TV Ya JF: 'Baba, Hela Hii Inanunua Nini?'

X-PASTER

JF-Expert Member
Feb 12, 2007
11,610
1,810
'Baba, Hela Hii Inanunua Nini?'

"Baba hela hii inanunua nini?" aliniuliza binti yangu mwenye umri wa miaka minne. Niligeuka na kuangalia, halafu baada ya kuona sarafu aliyoishika mkononi nilimjibu", hainunui kitu chochote". "Nataka nikanunue Big G", alisistiza. Mjadala huu ulikatizwa na kaka yake aliyemwambia kwa msisitizo, "hela hiyo ndogo hainunui Big G." Nilimshukuru kwa kunisaidia kumaliza hilo kasheshe lakini akili yangu ilisafiri kurudi miaka ya nyuma, zamani kidogo enzi hizo nikiwa shule ya msingi.

Niliangalia ile sarafu ya shilingi moja na kukumbuka jinsi nilivyokuwa mwingi wa furaha nikienda shuleni asubuhi nikiwa nimepewa Shs.1. Nakumbuka jinsi ambavyo niliweza kununua vitu vingi vya kula na rafiki zangu na bado nilibakisha senti 50/- kwa ajili ya matumizi ya shule kesho yake. Sasa hivi taswira ninayoiona kwenye Shs.1. hii inafanana na ile taswira niliyoiona enzi zile katika sarafu ya senti 1, ile yenye tundu katikati - pesa isiyo na thamani!

Hata hivyo mawazo yangu yanakatizwa mara kwa mara na kelele za watoto wangu wanao nyang’anyana pesa hii na huku wakizomeana "ooh! Hela yenyewe hainunui kitu hiyo!" Naamua kurudi kutoka zamani mpaka sasa na kujiuliza hali itakuwaje wakati watoto hawa nao watakapofikia umri kama wangu. Je, na wao watashuhudia haya maswali ya "baba hela hii inanunua nini?"

Watakapokumbuka jinsi walivyokuwa wanazomeana juu ya Sh.1 ambayo hainunui kitu watajisikiaje? Je ni pesa yenye thamani gani sasa hivi ambayo wakati huo itakuwa kama hii Shs.1 ya wanangu na ile senti moja yangu? Ni shilingi ngapi za sasa zitakuwa na taswira hii ya magazigazi (mirage)? Ya kuitegemea kununulia kitu lakini mara tu unagundua kuwa haiwezi kukidhi haja yako.

Wakati haya yanaendelea nakumbuka kuwa mimi mwanauchumi, japo katika anga la nyumbani kwangu. Lakini najipa moyo kuwa naelewa kidogo kuwa thamani ya pesa ina uhusiano na hali ya uchumi wa nchi. Kwa namna gani? Nawachia wachumi wenyewe. Hata hivyo hili linakumbusha suala la umaskini wa nchi yangu na hususan katika ule mkutano wa kuondoa umaskini katika nchi za dunia ya tatu, Tanzania ikiwa mojawapo iliyochaguliwa kutokana na kuonyesha mikakati ya kufuta umaskini.

Hata hivyo, mambo ya kwenye mkutano huu naona kama vile hayanipi matumaini ya kuondoa umaskini na hatimaye kupanda kwa thamani ya pesa. Naona kuna ukungu mwingi hasa kutokana na uzoefu wa huko nyuma, kuwa mikataba ikishasainiwa, pesa za misaada mbalimbali zinafujwa na watu wachache. Na kwa vile wahusika hawakukanusha, nafikiri ni za kweli. Hata hivyo wakipenda wanaweza kujitetea kuwa misaada ni ya watu maskini, na wao ni maskini pia. Kwani kuna ubaya gani wakianza kuondoa umaskini wao ili waweze kuwasaidia maskini wenzao baadaye? Kwa kweli mikakati ya nchi kuondoa umaskini haiwasaidii maskini wengi, bali wachache tu walioko mjini. Ama kweli hii ndio kasi mpya nguvu mpya na hari mpya, sina uhakika kasi na hari serikali tulio nayo inatupeleka wapi!?

Pamoja na haya yote ninayowaza, bado mwanangu anataka kwenda kununua Big G na ile Shs.1. Kwa nini asiweze kupata Big G au hata karanga dukani na ile ni hela? Labda hizi kampeni zitakapo anza rasmi nitaenda kusikiliza na kuuliza kule tunapopelekwa na hii kasi mpya na hari mpya, labda tunaweza kupata la kusaidia ili mwanangu huyu apate matumaini kidogo. Lakini, hawa wagombea kuna wale walio na madeni ya miaka mitano iliyopita. Ahadi zile hazijatimizwa watamsaidiaje mwanangu? Na hao wengine je wanaelewa tatizo la mwanangu?!

Ushauri wangu unaelewa fika juu ya kampeni na uchaguzi, na ningependa wagombea waelewe hili tatizo kwamba si suala la mtoto mtukutu, asiyeambilika la! Hili ni suala letu na kizazi kipya. Je watoto wetu warithi umaskini na thamani ndogo ya shilingi?

Wapiga kura wanahitaji mgombea atakayeleta mabadiliko, atakayeondoa kero hii ya kuwa na pesa isiyo na thamani, pesa isiyoweza kununua kitu. Ambaye atawafanya watoto na kizazi kipya wasizomeane kwa kuwa mmoja wao ana pesa isiyoweza kununua Big G ama karanga. Mgombea ambaye anajua namna ya kuwasaidia ipasavyo tabaka la "walalahoi".

Wanaosaini mikataba ya kuondoa umaskini wa nchi, lakini kwa makusudi kabisa wakaamua, Ah hapana, ....wakasahau na kuishia kuondoa umaskini wao tu. Labda thamani ya pesa itabadilika angalau kidogo na labda baada ya miaka mitano wanangu hawa watauliza "Baba hela hii inanunua vitu vingapi? Na si inanunua nini?

Wananchi watakuja tu kugundua kwamba mafunza hustawi kwenye kinyesi, na dawa ya mafunza ni kuondoa kinyesi. Kukizoa na kukitupilia mbali, kwa vyovyote vile, na kwa lolote lile, iwe kwa chepe, kwa jembe, au hata kwa mikono, wakiamua, hata wakichafuka watanawa.
 
Bado nina kitabu changu cha akiba NBC, MASDO House cha mwaka 81. Kinaonyesha entry ya mshahara wangu wa kwanza baada ya kugraduate Mlimani nikiwa mhandisi NEDCO. TSh 1,556 kwa mwezi. Ni ajabu inflation inavyokwenda kasi.
 
Nakumbuka siku moja niliokota noti nyekundu ya shs mia moja, aisee nilipiga ofa darasa zima lakini sikufikia shs kumi kwa matumizi. enzi hizo bungo kubwa sent tano, mhogo wa kukaanga senti tano, maji ya ukwaju senti tano, keki senti kumi, chapati senti kumi, andazi mulemule, bumunda senti ishirini (ya mtama na sukari guru), kubiti senti ishirini, sukari guru senti thelasini, mkate gloria shilingi moja, mkate wa siha shilingi moja na senti hamsini, muwa thumuni, kikombe cha ubwabwa (uji wa mchele, tena mtamu ukila kwa kutumia jani la mkorosho kama kijiko) senti sabin na tano, nauli uda senti hamsini (vingine ongezea wewe).

Yaani naona kama jana vile.
 
Na kwa mwendo wa infalation tulionao tayari tunahitaji noti ya sh 50,000. Hata wasio na ukwasi mkubwa wanapata tabu na mabunda ya fedha.
 
Sasa kama watanzania tunafanya nini kupunguza anguko hili la kasi la fedha yetu? nina ushauri... tuanze ubunifu ili tuwe na bidhaa bora za kuuza nje. fedha yetu itapohitajika kwa wingi itapanda thamani. tupunguze kutumia bidhaa za wenzetu kama nguo za china, maua ya china, nk. tuache mafuta pekee ndio yatuumize na ikiwezekana tupunguze matumizi ya mafuta kwa ku-substitute na gesi ya songosongo, halafu tujiulize kuna mabadiriko? au mnasemaje wakuu... au naota? sijui lolote kuhusu mkataba wa kampuni inayochimba uranium huko songea ambayo tayari imeanza kazi... itakuwana manufaa yoyote katika uchumi wetu au ndio yaleyale!
 
Nakumbuka siku moja niliokota noti nyekundu ya shs mia moja, aisee nilipiga ofa darasa zima lakini sikufikia shs kumi kwa matumizi. enzi hizo bungo kubwa sent tano, mhogo wa kukaanga senti tano, maji ya ukwaju senti tano, keki senti kumi, chapati senti kumi, andazi mulemule, bumunda senti ishirini (ya mtama na sukari guru), kubiti senti ishirini, sukari guru senti thelasini, mkate gloria shilingi moja, mkate wa siha shilingi moja na senti hamsini, muwa thumuni, kikombe cha ubwabwa (uji wa mchele, tena mtamu ukila kwa kutumia jani la mkorosho kama kijiko) senti sabin na tano, nauli uda senti hamsini (vingine ongezea wewe).

Yaani naona kama jana vile.

Ni kweli tumetoka mbali, ila tusipo angalia uko tunapokwenda panaweza kuwa mbali zaidi.
 
Back
Top Bottom