistahili ajiuzulu uwaziri baada ya kuchaguliwa


WIKI iliyopita niliandika kuhusu muundo na mwenendo wa Bunge letu la Katiba, linaloendelea na kikao chake mjini Dodoma, ulivyo na ukakasi hata kwa sisi kina yakhe ambao si wabobezi katika elimu ya mabunge ya Katiba.
Ukakasi wa karibuni kabisa ni wa juzi ambapo Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alishindwa kuwasilisha rasimu ya Katiba hiyo kutokana na wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupinga.

Hoja ya Ukawa ilikuwa kwamba kanuni inadai Rais alifungue kwanza rasmi bunge hilo ndipo rasimu iwasilishwe.

Ilikuwa ni udhallidshaji wa aina fulani kwa Jaji Warioba ambaye alisimama kwenye mimbari, bungeni, tayari kuwasilisha rasimu hiyo lakini akashindwa kufanya hivyo kutokana na kelele na ghasia nyingi kutoka kwa wajumbe hao wa Ukawa ndani ya Bunge.

Kituko hicho na udhalilishaji huo kwa Jaji Warioba ungeweza kuepukwa kama Mwenyekiti wa Bunge hilo la Katiba, Samuel Sitta, angekuwa makini na kuheshimu kanuni zilizopitishwa na bunge hilo. Kutokana na ghasia hizo, alilazimika kuliahirisha Bunge.


Lakini hicho ni kituko kimoja tu kati ya vingi vya Bunge hilo ambavyo tumevishuhudia mpaka sasa. Kwa hakika, vijukuu na vitukuu vyetu, na hasa wachambuzi wa historia ya taifa letu wa karne ijayo, watatushangaa tulikuwa tunafikiria nini kufanya tuliyofanya katika mchakato wa kuipatia nchi yetu Katiba mpya.


Watakuja kujiuliza, kwa mfano, ilikuaje nchi yenye watu milioni 44 bunge lake la Katiba lisheheni wajumbe kutoka chama tawala CCM ambacho wanachama wake nchi nzima hawafikii hata milioni 4!
Hakika, watakuja kujiuliza iwapo jambo hilo lilikuwa, nyakati hizo, ni kawaida (ni sawa) au ilikuwa ni bahati mbaya tu au ulikuwa ni ‘usanii uliochongwa’ na ‘kuchongeka ’ wa waliokuwa wamekamata dola nyakati hizo.


Watakuwa na mengi ya kujiuliza kuhusu vituko vya Bunge hili la Katiba. Watashangaa, kwa mfano, ilikuaje bingwa wa propaganda wa chama tawala (CCM) wa zama hizo, na ambaye alishika nyadhifa nyingi serikalini, ukiwemo ukuu wa mkoa na uwaziri, Kingunge Ngombale Mwiru, ateuliwe kuingia katika Bunge hilo la Katiba akiwakilisha waganga wa kienyeji!


Katika hilo, watahoji kama kweli zama hizo waganga wa kienyeji walikuwa ni wengi katika Tanzania kiasi cha kupatiwa nafasi hiyo ya uwakilishi katika Bunge la Katiba.
Watataka kujua kama kweli waganga wa kienyeji zama hizo walikuwa ni wengi nchini kuliko makundi mengine makubwa kama vile wachimba madini, wahandisi, madaktari au hata waendesha teksi au wanasoka nk kiasi cha wao kustahili upendeleo huo wa aina yake wa kuingizwa katika Bunge la Katiba!


Aidha, wachambuzi na wadadisi hao wa karne ijayo watakuja kujiuliza na kukosa majibu ya kuridhisha juu ya mazingira yaliyokuwepo yaliyosababisha ulazima wa Mwenyekiti wa chama cha siasa cha NLD, msomi, Dk. Emmanuel Makaidi, amteue mkewe, na wote wawili kuingia katika Bunge hilo la Katiba.


Zaidi, watamshangaa Rais wa zama hizo, Jakaya Kikwete, aliyeubariki uteuzi huo wa ‘mtu na mkewe’ kuingia katika Bunge hilo la Katiba. Watahoji na kujiuliza mantiki ya chama kidogo kama NLD kuingiza wajumbe wawili (mtu na mkewe) katika Bunge hilo la Katiba; ilhali makundi mengine makubwa nchini yalikosa uwakilishi katika bunge hilo.


Lakini si hayo tu ambayo vijukuu na vitukuu vyetu vitakuja kuyahoji karne ijayo na kukosa majibu kuhusu ukakasi wa Bunge letu hili la Katiba. Nina hakika watakuja kuhoji pia mantiki ya Jukwaa la Katiba Tanzania kunyimwa uwakilishi katika Bunge hilo la Katiba.


Hawataacha kuhoji hivyo, kwa sababu kumbukumbu watakazozikuta zitaonyesha kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na Jukwaa la Katiba Tanzania kuwaelemisha wananchi, kwa muda mrefu, masuala mbalimbali yanayostahili kuwemo katika Katiba kabla hata bunge hilo la Katiba halijaanza.


Kumbukumbu sitawaonyesha kwamba kama kuna asasi za kiraia zilizotumia muda na fedha zake nyingi kuandaa mijadala, semina, mikutano na hata kutoa machapisho ya kuwaelemisha wananchi kuelewa jinsi mustakabali wao wa maisha unavyotegemea uwepo wa Katiba nzuri, nambari wani itakuwa ni asasi hiyo ya Jukwaa la Katiba Tanzania.


Watajiuliza: Kama Jukwaa la Katiba Tanzania ndiyo asasi nambari moja ya kiraia iliyofanya kazi hiyo kwa mafanikio makubwa hata kabla rasimu yenyewe ya Katiba mpya haijatengenezwa, iweje leo isiwakilishwe kwenye Bunge la Katiba?

Je, wachambuzi na wanahistoria hao wa karne ijayo wataamini kweli kwamba waganga wa kienyeji walikuwa ni muhimu kuwakilishwa ndani ya Bunge hilo la Katiba kuliko Jukwaa la Katiba Tanzania?

Hata hivyo, funga-kazi katika mshangao wa wachambuzi hao wa karne ijayo kuhusu tulivyoipata Katiba yetu mpya itakuwa katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Bunge hilo la Katiba.

Ndugu zangu, kama kuna kituko cha Bunge hili la Katiba ambacho kitawashangaza vijukuu na vitukuu vyetu vya karne ijayo, ni uchaguzi wa Samuel Sitta kuwa Mwenyekiti wa Bunge hilo la Katiba.

Kituko cha uchaguzi huo wa Samuel Sitta kuwa Mwenyekiti (wengine huita Spika) wa Bunge hilo la Katiba hakipo kwenye uwezo wake. La hasha. Samuel Sitta – kama alivyotamba mwenyewe wakati akiomba kura, amekuwa waziri katika awamu zote nne za utawala katika Tanzania.


Amekuwa pia mbunge kwa miaka 29; achilia mbali ukweli pia kwamba alikuwa Spika katika Bunge la Jamhuri ya Muungano, na kipindi chake alileta mabadiliko kadhaa chanya katika uendeshaji wa bunge hilo chini ya falsafa yake ya “kasi na viwango”.

Kwa hiyo, Sitta ana sifa zote za kuwa Mwenyekiti (Spika) wa Bunge hilo la Katiba, isipokuwa kuna kasoro moja kubwa; nayo ni kwamba Samuel Sitta bado ni waziri katika serikali iliyoko madarakani. Hii ni kasoro kubwa sana ambayo wachambuzi na wanazuoni wa karne ijayo watatushangaa.


Tuambizane ukweli: Katiba ya nchi yoyote ndiyo sheria mama, kwa maana kwamba sheria nyingine zote zitakazotungwa msingi wake mkubwa ni sheria hiyo mama – yaani Katiba. Sasa, kama Katiba ndiyo sheria mama, haiwezekani Mwenyekiti wa Bunge linalotunga Katiba hiyo awe ni waziri wa serikali iliyoko madarakani.


Sihitaji kuwa mtaalamu wa masuala ya mabunge ya katiba kufahamu kwamba huo ni ukiukaji mkubwa wa kanuni ya utawala bora ya kutenganisha mamlaka kati ya mihimili mikuu – Serikali, Bunge na Mahakama.
Haingii akilini mtu ambaye ni waziri katika serikali iliyoko madarakani, na kwa maana hiyo anawakilisha mhimili wa Serikali, awe tena ndiye Mwenyekiti au Spika wa Bunge – tena Bunge la Katiba!


Au tuamini ya kwamba utenganisho wa mihimili hiyo mitatu (separation of powers) – Serikali, Bunge na Mahakama, haugusi Bunge la Katiba? Kwamba hata jaji aliyeko kazini (a sitting judge) anaweza wakati huo huo kuwa Mwenyekiti au Spika wa Bunge la Katiba na mambo yakenda sawa?


Nijuavyo, kama ambavyo isingewezekana miaka ile Samuel Sitta kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Muungano kama angelikuwa ni waziri, ndivyo pia sasa asingestahili kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge hilo la Katiba kwa kuwa bado ni waziri wa serikali iliyoko madarakani.


Vyovyote vile; huwezi kuwa waziri wa serikali iliyoko madarakani, na kisha wakati huo huo ukawa Spika wa Bunge la Katiba, na bado ukatenda haki kwa wote. Haingii akilini, labda kama siku hizi hii dhana ya separation of powers imepoteza maana na umuhimu wake!

Nimejaribu kutafiti kidogo kama kuna nchi barani Afrika ambazo maspika au wenyeviti wa mabunge ya Katiba walikuwa pia wakati huo huo ni mawaziri, lakini sikufanikiwa kupata nchi ya namna hiyo. Kama ipo au kama zipo, naomba nielemishwe.


Chukulia, kwa mfano, Bunge la nchi jirani ya Kenya ambalo mwaka 2010 lilipitisha Katiba mpya ya nchi hiyo iliyoandaliwa na jopo la wataalamu na kamati ndogo ya Bunge. Spika wa bunge hilo alikuwa Kenneth Marende. Huyu hakuwa waziri wakati huo huo, na wala hakupata kabisa kuwa waziri.


Chukua mfano mwingine wa Bunge la Katiba la Afrika Kusini lililoandika Katiba mpya ya nchi hiyo baada ya kutokomezwa ubaguzi – Katiba iliyoanza kutumika Februari 7, 1997. Mwenyekiti wa Bunge hilo la Katiba alikuwa Matamela Cyril Ramaphosa. Huyu hakuwa waziri katika Serikali ya Afrika Kusini wakati huo wa kutunga Katiba, na wala hajapata kuwa waziri katika serikali hiyo.


Chukulia mfano mwingine wa hivi karibuni wa nchi ya mbali kabisa – Nepal. Januari 20, mwaka huu, Bunge la Katiba la Nepal lilimchagua Surya Bahadur kuwa Mwenyekiti wake. Huyu bwana hakuwa waziri wakati anachaguliwa katika nafasi hiyo ila huko nyuma alipata kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo.


Kwa ufupi, ninachosema ni kwamba, unapozungumzia mihimili mikuu mitatu ya utawala – yaani Serikali, Bunge na Mahakama, si busara hata kidogo kumchagua mtu ambaye tayari ni waziri katika serikali iliyoko madarakani au jaji ambaye yuko bado kazini kuwa Mwenyekiti (Spika) wa Bunge la Katiba.


Sasa, yawezekana labda sheria zetu au kanuni zetu zilizopo hazikatazi jambo hilo, na ndiyo maana Sitta akagombea, lakini best practise ingekuwa ni kwa Sitta kutangaza kujiuzulu uwaziri mara baada ya ushindi wake huo wa kuwa Mwenyekiti (Spika) wa Bunge la Katiba.


Binafsi, ndivyo nilivyotaraji Sitta angefanya wakati akizungumza kutoa shukrani zake kwa wajumbe wa Bunge hilo la Katiba kwa kumchagua kuwa Mwenyekiti (Spika) wao, lakini sivyo alivyofanya.
Badala ya kutangaza kujiuzulu uwaziri ili kuifanya kazi yake hiyo ya miezi mitatu kwa uhuru mkubwa bila ya shinikizo lolote kutoka kwa mwajiri wake – yaani Serikali, yeye aliishia kusema tu ya kwamba hatawavumilia wanaotaka kuvunja Muungano.


Naichukulia kauli hiyo kama ni kitisho cha aina yake kwa wajumbe wa Bunge hilo la Katiba wanaoamini kuwa wakati umefika sasa wa kuuvunja Muungano. Kwa maneno mengine, kauli hiyo ya Sitta aliyoitoa hata kabla hajakalia kiti chake, ni ya kuwaziba midomo wajumbe wa Bunge hilo la Katiba wanaoamini kuwa wakati sasa umefika wa kuuvunja Muungano huo.


Sote tunafahamu kwamba hakuna kura yoyote ya maoni iliyopigwa ambapo wananchi – Bara na Visiwani waliulizwa kama wanataka Muungano au hawautaki na matokeo ya kawa wengi yakawa kwamba wanautaka.


Sasa, kama kura hiyo ya maoni haijawahi kupigwa, Sitta amepata wapi jeuri ya kujaribu kuwafunga mdomo wajumbe wa Bunge hilo la Katiba wanaotaka Muungano uvunjwe? Si mtu anasikilizwa hoja zake na anashindwa kwa hoja, sasa vitisho vya Sitta vya nini?

Bila shaka kauli hiyo ya Sitta ya vitisho kwa wajumbe wa Bunge la Katiba wanaotaka Muungano ufikie kikomo inatoka serikalini ambako yeye ni waziri; kwani huo ndiyo msimamo wa serikali iliyoko madarakani.


Sitashangaa huko mbele ya safari, kwenye kipengele cha rasimu ya Katiba mpya kinachozungumzia uwepo wa serikali tatu, yeye Sitta akashinikiza kibabe wajumbe kukubali serikali mbili. Sitashangaa kwani huo ndiyo msimamo wa serikali ambayo yeye bado ni waziri!

Na huo ni mfano mmoja tu wa kwa nini waziri aliye madarakani hakustahili kuwa Mwenyekiti (Spika) wa Bunge letu la Katiba.

Nina hakika watafiti na wachambuzi wa karne ijayo watakuwa na orodha ndefu ya vituko vya bunge letu hili la Katiba. Naam, orodha ndefu ya vituko itakayowashangaza wote.

Nihitimishe kwa kusisitiza kwamba; Samuel Sitta angejijengea heshima kubwa katika historia ya taifa letu kama angekubali ‘kufa kidogo’ kwa kujiuzulu uwaziri mara tu alipochaguliwa kuwa Spika (Mwenyekiti) wa Bunge letu la Katiba!


Chanzo raiam wema .
 
Moja ya makala nzuri na kutafakarisha! Nikiangalia vituko vinavyo endelea siamini kama utawala wa JK na Bunge Maalumu la Katiba lililojaa wana CCM lina uwezo wa kulipatia taifa Katiba itakayo dumu na kukubalika na wengi.

Kuhusu Samwel Sitta nilishangaa alipokua anapigiwa debe mpaka na baadhi ya Wapinzani. Sitta ninaye mfahamu hakustahili hiyo nafasi ambayo inahitaji mtu ambaye hayuko ktk ushabiki wa makundi ya siasa.

Sitta ni Waziri wetu wa EAC anatakiwa kuhudhuria mikutano ya Mawaziri wa EAC na kujibu barua za Watanzania na Wawekezaji wanaotaka kuwekeza kupitia Protocol za EAC. Ukifika kufuatilia unajibiwa Waziri hayupo, na Naibu wake kisheria hana haki ya kusaini barua hiyo!! Itaku ni heshima kwa Taifa letu kama atajiuzulu ktk hii nafasi apewe Mtanzania mwingine yeye abaki na Uenyekiti wa Bunge Maalumu.
 
Back
Top Bottom